nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,803
JUMATANO, FEBRUARI 06, 2013 04:37 NA MAGUZU MASESE, MWANZA
KATIKA hali ya kawaida na baada ya changamoto ambazo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekutana nazo, kilipaswa kuanza kuchukua hatua za dhati za kukabiliana nazo ili kuhuisha hadhi ya chama katika Mkoa wa Mwanza, ambao uliopata kuwa ngome ya chama hicho.
Bahati mbaya kwa wanaCCM ni kwamba wanacheza aina ile ile ya ngoma iliyowafanya wapoteze haiba yao mbele ya macho ya jamii. Na kosa kubwa wanalofanya ni kufikiri kwamba, adui yao mkubwa ni Chadema, hapa ndipo wanapoanzia kuachana na njia inayoweza kuwapatia ahueni waitarajiayo.
Kwa mtazamo huo, wanaCCM wanadhani kuwa na mvuto katika siasa za Mwanza ni kuhujumu Chadema na kukalia nafasi za Meya wa Jiji na Manispaa ya Ilemela.
Wanakosea ingawa wamefanikiwa kufikia malengo ya baadhi ya wanachama wake waliokuwa na kiu ya kusikia kuwa Chadema wamepoteza kila kitu.
Lakini katika kujenga chama mbele ya macho ya umma, hilo hawajalifikia hata robo kwa sababu wanakosea kufikiri kuwa mvuto ambao sasa Chadema kinao mbele ya jamii kubwa ya Watanzania unatokana na kupendwa tu na watu bila sababu.
Ukweli halisi na ambao wanaCCM hawataki kuusikia ni kwamba, wenzao wanazungumzia hoja za msingi na zenye mashiko, zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja, kitu ambacho CCM walishaachana nacho siku nyingi sana.
Wakati CCM kwa kuelemewa na sifa za kuwa chama dola wanafanya karibu kila kitu kwa jinsi itakavyowapendeza wao wenyewe na kuridhishana kwa mifumo wa huyu ni mwenzetu, wenzao wanajenga hoja za namna ya kukabiliana na matatizo ya wananchi na hiyo ndiyo inayowapa matumaini wananchi.
Wakati wa uchaguzi mkuu, kwa mfano ule wa CCM, walijikita kubomoa hoja za Chadema za kupunguza bei ya vifaa vya ujenzi kwa njia ya kupunguza kodi katika vifaa hivyo. Wakaibeza kwa kila walivyoweza, lakini sasa viongozi wao wakuu waliowachagua na ambao wanategemea wawavushe 2015 wameifanya kuwa ajenda yao.
Katika hali kama hii unawezaje kuwapuuza au hata kuwashinda Chadema kwa hoja mbele ya umma?
CCM Mwanza badala ya kujikita katika kujenga hoja za namna chama kitakavyorejea kwenye misingi yake ya kuwajali wananchi wanyonge! Nape na Mwigulu wanafanya safari kwenda Mwanza kushughulikia upatikanaji wa nafasi ya Meya wa Jiji na kuhadaiwa na mbwembwe za Meya anayejiita wa Mahakama, Henry Matata, na wanadhani hayo ni mafanikio ya chama. Wanakosea, wanapaswa kufanyakazi upya na vizuri zaidi.
Yanayofanyika yanazidi kuwatia hasira wananchi na kukifanya CCM kuwa mithili ya chombo kilichokosa mwelekeo kwa sababu gharama za uhuni wa kisiasa zinazofanyika Mwanza zimewagharimu wananchi kwa kiasi kikubwa.
Kupoteza nguvu na rasilimali za chama kwa ajili ya kuwakomoa Chadema ni kujikomoa wenyewe na kwa kumtumia Meya Matata kufanikisha mipango ya chama hicho, ni sawa na kujilisha upepo kwa sababu bado nalo kovu la uadilifu katika nafasi aliyonayo la kukiri kuhongwa milioni 20 ili kuhujumu uchaguzi wa awali wa Meya.
Hii ina maana kama chama kweli kina dhamira ya dhati ya kurejesha haiba yake, kwanza kilitakiwa kijisahihishe na kiukubali ukweli na kiyape sababu za kweli matatizo kinayokabiliana nayo na ndipo kiweze kujinusuru.
Katika kitabu chake Tujisahihishe, Mwalimu Julius Nyerere, anasema; "Mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na anashauri dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu za matatizo na jinsi ya kuyaondoa. Kila mmoja anacho chombo cha kutumia akili yake. Jambo la maana ni kuzipa akili uhuru wa kutafuta elimu, bila kutiwa kiini macho cha utashi wetu wa ubinafsi." (Tujisahihishe, 1962, ukurasa wa 8.)
CCM Kama wasipotaka kutumia akili zao kutafuta chanzo halisi cha matatatizo yao, wataendelea kujishibisha upepo huku wakiamini wanafanya jambo la maana kujenga chama wakati kimsingi wanafanya kinyume chake.
Wanadhani wao kwa kuwa viongozi wa chama tawala, basi wanajua kila kitu, lakini katika Tujisahihishe, Mwalimu anaonya; "Watu walio hatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala hawana haja ya kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo. Sababu moja ambayo ilituzuia sisi Waafrika kuendelea ni majibu ya urahisi kwa matatizo makubwa."
Kumtumia Matata kwa imani kuwa itaibomoa Chadema mkoani Mwanza, ni kutafuta majibu rahisi kwa matatizo makubwa. Hili haliwezi kukisaidia chama zaidi ya kuharakisha tamati yake.
Mwalimu anasisitiza katika kitabu chake cha Tujisahihishe kuwa, "Makosa ni makosa na dhuluma ni dhuluma, japo watendao makosa hayo au dhuluma ile ni wakubwa au ni wengi. Chama kinachopenda ukweli na haki hakina budi kiwape wanachama wake uhuru na nafasi ya kusahihisha makosa na kuondoa dhuluma.
Wanachama hawana budi waone kuwa ni wajibu wao kuutumia uhuru huo na nafasi hiyo. Wanachama wasiotumia uhuru huo na nafsi hiyo kwa sababu ya kuogopa kuchukiwa au kupoteza nafasi zao wanafanya kosa kubwa la ubinafsi ambalo ni adui wa haki na ukweli."
CCM kinapaswa kutambua ukweli pekee ndiyo utakiweka huru. Kama ni lazima kishindane kurejesha hadhi yake machoni pa Watanzania, kinapaswa kufanya hivyo kwa hoja za msingi badala ya kuhujumu haki za wananchi kihuni kama ilivyofanyika wakati wa kuwapata Mameya wa Jiji na Manispaa ya Ilemela.
Huo hauwezi kuwa ukombozi wa kweli wa chama. Ni bahati mbaya kwamba hata viongozi wanaotumwa Mwanza kuhuisha hadhi ya chama, wanaingia katika mkumbo huo huo.
Naambiwa Mwigulu alifurahia sana mbwembwe za Matata kujinadi kwenye kikao chake cha ndani kuwa yeye ni Meya wa CCM na Mahakama na bila shaka ripoti iliyotua mezani kwa Kinana itakuwa na taarifa nzuri kuhusu maendeleo ya chama mkoani Mwanza, lakini ukweli halisi walionao wananchi hususan wa Kitangiri anakotoka Meya huyo na wananchi wa Mwanza uko nafsini mwao.
Bahati mbaya nyingine ni ya hata Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, aliyekuwa tumaini la chama hicho na ameingia huko huko. Akiwa ziarani mkoani Mwanza naye alipambanishiwa na Meya Matata, akapandishwa jukwaani kama ishara ya ushindi wa chama mkoani Mwanza.
Lakini bila shaka mzee Mangula aliyapata majibu ya wananchi mara tu alipotoka nje ya Uwanja wa Nyamagana alipokutana na nguvu ya umma. Hata kama chama wanakanusha kuwa hakuzomewa, huko nako ni kujijaza upepo kwa aina nyingine, kwa kuwa ukweli haugeuki kuwa kitu kingine kwa kuukana.