n00b
JF-Expert Member
- Apr 10, 2008
- 1,007
- 2,675
Ongezeko la mikopo isiyolipika na kupungua kwa faida kwa takriban Sh50 bilioni mwaka 2016, kunaiweka njiapanda Benki ya CRDB na inabidi hatua za haraka zichukuliwe kurekebisha mwenendo.
Faida ya benki hiyo kubwa nchini imepungua na kuhitimisha dalili zilizojitokeza kwenye robo ya tatu ya mwaka 2016 ilipotangaza kupata hasara ya takribani Sh2 bilioni. Faida ya CRDB imeshuka kutoka Sh122.3 bilioni iliyopatikana mwaka 2015 mpaka Sh73.4 bilioni mwaka jana na kuwa miongoni mwa benki ambazo hazikufanya vizuri katika kipindi hicho.
Kupungua kwa faida ambayo kwa miaka mitano iliyopita imekuwa ikiongezeka, kunaweza kuwa kumesababishwa na mambo kadhaa ambayo yanaonyesha ugumu ambao taasisi hiyo kubwa nchini ilikumbana nao kwa mwaka 2016.
Mikopo zaidi ya kiwango cha amana
Ripoti ya mwaka ya hesabu za fedha za benki hiyo inaonyesha uwezekano wa kusitishwa kwa utoaji wa mikopo ili kuweka mambo sawa baada ya kuzidi ukomo uliopo kwa mujibu wa kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Miongoni mwa vipengele vilivyokiukwa ni kifungu cha 7 cha Kanuni za Benki na Taasisi za Fedha za mwaka 2014 kinachozitaka kutokopesha zaidi ya asilimia 80 ya amana walizonazo.
Mpaka mwisho wa mwaka, CRDB ilikuwa imefikisha asilimia 84, jambo linalomaanisha kuwa haitaendelea kutoa mikopo mpaka itakapofanya mabadiliko na kurekebisha kasoro hiyo.
Hiyo ni muhimu kwa sababu, kwa mujibu wa wataalamu, shughuli kubwa ya benki yoyote ya biashara, ni mikopo ambayo imetengenezewa kanuni na taratibu ambazo ni lazima zifuatwe.
Kuonyesha inachukua hatua, katika robo ya mwisho wa mwaka, kiasi cha mikopo kilichotolewa na benki hiyo kilipungua kwa Sh84 bilioni ingawa amana za wateja hazikubadilika ndani ya kipindi hicho, tofauti na ilivyokuwa katika robo ya tatu ya mwaka wakati amana hizo zilipoongezeka kwa asilimia moja.
Kwenye robo ya nne ya mwaka, benki hiyo ilikuwa imetoa mikopo yenye jumla ya Sh3.234 trilioni, ikilinganishwa na Sh3.318 trilioni ya robo iliyoishia Septemba.
Ripoti ya kundi la benki hiyo yenye matawi nje ya nchi, inaonyesha mikopo yake imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Katika taarifa yake ya mwaka 2015, mikopo iliongezeka na kufikia Sh3.34 trilioni kutoka Sh2.576 trilioni iliyokuwapo mwaka 2014 wakati kwa robo ya mwisho ya mwaka 2016 kundi lilitoa jumla ya mikopo ya Sh3.27 trilioni ikipungua kutoka Sh3.361 iliyokuwapo katika robo ya tatu.
Tatizo jingine ni mikopo isiyolipika. Hadi Desemba 2016, CRDB ilikuwa na mikopo isiyolipika kiasi cha Sh111.4 bilioni kikiwa kimeongezeka kwa takriban mara mbili ndani ya robo ya mwisho, kutoka Sh66.7 bilioni iliyokuwapo katika robo iliyoishia Septemba 2016.
Kiwango hicho ni sawa na asilimia 13 ya mikopo iliyotolewa, hivyo kuifanya kuvunja kanuni nyingine ya BoT inayotaka kiasi hicho kisizidi asilimia tano ya mikopo yote. Mikopo hiyo kwa kundi ilikuwa asilimia 11 ambazo, kama ilivyo kwa asilimia 13 za benki, iliendelea kutobadilika kati ya robo ya tatu na ya nne.
Hesabu za mwaka za CRDB zinabainisha kupungua kwa mapato yatokanayo na biashara ya kimataifa (fees and commissions) ambayo huiwezesha benki kupata kamisheni kutokana malipo yanayofanywa baina ya mteja na muuzaji.
Mapato hayo yalipungua kutoka Sh47.741 bilioni Septemba mpaka Sh43.059 bilioni kwa Desemba. Hata mapato ya kundi yalishuka pia kutoka Sh50 bilioni mpaka Sh42.734 bilioni ndani ya kipindi hicho.
Kutoka robo ya tatu kwenda ya nne mwaka 2016, amana za wateja wa CRDB ziliongezeka. Taarifa inaonyesha amana hizo zilifikia Sh3.996 trilioni Desemba kutoka Sh3.98 trilioni, likiwa ni ongezeko la Sh16 bilioni ndani ya kipindi hicho.
Licha ya amana za wateja kuongezeka kwa kiasi hicho, ukuaji wa amana zote (deposit growth) ulishuka kutoka asilimia moja iliyokuwapo katika robo ya tatu mpaka sifuri hadi kufikia Desemba.
Amana za wateja kwa kundi ziliongezeka kwa Sh12 bilioni zikitoka Sh4.063 trilioni mpaka Sh4.051 trilioni ndani ya kipindi hicho, ingawa ukuaji wa amana zote uliendelea kubaki asilimia moja ndani ya muda huo.
Katika ripoti yake ya mwaka 2015, CRDB iliainisha vihatarishi vitano vya biashara ambavyo inakabiliana navyo. Vihatarishi hivyo ni mikopo, kiwango cha fedha kinachohitajika kukidhi mahitaji ya uendeshaji na hatari zinazosababishwa na riba na viwango vya kubadilisha fedha.
Vihatarishi vingine vilikuwa katika kufuata taratibu au uratibu katika uendeshaji na vya kimkakati. Ripoti hiyo ilibainisha amana za wateja kuwa ndicho chanzo kikubwa cha mapato ya taasisi hiyo.
Pamoja na hali ngumu iliyojitokeza katika maeneo kadhaa, benki hiyo ilijiimarisha kwa kuongeza idadi ya matawi na kuajiri wafanyakazi wapya ili kuhudumia wateja wake kwa viwango bora.
Kwa mwaka mzima, benki iliongeza matawi sita kote nchini na kufikisha matawi 180. Ongezeko hilo lilienda sambamba na idadi ya wafanyakazi ambao jumla yao ilifikia watu 2,760 kutoka 2,377 waliokuwapo mwaka juzi ikimaanisha kwamba wafanyakazi wapya 383 waliajiriwa.
Kutokana na ongezeko la wafanyakazi hao, jumla ya mishahara (salaries and benefits) ilipanda kutoka Sh139.526 bilioni mwaka 2016 mpaka Sh165.015 bilioni mwaka jana sawa na ongezeko la Sh25.489 bilioni kwa mwaka huo.
Kundi liliongeza wafanyakazi 545 kutoka 2,651 waliokuwapo mwaka 2015 mpaka 3,196 mwaka jana baada ya matawi yake pia kuongezeka kutoka 199 mpaka 250 ndani ya kipindi hicho huku mishahara ya watumishi hao ikipanda kutoka Sh152.796 bilioni mpaka Sh184.554 bilioni sawa na ongezeko la Sh31.758 bilioni kwa mwaka 2016.
Jitihada za kuwapata watendaji wa CRDB ili kueleza kuhusu ripoti ya benki hiyo ya mwaka hazikuzaa matunda. Licha ya kumpata Mkurugenzi wa Uhusiano wa benki hiyo, Tuli Mwambapa ambaye alitaka atumiwe maswali kwa baruapepe, hakuyajibu.
Hata mwandishi wetu alipofuatilia na kukutana na meneja uhusiano wake, Godwin Semunyu ambaye aliomba apewe wiki moja ya kutafuta majibu hayo, hakutekeleza ahadi yake pia.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Benki Kuu, Kennedy Nyoni alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa hatua zinazochukuliwa kwa benki zinazokiuka kanuni zilizoweka, alijibu kwa jumla, “BoT inaweza ikaitaka benki husika kuwasilisha mpango wa kurekebisha hali hiyo baada ya kujua sababu zilizochangia au kuwataka wamiliki kuongeza mtaji kufidia kama kuna hasara.”
Wakizungumza na mwandishi wetu, wachambuzi wa masuala ya kibenki walikuwa na maoni tofauti.
Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya fedha, Reginald Baynit alisema kampuni za simu zimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa amana za wateja wa benki za biashara nchini.
“Wananchi wengi wanatumia zaidi mitandao ya simu licha ya gharama kubwa zilizopo kutokana na urahisi wa huduma uliopo,” alisema Baynit.
“Kinachotakiwa ni ubunifu wa kukabiliana na ushindani uliopo. Mawakala wa benki hizo waliopo mtaani watasaidia lakini jitihada zaidi zinahitajika,” aliongeza.
Meneja mmoja wa taasisi ya kimataifa ya ukaguzi wa fedha ambaye hakupenda kutajwa gazetini, alisema mapato ya benki yanatokana zaidi na riba itokanayo na mikopo ambayo hata hivyo, lazima itolewe kwa umakini.
“Benki yenye kiasi kikubwa cha mikopo isiyolipika inajiweka katika hatari ya kufilisika. Hii ndiyo iliyoifikisha Twiga (Bancorp) ilipo,” alisema na kufafanua kwamba mikopo hiyo ni mingi nchini.
“Tusipokuwa makini, mikopo hii itaziangamiza benki nyingi nchini,” alisema.
Kutokana na kuelemewa na mikopo isiyolipika, miongoni mwa sababu nyingi, mwaka jana, Benki ya Twiga Bancorp ilishindwa kujiendesha hivyo kuwekwa chini ya uangalizi wa BoT ambayo inatafuta mdau mwenye uwezo wa kuisimamia ili iendelee kutoa huduma.
Kuhusu kuongezeka kwa wafanyabiashara wanaoshindwa kurejesha mikopo yao hivyo kuathiri ufanisi wa benki za biashara, alisema kunatokana na Serikali kuchelewa kuwalipa wazabuni wake.
Chanzo: Mwananchi