CHADEMA, kwenye njia sahihi lakini kukosea uelekeo

Bams

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
16,564
41,082
WAZO LA JUMLA

Kati ya mambo ambayo CHADEMA imekuwa ikipigania ni pamoja na haki ya kuikosoa Serikali bila ya kutendewa kilicho kinyume na haki, sheria na katiba. Basi kama ilivyo haki kwa CHADEMA kuikosoa Serikali ndivyo ilivyo haki kwa Chama chochote, kiongozi yeyote na mwananchi yeyote, kukosolewa.

Jana CHADEMA ilifanya mkutano wake wa kwanza baada ya kuzuiwa pasipo halali, kwa miaka 7. Mkutano huo ulikuwa na mambo makubwa mawili, CHADEMA kutimiza miaka 30 tangu kusajiliwa, na pili kama ufunguzi wa mikutano itakayoendelea nchi nzima.

Katibu mkuu wa CHADEMA, Mnyika aliweka utangulizi mzuri. Alieleza kwa ufupi kuwa CHADEMA inapoadhimisha miaka 30 tangu kuanza kwanza, ni muda sahihi kuwakumbuka wanachama mbalimbali ambao katika kupigania kile ambacho CHADEMA daima imepigania, walikumbwa na masahibu mbalimbali ikiwemo kupoteza maisha na kuumizwa kwa namna mbalimbali.

Alimwomba Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Mbowe atoe wasaa wa kuwakumbuka mashujaa hao. Watu walitarajia Mwenyekiti angekuwa na orodha ya wahanga hao na hata maelezo ya kila mmoja juu ya mchango wake na namna alivyodhulumiwa, iwe ni uhai au namna nyingine yoyote.

Mnyika alimwomba pia Mwenyekiti wake aitangaze Januari 21 kuwa CHADEMA day.

Mnyika akatoa pendekezo kuwa wakati wa mikutano inayoendelea iwe pia ni wakati wa kuwatambua watu wenye dhamira za kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa chama, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Katibu huyo wa chama akaeleza pia kuwa mikutano itakayoendela iwe na ajenda kuu 2, yaani Katiba Mpya na Tume huru ya uchaguzi.

KUPOTEA UELEKEO KATIKATI YA NJIA SAHIHI

Hotuba ya Mbowe, kiukweli ilikuwa ni kupotea uelekeo ukiwa katikati ya njia sahihi.

NJIA SAHIHI

Kila Mtanzania mwenye dhamira njema anakubali kabisa kuwa maridhiano kwa nchi yetu mahali tulipokuwa tumefika, ulikuwa ni uamuzi sahihi na wa busara. Nchi haiwezi kujengeka kwa ubaguzi na kuviziana.

Lakini, japo ni sahihi sana kwa kiongozi kuwa na msimamo kwenye jambo muhimu lililo jema LAKINI NI SAHIHI ZAIDI kwa kiongozi kuwa na ushawishi kwa viongozi wenzake ili waungane naye katika jambo hilo muhimu lililo jema.

Hivyo ilikuwa ni muhimu sana kwa Mbowe na Samia, kila mmoja kwenye upande wake kuwa na ushawishi ili kuwa pamoja katika kutafuta maridhiano. Mbowe kuutumia muda mwingi kuwashambulia viongozi wenzake ambao labda hawakupenda maridhiano, haikuwa sahihi sana.

Kuwashabulia sana viongozi wenzake mbele ya hadhara ile ilikuwa ni kupeleka ujumbe kwa umma kuwa kuna mgogoro mkubwa baina ya viongozi ndani ya CHADEMA. Hata kama ingekuwa kuna hali hiyo, kuutangaza sana mbele ya wananchi, kulilenga jambo gani?

Mbowe kurudia mara kwa mara kuwa ni yeye tu na Mzee Masinde ndio waanzilishi wa CHADEMA walio hai mpaka sasa, ni kama kupeleka ujumbe kwa viongozi wenzake kuwa hawastahili kuhoji chochote dhidi yake kwa sababu wana haki pungufu kutokana na kutokuwa waanzilishi. Mbowe, kurudia mara kwa mara kuwa amepoteza mabilioni mengi kwaajili ya chama hiki, japo ni kweli, haikuwa sahihi sana.

Alistahili kutambua pia mchango mkubwa wa wanachama na viongozi wengine ambao japo siyo waanzilishi lakini baadhi yao wamepoteza mpaka maisha yao, wengine wamepata ulemavu wa kudumu na wengine mpaka muda huu bado wapo magerezani.

Mbowe, tofauti na alivyoombwa na katibu wake kuwakumbuka watu waliopoteza maisha yao katika harakati za kutafuta haki kupitia CHADEMA, yeye akatoa dakika moja watu kusimama kuwakumbuka waasisi tu wa chama. Haikuwa sahihi hata kidogo.

MARIDHIANO
Japo maridhiano ni jambo jema sana, lakini kutumia muda mwingi kumsifia tu Rais na kuelezea tu jinsi alivyochukua msimamo wa pekee yake badala ya kuelezea faida za maridhiano kwa kina, nayo ilikuwa ni kasoro katika hotuba ya Mbowe.

Angeweza kueleza mpaka sasa maridhiano yalivyowasaidia wahanga wa siasa za uhasama. Tunajua kuna watu wengi waliobambikiwa kesi na kufungwa, wameachiwa. Kuruhusiwa kwa mikutano alielezea mara nyingi (ilikuwa sahihi), lakini alitakiwa pia kuelezea maridhiano yanatarajiwa kuleta faida zipi katika siasa za ushindani, na ratiba yake ipoje.

Lilikuwa ni kosa la kiufundi kwa Mbowe kutumia muda mwingi kulalamikia ewatu wanomtuhumu kuwa analamba asali. Kauli moja yenye sentensi chache kama vile, "Mmesikia huko kwenye mitandao kuwa eti mimi Mbowe ninalamba asali ndiyo maana nimekubalia maridhiano, natamka sijawahi kupewa pesa yoyote iwe na Rais au Serikali ili nikubali maridhiano. Na kiuhalisia, ni mimi ndiye kila mara niliyemwomba Rais na CCM tuwe na majadiliano ya kutupeleka kwenye maridhiano.

Kama kuna mwenye ushahidi wowote wa mimi kuhongwa pesa au kitu chochote, alete ushahidi. Siwezi kuiuza CHADEMA kwa fedha ya aina yoyote. Kwa nyakati zote nimeyapokea mateso na dhuluma ili kubakia katika kupigania haki, haiwezekani mtu yeyote kunihonga.

Niliyaomba maridhiano tangu wakati wa utawala wa awamu ya 5, na nilitoa kauli hiyo mbele ya umma wakati wa sherehe za uhuru mbele ya Rais Magufuli, lakini fursa hiyo haikupatikana. Namshukuru Rais wa awamu hii aliyefanya jambo hilo kuwezekana".

Hiyo ingetosha. Kwanza kiuhalisia, kauli hizo za kusema kuwa Mbowe amelamba asali ni kauli za kejeli zinazotolewa na watu fulani ili kujifurahisha nafsi zao, na wala hazitiliwi umuhimu wowote na watu makini. Kuzijibu kejeli za watu ambao wanatoa kauli za viroja kama ajenda kuu ya mkutano wa maadhimisho ya miaka 30 ya CHADEMA lilikuwa kosa jingine la kiufundi kwa mwenyekiti.

Mimi ni kati ya watu wanaomheshimu sana Mbowe, wanaotambua mchango wake mkubwa katika kupigania haki, ujenzi wa demokrasia na uhuru wa kila mmoja na Taifa letu. Ni kati ya watu wanaotambua sadaka ya namna ya pekee ambayo Mbowe ameitoa ndani ya Taifa na ndani ya CHADEMA.

Amedhulumiwa sana, ameteseka sana, ameonewa sana, yote ni kwa sababu ya kupigania haki. Kama Mbowe angekuwa mtu laini, au mtu ambaye alikuwa anatafuta cheo au fedha kupitia siasa, alikuwa na fursa hiyo kubwa wakati wa awamu ya 5. Kama kila mbunge, tena mwanachama wa kawaida aliyeamua kuiasi CHADEMA na kuunga mkono juhudi, alipewa uwaziri, hivi Mbowe, mwenyekiti wa CHADEMA angeamua kuiasi CHADEMA na kuunga mkono juhudi wakati huo, angepewa nini?

Hivyo ukosoaji wangu dhidi ya hotuba ya Mwenyekiti Mbowe haina chembe ya chuki, au kukosa kuutambua mchango wa Mbowe katia Taifa hili, ila nimekosoa kwa dhamira moja kubwa ya kumtaka apangilie vizuri zaidi namna ya kuelezea yale mema mengi ambayo yeye na wenzake wameyatenda katika kupigania haki na ustawi wa demokrasia katika nchi hii.

Nahisi huenda hotuba yake kutokuwa na mtiririko mzuri pengine kulichangiwa na kukasirika kutokana na tuhuma alizozitaja, ambazo kwa kweli ni tuhuma ambazo hazikuwa na uzito wowote.

MBOWE mchango wako hauwezi kudhihakiwa na kila mzalendo wa nchi hii bila ya kujali kama yupo CHADEMA, CCM, chama kingine chochote au asiye na chama.

OMBI
Viongozi wa CHADEMA jipangeni vizuri katika kuwaeleza wananchi juu ya tulikotoka, tulipo, na ajenda kuu kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025.
 
..wanasiasa wengi wa Tz wakubwa na wadogo hawana utamaduni wa kuandaa hotuba au talking points.

..matokeo ya utamaduni huo mbaya ndicho ulichokishuhudia jana ambapo hotuba za viongozi zimekosa muelekeo mmoja.

..nategemea Chadema watajifunza kwa mapungufu yaliyojitokeza.
 
Kwenye ombi hapo ungesema jamaa asichukue fomu ya kugombea Tena Ili wampokee hiyo nafasi ataafu Kwa heshima.
 
Leo Musoma Wametambulisha operation katiba mpya kwamba watazunguka kuisemea katiba nchi nzima yaani unaona hawa operation imezuka kuziba aibu za jana, hawaeleweki kwa muda huu ajenda kuu ni ipi
 
Mmekuwa over critical kwa Mbowe kama vile mlitegemea muujiza wa siasa za siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mkuu!

Siku ya jana ni siku moja kati ya siku nyingi za mikutano ya siasa ijayo. Tutasikia mengi katika kila mkutano. Ni busara kuanza taratibu na kushika kasi taratibu. Je, hamuijui hekima hii?
 
Mmekuwa over critical kwa Mbowe kama vile mlitegemea muujiza wa siasa za siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mkuu! Siku ya jana ni siku moja kati ya siku nyingi za mikutano ya siasa ijayo. Tutasikia mengi katika kila mkutano. Ni busara kuanza taratibu na kushika kasi taratibu. Je, hamuijui hekima hii?
Mkutano wa jana ulikuwa ni muhimu kuliko yote kwa sababu ulikuwa unatoa dira ya mikutano yote itakayofuata.
 
Mkutano wa jana ulikuwa ni muhimu kuliko yote kwa sababu ulikuwa unatoa dira ya mikutano yote itakayofuata.
Na CCM na kila chama masikio dede ili kujua wadandie wapi kukosoa. Hivyo ndivyo ilivyo, taratibu.....
 
Leo Musoma Wametambulisha operation katiba mpya kwamba watazunguka kuisemea katiba nchi nzima yaani unaona hawa operation imezuka kuziba aibu za jana, hawaeleweki kwa muda huu ajenda kuu ni ipi
Kwa bahati mbaya sana walikuwa wame-panick na kutoka nje ya mad. Badala ya kujikita kwenye agenda yao wakajielekeza kujibu hoja za mitandaoni!
 
Mkutano wa jana ulikuwa ni muhimu kuliko yote kwa sababu ulikuwa unatoa dira ya mikutano yote itakayofuata.
Kwakuwa ulikuwa mkutano wa kwanza, nadhani ndio sababu ya Mbowe kumsifia Mama ili kuyapa nguvu maridhiano lakini huko mbeleni hawezi kufanya hivyo.
 
Back
Top Bottom