Katika uchaguzi huu wa Igunga CUF tumepambana na changamoto kubwa ya kujibu propaganda zilezile kuwa eti "Sisi ni CCM B", kila tulikoenda tumekutana na kikwazo hiki, tumejaribu kwa dhati kuwaelimisha wananchi bila mafanikio na muda umekuwa ukikimbia kuliko upepo.
Hata hivyo bado naamini kuwa tutapata fursa kubwa ya kuwaelimisha wananchi siku za usoni. Mimi na wenzangu hatutakata tamaa kwani MAFANIKIO KATIKA NYANJA YA SIASA huhitaji mioyo migumu.
Natambua kuwa uongozi ni dhamana nzito inayohitaji kujipanga zaidi na zaidi, Na CUF itazidi kujipanga zaidi na zaidi na kila tutakapoanguka tutanyanyuka na kuanza safari, hakika TUTAFIKA.
Chama changu kinakabiliwa na changamoto kubwa sana mbele ya safari na kwa hakika inahitaji tuzidi kujipanga na kujiimarisha. Kama chama hatutajilaumu kamwe, tumeonesha uwezo mkubwa na kufanya kampeni sahihi tukiwa na mgombea wa kiwango kizuri kwa mpiga kura yeyote anayehitaji kiongozi. Lakini kusimamisha mgombea mzuri na kufanya kampeni nzuri wakati mwingine siyo sababu ya kufanya vizuri. Maamuzi ya nani awe mbunge, ni mzuri au mbaya, anafaa au hafai yako kwa wananchi.
Wananchi wa Igunga tunawashukuru kwa namna walivyotuunga mkono na tunawaomba wawe kitu kimoja katika kuiendeleza Igunga yao kwani mshindi akishatangazwa yeye ni mbunge wa wananchi wote. Vyama vyetu hivi vipo ili kuisaidia jamii kupata kiongozi mzuri tu, nasi kama chama tumetimiza wajibu wetu.
Mimi kama kiongozi wa ngazi ya juu wa CUF - Tanzania Bara(Bila kujali nimekuwa kiongozi wa ngazi ya juu miezi minne tu iliyopita tu) nabeba dhamana kwa matokeo yote tuliyopita, najitwika mzigo wa kusimama imara kuiimarisha CUF.Sitatoka CUF na kukimbilia kwenye vyama vyenye nguvu Tanzania bara kama CHADEMA n.k. eti kwa sababu tu CUF imefanya vibaya kwenye uchaguzi. Ninaamini katika CUF na nitaisaidia Tanzania yangu nikiwa CUF, ninaamini siku moja wakati CUF imeimarika nitatajwa kati ya watu ambao hawakukata tamaa na hawakuyumbishwa na magumu yaliyowakabili na walisimama kidete kwenda mbele.