Ufipa-Kinondoni
JF-Expert Member
- Jan 3, 2012
- 4,582
- 2,783
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.
SASA ni wazi kwamba Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameingia katika kipindi kigumu cha uongozi wake ndani ya chama hicho, Raia Mwema limeambiwa.
Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana wa chama hicho; sasa ameanza kupingwa hadharani na kwa siri, kutokana na matukio matatu makubwa yaliyotokea katika siku za karibuni.
Kwanza ni kitendo chake cha kudaiwa kuingilia uchaguzi wa viongozi wa chama hicho katika Kanda ya Nyasa, ambako alidaiwa kulazimisha kuchaguliwa kwa Peter Msigwa, anayeelezwa kuwa swahiba wake wa kisiasa, na kukata jina la mtu aliyepewa nafasi kubwa ya kushinda, Patrick ole Sosopi.
Msigwa alikuwa mgombea pekee kwenye nafasi hiyo ya uenyekiti na hivyo ushindi wake uliamriwa kwa njia ya kura za Ndiyo na Hapana.
Jina la Sosopi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), lilikatwa kwenye Kamati Kuu kwenye dakika za mwisho, bila sababu rasmi za kufanya hivyo kutolewa.
Mbowe alikuwa Ujerumani lakini alirejea nchini siku chache kabla ya uchaguzi huo wa Nyasa na moja kwa moja alikwenda Mbeya na baadaye Iringa kuhakikisha kwamba mambo hayaharibiki.
Matokeo ya uchaguzi huo, kama yalivyotangazwa na msimamizi wake, John Mnyika, yanathibitisha pia namna Msigwa alivyokuwa hakubaliki na wapiga kura wake.
Kwa mfano, huku ikifahamika kwamba baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu huo walisusa kupiga kura na kuondoka; na pia ikijulikana Mbowe anamtaka Msigwa ashinde, mshindi alipata asilimia 58.49, huku asilimia 41.5 zikiwa ni kura zilizomkataa.
Kwa kawaida, Mbowe amekuwa akipata uungwaji mkono mkubwa na kambi ya vijana ndani ya chama hicho na ndiyo sababu hata baadhi ya vijana mashuhuri wa chama hicho; wamekuwa wakifahamika kwa kuzungumza kwa kuiga staili ya Mwenyekiti wao huyo.
Raia Mwema limeambiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kwamba kiwango cha kutomtii Mbowe kilichoonyeshwa na vijana kwenye Kanda ya Nyasa, hakijawahi kuonekana Chadema kwenye miaka ya karibuni.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), Patrobas Katambi amekiri kufanyika kwa uamuzi wa kuwaengua baadhi ya wagombea dakika za mwisho, uamuzi aliosema ulifanywa na kamati ndogo iliyoteuliwa kusimamia uchaguzi huo wa Kanda ya Nyasa.
“Lililonishangaza ni hilo la baadhi ya wagombea kuenguliwa, sasa siwezi kujua vigezo vilivyotumika kufikia uamuzi huo, tunasubiri kupata sababu,” alisema Katambi katika mahojiano na gazeti hili kwa njia ya simu.
Mwenyekiti huyo alienda mbali zaidi akisema kama ni kampeni chafu kwenye mitandao ya kijamii, basi iliendeshwa na Msigwa mwenyewe dhidi ya makamu wake ambapo yeye (Katambi) alimshauri msaidizi wake huyo kutojibu kitu.
Katambi alibainisha kuwa miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kuwapigania vijana ndani ya chama hicho, ikiwemo kuhakikisha wanapata nafasi za uongozi ndani ya chama.
“Mimi kama Mwenyekiti wa Vijana nitakuwa wa ajabu iwapo sitosimamia maslahi ya vijana, tusubiri, tuone sababu zilizotumika kumuengua, ndipo nasi tutoe kauli,” alisema Mwenyekiti huyo.
Uchaguzi huo wa Chadema Kanda ya Nyasa umeibua mjadala mzito ndani na nje ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini huku wapinzani wa uamuzi wa hatua ya kuenguliwa kwa baadhi yawagombea wakiuita kuwa ni udikteta.
Malumbano zaidi yako miongoni mwa vijana wa chama hicho ambao wanahoji mantiki ya kufungwa midomo wanapohoji baadhi ya maamuzi yanayofanywa na chama chao chini ya Mwenyekiti wake, Mbowe.
“Kumkosoa Rais John Magufuli kuwa ni dikteta inaonekana ni sawa, ila kumkosoa mwenyekiti wa chama ni dhambi. Mnapinga udikteta wa viongozi wa serikali, halafu mnatetea udikteta wa mwenyekiti wa chama, tena chama kinachojiandaa kushika dola,” aliandika Edger Mwankuga katika ukurasa wake wa Facebook.
Jambo la pili ambalo linadaiwa kuharibu taswira ya Mbowe kwenye chama chake hicho ni kitendo chake cha kukaa kimya wakati msaidizi wake, Ben Rabiu Saanane, akiwa hajulikani alipo.
Saanane, ambaye pia ni mmoja wa wanasafu wa gazeti hili, ametoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa takribani miezi miwili sasa, lakini Chadema haikuwa imetoa taarifa yoyote rasmi hadi lilipojitokeza kundi la vijana wa chama hicho kutoa taarifa.
Ben Saanane ni mmoja wa vijana maarufu ndani ya chama hicho na hatua ya bosi wake huyo (Mbowe) kukaa kimya kwa mwezi mzima bila kusema chochote ilionekana kuwaudhi vijana hao.
Hata hivyo, wiki iliyopita, mara baada ya uchaguzi wa Nyasa, Mbowe alizungumza na kusema kwamba hakutaka kuzungumzia jambo hilo kwa vile hakutaka kuingilia upelelezi wa dola na vyombo vya ulinzi vya chama chake.
Aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, ni miongoni mwa watu maarufu waliohoji ukimya wa Chadema baada ya tukio la kutoweka kwa Saanane ambaye ni mmoja wa viongozi vijana wa chama hicho.
Sababu ya tatu inaelezwa kuwa ni dhana iliyojengeka miongoni mwa viongozi vijana kwamba Mbowe si aina ya mwanasiasa anayeweza kumtia kashikashi Rais John Magufuli.
Gazeti hili limeelezwa na vyanzo vyake kuwa kuna vuguvugu linalohusisha baadhi ya wabunge wa chama hicho wanaoamini kwamba staili ya Magufuli inaweza kuendana zaidi na mwanasiasa wa aina ya Tundu Lissu na si Mbowe.
Mbowe, inaelezwa, kwa sababu ya biashara zake ambazo sasa zimeanza kuchunguliwa na vyombo vya dola, anaonekana kutoweza kupambana jino kwa jino na Magufuli na ndiyo sababu kundi hili jipya linaona wakati umefika wa Mbowe kuachia ngazi na kumwachia mtu kama Lissu nafasi yake hiyo.
Ulivyokuwa Uchaguzi wa Nyasa
Pamoja na nafasi ya Mwenyekiti, katika uchaguzi huo pia walichaguliwa Makamu Mwenyekiti, nafasi iliyochukuliwa na Shedrack Malila, wakati nafasi ya Mweka Hazina ilichukuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu, kupitia chama hicho, Sophia Mwakagenda.
Kuelekea uchaguzi huo, ulisambazwa waraka ukidaiwa kuwa ni wa Msigwa akielezea kujiengua kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo ya mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, hivyo kuibua maswali pale jina lake lilipopelekwa kwenye mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Ingawa Msigwa na Sosopi wote wanatoka katika chama kimoja, baadhi ya viongozi waandamizi na wanachama wa chama hicho walishtushwa na aina ya kampeni zilizoendeshwa na wagombea wote wawili – ambapo ziliendeshwa kampeni chafu kwenye mitandao ya kijamii.
Raia Mwema limelezwa na vyanzo vyake ndani ya chama hicho kuwa, kampeni hizo ikiwemo waraka uliodaiwa kuandikwa na Msigwa, ulisambazwa na kambi iliyokuwa ikimpinga kwa lengo la kumsafishia njia mpinzani wake, Ole Sosopi aliyekuwa akiungwa mkono na kundi la vijana ndani ya chama hicho.
Mchungaji Msigwa amethitisha kufanyika kwa kampeni chafu dhidi yake, ikiwemo kutengenezwa kwa waraka huo uliodai ameamua kwa hiari yake kujiengua kwenye kinyang’anyiro na kumwachia Ole Sosopi, aliyemwelezea kama mdogo wake.
Kwa mujibu wa Msigwa, kijana aliyetengeza waraka ule alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa, na aliachiwa baada ya wazazi wake kumfuata mbunge huyo na kumuomba msamaha.
Hata hivyo, Mbunge huyo alihusisha kampeni hizo chafu dhidi yake na mahasimu wao kwenye siasa za nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ni kampeni chafu yenye mkono wa CCM, hata hivyo tulishayamaliza, sasa tunaendelea na mengine,” alisema Msigwa katika mahojiano yake kwa njia ya simu na gazeti hili.
Ubabe wa Mbowe
Kabla ya Mkutano wa Uchaguzi, Kamati Kuu ilikaa jijini Mbeya chini ya Mbowe ambapo ilipitisha majina matatu tu, moja kwa kila nafasi.
Chanzo chetu cha uhakika kimelieleza gazeti hili kuwa Mwenyekiti alilazimika kutumia nafasi yake kushawishi wajumbe wapitishe jina moja kwa kila nafasi na kuwaengua wagombea wengine akiwemo Ole Sosopi.
“Mbowe alitumia ubabe, alipeleka kwenye Mkutano wa Uchaguzi majina matatu tu, ya mwenyekiti, makamu na mweka hazina, kura iliyopigwa ni ya ndio na hapana,” kilisema chanzo chetu.
Watetezi wa hatua hiyo ya kuengua baadhi ya wagombea, wanasimamia hoja kwamba chama hivi sasa kimekua hivyo demokrasia ndani ya chama lazima iwe na mipaka.
Inaelezwa kuwa hali iliyokuwepo haikuwa nzuri, tayari kulikuwa na mpasuko mkubwa, huku baadhi wakiichambua aina ya kampeni iliyofanywa na kambi ya Ole Sosopi kushahibiana na ile ya mtandao maarufu ndani ya CCM uliomwingiza madarakani Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete katika uchaguzi wa mwaka 2005.
Watetezi wa hatua hiyo wanabainisha kuwepo pia kwa viashiria vya siasa za ukanda, ambapo baadhi ya wanachama walihofu kuwa iwapo angechaguliwa Ole Sosopi basi mahasimu wao, CCM, wangeitumia kuthibitisha madai yao ya kila siku kwamba CHADEMA ni chama cha Kaskazini ya nchi.
Ili kuepuka huo mtego, watetezi wa hatua hiyo wanasema yalihitajika maamuzi ya kidikteta, ndivyo ilivyofanyika.
Mtandao wa Ole Sosopi, unaelezwa kuhusisha zaidi kundi la vijana ndani ya chama hicho, na inaelezwa kuwa kutokana na nafasi yake ndani ya jumuiya hiyo ya vijana alipata ungwaji mkono mkubwa kutoka kundi hilo la vijana wa chama.
Wapinzani wa hatua hiyo wanamlaumu mwenyekiti wao wa chama kukiuka misingi ya chama hicho, wakisema alitumia udikteta kwa lengo la kuwaengua kina Ole Sosopi kwa faida ya kina Msigwa.
Vijana wapinga udikteta
Upinzani dhidi ya uamuzi huo wa Kamati Kuu, ulidhihirika pia kwenye mkutano wa uchaguzi, pale kambi ya makamu mwenyekiti huyo wa BAVICHA walipoelezea hisia zao wakipinga kufikiwa kwa uamuzi wa kuengua baadhi ya wagombea.
Hata hivyo, Ole Sosopi hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi ambayo wakati wote ilionyesha haikuwa hewani.
Pamoja na kumtumia ujumbe mfupi wa simu kupata msimamo wake kuhusu hatua ya yeye kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho kinyume na utashi wake, hakujibu.
Chanzo: Raia mwema