WAGOMBEA ubunge katika Jimbo la Igunga, Leopold Mahona wa CUF na Mwalimu Joseph Kashindye wa Chadema, walimkaba koo mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu katika mdahalo uliofanyika mjini Igunga kuwa amehusika na mikataba mibovu ya madini.Walitoa maneno hayo kwenye mdahalo wa uchaguzi mdogo wa Igunga na Tanzania tunayoitaka ambao uliwahusisha wagombea hao watatu uliofanyika katika ukumbi wa Sakawa.
Mahona alimtuhumu Dk Kafumu kuwa ndiye aliyesaini mikataba mibovu ya madini inayoligharimu taifa hadi sasa akidai kwamba katika kila Sh100 ya Tanzania, nchi inapata Sh3.Hakuna wilaya ambayo mtu anaweza kutembea na kuokota almasi, isipokuwa Igunga. Lakini sekta hiyo iko chini na chanzo ni huyu bwana, nani asiyejua kuwa ndiye aliyesaini mikataba mibovu ya madini? alihoji Mahona.
Mikataba ambayo katika kila Sh100, Serikali ya Tanzania na watu wake inaambulia Sh3!alisema Mahona huku akishangiliwa na watu waliohudhuria madahalo huo.Akijibu hoja hiyo, Dk Kafumu alisema hakuwahi kuingia mikataba ya madini, bali alikuwa msimamizi wa sheria iliyotungwa bungeni.
Mimi kazi yangu ni kusimamia sheria na si kusaini mikataba. Kazi ya kusaini mikataba inafanywa na waziri na sheria inatungwa bungeni kina Zitto (Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Chadema) wanafahamu, alisema Dk Kafumu.
Hata hivyo, baada ya majibu hayo mgombea wa Chadema Kashindye, alisimama na kitabu kinachoelezea utafiti wa madini nchini alichoeleza kuwa hakijulikani kwa wananchi wa kawaida na badala yake, kimeuzwa Ulaya kutafuta wawekezaji.
Katika kitabu cha mgombea wa CCM kinaeleza kuwa Igunga kuna madini ya aina 11, kitabu hiki amekiuza na kukitangaza Ulaya kuvutia wawekezaji, woga wangu ni kuwa ule mpango wa kufukia wananchi katika Mgodi wa Bulyanhulu, unaweza kufanyika hapa Igunga, alisema Kashindye