Chozi Lisilofutika

Shunie

JF-Expert Member
Joined
Aug 14, 2016
Posts
157,054
Reaction score
463,869
Mtunzi Juma hiza 01

Suzani alikuwa amejifungia chumbani kwake, wakati huo alikuwa akilia kwa uchungu. Hakutaka kuamini kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yake.Mkononi mwake alikuwaameishikilia picha ya mwanaume mmoja. Aliitazama picha hiyo kwa muda wa dakika kadhaa huku machozi yakiendelea kumbubujika mashavuni mwake.

Moyo wake ulikuwa katika maumivu makali mno, kila alipokuwa akiendelea kuitazama picha ya mwanaume huyo ndivyo ambavyo maumivu yalizidi kuongezeka moyoni mwake.

Alijisikia vibaya sana, alijutia mambo mengi mno aliyoyafanya katika maisha yake na mwanaume huyo.Kuna muda aliona kama alionewa, hakustahili kabisa kupitia maumivu yale aliyokuwa nayo katika kipindi hicho.

Kitendo cha kuendelea kuitazama picha ya mwanaume huyo ambayo kiukweli iliendelea kumuumiza tu! aliona sio jambo zuri hivyo alichoamua kukifanya ni kuigeuza upande wa pili. Alifanya hivyo ili asiendelee kuumia.

Hilo bado halikuwa suluhisho la maumivu ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. Kichwani mwake bado taswira na kumbukumbu za mwanaume huyo zilimjia.
Alikumbuka mambo mengi mno aliyoyafanya na mwanaume huyo aliyekutana naye katika mtandao wa Facebook na kuanzisha mahusiano naye ya kimapenzi.

Katika kipindi hicho hakuwa naye, alimtelekeza tena na mimba ya miezi miwili. Hilo lilizidi kumuumiza mno.
Hakukuwa kuna kipindi ambacho moyo wake uliwahi kupata maumivu kama katika kipindi hicho, yalikuwa ni maumivu makali sana yaliyochanganyika na kumbukumbu zilizomuumiza kupita kawaida.

Muda mfupi kabla ya kuingia ndani ya chumba chake na kuanza kulia, alitoka kuzungumza na baba yake ambaye alimuweka kikao na kuanza kumuhoji juu ya ujauzito huo.

Baba yake aliyejulikana kwa jina la Mzee Mushi hakuonekana kupendezewa na tukio hilo hata kidogo na ndiyo sababu iliyompelekea mpaka akamuita mwanaye na kuanza kumuuliza juu ya mtu anayehusika kumpa ujauzito huo.

“Nakuuliza huu ujauzito ni wa nani?” aliuliza Mzee Mushihuku akimtazama binti yake kwa macho ya ukali.Suzani hakujibu kitu, alianza kulia kilio cha kwikwi.
Kilio hicho cha Suzani wala hakikumuingia akilini Mzee huyo ambaye tayari hasira zilikuwa zimempanda. Alichokuwa akihitaji kukifahamu ni mtu aliyehusika kumpa ujauzito mwanaye.

“Mwanangu baba yako si anakuuliza lakini mbona humjibu?” aliuliza Mama yake Suzani baada ya kumuona mumewe amezidi kupandwa na hasira.

“Mama na Baba naomba mnisamehee,” alisema Suzani huku akiendelea kulia.
“Jibu lako na swali langu ni vitu viwili tofauti, nimekuuliza huo ujauzito ni wa nani?” aliuliza Mzee Mushi huku macho yakimtoka.

Suzani hakujua ni wapi ambapo alitakiwa kuanza kuzungumza, hakujua ni lugha ipi ambayo alitakiwa kuitumia kuwaeleza wazazi wake juu ya mwanaume huyoambaye alihusika kumpa ujauzito.
Aliendelea kubaki kimya kitendo ambacho kilizidi kumuudhi mno Baba yake, akainuka pale kwenye kochi alipokuwa amekaa, akamsogelea mwanaye.

“Nakupa siku tatu uwe umeshaniambia mwanaume huyo aliyekupa ujauzito ni nani la sivyo hii nyumba utaiona ni chungu. Haiwezekani maana hii ni dharau kabisa yaani upo chuo tena nakusomesha kwa pesa zangu mwenyewe halafu unaniletea mimba kweli?” alisema Mzee huyo huku akimnyooshea kidole cha shahada mwanaye.

Baada ya Mzee Mushi kuzungumza hayo Suzani akainuka na kukimbilia chumbani kwake ambapo akajifungia mlango.Moyo wake ulikuwa katika maumivu makali mno, akakumbuka kuichukua picha ya mwanaume huyo aliyempa ujauzito na kuanza kuiangalia. Kila alipokuwa akiendelea kuitazama picha hiyo ndivyo ambavyo maumivu yalizidi kuongezeka moyoni mwake.

Baada ya kupita siku tatu Mzee Mushi alimuita tena mwanaye na kumuuliza. Hakutaka utani hata kidogo. Siku hiyo ndiyo siku ambayo alihitaji kumfahamu mtu huyo aliyehusika kumpa ujauzito mwanaye. Kama kawaida yake, macho ya ukali yakamtoka, akamtazama mwanaye ambaye ndiyo alikuwa akijiweka sawa kuzungumza, hofu ilikuwa imemtawala.
“Sema.”

“Anaitwa Enock,” alijibu Suzani huku akionekana kuwa ni mwenye wasiwasi.
“Anaishi wapi?” aliuliza Mzee Mushi kwa sauti ya ukali.
“Mwanza,” alijibu Suzani.
“Unapafahamu mpaka kwake?”
“Hapana.”
“Kivipi?”

“TulikutanaFacebook tukaanzisha mahusiano, alipanga kuja kuniona hivyo akafunga safari kutoka Mwanza akanifuata huku Moshi,” alijibu Suzani huku akionekana kuwa wasiwasi.
Wote wawili wakachoka, hawakutaka kuamini kile walichokuwa wakikisikia.Aliposikia jina la Facebook Mzee Mushi akaonekana kushangaa zaidi kushinda mke wake.

“Eti! mlikutana Facebook?” aliuliza kana kwamba hakusikia vizuri hapo mwanzo.
“Ndiyo.”
“Halafu ikawaje?”

“Tukaanzisha mahusiano na mwisho wa siku mpaka tukapanga kukutana,” alijibu Suzani kisha hapohapo Mzee Mushi akainuka na kumpiga kofi zito ambalo likamuacha na alama ya vidole shavuni mwake.

Kile kilichokuwa kimetokea kwa binti yake huyo kilikuwa ni aibu kubwa kwa upande wakehasa ukizingatia katika mtaa huo aliyokuwa akiishi Moshi mjini, Majengo kwa Mtei yeye ndiye Mzee aliyekuwa akisifika kuwana binti mrembo ambaye alijitunza na kuwa na hofu ya Mungu.
Kutokana na uzuri aliyokuwa nao Suzani kila mwanaume aliyemuona alimtamani na kuanza kumfuatilia.

Mpaka kufikia kipindi hicho hakukuwa kuna mwanaume hata mmoja katika mtaa huowala chuoniambaye alifanikiwa kuiona hata nguo yake ya ndani.Hilo lilizidi kuwachanganya sana wanaume ambao walitamani kufanya naye mapenzi tu!.

Kwa kile kilichokuwa kimetokea kwa binti yake huyo Mzee Mushi kilimuumiza sana, kilimchanganya mno. Kuna muda alitamani mpaka kulia kwa kufikiria ni wapi ambapo angeificha sura yake kutokana na aibu kubwa aliyoipata katika maisha yake.

Moyo wake uliingiwa na chuki kubwa, kila alipokuwa akimwangalia mwananye alihisi kumchukia vibaya mno. Hakutaka kumuona mbele ya macho yake kwani aliamini kwa kuendelea kumuona kuna jambo baya ambalo angeweza kumfanyia na dunia ingemshangaa.

Mke wake aliyejulikana kwa jina laBi Anna huruma ikamuingia,hakupenda kuona binti yake akiendelea kulia na kusononeka kila siku, kama ni kosa tayari alikuwa ameshalifanya hivyo hakukuwa na jinsi tena zaidi ya kusaidiwa.

Alichokuwa akihitaji kwa wakati huo ni kuona mume wake akimsamehe Suzani na kumsaidia kutokana na hali ambayo alikuwa nayo. Alimpenda mno binti yake huyo ambaye ndiye mtoto wa pekee ambaye alijaaliwa kumpata katika kipindi chote cha ndoa yake.

Hilo lilikuwa ni jambo gumu mno, Mzee Mushi hakutaka kukubali kirahisi msamaha huo kwa binti yake.
“Mume wanu lakini..”

“Nimesema sitaki kumuona hapa nyumbani kwangu. Nitamuua,” alisema Mzee Mushi huku uso wake ukiwa tayari umebadilika.

Kwa jinsi ambavyo alikuwa akionekana Mzee huyo na maneno aliyokuwa akiyazungumza. Vilikuwa ni vitu viwili vilivyofanana.Yaani kile alichokuwa akikizungumza ndicho hicho hicho ambacho alikimaanisha.

Uamuzi ambao aliamua kuuchukua ni kumfukuza binti yake huyo. Hakutaka kumuona.

Japokuwa mkewe Bi Anna alimsisitiza na kumuomba zaidi na zaidi asichukua uamuzi huo wa kumfukuzwa binti yaohuyo ambaye kwao alikuwa kama mboni ya jicho lakini hakutaka kumsikiliza. Aliamua kumfukuza Suzani.
Suzani hakutaka kuamini kama kweli alifukuzwa nyumbani kwao tena na Baba yake mzazi.

Machozi yalikuwa yakimdondoka. Kuna muda alianza kujutiayale yote aliyoyafanya katika maisha yake. Kitendo cha kukutana na mwanaume Facebook mpaka akamuamini na kumkabidhi moyo wake ambao aliuumiza.

Muda huo tayari alikuwa amechelewa kwani hata kama angeendelea kujutia kosa alilokuwa amelifanya bado ukweli usingeweza kubadilika.

*Je, nini kitaendelea?*
*Tukutane Jumamosi mahali hapahapa.*
 
Hii Hadithi vipi?

Kuna msichana mmoja anafungua akaunti Facebook. Anaonekana kuwa mwenye furaha kujiunga na mtandao huo. Baada ya kukamilisha usajili hatimaye anafanikiwa kuna na akaunti hiyo ya facebook. Anaanza kuAdd marafiki mbali mbali anaokutana nao Facebook. Wengine anawafahamu na wengine hawajui kwani hajawahi hata kuwaona.

Picha zake anazopost katika mtandao huo zinawapagawisha wanaume. Wengi wanavutiwa na muonekano wake.

Wanaume wanaanza kumtongoza. Hicho kinakuwa kipindi kigumu kwake.

Wanaume wote hawafanikiwi kumpata kimapenzi. Hilo linawachukiza na kuwaumiza baadhi yao.

Usumbufu unaendelea mpaka pale mwanaume mmoja kati ya wanaume wanaomsumbua anafanikiwa. Anaonekana kutokata tamaa.

Hatimaye wanakuwa wapenzi wa Facebook na mwisho wa siku wanakutana. Ahadi nyingi zinaahidiwa. Msichana anapagawa na mwanaume huyo pasipokujua kuwa ni mume wa mtu.

Msichana anapata ujauzito na mwisho wa siku huyo mwanaume anamwambia ukweli kuwa ni mume wa mtu na anamkimbia.

Huo ndiyo unakuwa mwanzo wa mateso, maumivu, visa, visasi na ukatili.

Kibaya zaidi nyumbani kwao msichana anafukuzwa na wazazi wake.

Anakipitia kipindi kigumu mno na chozi lake linakosa mtu wa kumfuta.

Je, nini hatma ya simulizi hii?

Anza nayo leo.
 
Asante sana shunie.mambo ya Facebook hayo.nina ndugu yangu mmoja mume wake alimpata Facebook ameshaolewa na amepata mapacha. Ila haja jf watu wanakulana. Asante shunie
 
Asante sana shunie.mambo ya Facebook hayo.nina ndugu yangu mmoja mume wake alimpata Facebook ameshaolewa na amepata mapacha. Ila haja jf watu wanakulana. Asante shunie

Kukulana ndio mpango mama
 
*CHOZI LISILOFUTIKA-02*
Mtunzi:Juma Hiza

Miaka miwili nyuma:
Ulikuwa ni mwaka wa kwanza Suzani kujiunga na chuo kikuu cha Ushirika kilichopo moshi mjini mwaka 2015.

Alikuwa ni mwenye furaha mno baada ya kujiunga na chuo hicho tena katika kipindi hicho ambapo akili yake ilikuwa ikiwaza chuo kuliko kitu chochote kile, alikuwa akisomea Uhasibu.

Siku ya kwanza kuonekana ndani ya chuo hicho kila mvulana hakutaka kuamini, uzuri wa msichana huyo ulitokea kuwachanganya. Hakukuwa kuna mvulana ambaye alimtazama Suzani mara moja kisha asiache kurudia kumtazama.

Uzuri aliyokuwa nao Suzani ulionekana kuwa tishio kwa chuo kizima kiasi kwamba ilipelekea kupata marafiki wengi na hata maadui ndani ya kipindi cha muda mfupi tangu alipojiunga na chuo hicho.

Baada ya kupita mwezi mmoja wavulana walianza kumsumbua, kila siku Suzani alikuwa akipata usumbufu kutoka kwa wavulana hao ambao walionekana kumuhitaji zaidi ya kitu chochote.

Katika kipindi chote hicho hakukuwa kuna mvulana ambaye alifanikiwa kuwa na Suzani kimapenzi.

Alionekana kuwa ni msichana mgumu mno kuingilika ambapo kama mvulana alihitaji kumtongoza basi alitakiwa kujipanga kisawasawa.

Muonekano wa msichana huyo na jinsi alivyokuwa ameumbika kuanzia sura mpaka shepu yake yenye mvuto wa kimapenzi ulizidi kuwachanganya wavulana.

Kila aliyejitokeza kumtongoza alishindwa na mwisho alibaki kuwa mpenzi mtazamaji tu! kwani hakukuwa na njia nyingine ya kumuingilia msichana huyo ambaye alionekana kusimamia msimamo wake wa kutojihusisha kimapenzi na mwanachuo mwenzake.

Siku ziliendelea kukatika, uzuri wa Suzani nao uliendelea kuwa gumzo katika chuo hicho. Habari zake zikasambaa kila kona na kila mwanachuo aliyezisikia alihitaji kumuona na kuthibitisha kwa macho, kwani sifa za msichana huyo zilionekana kutishia amani kwa wasichana wengine ambao hawakuwa na mvuto.

Revocatius Kisoka huyu alikuwa ni mwanachuo wa mwaka wa pili, kama ilivyokuwa kwa Suzani na yeye pia alikuwa akisomea Uhasibu.

Mara baada ya kuwasikia marafiki zake wakipiga stori kuhusu msichana huyo jinsi alivyokuwa ameumbika na uzuri wake ulivyokuwa tishio kwa chuo kizima alihitaji kumuona.
Mpaka kufikia muda huo tayari ilikuwa imepita miezi miwili.

Revocatius alipoomba kuonyeshwa msichana huyo, marafiki zake walimshangaa na kuanza kumcheka. Alishtuka baada ya kuona akichekwa kwa wakati huo, hakujua ni kitu gani alikifanya cha ajabu ambacho kilisababisha mpaka marafiki zake kuanza kumcheka.

“Nini sasa?” aliuliza huku akishangaa.
“Upo dunia ipi wewe, mtoto ana mwezi wa pili sasa hujawahi hata kumuona?” aliuliza Hiza rafiki yake Revocatius huku akiendelea kucheka.

“Acha utani kaka, demu kawa gumzo hivyo chuo kizima inamaana hujawahi kumuona?” aliuliza Fredy.
“Yeah…sijamuona nasikia habari zake tu, kwani yupoje ana nini?”

“Ni shida kaka, mtoto kajaaliwa kila sifa unayoijua wewe achana na hawa mademu wengine ambao hawajui kuoga, ukimuona huyu demu lazima utakumbwa na haja,” alisema Hiza maneno yaliyomfanya Revocatius kuzidi kuwa na shahuku ya kutaka kumuona msichana huyo.

Sifa za Suzani zilimchanganya mno Revocatius, kwa wakati huo hakukuwa kuna kuna kitu alichokuwa kikihitaji zaidi ya kumuona msichana huyo.

Alipoona Hiza na Fredy wanazidi kumsifia tu bila kumuonyesha, akaamua kuwaambia ukweli kwamba anahitaji kuonana naye, hilo halikuta tatizo, akaonyeshwa.

Macho yake yalipomuona msichana huyo kwa mara ya kwanza hakutaka kuamini, alihisi mwili wake ukiwa kama umepigwa ganzi. Alibaki akimshangaa kwa dakika kadhaa mpaka pale Hiza alipomshtua.
“Umemuona sasa?”
“Ndiyo ni mzuri anavutia,” alijibu huku akitabasamu.

Hakutaka kupoteza muda, alihitaji kumfuata na kuzungumza naye japokuwa Hiza na Fredy walimwambia msichana huyo alikuwa ni mgumu kuingilika lakini hilo hakutaka kukubaliana nalo, alichokuwa akikiamini ni bahati, aliamini siku hiyo bahati ilikuwa upande wake na angefanikiwa kumpata kitendo ambacho kingewashangaza watu wengi.

Muda huo Suzani alikuwa akitoka Stationery, mkononi alikuwa ameshikilia bahasha ya kaki. Baada ya kupiga hatua tano kutoka nje ya stationery hiyo mara kwa nyuma akasikia mtu akimuita, haraka akageuka, akakutana na Revocatius.

“Mambo Suzani,” alisema Revocatius huku akitabasamu kama kawaida yake.
“Safi mzima?”
“Yeah niko poa.”
“Niambie.”

“Unaelekea wapi nikusindikize?”
“Sorry nikusaidie nini?”
Jibu hilo lilimfanya Revocatius aishiwe na pozi, hakutarajia kama angejibiwa jibu hilo tena kwa muda mfupi ambao alikuwa akizungumza naye.

Hilo hakutaka kujali, baada ya kuulizwa swali hilo akajifanya kutabasamu.
“Naitwa Revocatius,” alijitambulisha.
“So,” (Kwahiyo) alisema Suzani maneno yaliyomfanya Revocatius ashindwe kuendelea kuzungumza.

Sio kwamba alikosa maneno ya kumueleza msichana huyo la isipokuwa majibu ya mkato aliyokuwa akiyatoa ndiyo yalisababisha mpaka akashindwa kuendelea kuzungumza.

Baaada ya kukaa kimya kwa muda, Suzani aliamua kuondoka eneo hilo. Revocaius akabaki akitazama sehemu za nyuma za maumbile ya msichana huyo. Alizidi kupagawa mno.

“Kwa gharama zozote zile lazima nikupate,” alijisemea Revocatius alipokuwa akimtazama Suzani mpaka alipopotea machoni mwake.
****
Licha ya kwamba Suzani alikuwa ni msichana mrembo lakini alitokea katika familia iliyokuwa ikimjua Mungu. Baba yake Mzee Mushi na Mama yake Bi Anna walikuwa ni waumini wazuri wa kanisa la Seventh Day Adventist.

Walijitahidi kumpa malezo bora binti yao huyo ikiwa ni pamoja na kumjua Mungu na kuwa na hofu naye. Katika kipindi chote cha maisha ya Suzani alikuwa ni msichana mtaratibu, mpole lakini pia alikuwa ni msichana anayekuwa akisimamia misimamo yake aliyojiwekea.

Mtaa wa majengo kwa Mtei aliyokuwa akiishi vijana wengi walikuwa wakimlia rada. Kila mmoja alihitaji kuwa naye kimapenzi lakini kutokana na misimamo aliyojiwekea msichana huyo lilikuwa ni jambo gumu mno kutokea.

Hakukuwa kuna kijana aliyetaka kukata tamaa mapema, kila mmoja alitaka kuonyesha urijali wake. Waliyomfuata ana kwa ana walimfuata na wengine waliyoamua kutafuta namba yake ya simu walitafuta na kuanza kuwasiliana naye lakini kila njia ambayo waliitumia vijana hao kama kumuingilia msichana huyo ilishindikana.

“Duh! Sijawahi kuona demu mgumu kama huyu, yaani utadhani chuma cha pua,” alisema jamaa mmoja ambaye alijaribu kumtongoza Suzani kwa njia ya simu lakini ikashindikana.

“Ila demu ni mzuri sana,” alisema jamaa mwingine ambaye na yeye alihitaji kuwa naye ikashindikana.

Hicho kilikuwa ni kipindi kigumu kwa vijana hao wa mtaani, kila aliyekuwa na ndoto ya kutembea na Suzani iliendelea kubaki kuwa ni ndoto tu! isiyotimia.
Sifa za Suzani hazikuishia tu kwenye uzuri wake bali hata tabia yake.

Kitendo cha kutoonekana akiwa amesimama au kutembea na mwanaume yoyote katika mtaa huo kiliwafanya wazazi wengi kumsifia Mama yake na hata kumwagia sifa Baba yake kutokana na malezi bora ambayo alikuwa amempa mwanaye.

Kipindi hicho kilikuwa ni cha Mzee Mushi kujisifia, kila alipokuwa akienda na kukutana na wazee wenzake hakuacha kuwaambia kuhusu mwanaye huyo.

Sifa zake zilisambaa kila kona na kila mtu hakuacha kumsifia na kutamani hata kijana wake kuoa katika familia ya Mzee huyo.

*Je, nini kitaendelea?*
*Tukutane kesho mahali hapahapa.*
 
Siku yngu imekwenda powa sana leo kwa hiki chuma kikali
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…