Busara za Mlosi K. Mtulutumbi zilizo sahaulika | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Busara za Mlosi K. Mtulutumbi zilizo sahaulika

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mkweremkwere, Jul 14, 2012.

 1. m

  mkweremkwere New Member

  #1
  Jul 14, 2012
  Joined: Jul 9, 2012
  Messages: 4
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Huyu jamaa alitabiri mambo mengi ynayoendelea! Jisomee


  Salamu zangu zikufikie......Mjomba daktari!

  Mjomba wangu daktari, salamu sana,
  Ama baada ya salamu,

  Kwanza nitoe shukrani kubwa kwa kunirudishia majibu ya kina nilipokuuliza swali kwa nini mama na mpenzi wake baba waliamua kuniita mtulutumbi. Nashukuru kwa kunieleza kwa uwazi kuwa mtulutumbi kwa lugha ya watani wetu kule kwenye mapanga shaa humaanisha 'mchawi', mwanzoni nilikereka kidogo lakini sasa naelewa busara zao, kwa maana kama mchawi anavyochukiwa na watu wengi, yawezekana kwa waraka wangu huu kwako watu wengi wakanichukia. Hii ndiyo sababu kubwa ya kufarijika kuitwa 'mtulutumbi' kwa maana watu wengi wasiopenda kufikirisha vichwa vyao kufikiria fikra za mtu aliyefikiria kuandika fikra, basi watanichukia japo najua wewe utanielewa mjomba daktari;

  Kwanza nikupongeze kwa kusitisha mgomo kwa hiari yako, hongera!
  Mgomo uliouanzishwa mwenyewe bila shinikizo, Hongera
  Ukasema unawatetea wananchi ambao hawakuelewa unawatetea kwa nini, hongera!
  ukakutana na 'mtoto wa mkulima' mtani wangu wakati akiwa amekufukuza kazi, hongera!
  Juzi nasikia uliwatuma wajumbe kupata kiyoyozi magogoni, hongera!
  Hongera! Hongera! hongera!

  Hata hivyo, baada ya hongera nyingi nirudi hasa kwenye hoja ya msingi;

  Moja: Kuwatetea wananchi kuhusu huduma bora

  Kwanza,nikusifu kwa jinsi ambavyo umeendelea kutoa huduma pasipo kujali kuwa fani yako inakaribia kuwa kama mganga wa kienyeji, na pengine kuwa chini ya hapo, hili litaliongelea baadaye na naomba unisamehe kukufananisha na 'mganga' wa kienyeji japo naamini wananchi kukuita 'bwana mganga' badala ya 'daktari' inawezekana wanakuona kama mganga wa kienyeji japo sina uhakika kuhusu hilo na mimi si mtaalamu wa kiswahili mjomba. Kama hujui mjomba, Wananchi wengi wa Tanzania "wameshadumaa" akili na hali hii imejengeka toka enzi za hata kabla ya uhuru. Hali hii ambayo inahitaji 'ukombozi wa fikra' kama alivyoeleza Mzee Mwanakijiji katika waraka wake hivi karibuni, ina safari ndefu sana hadi kupata ukombozi huu, na hilo tu ndilo litakaloboresha hali ya ndugu zangu si kisiasa tu bali kiuchumi,kiafya na kadhalika.

  Kama alivyosema mtanzania mmoja katika kitabu chake ambacho naamini hakijasomwa na watanzania wengine kiitwacho Sindano inayovuja, 'Serikali huboresha huduma kwa wananchi kunapokuwa na Service Demand". Service demand aliyoiongelea hapa si ya kusubiri serikali 'ione' uhitaji wa huduma bali 'wananchi' kuwa proactive na kuona kuwa wanahitaji huduma na kwa kuwa serikali ni mwajiriwa wa wananchi, basi 'wananchi wadai' huduma kama haki yao na kazi waliyoituma serikali kufanya. Mfumo huu wa service demand toka kwa wananchi ndiyo wanaoutumia wanaharakati kudai mabadiliko katika mambo kadhaa, mfano miswaada mingi ama mipya ama inayofanyiwa marekebisho au kuwekwa viraka katika nchi zilizoendelea hutokana na 'Pressure' za wanaharakati kutokana na makundi fulani ya kijamii kuona hitaji la huduma na kudai. Hali hii ni tofauti nchini mwetu mjomba, wewe mwenyewe ni shahidi kwani wananchi wamehalalisha umasikini, shida na karaha. Umasikini kwa wananchi umekuwa ni kama binadamu na nguo mjomba, kwamba unapompigania mwananchi anaona kama unataka kumvua nguo..

  Mwananchi huyu huyu mjomba,
  Nani asiyeelewa, haki yake ulidai?
  Ukasema kaelemewa, Huduma kwake hutoi?
  Glovu uletewe, Temeke hadi Moi?
  Vitanda uongezewe, mwanga siwe koroboi?
  Kaposho upewe, hata ukiwa kiomboi?
  Ukamwona Mizengwe, akakuacha hoi?


  Mwananchi wa Tanzania mjomba pengine ulipoteza muda wako kumtetea, au pengine pia nikusifu kwa kuwa umejihakikishia mwenyewe kuwa mwananchi huyu si wa kumkomboa kwani hayuko tayari kukomboka;au hata kukombolewa;
  Anaona kulala chini pale Mwananyamala, Ni haki yake ya msingi;
  Anaona kubebwa kwenye ambulance ya baiskeli kijijini, ni haki yake ya msingi
  Hana bima ya afya, ni haki yake ya msingi
  Anajinunulia dawa kwa kuwa hospitalini hazipo, ni haki yake ya msingi
  Hana uwezo wa kwenda hospitali ya binafsi, ni haki yake ya msingi
  Akuambukize magonjwa au umuambukize wewe kwa kukosa glovu, ni haki yake ya msingi
  Umtibu kama mganga wa kienyeji kwa kuwa huwezi kumfanyia vipimo, ni haki yake ya msingi.
  Analipa kodi katika kiberiti hadi ndala, ni haki yake ya msingi;
  Umuhudumie hata kama una njaa, ni haki yake ya msingi;
  Udaktari ni wito, uongozi wa kisiasa siyo wito, ni haki yake ya msingi;
  Atembee kilomita nyingi kwenda hospitali kwa kuwa mjomba umeng'ang'ania mjini, ni haki yake ya msingi!
  Haki ambayo wataka kumnyang'anya mjomba!

  Je mtu huyu anastahili kutetewa?

  Hapa ndiyo maana nikasema mjomba umepoteza muda wako, japo ni nafasi pia ya kujifunza. Leo ningeweza kuwanukuu wanafalsafa wengi sana lakini nataka suala hili niliongelee kwa lugha nyepesi mjomba wangu daktari...

  Mjomba, unadhani kwa nini mwananchi huyu yuko hivi?

  Kwanza, ni mfumo wa 'ndiyo mzee': Mfumo huu huanzia katika ngazi ya familia, malezi ya familia zetu hutuzuia kuhoji, mila na destruli zetu hutuzuia kuhoji. Wewe unakumbuka nilipohoji katika kikao kimoja pale kijijini kwa nini kila akichinjwa mbuzi au ng'ombe 'wazee' wale nyama laini ya mgongo na paja wakati wanawake wanakula utumbo na vijana wale mbavu? unakumbuka makalipio yaliyonipata? Wakasema mimi 'usomi' umenipotosha, ooh mara mi mlafi ati naingilia 'haki' ya wazee, nisubiri nami nikizeeka ati. Je unakumbuka pia nilipohoji kwa nini wanawake wale chakula jikoni wakati wanaume wanakula kwenye meza unakumbuka fimbo nilizopata toka kwa mzee ukaniokoa wewe? Huo ndiyo mfumo uliojengeka ambao mimi niliupinga mapema. Mila na malezi yetu yanatuandaa tuwe watu wa mapokeo.

  Unakumbuka nilivyomuhoji mchungaji kwanini Yesu alipaa bila mbawa? Unakumbuka nilikaribia kuondolewa kanisani kwa kuwa 'nimepotoka' , kuhojihoji kwangu ndiko kulikonifanya mzee aniite 'mtulutumbi' kwa maana kila niliporudi kijijni nilimchallenge kwa falsafa nilizosoma shule na kimsingi hakujua kuwa kunisomesha ina maana aliniandaa nitofautiane naye na mtu mwingine wa kijijini katika kufikiri, tuyaache hayo, lakini ili watanzania waanze kuhoji hoji, ni lazima tuanzie katika mila na ngazi ya familia, watoto waruhusiwe kuhoji na wapewe majibu ya uhakika.

  Pili, toka enzi za uhuru, kwa kuwa hatukumwaga damu basi watu walimwona Nyerere kama Malaika. Unabisha? Umesahau kanisa katoliki lilipendekeza apewe heshima ya 'Utakatifu'? Sijui walishampa au la lakini ninachoongelea hapa ni kuwa katika mfumo wa kufanya maamuzi, japo walisema ni demokrasia lakini watu wote macho yalikuwa kwa Nyerere. Kama ilivyokuwa kwa mkoloni kuwaamrisha kulima mashamba yao wenyewe bila ujira au kwa ujira mdogo tu kisha mazao yote ya mkoloni na tena wakalipa na kodi na wakaitikia 'Ndiyo mzee' huku wakiimba nyimbo za 'Mungu mbariki mkoloni' sijui kutawaliwa na wakoloni kuliitawala akili yetu mjomba yaani hata sijui kwani mawazo hayo hayo ya ndiyo mzee yakahamishiwa kwa Nyerere na kwa kuwa viongozi wengi wa kisiasa kuanzia mwenyekiti wa kijiji walikuwa wakimwakilisha Nyerere basi kila walichosema kiongozi kasema Nyerere.

  Kama unabisha, post hii tazama
  Nyimbo nitaimbishwa, Nyerere kumsema
  Naweza aibishwa, ati mi si mwema

  Kwa sababu tu, Nyerere ni malaika
  Alitenda mazuri tu, hana alipopotoka
  Basi tumpe sifa tu, apumzike kwa rabuka!


  Hali hii ya 'kutomsema' Nyerere ni ushahidi tosha kuwa msingi uliojengeka ni wa 'hewalaa' pasipo kupewa nafasi ya kuhoji. Hali hii imemjenga mtanzania kuwa mtumwa wa fikra za viongozi. Hali ambao ukihoji tu ati unatishia 'usalama wa taifa' na wala usije kushangaa nami natafutwa kuhojiwa na polisi mjomba. Hii ndiyo maana hata ulipojieleza kuwa umegoma ili upewe mazingira mazuri ya kumuhudumia mtanzania;

  Kiongozi alipoongea, aliaminiwa
  Wewe ulipoongea, Ulilaumiwa
  Kila uliloliongea, ulilaaniwa

  Wakakuita mbinafsi, usiyewajali wenzako
  Waijali yako nafsi, si maadili fani yako
  Ati umeitupa nafasi,umeivunja miiko


  Huyu ndiye mwananchi uliyekuwa unamtetea mjomba!

  Tatu, hadi sasa serikali inaendelea mtindo wa kuwatawala wananchi kifikra
  Nina mifano kadhaa, moja mwaka fulani nilihudhuria kampeni za CCM, katika jimbo hilo ambalo chama cha upinzani kilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda, uelekea mwishoni mwa kampeni CCM ikaleta malori, Kofia, vitenge, chumvi na mgombea aliwanunulia wazee pombe ya kienyeji na ile bendi ya CCM na wanenguaji wake wakakata viuono. Matokeo CCM ilishinda kwa kishindo mjomba
  Nikawa najiuliza; Je Pombe ziliwalewesha wananchi wakawa hawaoni vizuri karatasi ya kupiga kura?
  Je, t-shirt za 'mchina' walizovaa ziliwabana mikono kuilekeza kwa mgombea wa CCM?
  Je, vitenge walivyofunga akina mama viliwabana viunoni na kuwaelekeza kupigia kura CCM?
  Je, chumvi waliyokula kabla ya uchaguzi iliwadumaza akili, wakaona picha ya CCM tu?
  Au ni viuno wa wana TOT viliwachanganya akili? Si unajua tena watanzania kwa mambo yetu yalee....
  Basi sijapata jibu hadi leo!

  Lakini falsafa yangu ni kuwa Watanzania wanaridhika sana na faida au wema wa muda mfupi huku wakisahau madhara yatakayojitokeza baadaye. Hii ndiyo sababu ulipogoma mjomba kila mtu aliyeugua homa alitaka urudi kazini pasipo kujali anaweza kupata tatizo litalohitaji huduma ya muda mrefu kama vile kisukari au hata Hypertension na kama mazingira ya kazi hayajaboreshwa madhara yake ni ya muda mrefu. Yeye alitaka siku hiyo anayoumwa atibiwe basi! Akawa anaangalia wagonjwa waliolazwa sasa pasipo kuangalia ni wangapi watalazwa baadaye iwapo hali ya afya nchini itabaki kuwa hivi hivi kwa miundombinu afya hii hii.

  Nne, mjomba watanzania ni WABINAFSI. Kama hukujua hili basi tambua leo
  Hujifikiria wenyewe, daktari sawa na roboti,
  Huna familia wewe, inayohitaji sapoti
  Huugui wewe,wala hutaki noti


  Huyu Mtanzania huyu mjomba,
  Yeye ahudumiwe, Hata kama una njaa
  Bora tiba apewe, basi asikia rahaa
  Hata posho usipewe, kwake mambo mwaa

  Vipimo usimfanyie, bora dawa andika
  Nafuu ajisikie, arudi kwake Tandika,
  Kwa Lipi akusifie, mshahara wa mashaka?
  Huduma mpatie,ajua huwezi choka!


  Ubinafsi huu mjomba ndiyo uliosababisha kashfa nyingi kama Dowans, Richmond na kadhalika. Ubinafsi huu ukichanganywa na tabia na mila za kutohoji umefanya watanzania wahalalishe GIZA la kila mara. Juzi niliongea nawe nikasikia muungurumo ukanambia majenereta yanashindana kuunguruma kama kwaya za kwenye tamasha la injili. Umeme kwa mfano, unahitajika mahospitalini ili huduma kama za upasuaji na usafishaji wa vyombo vya hospitalini ufanyike. Maji yanahitajika ili huduma za hospitalini ziendelee.

  Mwananchi huyu mbinafsi, uliyekuwa unamtetea, hata haoni madhara ya sekta nyingine katika huduma za afya.

  Yeye anaona ndugu yake akifariki kwa kuwa huwezi kufanya operesheni theatre hakuna umeme, ni haki yake ya msingi
  Kutumia kibatari mjini Dar Es salaam karne ya 21, akapata magonjwa yatokanayo na moshi au akaungua moto. Ni haki yake ya msingi.

  Kuogea makopo wakati kuna bomba bafuni linaleta hewa tu, makopo yaliyojaa fangasi na vimelea vya magonjwa,ni haki yake ya msingi.

  Kupata 'Noise pollution' utokana na miungurumo ya jenereta , ni haki yake ya msingi.

  Kubanana kwenye daladala akapata magonjwa ya kuambikizwa mpaka chawa, ni haki yake ya msingi.

  Ati huyu huyu ndiye uliyekuwa unamtetea

  UMEPOTEZA MUDA WAKO MJOMBA

  Mjomba daktari kama mganga wa kienyeji

  Unakumbuka nimekufananisha na mganga wa kienyeji au babu wa loliondo huko awali?


  Sina lengo la kukukosea heshima hata kidogo. Lakini hebu fikiria, machine ya x ray wilayani kwako ni mbovu toka mwaka juzi; Je, mgonjwa unayehisi kavunjika mbavu utafanyaje kuwa na uhakika? Stethoscope yako siku hizi inapima malaria kama hakuna reagent maabara? Nasikia Ukimwi siku hizi umepamba moto huko, Je, hao akina mama hapo labour ward unawazalishaje kama hakuna glovu? huyo mama mwenye 'Pregnancy induced hypertension' unampa panadol badala ya magnesium sulphate? Je maiti pale mochwali unazitunzaje kama hali ndo hii? Kama jibu ni hapana kwa moja wapo ya maswali haya rahisi basi wewe ni mganga wa kienyeji, tofauti tu ni kuwa huna tunguli. Nakuahidi nitakutafutia mjomba tena lenye bendera ya taifa kwa kuwa naja wewe ni mzalendo kuanzia ngozi hadi moyo.
  Wamama sakafuni, wamelaliana
  ICU huwaoni, hapo amana?
  Utawapa nini, kama dawa huna?


  Mganga wa kienyeji anakuzidi kwani microscope yake ni tunguli, vibuyu vimejaa ukerewe anaweza kuagiza
  Quinine zake ni mitishamba, bado tuna mapori singida anaweza kwenda kuchimba
  Wagonjwa wake wakija,awe bosi au masikini ataingia kwenye kijumba kidogo kikuukuu
  Wewe mabosi wako si wanatibiwa India?
  Ndugu za mabosi wako si wanakuja na vimemo na wewe unawatibu haraka haraka? mabosi hao hao ambao wanakalia nafasi za kusoma huko wizarani....Nafasi za kusoma nje ya nchi zipo lundo waizarani unajua nani anaenda?

  Wewe ni mganga wa kienyeji mjomba, nitakuletea ngozi ya mbuzi hapo hospitalini kwako utibie!

  Tatu, unajua kwa nini hata wataalamu wetu siku hizi wanaishia kufanya tafiti za Prevalence tu?

  Najua hulijui hili mjomba, acha nikutonye, watafiti wengi wa kitanzania wanfanya case studies na prevalence studies!


  Kati ya tafiti kumi utakazo soma za watanzania, 8-9 ni za prevalence na KAP, mara prevalence of HIV, mara knowledge attitudes and practices of....Kiufupi ni tafiti zinazoelezea tatizo bila kutafuta mbinu sahihi za kutatua tatizo.Utasikia prevalence of anemia kwa wato wachanga badala ya a randomized controlled trial of substance x in treatment of anemia. Hali hii ya kufanya tafiti za kuelezea tatizo zimefanya kwanza:


  • Tafiti nyingi za watanzania kutokuwa na tija au kuongeza maarifa mapya
  • Si ajabu kumwona hata profesa anafanya prevalence study badala ya kufanya randomised trial


  Unajua kwanini naongelea haya? Namaanisha hata wasomi wetu hawana mchango stahili kwa taifa letu. Kwani Mponda hana PhD? Kikwete hana PhD (japo ni ya shortcut)? Lucy Nkya hana elimu?. Iwapo wanayo kwa nini unawalaumu leo kuwa hawaongozi vizuri? Kwa nini wameng'ang'ania madaraka hadi leo-Jibu ni lile lile-Nina wasiwasi mkubwa na uwezo wa wasomi wetu kufikiri! Ndiyo maana profesa anafanya prevalence ya HIV, kwa kuwa ama hana uwezo wa kufikiri au hawana uwezo wa kuzifikirisha akili zao kwa uwezo wake. Kisha wanalalamika ati tafiti zao hazitumiki kutengeza sera Tanzania. Hivi waweza kutumia utafiti wa kupima kiwango cha chumvi baharini kutengeneza undeground tunnel kwenda Zanzibar wakati maji chumvi waweza kuyapima hata kwa ulimi?

  Kuna aina mbili za kufikiri mjomba:

  Kwanza ni kufikiri kuhusu jambo fulani kwa uwezo wa kawaida tu "common sense" wa kila binadamu na ukifikiri vizuri kidogo basi hii huitwa busara, yaani uwezo wa kufikiri na kutoa fikra njema kwa uwezo wa kawaida wa kiakili kuliko watu wengine wenye uwezo sawa na wako. Hii ni tafsiri yangu ya busara mjomba.

  Aina ya pili ya kufikiri, ni uwezo wa kuifikirisha akili yako kufikiri kwa kiwango chake stahili. Kiwango chake stahili hapa humaanisha uwezo wa kielimu. Kama mtu ana PhD katika afya ya jamii naamini anaweza kufikirisha akili yake kwa kiwango chake stahili na akapata solution na hawa ndiyo tunaowaita 'mapioneer au wanafalsafa .
  Kwa hiyo kama mtu ana PhD halafu anafanya mambo uliyonisimulia na bado anang'ang'ania madarakani basi huyu hana busara wala haifikirishi akili yake kwa kiwango kinachohitajika kufikiri na hiyo PhD si yake kwani ni sawa na Professor anayefanya tafiti za prevalence au knowledge, attitudes and practices (KAP) ambazo zatakiwa zifanywe na wanafunzi.

  Mjomba, nasikitika kuwa nawe umenaswa katika mtego wa wanasiasa. Japo najua umetumia busara kurudi kazini lakini unarudi kazini ukiwa na vidonda vibichi. Bado faida ya kugoma kwako haiko wazi.
  Kwa maana wakati kima cha chini cha mshahara kwa mfanyakazi katika nchi moja ya majuu niliyotembelea ni dola 8 kwa saa, mjomba wewe unalipwa dola 12 kwa masaa 24 ya calls.

  Hapo hujaweka;
  Gharama ya kumkosa mkeo ambayo unajiweka katika hatari ya kulea watoto wasio wako.
  Gharama ya kung'atwa na mbu mjomba ukaugua Malaria na bado Bima yako ni sawa na ya mwanapollo wa Mererani
  Gharama za kuambikizwa magonjwa unapomhudumia mgonjwa ukiwa na usingizi
  Gharama za msongo mawazo wa kumkosa mkeo usiku.

  Katika vita mjomba, ukiamua kushambulia shambulia hadi ushindi. Kurudi nyuma bila kuwa na mbinu mbadala yenye nguvu zaidi ya awali ni kumpa nafasi adui kukushinda. Kama nilivyosema najua umetumia busara, yaani uwezo wako wa kufikiri kwa akili ya kawaida au common sense. Kwa maana hiyo umefanya jambo jema na la kupongezwa japo umenasa kwenye mtego wa ahadi za Wanasiasa!

  Mjomba wanasiasa wameiharibu nchi yetu! Mchango wa Siasa katika Nchi hii HAUONEKANI mjomba!

  Tanzania ilikuwa mahali pazuri, sawa pamekuwa kama kuzimu
  Japo kuna magari mazuri, ni ya wachache wanaharamu,
  Wao kila siku waishi swari, masikini waishi kama mizimu
  Umasikini kwao si habari, viyoyozi kwao kitu muhimu


  Hivi mjomba nikuulize, hivi kama asilimia 98 ya watu wanaokuzunguka ni mafukara, wewe unajisikiaje?
  Kanisani waenda kufanya nini?
  Kama posho zote Bungeni
  Waongeza mara ishirini?
  Huwaoni masikini?


  Hivi mjomba maisha huchagua kuwa magumu, kwa watu wenye vyeo fulani?

  Kuna wakati mjomba najiuliza maswali mengi, machozi yajaa machoni!
  Naipenda nchi yangu, wala siwezi kuihaini
  Watanzania wenzangu, hata siwezi kuwalaani
  Kila siku moyo wangu, waumia uchunguni
  Hata ndoto zangu, naona tu manyani
  Yasojali wenzangu, yaso na haya usoni
  Yadhurumu ndugu zangu, nyoyo zao za Nyani
  Hakika njomba wangu, Sitafika msibani
  msiba wa adui yangu, fisadi muhaini!


  Mjomba nikuache kwa kashairi haka ka kimombo, naamini bado wakikumbuka toka Medical School mjomba!

  A shoe less leg, a no-mattress bed


  A roofless house, a crop-less farm
  An empty pocket, a numberless check
  A man's slave, a victim of fate
  A nearly dying body, leaving no tales
  Worthless on Earth, a worry-less mind
  Burdens to carry, like a horse's hoof
  An Injustice of mortals, exploit of men
  Death it awaits, a citizen of paradise
  Poor on the Globe, a heaven's allures
  Mtulutumbi on Earth, a king in heaven!

  Salamu zangu zikufikie mjomba Daktari

  Nisemehe kama kuna makosa ya kisarufi mjomba, muda umenitupa mkono
   
 2. IsangulaKG

  IsangulaKG Verified User

  #2
  Jul 14, 2012
  Joined: Oct 14, 2010
  Messages: 702
  Likes Received: 90
  Trophy Points: 45
  Shukrani mkuu kwa kuukumbushia huu uzi!
   
 3. babalao 2

  babalao 2 JF-Expert Member

  #3
  Oct 25, 2014
  Joined: Apr 6, 2012
  Messages: 4,218
  Likes Received: 1,270
  Trophy Points: 280
  Ukihoji utendaji wa Nyerere unatishia usalamawa Taifa.
   
 4. Obama wa Bongo

  Obama wa Bongo JF-Expert Member

  #4
  Oct 25, 2014
  Joined: May 10, 2012
  Messages: 4,767
  Likes Received: 2,494
  Trophy Points: 280
  mlozi mtulutumbi wa jf
   
Loading...