Money Stunna
JF-Expert Member
- Aug 9, 2011
- 13,053
- 6,328
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kata ya Igoma, jijini Mwanza, imejitolea kukarabati nyumba ya bibi kizee, Magdalena Thomas (64), mkazi wa Soko la Chini Igoma, iliyokuwa imebomoka na kuhatarisha usalama wa maisha ya familia hiyo.
Msaada huo umekuja baada ya viongozi, wanachama na mashabiki wa CHADEMA kata hiyo ya Igoma, kutembelea na kujionea jinsi familia hiyo ya watu 12, inavyonyeshewa mvua na kukesha ikiwa imesimama.
Wakizungumza juzi na waandishi wa habari kwenye mji wa bibi kizee huyo, Katibu mwenezi wa CHADEMA Kata ya Igoma, George Said Lujina, na mwenyekiti wa chama hicho kitengo cha Movement fo Change (M4C), kata hiyo, Ezekiel Nkuba, walisema msaada huo umetolewa Novemba 17 mwaka huu, baada ya kuguswa na tatizo hilo.
Akifafanua zaidi kuhusu msaada huo, George alisema, walipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema jinsi familia hiyo inavyoteseka, hivyo kuamua kuchangishana fedha.
Kama inavyofahamika kwamba CHADEMA ni chama kinachojali wanyonge. Baada ya kupata taarifa, tulichangishana fedha kisha kwenda kufanya ukarabati wa nyumba hiyo sisi wenyewe na kwa gharama zetu.
Tulifika tukakuta bibi ana watoto watatu na wajukuu zake wanane wanalala kwenye chumba kimoja. Chumba chenyewe kina bati moja tu zima, mengine yameoza na kuchanikachanika. Mvua inanyeshea ndani, na ikinyesha usiku hakuna kulala, wote wanaamka na kusimama, alisema George.
Bibi Magdalena alieleza kwa furaha msaada huo akikishukuru chama hicho. Alisema msaada aliopewa na CHADEMA hauelezeki, kwani walikuwa wanalala watu 12 katika chumba kimoja, na walikuwa wakiumwa na panya na mbu usiku kucha, na mvua inapokuja wanalala huku wamesimama.
Kwanza sikuamini nilipoona watu wamekuja nyumbani hapa na vifaa vya ujenzi. Nilitaka niwasaidie angalau hata kusogeza bati na maji, wakaniambia wewe kaa tu bibi tuachie kazi hii sisi.
Siku hiyo sikulala kabisa, maana nilikuwa na furaha sana. Wamekarabati na kupatikana vyumba viwili ambavyo sasa mimi nalala huku, wanangu wakubwa na wajukuu wanalala chumba kile, alisema bibi kizee huyo, Magdalena huku akiiombea CHADEMA itawale mwaka 2015.
Imeandikwa na Sitta Tumma
Source: Tanzania Daima