Ccm tano ndani ya jangwani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ccm tano ndani ya jangwani

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by andrews, Jun 13, 2012.

 1. a

  andrews JF-Expert Member

  #1
  Jun 13, 2012
  Joined: Mar 28, 2012
  Messages: 1,680
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  ISHARA zinazidi kudhihiri kwamba wakati wa ukombozi nchini umewadia. Kama tunavyoelezwa kwenye vitabu vitakatifu juu ya ishara za mwisho wa dunia, ndivyo matukio ya leo yanavyoeleza kwa ufasaha juu ya ishara za mwisho wa utawala wa kifisadi hapa nchini!
  Katika mojawapo ya maandiko ya Mungu katika kitabu kitakatifu imeandikwa hivi: “Kama vile uchungu umjiavyo mwanamke, ndivyo na machafuko yatakavyowajia ghafla na hawataokolewa. Wakati wasemapo kuna amani na mambo yote ni salama, ndipo uharibu utakapowaijia kwa ghafla”.
  Maneno haya ya maandiko matakatifu yaliyoelekezwa kwa wanadamu wasiotaka kulitii neno la Mungu wao na kuepuka madhara ya mwisho wa dunia, ni sahihi pia kwa CCM isiyotaka kuyatii matakwa ya umma na kuepuka anguko kuu na madhara yake ni mwisho wa enzi za utawala wa enzi ya giza.
  Enzi za utawala wa CCM hii ya leo zimekuwa kama enzi za giza, enzi ambazo Watanzania walipelekwa bila kujua wanapelekwa wapi, bila kuhoji kwa nini wala kuuliza kuna nini huko. Mfumo ambao CCM imewaongoza Watanzania kwa miaka mingi sasa unaweza kuelezwa kwa maneno ya Vicent Nyerere aliyoyatumia kueleza mfumo wa utendaji wa askari polisi wetu.
  CCM walikuwa wakisema “vijiji vya ujamaa”, wananchi wanaitikia “hoyee” bila kuuliza vitatusaidia nini. Walioambiwa Azimio la Zanzibar wakasema sawa bila kuuliza la Arusha limekosa nini. Wakiambiwa nchi ya ujamaa na kujitegemea wanasema haswaaa, bila kuhoji mbona kwenye matendo ni ubepari na soko holela! Wakiambiwa MKURABITA hawaulizi kama huyo mdudu ana sumu kuliko wadudu waliomtangulia akina MKUKUTA na MKUZA.
  Wanaimbiwa ari, nguvu na kasi zaidi hawaulizi hiyo ziada tutaiweka wapi wakati ari, nguvu na kasi mpya amekufa! Wanaambiwa Kilimo Kwanza wanasema hewala bila kugeuka kuangalia kama Siasa ni Kilimo kuna alichokifanya! Walipoambiwa rais lazima awe na madaraka makubwa walikubali ndiyo! Bila kuuliza kama anataka kuwa muumbaji wa nchi hii. Walipoambiwa matokeo ya uchaguzi wa rais yakishatajwa hayapingwi wakasema hilo ni sawa bila kupata maelezo kama Tume ya Uchaguzi itaongozwa na Malaika Gabriel.
  Sasa kumekucha. Enzi za giza zimepita! Watanzania wameamka na kukataa kupelekwa kama kondoo. Wanahoji kila kitu kinachofanywa na watawala na kutafuta maelezo ya kila tendo la watawala wetu, huku wakipima kila neno linalosemwa na watawala. Walio kwenye utawala wanaanza kuweweseka. Wanapambana na CHADEMA wanasahau kwamba tatizo la msingi la kupambana nalo liko ndani yao wenyewe.
  CHADEMA ni chama cha siasa cha upinzani, chama mbadala cha CCM na mshindani mkuu wa CCM. Kinatumia udhaifu wa CCM yenyewe kujipatia umaarufu na uhalali mbele ya wananchi wa kujiandaa kuingia Ikulu badala ya CCM ili nao waoneshe utawala wao. Mimi ni mwana CHADEMA na waandishi wengi wa hizi makala wana vyama wanavyovipenda hata kama hawana kadi za uanachama.
  Lakini kwa pamoja bila kujali u-CHADEMA wetu ama u-CCM wetu ama u-CUF wetu, nk, tumejitahidi sana kuiokoa CCM. Tumetumia muda mwingi kuikosoa CCM na kuielekeza cha kufanya kuliko hata tulivyoiasa CHADEMA ama CUF ama chama kingine chochote kujipanga kwa ajili ya kuchukua nafasi ya CCM.
  Lakini CCM haikutuelewa na badala yake tumeshutumiwa na kubambikiwa makosa na kutishiwa hata maisha. Kabla ya kufikishwa mahakamani na hatimaye kulazwa gereza la Keko kwa siku saba na Serikali ya CCM nilishatishiwa kushtakiwa si chini ya mara tatu na gazeti letu pendwa limetishiwa kufutwa si mara mbili wala tatu bali mara nyingi tu ikiambatana na kunyimwa matangazo kutoka serikalini.
  Kesi za wana CCM za kulishtaki gazeti hili kwenye Baraza la Habari na mahakamani ni nyingi hata hatuzikumbuki zote. Lakini mpaka sasa hawajagundua kwamba wamefanya hivyo kwa hasara yao wenyewe. Laiti wangefanyia kazi yale tunayoyasema kila siku, CCM ingeweza kudumu madarakani kwa miaka mingi ijayo mpaka Watanzania waseme sasa tunabadilisha chama ili kuonja tu utawala wa chama kingine na si kwa sababu chama kilichoko madarakani kimeshindwa kazi. Sasa angalia yanayowatokea CCM waliochanganyikiwa.
  Mkutano wa Jangwani umeonesha jinsi CCM ya leo ilivyochanganyikiwa. Wanaiga kila kinachofanywa na CHADEMA siku hizi, na kiukweli ukiiga kila anachokifanya mwenzako lazima katika pointi fulani utaonekana chizi.
  Kwa sababu jamaa mwenzako akishajua unaiga kila kitu, kuna siku atakaa nje ya nyumba yake akiwa ameinua kichwa na kutazama juu ili kuzuia damu inayotoka puani mwake halafu wewe utapita na kumwona na kudhani hiyo ndiyo stahili ukajikuta unatembea mitaani umeinua kichwa na kuelekeza pua angani na ndipo watu wanaokufahamu watakaposema, “keshachizika huyo!”.
  CHADEMA ni chama cha upinzani na kina kila sababu ya kuitisha mkutano wa hadhara na kuelezea mapungufu na madhaifu wanayoyaona kwenye utawala wa CCM na kueleza mipango waliyonayo wao kama Watanzania wataiondoa CCM madarakani na kuwachagua wao kuongoza serikali.
  Kitendo cha CCM kuiga kila kitu cha CHADEMA kuanzia sera, mbinu za kampeni hadi namna ya kueneza chama, kinaifanya kionekane kama chama cha ‘machizi’. Wameiga ilani ya uchaguzi ya CHADEMA katika mambo kadhaa baada ya uchaguzi wa 2005 na 2010, baadhi ya mambo yakiwamo kupitia upya mikataba ya madini, kurejesha nyumba za serikali zilizouzwa, kushughulikia ufisadi na mafisadi, katiba mpya, posho ya vikao, nk na wameshindwa kuyatekeleza itakiwavyo.
  Wakaiga kufanya kampeni kwa helikopta, wameshajaribu kuiga kufanya maandamano na sasa wamejikuta ‘wamechizika’ pale CHADEMA walipozindua mkakati wa M4C na Operesheni Vua Gamba Vaa Gwanda, na wao wakafanya mkutano siku ya Jumamosi kama CHADEMA, viwanja vya Jangwani kama CHADEMA, wakarusha kwenye TV kama CHADEMA, wakazindua operesheni ya “Vua Gamba, Vua Gwanda, Vaa Uzalendo” inayoshabihiana na CHADEMA na mwisho wakajikuta wanaiga kuongea kama CHADEMA na hatimaye makada wao kujikuta wakisambaratika kama wajenzi wa mnara wa Babeli na kuzungumza kama vyama vitano vya siasa kwenye mkutano mmoja wa hadhara na kuonekana ‘machizi’ mbele ya umma.
  Pale Jangwani CCM tano zilihutubia. Ya kwanza iliwakilishwa na Abdulrahman Kinana ambaye aliwakilisha CCM ambayo ni chama tawala cha nchi hii na kusema kimefanya mambo mengi ya maendeleo ambayo aliapa kwamba hawaoni aibu kuyatangaza na akatoa rai kwa kila mkoa wa CCM hiyo kuandaa mkutano kama huo wa Dar es Salaam na yeye na wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya CCM yake wako tayari kuhudhuria na kutangaza mafanikio ya CCM hiyo.
  CCM ya pili iliwakilishwa na Nape Nnauye, ambayo ni chama tawala, lakini hakijui kifanyalo. CCM ya Nape inaona ufahari kutumia mamia ya mamilioni ya shilingi ilizopata kihalali kutoka kwenye kodi za Watanzania na huenda na zingine kiharamu kwa njia za ufisadi, kuwaalika watu kwenye mkutano na kuwapa usafiri, posho na viwalo kama kapelo, t-shirt na khanga ili waje kusikiliza mipasho ya akina Khadija Kopa na wasanii wengine wa bongo fleva ambao hawakuzungumza hata sentensi moja ya maana zaidi ya kuimba mipasho dhidi ya CHADEMA na kunengua viuno.
  CCM ya Nape Jumamosi ya Juni 9 ndiyo imepata habari za vurugu zilizotokea Zanzibar wiki mbili kabla ya siku hiyo na ndipo inatoa agizo la serikali kuwakamata waliochoma makanisa eti ni majambazi!
  Kuna CCM ya tatu iliyohutubia pale Jangwani. Hii ni ya Wassira, Maghembe na Tibaijuka. Wassira alianza kwa kukariri mipango mingi ya uchumi na maendeleo ambayo serikali yake inayo. Alifuatiwa na Jumanne Maghembe aliyeorodhesha miradi mingi ya maji ambayo wako mbioni kuitekeleza na zamu yao ikahitimishwa na Anna Tibaijuka ambaye yeye alitumia sana neno “tunajipanga” katika kuelezea mipango mingi ya serikali yake juu ya ardhi.
  Kwa aliyewasikiliza vizuri akina Wassira, Maghembe na Tibaijuka, walikuwa wakitoa ahadi kwamba wakipewa kuongoza nchi hii CCM yao ina mipango gani ya kuifanyia nchi. CCM hii ya hawa makada watatu haina tofauti na CUF, NCCR, UDP, TLP, CHADEMA, nk. Ni CCM ambayo haijaingia madarakani na sasa pale Jangwani ilikuwa inatangaza mipango ambayo itatekeleza na kuleta maendeleo baada ya kupewa madaraka.
  Kuna CCM ya nne ambayo pia ilipata fursa ya kuhutubia mkutano ule. Hii ni ya Harrison Mwakyembe. Yenyewe imeingia madarakani mwezi uliopita siku ambayo sisi tulifikiri JK alikuwa anafanya tu mabadiliko ya Baraza la Mawaziri akaacha baadhi na kuchagua wapya ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi na hata kuanzisha wizara isiyoeleweka kazi yake inayoitwa wizara maalumu.
  Kumbe kwa mujibu wa Mwakyembe lile ni baraza jipya kabisa, chini ya waziri mkuu mpya na rais mpya na makamu wake. CCM ya Mwakyembe iliingia madarakani siku hiyo baada ya kuwa chama cha upinzani kwa muda mrefu.
  Mwakyembe katueleza kwamba CCM yake ilikuta madudu mengi sana kwenye wizara ambayo inaonekana sasa yaliachwa na chama kilichokuwepo madarakani, yaani CHADEMA. Maana tukubaliane kwamba mkutano ule ulikuwa ni wa CCM zote kujibu mapigo ya CHADEMA na kuitwisha matatizo ya nchi hii.
  Kwa hiyo CCM ya Mwakyembe imeingia madarakani mwezi uliopita baada ya kuiondoa CHADEMA madarakani, na sasa anatutangazia madudu aliyoyakuta yameachwa na CHADEMA wizarani. Akatangaza pia nini CCM yake imekifanya ndani ya wiki tatu na tutegemee nini ndani ya miezi mitatu.
  CCM ya tano iliyofunga kazi na kupokea wanachama wapya kutoka CHADEMA ni ya John Pombe Magufuli. Hii imeingia madarakani mwaka 2005 baada ya kuing’oa CHADEMA ambayo imekaa madarakani tokea uhuru. Magufuli akatutangazia kwamba CHADEMA imekaa madarakani kwa miaka 44 tokea uhuru mwaka 1961 mpaka 2005 ilipoondolewa na CCM ya Magufuli na JK, lakini iliweza kujenga barabara za lami zenye urefu wa kilometa elfu 4 tu.
  Akasema CCM yake iliyokaa madarakani kwa miaka saba tu yaani 2005 mpaka 2012, imefanikiwa kujenga barabara za lami zenye urefu wa kilometa elfu 11. Akatuelezea jinsi wanavyojipanga sasa kuingia kwenye suala la kuondoa msongamano wa magari Dar es Salaam.
  Akiwa amechanganyikiwa vya kutosha akajikuta anawaita wale wanaotaka kurudisha kadi za CCM badala ya kuwaita wanaotaka kurudisha kadi za CHADEMA.
  CCM ya sasa inatia huruma, inaelekea kuzama ndani ya bahari ya upinzani. Inajaribu kupiga piga mikono na miguu huku na kule, lakini inazidi kuzama, imeshindwa kujiokoa.
  Kama pale Jangwani walikusudia kupunguza kasi ya CHADEMA ili waendelee kuwa madarakani 2015, Arusha tuna msemo wetu tunasema, “ imekula kwao!”.
  :confused2:
   
Loading...