[h=2][/h]JUMATANO, SEPTEMBA 26, 2012 10:59 NA JOHN MADUHU, MWANZA
*Makao makuu wachanganyikiwa, wamtuma Kigaila kutuliza upepo
*Mbunge Highnes Kiwia atupiwa lawama
HALI ya mambo ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Mwanza ni tete.
Hali hiyo imekuwa tete, baada ya Kamati Kuu ya chama hicho, kutengua matokeo ya ndani ya chama yaliyohusu washindi wa nafasi ya kuwania kiti cha Meya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela.
Pamoja na mambo mengine, matokeo hayo yametenguliwa baada ya Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, kutishia kujiuzulu ubunge, kwa kuwa alikuwa akipinga uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho, Wilaya ya Ilemela, ambayo iliwapitisha Marietha Chenyenge kuwania nafasi ya Meya na Rosemary Brown, kuwania nafasi ya Naibu Meya.
Kutokana na mvutano huo, CHADEMA makao makuu, wamelazimika kumpeleka jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila, ili akarejeshe hali ya amani iliyotaka kutoweka ndani ya chama hicho, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilemela, kesho kutwa.
Habari za uhakika kutoka katika kikao cha madiwani wa CHADEMA, waliokutana katika ofisi zao za mkoa zilizopo eneo la Pasiansi, zinaeleza aliyekuwa mgombea nafasi ya Meya, Dan Kahungu ambaye inasemekana alikuwa akiungwa mkono na Mbunge Kiwia, aliamua kukata rufaa kupinga maamuzi ya Kamati ya Utendaji, kuwapitisha Marietha Chenyenge pamoja na Rosemary Brown.
Inadaiwa Marietha na Rosemary, walikuwa na onyo kali kutoka kwa uongozi wa juu, kutokana na mwenendo wao uliosababisha kung'olewa kwa aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza kupitia chama hicho, Josephat Manyerere.
Taarifa zaidi kutoka katika kikao hicho cha madiwani, zinasema kutokana na rufaa hiyo, uongozi wa CHADEMA uliamua kufanya uamuzi wa kufuta matokeo hayo na kuagiza Kigaila kwenda Mwanza kuwaeleza wanachama wa chama hicho ni kwa nini uongozi wa juu, umeamua kufuta matokeo hayo na kumteua Abubakar Kapera kuwa mgombea nafasi ya Meya wa Manispaa ya Ilemela na Dan Kahungu kwa nafasi ya Naibu Meya.
"Kigaila alipoanza kueleza msimamo wa chama hali ilikuwa tete, kwani madiwani hatukukubaliana na uamuzi huo, kwani yalifikiwa kwa manufaa ya Mbunge Kiwia ambaye ndiye anayekivuruga chama kwa manufaa yake binafsi.
Madiwani waliweka wazi, kwamba wako tayari kuwapigia kura wagombea wa vyama vingine, ili kuonyesha msimamo wetu kuhusu kutokubaliana na uamuzi huo kwani inavyoonyesha wanawake hawakubaliki ndani ya CHADEMA, alisema mtoa taarifa wetu.
Taarifa zaidi zinaeleza, idadi kubwa ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya ya Ilemela, wanatarajia kutoa tamko la kuachia ngazi, baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa makao makuu ya chama yaliyoko Kinondoni Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, walisema viongozi wa CHADEMA, makao makuu, wamekiuka na kushindwa kuheshimu uamuzi uliofikiwa na kamati hiyo, ambayo iko kwa mujibu wa Katiba ya chama chao.
"Tuko na Kigaila ambaye ametumwa kuleta ujumbe wa makao makuu na kimsingi hatukubaliani na uamuzi wa makao makuu.
Kitendo walichokifanya ni kuingilia uamuzi wa Kamati ya Utendaji, kwani barua za onyo wanazodaiwa kupewa wahusika kwamba walishiriki kumwondoa madarakani Meya Manyerere, wahusika ndiyo wamezipata leo.
Kama walikuwa na uamuzi huo tangu mwanzo, basi wangeusema mapema na tusingeweza kupoteza muda wetu bure, alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Kiwia alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, hakuweza kupatikana kwa kile kilichoelezwa kuwa, alikuwa katika kikao cha Kamati ya Uendaji ya chama hicho.
[h=4][/h]