CCM inavyoumia kwa kupuuza ushauri wa Jakaya Kikwete

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Jakaya Kikwete.jpg


Kwa ufupi
  • Siku hizi salamu hii imewekwa kapuni na vivyo hivyo fikra za mwenyekiti zinatupwa, hakuna mtu wa kuzidumisha.

By Kelvin Matandiko, Mwananchi kmatandiko@mwananchi.co.tz


Miaka ya nyuma CCM ilikuwa na salamu maarufu “Zidumu fikra sahihi za mwenyekiti wa CCM” ambayo iliitikiwa: “Zidumuu”.

Siku hizi salamu hii imewekwa kapuni na vivyo hivyo fikra za mwenyekiti zinatupwa, hakuna mtu wa kuzidumisha.

Mwaka 2012 akiwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alitoa ushauri muhimu kwa CCM ili iweze kuimarika. Aliitaka iache kubweteka na kuwategemea polisi katika masuala ya kisiasa, lakini kama ilivyo salamu ya ‘zidumu’, ushauri huu haukudumu.

Katika ushauri huo, Kikwete alisema kitendo cha CCM kuitegemea polisi ni kujidanganya na kimepitwa na wakati.

“Mnaishia kulalamika tu kila siku, eti wanatukana halafu mnaishia kusema ndiyo kawaida yao au utasikia mtu anasema eti Serikali haipo! Kazi ya Serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa maana hao ndio wenzenu.

“Sasa mnataka wakisema Serikali ya CCM haijafanya kitu polisi wawafuate au wakisema Kikwete nchi imemshinda polisi wawakamate? Kama wakisema hatujafanya kitu ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu, waonyesheni barabara, shule na ambo mengine,” alisema.

Kikwete alitoa ushauri huo Novemba 13, mwaka 2012, siku mbili baada ya kuchaguliwa mara ya pili kuwa mwenyekiti wa CCM. Alikuwa anafunga Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM.

Huku akirudia mara kadhaa maneno hayo alisema, “Nataka mfahamu ndugu zangu kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu, tutakwisha na tutakwisha kweli.

“Mkijibu kwa hoja wanatulia, sio polisi. Nakumbuka Mwigulu (Nchemba) aliwajibu pale bungeni kuhusu bajeti yao mbadala. Walipoitoa kijana wetu akasimama na kupiga msumari kweli wakachanganyikiwa, sasa hizo ndiyo kazi zinazotakiwa jamani,” alisisitiza Kikwete.

Kikwete aliwatuhumu viongozi wa upinzani kwamba ni waongo na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakizusha mambo ambayo hayapo, huku wakijifanya kuwa na ushahidi wa kimaandishi.

Hizi ni fikra za Kikwete zinazoendelea kuishi, japokuwa zimepuuzwa, hasa sasa kipindi hiki wakati Jeshi la Polisi likipambana kudhibiti kauli na shughuli za kisiasa zinazotolewa au kufanywa na vyama vya upinzani.

Ushauri huo ambao Kikwete aliurudia mara kadhaa kwenye sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa chama hicho, zinapata uhai zaidi sasa wakati vigogo wa chama wakionekana “wapenzi watazamaji” katika mchezo wa siasa.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limekwishasema kuwa utekelezaji wa majukumu yake hautakiwi kuhusishwa moja kwa moja na masuala ya siasa.

Pia, limesema halitasita kuchukua hatua kwa matukio ya kihalifu kama vile uchochezi, kwa sababu ya kuhofia tuhuma za kukisaidia chama tawala.

Mchambuzi wa siasa, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, anasema ujenzi wa demokrasia kwa nchi za Kiafrika ni kazi ngumu na ushindani wa vyama vya siasa unatafsiriwa katika nguvu ya hoja.

Msomi huyo anasema demokrasia imeweka wazi tofauti ya Serikali ya awamu ya tano na ile ya awamu ya nne ya Kikwete, hali ambayo inatia dosari katika uongozi wa Rais John Magufuli anayejipambanua katika kuwaletea wananchi maendeleo.

“Chama tawala kina dola lakini vyama vya upinzani havina dola. Unapotumia dola ushindani unakosekana na inakuwa si sawa kuwashindanisha katika mazingira yaliyopo kwa sasa, kwani wengine wanakamatwa, wanahojiwa, wanapandishwa mahakamani. Hii haikuonekana kwa kipindi cha Kikwete na ndiyo maana hakutaka polisi watumike katika masuala ya kisiasa,” anasema Profesa Mpangala.





INAENDELEA UK 18

INATOKA UK 15

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz anasita kuzungumzia ushauri wa kiongozi huyo mstaafu akisema waulizwe CCM wanaohusika.

Kuhusu tuhuma za polisi kutumiwa kisiasa kukisaidia chama tawala, Boaz anasema dhana hiyo ni potofu na haina ukweli wowote.

Boaz anasema Jeshi la Polisi ni chombo kinachofanya kazi kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi na hakiingiliwi na misukumo ya kisiasa.

Anasema hakuna mwanasiasa atakayefanya uhalifu akajificha nyuma ya kivuli cha vyama vya siasa.

Kuhusu kipimo wanachotumia kati ya kauli za uchochezi na maoni au hoja za wapinzani, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa anasema uchochezi ni kosa la jinai na hakuna uhuru usiokuwa na mipaka.

Anasema haiwezekani kuibua hoja au maoni yanayomkejeli au kumtusi mtu mwingine.

“Ushauri wa Kikwete hauna uhusiano na kazi zinazofanywa na Jeshi la Polisi, sijaona uhusiano hapo,” anasema.

Mwakalukwa anasema mlalamikaji anapojitokeza katika kauli zinazotolewa, Jeshi la Polisi lazima limkamate aliyezitoa na endapo hakutakuwa na ushahidi wa kutosha linamwachia huru.

“Kosa la uchochezi lina vipengele vyake, mlalamikiwa anakamatwa, ushahidi unaandaliwa na kesi inafunguliwa mahakamani ambako sheria itatafsiriwa.

Msomi wa Falsafa, Dk Azaveli Lwaitama kutoka Chuo Kikuu cha Josiah Kibira (JoKUCo) anasema licha ya ushauri huo, hata Kikwete kwa wakati wake wakati anamalizia muda wa Ikulu, hakusimamia ushauri huo.

Dk Lwaitama anatoa mfano kuwa nguvu za dola zilitumika kupokonya ushindi wa CUF Zanzibar.

“Hata Kikwete mwenyewe alinunua magari ya washawasha, kwa hiyo alikuwa anasema tu lakini ni vigumu kutekeleza. CCM ni chama dola, hakihitaji kufanya siasa ya kushawishi wananchi. Kuna mtu anaitwa Jecha (Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha)) kwa tume hiyo ya kusimamia uchaguzi ikageuka kuwa mahakama, hali hii ipo hata Msumbiji, Uganda na Burundi, ndiyo sifa ya chama dola, hakina sababu ya kufanya siasa,” anasema.



Hali ilivyo

Maoni ya Dk Lwaitama yanasadifu hali ilivyo kuhusu utendaji wa CCM. Ni mara chache viongozi wa chama hicho, mbali na bungeni, wakijibu hoja za wapinzani, bali wamekaa wakisikilizia kauli za Rais ambaye ndiye mwenyekiti wa chama.

Mathalan, kwa miaka kadhaa Chadema imekuwa ikiikosoa Serikali ya CCM na chama chenyewe kwamba ni dhaifu, lakini hakuna majibu ya msingi yanayotolewa kufafanua hali hiyo .

Katika hoja za karibuni kabisa, Chadema kupitia mwanasheria wake mkuu, Tundu Lissu ilizungumzia uwezekano wa Serikali kufilisiwa na wawekezaji wa kigeni kutokana na uamuzi wake wa kuvunja mikataba bila kufuata sheria.

Hoja hiyo iliyotolewa sambamba na sakata la kushikiliwa kwa ndege ya Bombardier nchini Canada, ilijibiwa kwa vitendo kwa polisi kumkamata Lissu na kulala rumande siku tatu.

Pia, Lissu anadai Serikali haikutumia busara kukiuka mikataba na kampuni za madini nchini na aliwahi kutamka kwa kuwataka wahisani wainyime misaada Tanzania kwa sababu ya ukandamizaji wa demokrasia hasa kwa vyama vya upinzani. Hoja zote hizo zilimtia matatani Lissu.

Hoja kubwa pengine ambayo imekuwa gumzo la muda sasa ni hatua ya Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM, kuzia mikutano ya kisiasa, ambayo inaendelea kutekelezwa na polisi kwa ama kuzia, au kuwakamata na kuwashtaki wanaoikiuka.

Juni mwaka jana, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alizuiliwa kufanya kongamano la kujadili na kuikosoa Serikali kuhusu bajeti na kuelezwa kuwa kongamano hilo lililenga kuhatarisha usalama wa raia.

Wakati huo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, alisema hakuna siasa itakayofanyika bila kuwa na amani na kila wanapoingilia kuzuia mikutano hiyo hufanya hivyo kwa nia njema.

Hata wiki hii tumesikia polisi wakipambana kuzuia maombi ya Lissu ambaye anapigania uhai wake baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

Katika tukio hilo, polisi wanadaiwa kuingia mitaani hadi Makao Makuu ya Chadema kusaka fulana zilizoandikwa Pray for Lissu (Mwombee Lissu).

Mbali na polisi, mwelekeo pia umehamia hata katika mhimili wa Bunge ambako hoja za kisiasa pia zimegeuka mwiba kwa upinzani na hatua za kukamatwa na badala ya kujibiwa amri hutolewa kwa polisi kwa wabunge kufuta hotuba zao, kutoka ukumbini polisi huamriwa kuwatoa kwa nguvu ukumbini zimekuwa za kawaida.

Haya yanatokea wakati Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini na Saed Kubenea wanasubiri kuhojiwa na kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Maadili kwa kauli yake kwamba Bunge linautumikia mhimili fulani na kukosoa matamshi ya spika.



Athari kwa CCM

Kutokana na hayo yanayoendelea, ni dhahiri CCM itapata wakati mgumu kufafanua hoja zake kwa wananchi baada ya ukosoaji wa muda mrefu wa wapinzani.

Wakati Kikwete anatoa angalizo hilo alikuwa anaona ugumu ambao chama hicho kingepata wakati wa Uchaguzi Mkuu, na ndio maana Katibu mkuu, Abdulrahman Kinana na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye waliamua kutoka mitaani kujibu hoja na kurudisha chama hicho kwa wananchi.

Kutokana na ziara hizo za Kinana na timu yake, wengi wanakiri kuwa zilikuwa msaada mkubwa wakati wa uchaguzi 2015.

Akizungumzia hali hiyo, Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu, Gemma Akilimali anasema athari kubwa inayoweza kujitokeza kwa kutojibu hoja kisiasa badala yake kutumia kuzizima, ni pamoja na Serikali kukosa mawazo mbadala ambayo yangeibuliwa na vyama vya upinzani.

“Polisi wanazuia juhudi za CCM kukusanya ajenda zinazoibuliwa. CCM inatakiwa izipate ajenda za upinzani ili kuisaidia Serikali yake, badala yake polisi kuingilia kati na kuzuia.
chanzo.CCM inavyoumia kwa kupuuza ushauri wa Jakaya Kikwete
 
Ushauri wa Kikwete unaweza kuuona ulikuwa wa maana, lakini ujue kwamba CCM hawawezi (siyo kwa makusudi) kujibu hoja nyingi nzito zinazotolewa na upinzani. Sasa wewe umeiba na umekamatwa live ukiwa katikati ya kufanikisha huo wizi. Hoja gani utakuwa nayo hapo sasa - zaidi ya kutoa mimacho tu na kujipa ugangwe kujaribu kumdhuru aliyekukamata.

Ndo wanachopitia CCM hata sasahivi. Hoja zinazotolewa dhidi yao nyingi ni za kweli. Reaction yao ni kujaribu kumdhuru mleta hoja.
 
CCM ya Magufuli ingepata support ya wananchi sana kama ingeshirikiana na wapinzani kuweka nchi sawa . . , kwa sababu kwa ukweli ni wapinzani ndio walioibua scandals za ccm ya Mkapa na Kikwete . .

Sasa Magufuli alipaswa ajitenge na ccm ya wazee hawa kwa kuwatumia wapinzani . . , na sio kuwalinda wazee hawa na ccm yao
. .
Na namna bora ya kupambana na ccm na mafisadi ilikuwa ni kuhakikisha anajenga mifumo imara itakayovunja nguvu za uccm ktk Serikali . .
Halafu angejiandaa kutupatia Katiba mpya ya Warioba, basi hapa angejizolea wafuasi wote . .
 
Ushauri wa Kikwete unaweza kuuona ulikuwa wa maana, lakini ujue kwamba CCM hawawezi (siyo kwa makusudi) kujibu hoja nyingi nzito zinazotolewa na upinzani. Sasa wewe umeiba na umekamatwa live ukiwa katikati ya kufanikisha huo wizi. Hoja gani utakuwa nayo hapo sasa - zaidi ya kutoa mimacho tu na kujipa ugangwe kujaribu kumdhuru aliyekukamata.

Ndo wanachopitia CCM hata sasahivi. Hoja zinazotolewa dhidi yao nyingi ni za kweli. Reaction yao ni kujaribu kumdhuru mleta hoja.
 
Back
Top Bottom