CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa ubani wa sh milioni moja kwa familia ya Masoud Mbwana, aliyeuawa kikatili huko Igunga wakati wa uchaguzi mdogo huku kikitaka uchunguzi wa suala hilo ushughulikiwe haraka.
Akihutubia waombolezaji nyumbani kwa marehemu Mburahati juzi jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa wamepata pigo kubwa ndani ya chama kuondokewa na kada huyo kwani alikufa akisimamia haki.
CHADEMA tumesikitishwa na kifo hiki, hivyo tumeweza kutoa rambirambi yetu kiasi cha sh milioni moja kwa familia na pia tutaendelea kushirikiana na familia katika kuhakikisha haki inapatikana na hatutaishia hapa tutaendeleza yale yote marehemu aliyoyaacha, alisema Dk.Slaa.
Dk. Slaa aliitupia lawama idara ya usalama kuwa ndiyo inatoa mafunzo kwa vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) maarufu kama Green Guard waliohusika katika vitendo vya vurugu huko Igunga, yakiwemo matukio ya kuwamwagia watu tindikali.
Kwa upande wa familia ya marehemu kupitia kaka mkubwa wa marehemu, Ally Matumla, aliishukuru CHADEMA na kutangaza rasmi kuwa kuanzia sasa familia yao inajiunga na chama hicho.
Kwa niaba ya familia ya Mbwana tunashukuru kwa kila jambo na tumeamini CHADEMA si chama cha udini kama inavyovumishwa na vyama vingine, hivyo tunatumia fursa hii bila kushurutishwa, tunajiunga na CHADEMA kuanzia sasa, alisema kaka wa marehemu.
Naye mbunge wa jimbo hilo la Ubungo, John Mnyika, alisema kuwa atahakikisha analifuatilia suala hilo akiwa kama mbunge kwa mwanachama wake huyo sambamba na kusaidiana na familia kwa hali na mali katika kipindi chote.
Kifo cha kada huyo ambaye alienda Igunga kama wakala kililipotiwa kutokea Oktoba 2 mwaka huu na mwili wake kuokotwa Agosti 9, mjini Igunga, mkoani Tabora, ukiwa umeharibika vibaya na kutobolewa macho na hivyo kulazimika kuzikwa huko.