Changamoto kwa wasomi wa afrika katika uchambuzi, upembuzi na kufikiri kuhusu mustaka

Yona F. Maro

R I P
Nov 2, 2006
4,202
218
MPENDWA MWANAHABARI,

Nimekuwa nikisoma kwa makini mada pamoja makala mbalimbali ambazo nimekuwa nikizipata kupitia baruapepe za Mwanahabari, hususan zile zinazohusu nchi yetu na mustakabali wa Taifa letu. Kwenye miaka ya 70, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kiliwahi kufungwa baada ya Wanafunzi kufanya maandamano ambayo yalitawanywa na Vikosi vya FFU katika maeneo ya Manzese. Baada ya Chuo kufunguliwa tena na Wanafunzi kurejea masomoni, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Chancellor wa UDSM wakati ule, alikwenda Chuoni kuongea na jamii nzima ya Chuo kwa maana ya Maprofesa, Wahadhiri na Wanafunzi. Katika mazungumzo hayo, Hayati Baba wa Taifa aliwaambia Wanafunzi kwamba ikiwa atatokea mtu akawauliza "/What is the future of Tanzania/?", basi Mwalimu Nyerere aliwaasa vijana hao kila mmoja wao awe tayari kuwajibu hivi watu hao (yumkini kwa jeuri ya kujiamini kama Mwafrika Mtanzania) :"/I am the future of Tanzania"/. Kwa hiyo, ni vema na haki siku zote kwa vijana wetu kushughulishwa na kutaka kufahamu kwa karibu, pamoja na kushiriki katika kufanya yale ambayo yanaelekeza na kutengeneza mustakabali wa Taifa letu, kwa sababu wao *Vijana ndiyo Taifa la leo na Viongozi wa kesho. *

Katika kipindi cha zaidi kidogo ya miaka mitatu hadi sasa, nimepata bahati ya kuishi katika mazingira ya utulivu ambao umenipa fursa ya kufikiri na kutafakari mambo mengi yanayohusu yale ambayo kizazi changu kimeyaona na kushiriki katika nchi yetu kwa takriban miongo mitano hivi, sambamba na yale yanayonihusu mimi binafsi. Lakini, yale ambayo ni yangu binafsi tuyaache pembeni, tuzungumzie ya nchi na Taifa letu. Ukisoma mada au makala mbalimbali wanazoandika vijana au ukiongea nao, ujumbe wa wazi unaoupata ni kwamba, vijana wanataka mabadiliko ambayo yataleta hali nzuri ya maisha. Baadhi ya vijana hao, wamefikia hatua ya kuambizana kwamba ni lazima waendeshe harakati za kuleta mabadiliko, hata kama inabidi kutumia nguvu. Kwa sisi "Vijana wa Zamani" hayo si mawazo mapya au ya kushangaza. Hata "Enzi za Mwalimu" wapo vijana wenzetu wa wakati ule waliotaka kuiondoa kwa nguvu madarakani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na walipanga hata kumtoa roho Baba wa Taifa kama sehemu ya mkakati wa kuleta mafanikio kwa mujibu wa mawazo yao. Leo tunamshukuru Mungu kwamba Vijana wenye uzalendo waliopewa jukumu la kulinda usalama na amani ya nchi yetu walikuwa macho na imara, hivyo hizo njama za kuleta vurugu zilizimwa, tukaweza kuinusuru nchi yetu na tukadumisha amani. Nchi karibu zote za Africa ambazo zilipata uhuru wa kujitawala bila kutumia mtutu wa bunduki, zimewahi kukumbwa na balaa ya Serikali kuondolewa madarakani kwa nguvu za kijeshi. Aghalabu, mabadiliko hayo ya serikali yamekuwa yakifanyika mara kadhaa kwa madai kwamba Serikali iliyokuwa madarakani, ilkuwa imeshindwa kutekeleza wajibu wake na hivyo ilibidi iondolewe kwa nguvu kunusuru taifa. Mashtaka ya kawaida na shutuma zilizoelekezwa kwa Viongozi walioondolewa madarakani zilikuwa zinafanana : rushwa, udini, ukabila, kujilimbikizia mali, kutowajali wananchi na mengine yanayoshabihiana na hayo. Lakini, aghalabu walioingia madarakani baada ya kuiangusha serikali dhalimu iliyojaa rushwa, viongozi wapya walishindwa kutekeleza ahadi na badala yake wakageuka "mafisadi" kama wale wlioangushwa. Hiyo ndiyo ilikuwa "/vicious cycle/" ya kuondoana madarakani iliyowasibu Waafrika wenzetu wengi wakiwemo wale wa nchi za Ghana, Nigeria na Sudan. Sifa kubwa ya Bara la Africa Ulimwenguni ikawa ni jinsi gani tunavyogombea madaraka kwa nguvu, badala ya kutumia njia ya kistaarabu ya demokrasia kama "wenzetu wegine".

Sina nia ya kuelezea mengi kuhusu tuliyojifunza katika kipindi kile kigumu sana cha miaka ya 60 na 70, baada ya nchi nyingi za Africa kupewa uhuru wa kujitawala. Katika kipindi hicho, nchi zilikuta seikali zao zikiondolewa madarakani kwa mtutu wa bunduki za Majeshi ya Nchi zao.Lakini uzoefu ulionesha kwamba aghalabu kila "Wakombozi Wapya" walipoingia madarakani kwa kutumia nguvu za Kijeshi na kutawala, baada ya muda mfupi Wananchi walijikuta hali zao bado ni mbaya, kama si mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa awali kabla ya serikali kupinduliwa na Jeshi. Aidha, Watawala hao wapya walijikuta wakilaumiwa kwa kutenda dhambi zilezile za wale waliowatangulia na ikawa ndiyo hoja na sababu ya kuondolewa madakani kwa nguvu ili kulinusuru taifa (natoa angalizo pia kwamba nimewaita "Watawala" siyo "Viongozi" kwa makusudi kabisa). Ukweli ni kwamba, wale ambao walikuwa wanataka kuleta mabadiliko, walikuwa hawaelewi kwamba wao walikuwa wanalaumu na kuelekeza hasira au chuki zao kwa "Watu Binafsi" (/individuals/) waliokuwa madarakani ambao nao walikuwa ni Wanyapara au Wasimamizi tu wa mfumo dhalimu wa uchumi duniani ambao ulikuwa haulengi kuwastawisha Waafrika kwa kuwapatia stahili ya gawio la thamani halisi ya rasilimali ambayo huvunwa kwetu na kwenda kustawisha wengine. Kwa hiyo, mabadiliko yalikuwa ni ya kushughulikia watu kana kwamba wao ndiyo tatizo, badala ya kushughulikia mfumo ambao ndiyo tatizo la msingi. Hayati *Patrice Emery Lumumba *alielewa kwamba rasilimali kubwa ya madini ya Congo ilikuwa haiwasaidii Wananchi wa Congo, bali waliojijengea ustawi mkubwa kwa kutumia rasilimali hiyo walikuwa ni Wabelgiji na wengineo. Katika hotuba yake ya kwanza siku ya Congo kusheherekea uhuru wa kujitawala (01 June 1960), Hayati Lumumba alitamka kwamba chini ya uongozi wake angeleta mabadiliko ya hali hiyo ili rasilimali ya Congo iwanufaishe Wakongomani. Inafahamika wazi na ushahidi wa maandishi upo, kwamba kauli hiyo ndiyo ilkuwa hukumu ya kuondolewa madarakani kwa nguvu na hatimaye kuuawa chini ya mpango na mkakati wa USA, Belgium na uliotekelezwa kwa kushirikiana na Maafisa Waandamizi wa UN. Tangu mwaka 1961 alipouawa Lumumba, Wakongomani wameendelea "kushughulikiana", mara* Moise Tschombe,* halafu *Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga* ( a.k.a. /Joseph Desire Mobutu/), kafuata *Laurent Desire Kabila *na bado Wakongomani hawaoni mustakabali wenye kuleta matumaini ya hatma ya Taifa lao. Watu wanaonekana ndiyo tatizo, lakini yumkini hakuna wengi ambao wanao uwezo wa kufikiri na kufanya uchambuzi wa mambo kwa kina, ili kubaini tatizo la msingi linalopaswa kushughulukiwa.

Somo la awali ninalotaka tujifunze kutokana na ushahidi wa uzoefu ("/empirical evidence"/) wa Bara la Africa baada nchi zetu kupata uhuru wa kujitawala, ni kwamba, kubadili Uongozi wa Nchi au Chama Tawala cha Siasa siyo dawa ya matatizo ya nchi yoyote ile, ikiwa wanaofuatia katika kushika madaraka hawana programmu ya maendeleo na ustawi wa jamii inayotokana na upembuzi, pamoja na uelewa wa kina wa kiini cha matatizo. Kwa mfano, ikiwa watu wanafanya vurugu na kulazimisha Serikali kuondoka madarakani kwa namna moja au nyingine kwa sababu kuna uhaba wa chakula, tukio au tendo pekee la kuingia madarakani Watawala wapya "/haliwezi kuongeza/ /sufuria za ugali"/. Enzi hizo za miaka ya 60 na 70, Tanzania na Afrika kwa ujumla ilikuwa na Wasomi wachache sana, ukilinganisha na Afrika ya leo iliyojaa wasomi ambao wanatarajiwa na kutegemewa wawe pia na uwezo mzuri wa kufikiri kwa kiwango cha kuweza kuchangia katika kubaini, kupanga na hatimaye kupata mbinu za kuharakisha upatikanaji wa ustawi na maendeleo ya jamii.

Wengi tunahusisha usomi na uwezo wa kufikiri. Hivyo ndivyo inavyotakiwa iwe, lakini nimepata somo hivi karibuni ambalo limenihakikishia kwamba mtu anaweza kuwa amesoma sana lakini bila kuelimika na kujijengea uwezo wa kufikiri, isipokuwa akawa mahiri katika kukariri.
Mada hii inahusu Wasomi wa Bara la Afrika, ambao wao ndiyo wenye jukumu la kuongoza kwa fikra zitakazoelekeza njia sahihi ya mapinduzi ya kumkomboa Mwafrika kutoka utumwa wa ujinga, umaskini na maradhi. Nchi ya Nigeria iliwahi kuwa na mwanaharakati, mwanasiasa,mwanasheria na kiongozi msomi, aliyejulikana kwa jina rasmi la /*Chief Jeremiah Obafemi Awolowo*/ ( 1909-1987 ),lakini alijulikana maarufu pia kama " /*Awo*/", hasa kwa washabiki wake. Katika miaka ya 70 mwishoni au 80 mwanzoni, niliwahi kusoma makala ya masailiano katika jarida lilokuwa likihaririwa na Mwandishi/Mwanahabari maarufu, mwananchi wa Nigeria anayeitwa /*Peter Enahoro*/. Katika masailiano hayo, Enahoro alimuuliza Chief Awolowo alikuwa anasemaje kuhusu wale ambao walikuwa wamesema kwamba, yeye Chief Awolowo ndiye Rais bora wa Nigeria kuliko wote, ambaye hakuwahi kupata nafasi ya kuingia Ikulu kama Rais. Wakati huo, Chief Awolowo alikuwa ameshindwa na */Alhaji Aliyu Shehu Shagari/* katika uchaguzi wa Rais wa Nigeria mwaka 1979. Inaarifiwa kwamba aliyetoa sifa hizo za uongozi kwa Chief Awolowo, alikuwa ni */Chukwuemeka Odumegwu Ojuku, /*aliyekaririwa kama ifuatavyo "/ Chief Awolowo is the best President/ /Nigeria never had/." Aliyewahi kuwa Rais wa Nigeria /*Ibrahim Badamasi Babangida*/ ("IBB"), naye aliwahi kusema "/Awo is the main (political) issue (in Nigeria ).You are either for or against him."/ Chief Awolowo alimjibu Enahoro katika mahojiano hayo kama ifuatavyo : " /When you are ahead of others and show the way with ideas while they follow you, then there is no issue of you becoming their leader because you are (already) the leader." /Kwa kauli hiyo, Mzee Awo alikuwa anatofautisha kati ya uongozi katika jamii, uongozi ambao yeye anaamini unatokana na uwezo wa kufikiri, na nafasi za utawala ambazo jamii hunuia kuwapa watu ambao ni viongozi wenye hekima, pamoja na uwezo wa kufikiri. Kwa mantiki hiyo basi, Wasomi katika jamii wanalo jukumu la kuongoza kama alivyoeleza Mzee Awo kwa kutarajia kwamba, Wasomi hao wameelimika. Lakini, kigezo pekee cha usomi wa kweli kwa maana halisi ya kuelimika, ni uwezo wa kuchambua, kupembua, na kufikiri. Uwezo huo huendana na ubunifu katika kukabili changamoto mbalimbali, na wala siyo kuishia kukariri au kuiga bila kuelewa misingi na undani wa yale unayoyaiga. Niseme kwamba, kwa mtazamo wangu uwezo wa kufikiri, unabainika katika yule ambaye anajitambua nafasi yake katika jamii, sambamba na kuyafahamu vizuri mazingira yake. Kisha hutumia elimu yake kukabili changamoto za maisha na ustawi wa jamii. Mada hii inahusu changamoto kwa Wasomi ili wajenge uwezo na tabia ya kutumia vipaji vyao vya akili katika kuchambua, kupembua na kufiri kwa kina ili kuongoza jamii yetu, hususan Watanzania na Waafrika wengine, waweze kukabili changamoto mbalimbali zinazotukabili za kisiasa, kiuchumi, ustawi wa jamii, na kutunza mazingira.

Hivi sasa yapata miaka 3, tangu nilipoanza kupokea baruapepe kutoka kwako Mwanahabari, kupitia mtandao. Nimekuwa nikizisoma baruapepe hizo kwa makini na kutafakari yalioandikwa. Ninafahamu barua au makala nilizoletewa zimeandikwa na watu tofauti, lakini nimebaini kwamba maoni yanayotolewa katika midahalo au mada kupitia mtandao yanahusu zaidi watu na matukio,kama vile Mafisadi wa EPA, Uchaguzi Mdogo wa Tarime, Mkutano wa NEC ya CCM Butiama, Uchaguzi Mkuu wa Kenya, Uchaguzi wa Rais wa Marekani. Yote hayo ni matukio na habari muhimu kwetu, kwa sababu yanatuathiri kwa namna moja au nyingine. Huenda, tatizo liko kwangu kwa sababu huu ni mtandao wa Mwanahabari. Sasa ningetegemea kipaumbele kiwe ni nini zaidi ya habari, pamoja na mazungumzo baada ya habari. Lakini, ninashawishika kuamini usahihi wa matarajio yangu kwamba, "*Mwanahabari*" ni jukwaa la Wasomi. Upo usemi kwamba watu wenye akili na mawazo finyu hadi wastani, wao hujadili zaidi watu na matukio. Watu huonekana kwa urahisi na mtu yoyote, pamoja na matukio yanayowahusu, kwa hiyo haihitaji fikra kuweza kuwajadili watu au matukio. Lakini hoja na maswala ya msingi katika jamii, pamoja na mawazo (/ideas)/ hushughulisha wenye akili ya kina, pana na pevu kwa sababu yanahitaji umakini, sambamba na uwezo wa kufikiri.

Muda si mrefu sana uliopita niliporejea kutoka ziara ya siku mbili vijijini, nilikuta makala katika baruapepe ya mtandao wa Mwanahabari, yenye kichwa cha habari "*CCM KUMEGUKA NI MUHIMU KWA TAIFA*". Niliisoma kwa shauku kubwa (/with great interest/) makala hiyo kwa sababu haikuwa makala ya kujadili watu na matukio, bali juu ya Chama kinachoongoza nchi yetu. Kwa hiyo, kwa kukusudia na kupanga au hata kama wapo watakaosema ni kwa kudra, ukweli na hali halisi ni kwamba CCM ndiyo mwamuzi na mwelekezi wa sasa wa mustakabali na hatma ya Taifa la Tanzania, kwa ridhaa ya wananchi kupitia uchaguzi mkuu. Kwa hiyo nilitaka kujifunza uchambuzi, upembuzi na kina cha fikra za mwandishi kuhusu swala hilo. Hoja ya msingi na maoni ya mwandishi ni kwamba, hata baada ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi, bado hakijaweza kupatikana Chama cha kisiasa ambacho kinaweza kuiongoza nchi vizuri, lakini yeye anaona kwamba ipo haja ya kuwa na Chama kingine cha kisiasa kitachoweza kuwa mbadala makini wa CCM (/serious alternative to CCM)/. Anamkariri Baba wa Taifa Hayati /*Mwalimu Julius Kambarage Nyerere */aliyesema kwamba, upinzani wa kweli wa Chama cha kisiasa utatoka ndani ya CCM. Kwa kuongezea, huyohuyo Baba wa Taifa aliwahi kusema kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kwamba, Rais (wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ) anaweza kutoka Chama chochote, lakini Rais bora atatoka ndani ya CCM. Tukijumlisha yote mawili yaliyotangulia katika kukubaliana na fikra za Baba wa Taifa, kwanza ni dhahiri kwamba CCM yenyewe ni "/Multiparty/" kwa maana ya kuwa ni "/microcosm/" ya mchanganyiko wa Watanzania katika makabila, dini, mrengo wa itikadi za kisiasa, rangi ya ngozi, jinsia, rika, elimu, uwezo wa kiuchumi na kutoka katika kila Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata na Kijiji Tanzania Bara. Sina hakika hali ni hiyohiyo Zanzibar, kwamba tukifika Pemba CCM ipo kila kijiji . Pili, Mwandishi wa Mada anakubaliana na Baba wa Taifa kwamba, Viongozi wa Kisiasa wenye uwezo wa kuongoza Nchi yetu vizuri wanapatikana ndani ya CCM, vinginevyo haina maana yoyote kuzungumzia umuhimu wa CCM kumeguka kwa maslahi ya Taifa, kama hicho Chama kipya ambacho angependa kianzishwe hakitakuwa na uongozi bora. Hebu, basi na tupime kwanza uzito na kina cha fikra ya hiyo hoja ya CCM kumeguka kwa maslahi ya Taifa. Ninapenda kuitumia hoja hii kama kielelezo cha mfano wa umuhimu wa uchambuzi na uzamivu wa fikra ambao unahitajika katika kupata majibu na ufumbuzi wa maswala magumu. Ninayoandika siyo majibu ya hoja na wala hoja siyo yangu, bali ninakusudia kuinyambua hoja kuonesha kiwango na mapana yake ambayo yanahitaji fikra zenye kina kuelewa matatizo na ufumbuzi wake.

Hoja ya mtoa mada tunayoijadili imejichukulia dhana kwamba (/ is based on the assumption that /) CCM ikimeguka (kwa utabiri na dua zake mtoa mada pamoja na wengine wenye mtazamo kama huo), basi mambo yatakuwa mazuri kwa sababu kumeguka huko kwa CCM hakutatokea kwa misingi ya ukabila, udini, ukanda, elimu, tabaka za kiuchumi au kwa namna nyingine yoyote ya kudhoofisha na kupelekea kuvunja utaifa,umoja na muungano wetu. Aidha, hoja hiyo inataka ikubalike kwamba, kumeguka huko kunakozungumziwa, kutawachukua viongozi bora nje ya CCM. Kama hoja kuu ya mada msingi wake, kwa maana ya dhana iliyoelezwa hapo juu ni imara, basi itakubalika kwamba kumeguka kwa CCM ni muhimu kwa mustakabali na hatma ya Taifa letu, kwa sababu kumeguka huko kutazaa Chama kipya ambacho kitakuwa ni mbadala makini wa CCM kwa sababu kitakachokuwa na viongozi bora. Ikiwa CCM itameguka, upo uwezekano tukio hilo likawa ni la kujisafisha ("purge"). Yaani, wale viongozi na wanachama wasiofaa wakaondolewa. Kwa hiyo unabaki na Chama "kipya" kwa maana upya wa usafi. Ninakumbuka kwamba wakati Tume ya Nyalali lipowahoji Watanzania kuhusu swala la kuanzisha mfumo wa vyama vingi, wapo wengi zaidi ya waliopendelea mfumo wa vyama vingi, ambao walitaka kuendelea na Chama kimoja lakini "CCM ijisafishe". Kumeguka kwa CCM kunaweza vilevile kukawa ni tukio la "Wasafi" kujitoa na kuanzisha Chama kipya ambacho kitakuwa ni chama makini mbadala wa CCM.. Sifahamu mtoa mada anaona "scenario" ipi yumkini inao uwezekano mkubwa zaidi wa kutokea.Sina nia wala muda wa kuzamia zaidi hoja katika kutabiri nini kitakachotokea. Inatosha kutambua tu kwamba, hoja ya msingi iliyotolewa katika mada tunayoijadili ni kwamba, Tanzania inahitaji Chama makini ambacho kitatokana na CCM kumeguka.Kinyume cha usahihi wa dhana hiyo, basi kumeguka kwa CCM ndiyo kutakuwa mwanzo wa kumeguka Taifa letu kwa misingi ya ukabila, udini, ukanda au kwa kufuata nyufa nyingine zitakazo vunja misingi ya umoja, muungano na utaifa wetu.

Labda ni vema tukakumbushana pia kwamba Baba wa Taifa alitamka, " *Bila CCM imara, Nchi yetu itayumba*." Ukiitafsiri kauli hiyo ya Baba wa Taifa kwa dhana ya CCM kumeguka, ni dhahiri utakuwa unachukulia kwamba CCM itajisafisha na hivyo kubaki Chama imara chenye uwezo wa kuongoza nchi vizuri kwa maslahi ya Taifa, kama inavyotakiwaka. Kama nilivyoeleza awali sina nia ya kuendelea kujadili hoja hii kutafuta majibu kwa sababu bado inahitaji uzamivu zaidi, isipokuwa ninatumaini nimeweza kuonesha kwamba Wasomi wanao wajibu wa kuumiza vichwa vyao kufanya kazi ngumu ya kufikiri na siyo kutafuta majibu rahisi ya maswala makubwa na magumu, hususan yale yanayohusu mustakabali wa Taifa letu. Angalizo ninalotaka kutoa mintarafu hoja iliyotolewa ikidai kumeguka CCM kukitokea itakuwa ni kwa maslahi ya Taifa, ni kwamba hoja imetolewa pasipo kuonekana ushahidi wa uchambuzi, upembuzi na fikra pevu zenye kina. Kwa bahati mbaya, si aghalabu nimekuwa nikiona makala au mada zenye hoja zilizojengwa kwa fikra za kina katika kujadili, hasa mambo yale ambayo ni ya msingi kuhusu mustakabali na hatma ya Nchi yetu, iwe ni maswala ya kisiasa, kiuchumi au ya kijamii. Upo usemi wa Kifalsafa ambao unajieleza kwamba " /Thinking is the hardest there is, and that is why there are very few persons engaged in it/."Inaelekea tatizo hili la kutopenda kuumiza vichwa kwa kufikiri ni la Afrika nzima, kwa sababu miaka takriban 50 tangu nchi zilipoanza kujitawala, bado Waafrika ni tegemezi katika kubuni sera, mipango na mikakati endelevu itakayoongoza maendeleo ya uchumi, pamoja na juhudi za kujijengea jamii inayoishi maisha bora. Tunategemea /*World Bank*/, */IMF/*, na "*/Develpoment Partners/*" wengine watuelekeze la kufanya, na tunaona fahari sana iwapo sera au mipango yetu inakidhi masharti na kuwaridhisha wakubwa hao, hata kama utekelezaji wa sera na mipango hiyo hauleti ustawi au nafuu kwa Wanachi walio wengi. Ni ajabu na kweli kwamba, tabia hii ya uvivu wa Wasomi wa Kiafrika kutopenda kufanya kazi ngumu ya kufikiri, ilitabiriwa na Mwafrika mwezetu katika miaka ya mwanzo ya 60. Inasikitisha kwamba, utabiri huo umetimia katika kizazi kimoja na kuna changamoto kubwa sana ya kusahihisha hali hii mbaya. Hata hivyo ni jambo, linalowezekana kwa Wasomi wa Kaafrika kubadilika kwa kutumia fikra za Wasomi Waafrika waliotutangulia ambao walikuwa wanaharakati na wanamapinduzi, kama kurunzi ya kuonesha njia ya kututoa gizani na msingi wa kuendeleza mapambano ya kujipatia uhuru wa kweli, uhuru kamili. Mtu ambaye amekamatwa na kuzuiliwa kwa nguvu, hawezi kukubaliana na hali hiyo inayomnyima uhuru. Kwa hiyo, hulazimika mtu huyo achungwe na pengine afungwe pingu za aina mojawapo ili asitoroke. Lakini, ikiwa mtu ametekwa katika mawazo yake kufikia kuikubali hali yake ya utumwa, basi huwa hakuna haja tena ya kumfunga au kumchunga kwa sababu hawezi tena kutoroka. Ni dhahiri ipo tofauti ya msingi ya kuwa *"mfungwa"* (kama babu zetu waliofungwa minyororo wakapelekwa kwa karaha kwenda kuishi na kufanya kazi ughaibuni) na kuwa *"mtumwa"*(anayejipeleka mwenyewe kwa "kuzamia" kwenda kuwa kibarua ughaibuni au anabaki nchini lakini mawazo hana ya kwake sipokuwa ya kuiga Wageni). *Kwa hiyo ni dhahiri kwamba uhuru kamili na wa kweli, ni lazima uwe ule wa fikra kwanza. *Lakini kila mtu anayo haki ya uhuru wa kujenga fikra zake anazo zitaka. Kwa hiyo ni lazima kujiuliza ni fikra zipi tunazozungumzia zinaendana na uhuru wa kweli ? Hebu tutafakari fikra za mmoja kati ya baadhi ya Wasomi Wanaharakati wa Afrika.

/*Frantz Fanon*/ ni Mwanaharakati na Mwanamapinduzi Mwafrika,aliyeshiriki katika mapambano ya kupigania uhuru wa Algeria kwa mtutu wa bunduki. Kabla ya kufariki kwake kwa ugonjwa wa leukemia akiwa na umri mdogo wa miaka takriban 36, Fanon aliandika kitabu kinachoitwa kwa lugha ya Kifaransa, " */Les Damnes de la Terre/*". Kitabu hicho kilitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kuitwa " /*The Wretched of the Earth*/ ". Maandiko ya kitabu cha Fanon kwa lugha ya Kiingereza, ndiyo yanayotumiwa katika kujenga hoja katika mada hii. Kitabu hicho kiliandikwa katika miaka ya mwanzo ya 60, wakati ambao nchi nyingi za Bara la Afrika zilikuwa zimeanza kupata uhuru au zinaelekea kupata uhuru, na wakati huohuo, baadhi ya nchi kama vile Angola, Mozambique na South Africa wakijiandaa kuanza harakati za vita vya ukombozi kwa mtutu wa bunduki. Kwa hiyo, Kijana Msomi Fanon hakuwa na mifano au uzoefu wa kumwezesha kufanya utafiti, ili aweze kutoa maonyo na tahadhari kuhusu mustakabali na hatma ya nchi za Kiafrika baada ya kupata madaraka ya kujitawala. Hata hivyo ni ajabu na kweli kwamba, Sura ya 3 ya kitabu tajwa hapo juu yenye kichwa cha habari " */The Pitfalls of/* /*National Consciousness*/ " inatabiri kwa usahihi mkubwa, yale makosa ambayo Viongozi na Wasomi wa Afrika watafanya baada ya kujipatia mamlaka ya kujitawala, pamoja na matokeo yake. Ukiyasoma maandiko ya Fanon katika hiyo sura ya 3 inayotajwa, utaelewa nini kimesibu Bara la Afrika tangu Wakoloni walipotuachia madaraka ya kuendesha Serikali zetu hadi leo. Kwa mfano maneno yafuatayo yaliyoandikwa na Fanon kabla ya Tanganyika kujitawala mwaka 1961, yalibashiri kwa usahihi unaoweza kushangaza, ukweli wa hali ya nchi nyingi za Afrika, baada ya zoezi la" kurekebisha uchumi " (/Structural Adjustment Program/ ) tulilolazimishwa kutekeleza na "*Wafadhili*",ili kuvunja misingi iliyoanzishwa na kizazi cha Wanamapinduzi Waasisi wa Nchi yetu, hususan sera za kujenga uchumi wa Taifa usio tegemezi, na unaomilikiwa na Wananchi wenyewe kama ilivyokusudiwa katika Azimio la Arusha. Fanon aliandika kwamba yafuatayo yangezisibu nchi zetu baada ya kujipatia mamlaka ya kujitawala na kujaribu kujenga uchumi wa Taifa huru :

" .../The economic channels of the young state sink back inevitably into neo-colonialist lines. The national economy, formerly protected, is today literally controlled. The budget is balanced through loans and gifts, while every three or four months the chief ministers themselves or else their governmental delegations come to the erstwhile mother countries or elsewhere, fishing for capital. The former colonial power increases its demands, accumulates concessions and guarantees and takes fewer and fewer pains to mask the hold it has over the national government/...."

Hayo ni maneno yanayoelezea fikra pevu za Fanon zilizozotokana na upembuzi wake wa udhaifu wa Nchi zilizokuwa zinaaanza safari ndefu ya kujenga Taifa huru ,sambamba na ujenzi wa uchumi, baada ya Wakoloni kukabidhi mamlaka ya utawala. Kwa mujibu wa uchambuzi wa Fanon kupitia kitabu tajwa hapo juu, yafuatayo ni maelezo ya chanzo, sababu na udhaifu wa ndani ( /systemic weakness/ ) ambao unajenga mazingira ya mambo kuharibika katika Nchi ambazo zimetoka katika utawala wa Wakoloni, kama inavyonukuliwa hapa chini kutoka mwanzo wa Sura hiyo ya 3.:

"/ History teaches us clearly that the battle against colonialism does not run straight away along the lines of nationalism....This fight for democracy against the oppression of mankind will slowly leave the confusion of neo-liberal universalism to emerge, sometimes laboriously as as a claim to nationhood.....National consciousness, instead of being the all-embracing crystallization of the innermost hopes of the whole people, instead of being the immediate and most obvious result of the mobilization of the people, will be in any case only an empty shell, a crude and fragile travesty of what it might have been.....We shall see that such retrograde steps with all the weakness and serious dangers that they entail are the historical result of the incapacity of the national middle class to rationalize popular action, that is to say their incapacity to see into the reasons for that action. /*/This traditional weakness, which is almost congenital to the national consciousness of under-developed countries, is not solely the result of the mutilation of the colonized people by the colonial regime. It is //also the result of the intellectual laziness of the national middle class, of its spiritual penury, and of the profoundly cosmopolitan mould that its mind is set in." /*( emphasis has been supplied by me ).

Hapo juu, Fanon amezungumzia swala la uvivu wa kufikiri unaotawala katika Wasomi wengi wa Nchi zetu zilizo nyuma katika maendeleo, na kulaumu kuwepo kwa "*cosmopolitan mould of mindset ."* Kwa msamiati wa leo, maneno yanayotumika kwa mantiki hiyohiyo, lakini yanatamkwa kwa fahari na kukubali kusalimu amri kwamba hakuna uwezekano wa kuwa na fikra mbadala, ni "*globalization*" na "*best practise*". Hoja ni kwamba, tunaishi katika dunia ya utandawazi na wapo waliotutangulia katika maendeleo, na kwa hiyo wao tayari wanayo majibu ya yanayotosheleza changamoto mbalimbali zinazotukabili. Kwa hiyo hatuna haja ya kufikri sana ili tuweze kutatua matatizo ya Nchi yetu. Inatosha kuangalia wengine waliofaulu na kuiga kutoka kwao hiyo "/best practice/". Hapo wanataka tukubali (/na kwa bahati mbaya tunakubali kabisa/) kwamba, ipo sehemu ya jamii ya Wanadamu ambao wamekwishapata uzoefu, maarifa na ujuzi wote wa kuendesha nchi, na kushughulikia maswala ya kiuchumi na ya kijamii. Kazi iliyobaki kwa sisi Binadamu wengine, ni kukariri na kuiga kutoka kwao, hiyo "/ best practice/ ". Kitendo cha kukataa kwamba jamii fulani haina mchango wowote wa maana katika fikra, mipango na mikakati ya kumkomboa Mwanadamu na kuendeleza maslahi yake, ni sawasawa na kuukataa ubinadamu wa jamii hiyo. Inaelekea sisi Waafrika tnaikubali sana hali hiyo ambayo ndiyo msingi wa kuendelea kuwa nchi masikini licha ya kuwa matajiri wenye rasilimali asili nyingi sana bila mfano ulimwenguni. Afrika na Asia tulipata uhuru wa kujitawala karibu wakati mmoja, lakini wenzetu Asia hawakukubali utegemezi wa kufikiri. Mwaka 1997, nchi kadhaa za Asia ikiwemo Malaysia, zilikumbwa na msukosuko mkubwa wa kiuchumi kufuatia kuvurugika kwa mabenki yao, kuanguka thamani ya sarafu za nchi hizo kwa kulinganisha na Dola za Kimarekani, pamoja na kuanguka kwa Masoko ya Mitaji. Kama ilivyo ada IMF walifika katika nchi hizo za Asia kwa nia ya kutoa msaada wa fedha kwa nchi hizo, ili ziweze kujenga upya uchumi wake. Ahadi hiyo ya msaada ilitaka kila nchi husika ikubali kuingia mkataba maalum wa kurekebisha uchumi kulingana na maelekezo ya IMF, ikiwa ni mfumo na utaratibu unaoshabihiana na " /Structural Adjustment Program /" ("SAP") iliyotekelezwa na nchi nyingi za Afrika . Malaysia ni nchi pekee ya Asia kati ya zote zilizopata msukosuko wa kiuchumi, waliokataa msaada ambao ulikuwa na masharti ya kutekeleza sera za kiuchumi ambazo IMF wanageelekeza. Baada ya kukataa kufuata hiyo " /best practice/ " ya IMF, Serikali ya Malaysia waliwatumia Wataalamu wao wa uchumi kuandaa mpango wa kufufua uchumi, ambao ulitekelezwa baada ya kujadiliwa na kufikia makubaliano yaliyohusisha wadau wakuu wa uchumi, yaani Serikali ya Malaysia, Vyama vya Wafanyakazi na Wafanyabiashara. Ilipofika mwaka 1999, uchumi wa Malaysia ulikuwa umetengemaa. Kabla ya kufikiwa na msukosuko wa kiuchumi mwaka 1997, akiba ya fedha ya Malaysia ilikuwa Dola 20 billioni. Baada ya kutekeleza mpango wa uchumi walioubuni Wataalamu wa Malaysia, akiba ya fedha mwaka 1999 ilifikia Dola 40 billioni. Baadaye, IMF walikiri kwamba uchumi wa Malaysia ( /nchi/ /ambayo waliukataa mpango na sera za kufufua uchumi za IMF)/ ulikuwa umetengemaa, wakati nchi nyingine za Asia kama vile Korea ya Kusini, Taiwan,Indonesia na Thailand, zilizokubali kufuata sera za kufufua uchumi na masharti ya IMF zimechukua muda mrefu zaidi kwa uchumi wake kurudia hali ya awali kabla ya msukosuko wa 1997, na hatimaye kuimarika.


Uchumi wa Malaysia ulitengemaa na kuimarika baada ya muda mfupi, kwa sababu Wataalamu Wasomi wa Nchi hiyo waliipokea changamoto ya kufanya kazi ngumu ya kufikiri. Wasomi wa Malaysia hawakuwa na "/cosmopolitan mould of mindset/" inayopokea kila mawazo yaliyofungashwa ndani ya vifurushi vyenye nembo ya "/globalization/ " na kufungwa kwa lakiri yenye muhuri wa "/best practice/". Je, sisi Wasomi wa Afrika tunajifunza nini kutoka Malaysia ? Baada ya kuanguka kwa Serikali ya Muungano wa Jamhuri za Kisovieti ( "*USSR*") pamoja na tawala za nchi za Ulaya Mashariki zilizofuata itikadi ya Kikomunisti, Nchi za Marekani (USA), Uingereza na wenzao wengine wanachama wa NATO na OECD, walitangaza ushindi wa itikadi ya uchumi wa soko dhidi ya mahasimu wao waliofuata itikadi ya Usoshalisti wa Kisayansi unao ongozwa na fikra za Marxism-Leninism. Hali kukawa hakuna mjadala tena kwamba, Afrika ni lazima ikubali " /globalization/ " na kutekeleza masharti ya World Bank na IMF ambayo ni " /best practice/ ", ili nchi husika ziweze kupewa misaada na mikopo ya fedha chini ya mpango wa SAP. Ukweli ni kwamba, nchi nyingi za Afrika zilizokuwa na matatizo ya kiuchumi na hazikuwa na mikakati au mipango yao wenyewe ya kuweza kujikwamua. Kwa sababu hiyo, njia pekee iliyo onekana ni mwafaka ilikuwa ni kukubali kutekeleza SAP. Inafahamika katika taaluma ya uchumi kwamba inapotokea kwamba masoko ya uchumi yamevurugika au kukumbwa na migogoro mikubwa inayohatarisha hali ya uchumi wa Taifa, Serikali inawajibika kuingilia kati ( *to intervene* ) na kujihusisha moja kwa moja na swala la kuendesha uchumi. Serikali za USA, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Mataifa mengine yenye uchumi mkubwa duniani, hivi karibuni zimeingilia kati na kuchukua hatua zitakazozifanya Serikali hizo kuhusika moja kwa moja na uendeshaji uchumi. Zoezi hilo linaendelea sasa na itachukua muda kabla Serikali zitaweza kujiondoa na kuachia sekta binafsi iendeshe tena uchumi, bila nchi zao kuathirika vibaya. Yumkini, hiyo ndiyo "/best practice/" ili kuweza kunusuru uchumi wa nchi zao. Inafahamika vilevile katika taaluma ya uchumi kwamba katika nchi ambazo masoko ya uchumi hayapo, Serikali inao wajibu wa kuingilia kati na kujihusisha moja kwa moja katika kuendesha uchumi. Lakini kwa mujibu wa "/best practice/" tofauti chini ya mpango wa SAP uliosimamiwa na IMF wakishirikiana na World Bank, Serikali za Nchi za Afrika ziliambiwa ni lazima zijiondoe katika biashara. Baba wa Taifa Hayati *Mwalimu Julius Kambarage Nyerere* ( "*Mwalimu*" )aliwahi kusema : " /Kama mtu mwenye akili akikushauri jambo la kipumbavu ukakubali, basi atakudharau /". Waafrika tumeshauriwa mambo ya kipumbavu na Watu wenye akili ( miongoni mawo wakiwemo akina World Bank na IMF), na sisi tukayakubali wakati wenzetu Asia wakayakataa. Hebu tujikumbushe yaliyojiri *Jamhuri ya Watu wa China.*

Jamhuri ya Watu wa China ( "China") ilitangazwa mwaka 1949, baada ya Chama Cha Kikomunisti kilicho ongozwa na Hayati Mwenyekiti *Mao Tse Tung *("Mao") kushinda vita vya ukombozi wa nchi hiyo. USSR ilitoa misaada mingi kwa Jamhuri hiyo changa, ikiwa ni ishara wazi ya mshikamano wa Vyama vya Kikomunisti. Hata hivyo, uhusiano huo ulivunjika haraka sana baada ya China kukataa kuiga "/best practice/" ya Ukomunisti kutoka USSR ambayo msingi wake ni Marxism-Leninism, na badala yake Wachina wakadai kwamba Mwenyekiti Mao amerekebisha Marxism-Leninism na kujenga upya itikadi ya Kikomunisti kwa kuzingatia hali halisi na mazingira ya China. Baada ya kuingia katika misukosuko ya kisiasa na kijamii iliyofuatia kutofaulu kwa mpango kabambe wa maendeleo uliojulikana kama "*The Great Leap Forward* " na kuingia katika kipindi ambacho China ilianza kuongozwa na ile "*cosmopolitan mould of mindset *" iliyotajwa katika maandiko ya Fanon. Matokeo yake ilikuwa ni China kuongozwa na "Bureaucrats" ambao ni wataalamu na hawawajibiki moja kwa moja kwa Wananchi. Matokeo yake, Wananchi walio wegi walizidi kuwa maskini zaidi, wakati Viongozi wachache na Watumishi wa Umma walionekana kuanza kuwa matajiri. Kufuatia kujitokeza kwa hali hii mbaya, Mwenyekiti Mao alianzisha Mapinduzi ya Utamaduni ( " *The Great Cultural Revolution* "), yaliyolenga kubadilisha fikra ( *change of mindset*) hasa ya Viongozi wa Chama Cha KIkomunisti, Watumishi wa Serikali na Wasomi wa China. Mwisho wa yote,* Deng Xiao Ping *aliongoza China katika mageuzi makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, bila kuiacha itikadi ya Kikomunisti. Hakuna ubishi kwamba China ni moja nchi zenye uchumi mkubwa, na ambao umekuwa ukikua kwa kasi kubwa katika miongo miwili ya hivi karibuni, hadi sasa. Aidha, China ni moja ya nchi zenye uchumi mkubwa, wenye nguvu duniani na mwenendo wa uchumi huo una athari kwa uchumi wa dunia nzima. Hayo yote yamewezekana kwa sababu Wachina walikuwa tayari kufanya kazi ngumu ya kufikiri na kubuni sera, mipango,mikakati na mbinu za kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia kulingana na hali halisi ya bila kukubali mapokezi ya "/best practice/" kutoka USA na Nchi Washirika wake au kutoka USSR.

Bado tukiwa Asia, tujikumbushe kwa kifupi mambo yalivyojiri India, Nchi nyingine ambayo uchumi wake umekuwa ukikua kwa kasi, na vilevile ni nchi moja muhimu sana kwa uchumi wa Dunia hususan katika maswala yanayohusu *Teknolojia ya Habari na Mawasiliano* ( " *TEKNOHAMA*" au " *ICT *" ). India ilipata mamlaka ya kujitawala kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza mwaka 1947. Baada ya miongo sita (6), India siyo nchi maskini tena na inazidi kuendelea mbele kiuchumi na kiteknolojia. Mafanikio ya India yamepatikana kutokana na ubunifu wa ndani wa sera, mipango, na mikakati ya maendeleo, yote hayo yakiwa ni matokeo ya kazi ngumu ya kufikiri, iliyofanywa na Wasomi wa India. Changamoto kubwa za maendeleo ya uchumi zilizokuwa zikiikabili India mwaka 1947 na China mwaka 1949 zilikuwa zikifanana, hususan nchi zote mbili zilikuwa na idadi kubwa ya watu na zilikuwa hazijitoshelezi kwa chakula. China na India wameweza kukabili na kupata ufumbuzi wa swala la upungufu wa chakula, baada ya kila moja ya nchi hizo mbili, kubuni na kutekeleza sera, mipango na mikakati yake ya sekta ya kilimo kulingana na mazingira ya nchi husika, bila kutegemea ushauri wa "/best practice/". Katika miaka ya karibuni, limetokea kundi la Wasomi Watafiti wa Uchumi ambao hawakubaliani na nadharia ya "/Neo-Liberal Economics/", sambamba na "/best practice/" ya sera za "*Washington Consensus*", na badala yake wamejenga hoja ya ulazima wa kutazama upya swala zima la Maendeleo ya Uchumi *("Rethinking Development Economics").* Wasomi hao ambao wakakaa chini na kukuna vichwa vyao kuhusu sera za uchumi na mikakati ya maendeleo inayofaa nchi changa, karibu wote wanatoka Asia, Europe, USA na Latin America, yaani nchi ambazo nyingi ziko mbali sana katika maendeleo ya uchumi. Sina hakika wapo Wasomi Waafrika ambao wanajishughulisha katika kufikiri sera mbadala za uchumi na maendeleo zitazotukomboa na kutuletea uhuru wa kweli. Ama kweli, uchambuzi wa Fanon kuhusu "/intellectual/ /laziness/" ya Wasomi Waafrika unaelekea kuwa ni sahihi kabisa.

Huenda tatizo la msingi ni kwamba, Wasomi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla hawajafanya uchmbuzi kuelewa nini kimetokea baada ya kutekeleza "*Structural Adjustment* *Programme*" iliyosimamiwa na World Bank na IMF. Hapa kwetu Tanzania, Taifa limeanza kupata ufa wa kitabaka katika mapato na uwezo wa kumudu maisha kwa mwelekeo ambao hauna mustakabali mzuri kwa Taifa letu ambalo lilikuwa limejenga misingi ya mshikamano na uzalendo. Ni kazi ngumu sana, kuchambua na kupembua ili kubaini ni nini hasa kilichotokea na tufanye nini kujinusuru. Hata hivyo, hebu tuone mawazo ya Mtanzania mwenzetu ambaye amefanya uchambuzi wake kubaini kwa nini utekelezaji wa sera za ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma, sambamba na ukuaji wa sekta binafsi ya Tanzania umeshindwa kuwa chachu ya kukuza uchumi ("/private sector to become the engine of growth/") kwa maslahi ya walio wengi. Hebu tusikilize maoni yake:-

".../Implementation of the Structural Adjustment Program in Tanzania and the attending privatisation of State Owned Enterprises ("SOEs"), precluded a transition from a predominantly state owned socialist economy to a nationalist economy owned and controlled by a Tanzanian entrepreneurial class, and supported by the economic and social policies of the Tanzanian Nation State. Foreign capital interests and a Local Comprador class who act as intermediaries and gateway for foreign capital to the local economy, acting together they have taken over from SOEs, the role of Financiers as well as the Captains of Industry, Public Utility Service, Petroleum Sector and Commerce. They control all the strategic commanding heights of the economy. *The overriding agenda of these new Masters of the economy of Tanzania, is the export of capital (by the foreign capital interests) and the creation of personal wealth (by the local comprador class), as opposed to the creation of national wealth and the reinvestment of capital by a nationalist capitalist class..."*/

Mawazo haya ya mtu mmoja bado hayatoi majibu ya nini kifanyike ili tuweze kujenga Tanzania yenye uchumi endelevu ambao uatoa fursa ya maisha bora kwa wote, bila kujenga tabaka za mabwana wenye utajiri wa kufuru na watwana walio maskini wasioweza hata kujikimu. Hata hivyo, maelezo ya hapo juu yanaonesha kwamba tatizo la msingi ambalo linahitaji kushughulikiwa ili kulinda maslahi ya nchi yetu pamoja na walio wengi, ni kuwepo nchini mwetu mfumo mpya wa uchumi ("structural adjustment") unaojali zaidi maslahi binafsi. Mfumo huo umerekebisha na unalenga kufuta ule mfumo wa miliki ya njia kuu za uchumi kwa maslahi ya nchi na Wananchi walio wengi, ulioanzishwa chini ya Azimio la Arusha. Mawazo haya yametolewa kama kielelezo cha mfano wa kazi ya kuchambua na kupembua tulikotoka na tulipofikia kwa sasa, kabla ya kuanza kazi ngumu zaidi ya kupendekeza mustakabali wa kwenda mbele ("/Way Forward/") ili nchi yetu iweze kujikwamua kiuchumi. Hii ndiyo changamoto ya Wasomi. Ubora na idadi ya wingi wa Rasilimali Watu ("Human Capital") ndiyo siri ya maendeleo. Ifikapo mwaka 2050, Afrika inatarajiwa kuwa na idadi ya watu inayolingana na China kwa sasa, lakini kiwango cha maendeleo ya kiuchumi Afrika yatategemea ubora wa rasilimali watu, yaani idadi ya watu wenye kuweza kufikiri na uongoza katika kuleta maendeleo. Lakini hata iweje, Africa haiwezi kukwepa au kujiweka nje ya mabadiliko ya ulimwengu. Hilo halina mjadala. Swala si kwamba Afrika ina hiyari ya kuchagua kama itahusika na mabadiliko yanayotokea ulimwenguni sasa au la. Hapo hakuna hiyari ya kuchagua. Wanachoweza kuchagua Waafrika ni kuamua kushiriki katika maendeleo na mabadiliko ya ulimwenguni kwa kuongozwa na agenda ya maslahi inayotoka katika bongo zao, au Waafrika wanapenda kuwa ombaomba hata wa mawazo watakaosubiri kuelekezwa katika mustakabali utakaobuniwa na wanaotutawala kifikra.

Mada hii naitoa kama changamoto kukuchokoza na kukufikirisha wewe Msomi Mzalendo kwa sababu ni wajibu wako kuwa kiongozi katika harakati za kumkomboa Mwafrika wa kijijini, ambaye hakuhitaji sana wewe kwa sababu analima chakula chake na kutibiwa kwa dawa za jadi. Wewe na mimi hatuna hakika tutasalimika ("/survive"/) vipi hao wa vijijini wasipolima chakula chetu pamoja na kahawa, pamba na korosho inayoingiza fedha za kigeni za kununulia dawa za matibabu, simu za mkononi, mavazi, kompyuta, magari na mafuta ya petroli. MUNGU IBARIKI AFRIKA NA VIONGOZI WAKE. MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE.

BY SIMBA
 
Back
Top Bottom