BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,015
Date::8/18/2009
CCM yawafunga midomo vinara wa kupinga ufisadi
Na Habel Chidawali, Dodoma
Mwananchi
CCM yawafunga midomo vinara wa kupinga ufisadi
Na Habel Chidawali, Dodoma
Mwananchi
HALMASHAURI Kuu ya CCM juzi ilifikia uamuzi wa aina yake baada ya kuunda kamati maalumu ya kuwashughulikia wabunge wake wanaoikosoa serikali ya chama hicho tawala, huku ikimwekea kinga rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
"Bunge limeanza kuwa kama mchezo wa (kikundi cha televisheni cha vichekesho) The Comedy," alisema katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.
"Yaani kila mtu anafanya mambo yake mwenyewe, hali ambayo inaweza kusababisha watu kurushiana hata viatu ndani ya Ukumbi wa Bunge, sasa hali hii maana yake nini?
"Kwa hiyo tumesema inatosha, hapo tulipofikia tusiendelee mbele. Wanaoropoka ovyo ni walevi na tumeona kuna kundi dogo ambalo limejiona kama ni wateule wa kuzungumzia sakata hilo (la ufisadi) bila ya kujua wabunge wote wana haki ya kuzungumzia suala hilo, lakini kwa utaratibu tena kwa kupitia katika vikao vya kamati za wabunge."
Tamko hilo la Chiligati limetolewa mwishoni mwa kikao cha Nec ambacho imeripotiwa kuwa kilimweka kitimoto Spika Samuel Sitta kwa madai kuwa analiendesha Bunge kwa kuwapa upendeleo wabunge walio katika kundi lake ambao wamekuwa wakipiga vita ufisadi.
Katika kikao hicho cha Nec, wachangiaji wengi walitaka Spika anyang'anywe kadi ya CCM kwa madai kuwa amekuwa akiruhusu na kushabikia mijadala inayoichafua serikali na chama hicho kikongwe.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao hicho, Chiligati alisema uamuzi wa kuunda kamati hiyo umefikiwa ili kurudisha nidhamu ndani ya chama hicho tawala.
Kwa mujibu wa Chiligati, kamati hiyo ya watu watatu itaongozwa na rais wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, spika wa zamani, Pius Msekwa na waziri wa zamani, Abdulrahman Kinana.
Alisema kamati hiyo itawashughulikia wabunge wote wanaoibomoa serikali bungeni na adhabu yake kwa watakaopatikana na hatia ni kuondolewa madarakani au kufukuzwa kabisa uanachama.
Alisema kamati hiyo imepewa jukumu kuhakikisha wabunge wa CCM na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa chama hicho wanarudi katika nidhamu ya chama kwa kuacha malumbano yasiyokuwa ya msingi.
Alisema kitendo cha wabunge wa CCM kuwashambulia viongozi wa CCM, wakiwemo mawaziri, si cha kiungwana na kwamba kimekuwa kikidhalilisha chama na baadhi ya Watanzania.
Katika mkutano uliopita, wabunge wengi waliwashambulia mawaziri na Baraza la Mawaziri wakilituhumu kubariki mikataba ya kifisadi na ilifikia wakati mbunge mmoja aliomba Mungu alilaani kwa sababu ya ubinafsi.
Katika hali iliyoonyesha vita hiyo kuwa kubwa, wakati fulani Spika Sitta alisimama bungeni kushambulia magazeti yaliyoripoti tuhuma za ufisadi kwenye ofisi yake, akisema ni ya mafisadi na hivyo kuomba ulinzi zaidi kutoka kwa waziri mkuu kwa madai kuwa usalama wake sasa uko shakani.
Kabla ya kikao cha Nec, makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, John Malecela aliamsha mjadala wa nafasi ya wabunge wa chama hicho kwenye uchaguzi ujao aliposema kuwa, wengi watapoteza viti vyao kutokana na tuhuma za ufisadi, kauli ambayo ilichochea mjadala mkali.
Katibu wa CCM, Yusuf Makamba alimjibu kwa kusema kuwa, haoni kama kuna mafisadi wala kama chama hicho kitakuwa kwenye wakati mgumu mwaka 2010, lakini akatabiri ushindani mkubwa ndani ya chama hicho tawala.
Spika Sitta aliingia kwenye mjadala huo na kusema kukubaliana na Malecela kuwa wabunge wengi wa CCM watakuwa kwenye wakati mgumu.
Baadaye Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga akaibuka na kukemea mjadala huo, akisema wale wanaodai wanapambana na ufisadi, hawana budi kuwataja; kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria au kuwaripoti kwenye chama na kwamba kupambana nje ya vikao ni kuichafua CCM, kauli ambayo imerejewa na Nec.
Chiligati pia alisema kuwa, CCM imewaonya viongozi wake, wakiwemo wabunge, wanaomshambulia rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.
Mkapa, ambaye aliingia Ikulu akijulikana kama mtu safi (Mr Clean), amekuwa akituhumiwa kwa ufisadi na baadhi ya wabunge wa CCM na wa upinzani kutokana na kununua mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kwa bei ndogo, kuanzisha kampuni ya ANBEN akiwa ikulu na kutumia ofisi hiyo ya serikali kuendesha shughuli zake binafsi za kibiashara.
Lakini jana Chiligati alisema mkutano wa siku mbili wa Nec umewakumbusha viongozi wa CCM na Watanzania wote umuhimu wa kudumisha utamaduni wa kuwaheshimu na kuwaenzi viongozi wastaafu hasa marais.
Chiligati alisema Nec imesikitishwa na kitendo cha baadhi ya watu kumshambulia kwa maneno makali na kejeli Rais Mkapa huku wakisahau mazuri yote aliyoyafanya katika kipindi chake cha uongozi.
Alisema Mzee Mkapa katika kipindi cha uongozi wake alifanya mambo makubwa, ikiwemo kuinua hali ya uchumi, kuendeleza miundombinu, huduma za kijamii, elimu pamoja suala la maji.
"Hayo yote ni mambo mazuri, lakini bado Watanzania wanaona kuwa alichokifanya Mkapa kilikuwa ni kazi bure, jamani sisi ni watu gani tusiokuwa na shukrani yaani kila jambo kwetu ni baya, tukumbuke kuwa nchi hii ilikuwa katika hali ya kuwa mufilisi; ilikuwa haikopesheki lakini sasa tunakopesheka," alisema Chiligati.
"Mkapa anastahili pongezi sio kejeli; anastahili heshima sio dharau na pia anastahili kuenziwa sio matusi." Kwa mujibu wa Chiligati Nec imewataka Watanzania wote na wana-CCM wenye nia njema na Tanzania kumwacha kiongozi huyo apumzike kwa amani bila ya kumbughudhi na kuongeza kuwa, inasikitisha zaidi pale wana-CCM wanaposhiriki kumkejeli.