Corona yatajwa kambi Yanga

rodrick alexander

JF-Expert Member
Feb 12, 2012
15,190
20,156
KLABU ya Yanga imesitisha kambi yake nchini Morocco kwa sababu mbalimbali na baadhi ya wachezaji wakirejea Tanzania jana
huku wengine wakilazimika kusalia nchini humo.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa na uongozi wa Yanga ni idadi ya wachezaji kupungua baada ya baadhi kwenda kujiunga na timu
zao za taifa kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mapema mwezi ujao.

Lakini kwa taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka chanzo chetu ndani ya kambi hiyo iliyopo jijini Marrakech, Morocco na vyonzo vyetu
hapa nchini, zimedai kwamba kuna baadhi ya wachezaji wamekutwa na maambukizi ya virusi vya corona na hao hawatarejea kwani
watalazimika kubaki karantini kwa wiki moja.

"Kuna wachezaji 14, wamepata maambukizi ya virusi vya corona na si 19 kama ambavyo baadhi ya taarifa zinadai, hivyo wametakiwa
kukaa karantini kwa wiki moja," kilieleza chanzo chetu na kuomba hifadhi ya jina lake.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Mhandisi Hersi Said, aliyeko
kambini nchini Morocco na timu hiyo, alipoulizwa sababu ya kuvunja kambi na kurejea kwa mafungu, alisema ni kutokana na ratiba ya
ndege.

"Ni kweli tumelazimika kuvunja kambi na timu ilitakiwa kurudi kwa pamoja, lakini kwa sababu ya tatizo la kubadilisha tiketi kuna watakaorudi leo [jana] na wengine tarehe 27,’’ alisema.

Wakati Hersi akiyasema hayo, taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kwa vyombo vya habari jana ilieleza: "Uongozi wa Klabu ya Yanga unapenda kuutaarifu

umma kwamba umeamua kusitisha kambi ya msimu (Pre-season) na timu itarejea leo (jana). "Awali, timu ilipanga kuwa na kambi ya siku 10 za mazoezi, ambazo zilikuwa zikamilike Agosti 27, lakini kutokana na sababu mbalimbali na kwa maslahi mapana ya klabu, uongozi umeamua kuchukua hatua ya kusitisha kambi hiyo na maandalizi yataendelea kambini Avic Town."

Katika taarifa hiyo, pia ilieleza kuwa klabu hiyo itafanya uzinduzi wa jezi mpya za msimu ujao Jumatano wiki hii na baada ya uzinduzi huo, zitapatikana madukani kwa ajili ya wapenzi, mashabiki na wanachama kununua.

"Uongozi unawaomba, wanachama, wapenzi na mashabiki kuendelea kuhamasishana kwa ajili ya Wiki ya Mwananchi ambayo kilele chake kitakuwa Agosti 29, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa," ilieleza.

Yanga iliweka kambi nchini humo kujiandaa na msimu mpya hususan kuelekea mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United itakayochezwa kati ya Septemba 10-12, mwaka huu ikiwa ni zaidi ya wiki mbili kabla ya Ligi Kuu Bara kuanza.

Ligi Kuu Bara itaanza Septemba 29 ikiwa ni siku nne baada ya Simba na Yanga kufungua pazia la ligi hiyo kwa kucheza mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mujibu wa gazeti la Nipashe
 
Back
Top Bottom