Ninapotazama kwa ukaribu hali halisi ya Taifa langu Tanzania kwa sasa napata mashaka sana. Ni wazi mengi yanasemwa kutoka kila upande na watu tofauti; ikiwa ni wasomi na watu wa kawaida kabisa. Ila cha kushangaza hasa ni kwa wasomi wetu wa leo walio wengi ambao wametupilia mbali mwanga-ukweli, na kukumbatia giza-upofu.
Wasomi walio wengi leo Tanzania hasa wenye elimu ya sayansi ya siasa, hawana mchango wowote zaidi ya kukumbatia upofu na kuwa watambiri wa yasiyowezekana kwa manufaa ya kuficha ukweli kwa faida yao na wale wanaowatumikia. Wanaishi kama waganga wa kienyeji kwa kuendesha shughuli zao kiramri ramri. Watu hawa wamekosa mwelekeo kabisa. Leo wanasema hili na kesho wanaibuka na hili ili mradi kuwafurahisha mabwana wao wanaowaweka mjini. Wanachama na viongozi wa chama tawala nao wapo katika wimbi zito hili. Ni sawa na mbwa aliyezeeka ambaye afundishiki tena kukabiliana na njia mpya za uwindaji.
Jambo hili linajionesha wazi katika namna ya kufikiri kwao, kutenda kwao, na vipaumbele vyao. Wanafanya yale yale miaka yote bila ya kutendea haki muda, nafasi walizonazo, na fursa tulizonazo kama Taifa. Hii ni dhambi ya kijamii-social sinkubwa kupita zote.
Hivi karibuni dhambi hii-social sin, imejionyesha wazi katika mjadala wa Bunge la kutunga katiba mpya, upitishwaji wake, na mwendelezo wake. Huwezi amini kama haya yanaweza tokea kwa binadamu mwenye ufahamu sahihi katika karne ya leo. Nasema ufahamu sahihi nikimaanisha uelewa kawaida tu wa kutofautisha mambo uliyofanya jana, unayofanya leo, na matazamio yako ya kesho. Jambo hili kwa kiumbe kama kuku ni mtihani mkubwa sana. Nachelea kusema kundi hili la watu tulionao ufahamu wao hauna utofauti na wa kuku. Ukitaka kujua ufahamu wa kuku mrushie nyanya tu na ukweli utaujua kwa hili nilisemalo. Kuku hutoboa upande mmoja wa nyanya na wakati huo huo husahau tendo hilo na kutoboa upande mwingine.
Umekuwa ni wimbo wetu kama Taifa kupambana na maadui watatu; ujinga, maradhi, na umaskini. Ngonjera hii ishatimiza zaidi ya miaka 50 sasa bili mafanikio ya kuridhisha. Tatizo lipo wapi? Nionavyo mimi na walio wengi pia, tatizo lipo katika upumbavu. Tunatumia muda mwingi kupiga vita dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini tukisahau gonjwa letu kubwa na baya kuliko yote kama Taifa likiwa ni upumbavu.
Je, si upumbavu kwa kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kuongoza anapoikimbia elimu ya nchi yake na kupeleka watoto wake kusoma nje ya nchi yake? Lini basi ataweza kurekebisha elimu hiyo mbaya katika kijiji chake, jimbo lake, na nchi yake?
Je, si upumbavu kwa kiongozi kama huyo na familia yake kutumia kodi za wananchi waliompa dhamana, kwenda kutibiwa nje ya nchi na kuacha huduma hiyo ikiwa ovyo kijijini mwake, jimboni mwake na nchini mwake? Je ni watazania wangapi wenye uwezo wa kwenda kutibiwa nje kwa mfano India, Afrika ya kusini na kwingineko? Je, kutokana na rasilimali tulizonazo kama Taifa hatuwezi kuboresha huduma hizo hapa nyumbani? Je, kupambana na malaria ni kutengeneza kiwanda cha neti au kutumia neti ili hali hatuteketezi mazalia ya mbu? Wenzetu wa ulaya na hasa Italia ya kusini waliwezaje kusahau gonjwa la malaria? Tunapokwenda katika nchi za wenzetu kujifunza huwa tunakwenda kufanya nini? Huu katika ujumla wake ni upumbavu.
Je, si upumbavu wa kiongozi ambaye anajua wazi nchi yake ina rasilimali na utajiri wa kutosha, na badala yake anakuwa ombaomba katika mafaifa jirani na ngambo? Jambo hili linanikumbusha marafiki wawili. Jamaa alienda mtembelea rafiki yake kijiji cha jirani nyakati za jioni. Akiwa kwa rafiki yake, mvua kubwa ilinyesha bila kukoma na hivyo kumwiya vigumu kurudi nyumbani kwake. Hata hivyo rafiki yake alimpa ukarimu wa kulala kwake kwa makubaliano atalala sebuleni kutokana na udogo wa nyumba na vile vile hana shuka za kujifunika. Alichofanya jamaa huyu ni kurudi nyumbani kwake akinyeshewa mvua na kuchukua shuka na kurudi kulala kwa rafiki yake. Hoja yake ni kwamba kwa rafiki yake kuna umeme na sebuleni pake kuna sofá nzuri, ili hali nyumbani mwake ameacha nyumba kubwa ikiwa na kitanda kikubwa pia. Jamaa huyu hana tofauti na mtu anayejisifia kuwa na kitambi kikubwa kinachotokana na kula kwa jirani yake. Jamaa huyu hana tofauti na viongozi wetu wa chama tawala katika vita dhidi ya umaskini. Kilichobaki ni kuuza nchi na rasilimali zake kwa bei poa, na kujidhalilisha kwa mataifa ya kigeni. Huu ndiyo upuuzi ninaousema!!
Tukio la hivi karibuni la baadhi ya vyamba vya upinzani kuunda umoja wao katika kile kinachoaminika kuunganisha nguvu kupigania haki na mabadiliko katika utendaji mpya wenye nafuu katika maisha ya Watanzania, viongozi wa chama tawala na baadhi ya wasomi waliopoteza ufahamu kwa upofu wao na kusaliti elimu yao, wameubeza umoja huu.
Nitajikita katika hoja zao za kupinga umoja huu wa baadhi ya vyama hivi vya upinzani. Hoja zenyewe ni nyingi ila initasema chache tu kama ifuatavyo; umoja huu ni feki, umoja huu hauna baraka kwa wanachama wa vyama husika, umoja huu utakufa kwa sababu za (udini, ukabila, na ukanda), umoja huu ni kundi la wasaka tonge, umoja huu hauna ushawishi wa umma, na mengine mengi.
Kwa ufupi, mara nyingi binadamu huyatoa yale yaujazayo moyo na akili yake. Pili, huwezi kutoa usichokuwa nacho. Najiuliza sana sababu ya hoja hizi ni nini hasa? Kama umoja huu ni feki, je, umoja kati ya TANU na ASP Na kuzaliwa CCM upo salama? Je, majimbo yanayoshikiliwa na vyama pinzani mwanzoni yalikuwa chini ya chama gani ambacho kinajinadi ni dhabiti? Kwa jambo kama hili huitaji shule ya pekee kujua jambo hili. Wenye kutoa kejeli hizi ni sawa na mbwa aliyezeeka na amebakia kubweka hovyo tu kuthibitisha uwepo wake.
Lingine ni kuwa umoja huu hauna baraka kutoka kwa wanachama wa vyama husika. Je, unajuaje hauna baraka? Je, ulitaka waeleze kila kitu hadi hatua waliyofikia kuungana hata kama hilo silo jambo la muhimu? Nia na sababau ya kuungana waliyokubaliana haitoshi kuthibitisha utashi wao kisiasa? Kwa upande mwingine, hasa viongozi na serikali ya CCM ni yapi yaliyopata baraka kwa wanachama wake na hasa sisi wananchi wa kawaidi kwenye maswala ya mikataba feki na ya dhuluma tunayoshuhudia leo?
Hoja nyingine ya kushangaza ni hii ya udini, ukabila na ukanda. Hii imekuwa silaha kubwa kwa chama tawala kuwagombanisha wananchi wake kwa kuwagonganisha hasa kwenye mambo haya ambayo huwezi kufikiria kwa mtu mwenye ufahamu wa kawaidi kuyanadi wazi kwa watu. Katika vyamba vilivyounda umoja huu, hakuwa hata jambo moja katika hayo hushikiliwa kama será ya vyama vyao. Leo mtu anapoibuka na hoja hizi ni wakuogopa kama ebola. Jambo hili halina mashiko tena. Mulitudanganya mara kadhaa hasa katika chaguzi za mwaka 2005 na 2010 mkafanikiwa, na sasa hatudanganyiki tena. Hatuitaji tena elimu ya pekee na utafiti wa pekee kutambua uovu wenu. Mnavaa miwani ya utakatifu wakati macho yenu ni maovu na ya kishetani.
Mwisho nimalize na jambo hili. Taifa letu la leo Tanzania limebadilika sana. Kwa viongozi wa chama tawala mfahamu kuwa mabadiliko ni sehemu ya maisha ya binadamu yeyote. Jambo hili huwezi kulizuia kwa mikono yenu nikimaanisha vyombo vya ulinzi na usalama. Jueni kuwa hata kwenye taasisi hizo waliopo ni binadamu ambao silka yao ni mabadiliko.
Leo kwa utafiti wa moja kwa moja utaona tunaelekea katika mfumo wa kimonaki usio rasmi. Viongozi wengi waliopo madarakani ni familia zile zile zilizowahi kuwa madarakani kwa nyakati na nafasi tofauti. Sipingi mtu kuwa kiongozi eti kwa sababu baba au mama yake aliwahi kuwa kiongozi serikalini. Ninachopinga ni namna ya kiongozi huyu kuwa kiongozi na mbinu au njia iliyotumika kuwa madarakani. Leo bila aibu utasikia baba mzazi awe amestaafu au yupo madarakani kumnadi mtoto wake kuwa kiongozi au kupigania nafasi za uongozi. Je, huku sio kusaka tonge na mtiririko wa matonge? Kundi na jamii hii ya watu wanaojijengea himaya kwa mtindo huu ni hatari sana katika maendeleo sawiya ya wananchi