[h=2][/h]JUMAPILI, FEBRUARI 02, 2014 06:34 NA AGATHA CHARLES
BAADHI ya wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu kutoka vyama vya Chadema na NCCR-Mageuzi, wanatazamiwa kujiunga na chama kipya cha siasa kinachodaiwa kuundwa na wanachama waliomeguka kutoka vyama vya upinzani nchini, Alliance for Change and Transparence (ACT-Tanzania).
Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa chama hicho kimejiandaa vya kutosha ili kuweza kuchukua wabunge hao pamoja na wale wa chama tawala, ili kujiimarisha katika harakati zake za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mpaka sasa kuna wabunge kadhaa kutoka Chadema na NCCR-Mageuzi ambao tayari wamethibitisha kujiunga na chama hicho.
Nakwambia chama kimejipanga, kwani kitakuwa cha kipekee na hakijawahi kutokea nchini, kuanzia sera za chama, wanachama watakaojiunga, kwani mpaka sasa kuna watu wakubwa wanatazamiwa kujiunga nacho na kitafika 2015 kikiwa imara sana, alisema mtoa habari huyo.
Taarifa za awali zilizolifikia MTANZANIA Jumapili, ziliwataja viongozi waliofukuzwa Chadema hivi karibuni ambao ni aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo pamoja na Samson Mwigamba, kujiunga na chama hicho, ingawa wenyewe hawakuwa tayari kukiri.
Mwingine ambaye gazeti hili lilidokezwa kuwa anapewa nafasi ya juu kuingia ndani ya chama hicho iwapo kitasimama vyema, ni Zitto Kabwe, ambaye kwa sasa ubunge wake unashikiliwa na Mahakama.
Chanzo cha gazeti hilo kilibainisha kuwa ACT-Tanzania, ambacho harakati zake zimekuwa za kimya kimya, kinatazamiwa kuzinduliwa mara kitakapokamilisha usajili wa kudumu, ambapo mpaka sasa kina wanachama Tanzania Bara na Zanzibar.
Gazeti hili limefanikiwa kuziona rangi za bendera ya chama hicho, ambazo ziko nne, ikitawaliwa na ile ya zambarau.
Alipotafutwa Mwigamba ili kupata ukweli kuhusu madai hayo, alisema kwa sasa hakuna chama ambacho viongozi wake wamemfuata ili ajiunge nacho, lakini kama chama hicho kitakuwa na sera anazozitaka, anaweza kujiunga nacho.
Alisema mpango alionao ni kuanzisha chama kipya ambacho kitaweza kuwa na sera za kujali Watanzania pamoja na kusimamia rasilimali za nchi.
Kwa sasa nawasiliana na Kitila ili tushauriane, akikubaliana na mawazo yangu tutaanzisha chama kitakachoshiriki uchaguzi kuanzia wa Serikali za mitaa mwaka huu, iwapo hatutaangushwa na Ofisi ya Msajili na pia uchaguzi mkuu 2015 kwa kusimamisha wagombea mpaka ngazi ya urais, alisema Mwigamba.
Alisema chama anachofikiri kuwa kinamfaa ni kile kitakachotetea wanyonge, fursa kwa watu katika rasilimali za nchi, huduma za jamii, kodi kulingana na pato la mtu pamoja na pensheni kwa wazee.
Dk. Kitila Mkumbo alipotafutwa juzi kwa njia ya simu, alisema bado anatafakari kwa kina kuanzisha chama ama kujiunga na chama chochote cha siasa kutokana na kuwa na majukumu ya kitaaluma zaidi.
Nina kazi ya taaluma yangu, bado kwanza nafikiria, nikiona chama kinachonifaa nitajiunga nacho. Hivi sasa kuna ujio wa Katiba mpya, hivyo ngoja tusubiri, haina haraka, alisema Dk. Mkumbo.
Gazeti hili liliwahi kuripoti kwa mara ya kwanza juu ya kuanzishwa kwa chama hicho kipya, kikiitwa African Alliance for Change and Transparence (AACT), lakini baadaye kilibadilishwa katika hatua za kukisajili na kuitwa ACT-Tanzania.