Buriani Balozi Christopher Pastory Ngaiza | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Buriani Balozi Christopher Pastory Ngaiza

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Felixonfellix, Apr 30, 2010.

 1. Felixonfellix

  Felixonfellix JF-Expert Member

  #1
  Apr 30, 2010
  Joined: Feb 16, 2010
  Messages: 1,680
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135


  [​IMG]
  Padri Privatus Karugendo​
  Aprili 28, 2010[​IMG]
  MWAKA jana siku chache kabla ya Krisimasi nilisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Karagwe. Ndege yetu ya kutoka Mwanza kwenda Bukoba, ilishindwa kutua Bukoba kwa sababu ya hali mbaya ya hewa.
  Tulilazimika kurudi Mwanza, kusubiri mvua iliyokuwa ikinyesha mjini Bukoba ikatike. Tulikaa Mwanza, kama saa mbili hivi ndipo tukajaribu tena kuruka kwenda Bukoba. Abiria wawili ambao kama hali ya hewa ingekuwa nzuri kule Bukoba tusingesafiri nao; waliungana na sisi kwa jaribio letu la pili la kuruka kwenda Bukoba.
  Mmoja kati yao alikuwa Balozi Christopher Ngaiza, ambaye alikuwa anasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda kijijini kwao Kamachumu kuwahi mazishi ya mama mkwe wake. Tulikuwa hatujaonana kwa siku nyingi, hivyo tulikuwa na mengi ya kuzungumza. Mungu alitusaidia tukatua Bukoba salama.
  Safari ya ndege kutoka Mwanza kwenda Bukoba ni kama dakika 45 hivi; unaonekana kuwa muda mfupi sana lakini kwa vile ndege hii ndogo inayobeba abiria 12 inaruka juu ya Ziwa Victoria muda wote wa safari, kuna dalili za kuogopa na kuwa na mawazo mengi kiasi kwamba muda huo mfupi wakati mwingine unaonekana kuwa mrefu sana. Bahati nzuri nilikaa kiti kimoja na Balozi Ngaiza, maongezi yetu yalitusaidia kusahau kuangalia chini, hivyo mawazo na kuogopa kwamba tunaruka juu ya Ziwa Victoria yalipotea kabisa! Na kweli muda wa safari ulikuwa mfupi.
  Mbali na mambo ya siasa, Balozi Ngaiza, alinielezea juu ya miradi yake anayoifanya kule kijijini kwao Kamachumu: Hoteli ya Kamachumu Inn, kiwanda cha mikate na kiwanda cha kusindika maji na kwamba amekuwa akishirikiana na wadau wengine wa sekta ya utalii kutangaza vivutio vya utalii vya Mkoa wa Kagera. Ni kati ya Watanzania wachache wanaostaafu na wakakubali kurudi vijijini kwao, kuishi na kuwekeza.
  Miradi yake ilikuwa imetengeneza ajira kwa vijana wa Kamachumu na kutengeneza soko la mazao mbalimbali kwa wakulima. Wale waliolima nyanya na mboga mboga nyingine walipata soko kwenye hoteli yake ya Kamachumu Inn, pamoja na kwamba Kamachumu Inn, ilizalisha ajira kwa vijana na watu mbalimbali kutoka karibu na mbali, lilikuwa ni soko la ndizi, mayai, kuku, nyama ya mbuzi na ng’ombe nk. Mradi ulionivutia zaidi ni ule wa kusindika maji yenye jina la Kabanga.
  Huu umeleta mabadiliko makubwa Bukoba. Ingawa kiwanda hiki hakijafanikiwa kutosheleza mahitaji ya maji ya kunywa (kwenye chupa) ya Mkoa wa Kagera, kuwapo kwake ni changamoto kubwa kwa wasomi wetu wanaosoma na kukataa kurudi vijijini.
  Mambo ya kuzungumza na Balozi Ngaiza yalikuwa mengi, muda ulikuwa mfupi. Tuliagana pale uwanja wa ndege wa Bukoba, yeye akaenda zake Kamachumu, mimi Karagwe. Afya yake ilikuwa nzuri na nilimshukuru Mungu, kwa kumpatia afya njema katika umri mkubwa wa miaka 80. Hivyo kifo chake, mwezi uliopita kimekuja kama mwizi wa usiku.
  Siandiki tanzia hii kumlilia Balozi Ngazi, nina imani ana wengi sana wa kumlilia! Ingawa nina sababu zote za kumlilia maana alikuwa rafiki, ndugu na Mtanzania mwenzangu, sina wajibu wa kumlilia kwa kuandika tanzia. Niandike nini juu yake? Niandike nini ambacho hakifahamiki na hakikuandikwa na wengine wengi waliomlilia kwa njia mbalimbali pamoja na kuandika tanzia?
  Ni nani asiyefahamu kwamba yeye aliitumikia Tanzania maisha yake yote? Alianza utumishi wake kama hakimu wa halmashauri ya Bukoba kati ya mwaka 1952 na 1953, na baadaye kuwa Meneja wa Chama cha Ushirika wa Walaji wa Buhaya. Pia wakati huo alishiriki kuisimika TANU Mkoa wa Kagera; aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kama Marekani, Uingereza, Uholanzi, Zambia, Botswana, Swaziland, Misri, Sudan, Syria, Umoja wa Falme za Kiarabu na Umoja wa Mataifa. Aliiwakilisha Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 na pia katika Shirika la Maendeleo ya Bonde la Mto Kagera lililokuwa na makao yake makuu mjini Kigali, Rwanda. Ukiangalia mchango wake, huyu ni mtu aliyestahili mazishi ya kitaifa!
  Siandiki tanzia hii kutaja sifa za elimu ya Balozi Ngaiza. Ni nani asiyefahamu kwamba huyu ni miongoni mwa Watanzania wa kwanza kuhitimu Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda? Ni nani asiyefahamu kwamba huyu ni kati ya Watanzania wachache walioitumia elimu yao kubaki nchini. Angeweza kuikimbia nchi kwenda kufanya kazi nje kama walivyofanya wengine.
  Hivyo siandiki tanzia hii kumlilia Balozi Ngaiza, yeye amepumzika na Mungu Mwenyezi mwenye huruma ampumzishe mahali pema peponi! Amina! Naandika tanzia hii kutekeleza lile ambalo Yesu wa Nazareti aliwaambia waliokuwa wakimlilia kwamba wajililie wao na vizazi vyao. Naandika tanzia hii kulilia utamaduni wa kishenzi tunaoujenga na kuusimika nchini.
  Mbali na Wilson Masilingi, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM) na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, hakuna viongozi wengine wa Mkoa na Kitaifa waliofika kwenye mazishi ya Balozi Ngaiza. Hakupata mazishi yanayolingana na mchango wake mkubwa. Hili ndilo la kulilia, hili ndilo la kuandikia tanzia!
  Matatizo aliyoyapata Balozi Ngaiza ya kuhusishwa na mpango wa mapinduzi ambao haukufanikiwa, uliosababisha awekwe kizuizini kwa muda, yalikwisha kusafishwa. Baada ya kutoka kizuizini Balozi Ngaiza aliamua kuingia kwenye siasa na biashara; alijiunga na chama cha upinzani cha United Democratic (UDP) chini ya John Momose Cheyo, mwaka 2000 akagombea ubunge katika Jimbo la Muleba Kaskazini kupitia chama hicho na hakufanikiwa kushinda.
  Baadaye aliamua kurudi CCM. Mwaka 2005 aliweza kuibuka mshindi wa kwanza katika kura za maoni, lakini jina lake lilienguliwa katika kikao cha kuteua wagombea mjini Dodoma na ndipo alipoamua kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Aligombea tena Kiti cha jimbo la Muleba Kaskazini, mizengwe ikapikwa kwa nguvu zote, akashindwa!
  Wakati wa mazishi yake Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema: “ Ndugu waombolezaji, nawaomba sana mjifunze jambo kutoka kwa baba yetu. Mimi nilikutana naye mara ya kwanza mwaka 2005, lakini ilinichukua muda mfupi sana kufahamu uadilifu wake, unyenyekevu, upole na uanadiplomasia wake, jambo ambalo si kawaida kwa watu wengi”.
  Hizi ni sifa za Balozi Ngazi, mwadilifu, mnyenyekevu, mpole na mwanadiplomiasia mahiri, ambazo hakuna anayeweza kuzikana iwe CCM, serikalini, kanisani, nje na ndani ya nchi hata kijijini kwake Kamachumu. Sifa hizi pamoja na utumishi wake wa miaka mingi katika Taifa, zilitosha kumpatia mazishi ya kitaifa ambayo hakuyapata kwa sababu ya dhambi kubwa aliyoifanya ya kukihama Chama cha Mapinduzi.
  Huu ndiyo nimeubatiza utamaduni wa kishenzi. Tumejenga utamaduni na tunausimika katika Taifa kwamba kuhama Chama Chama cha Mapinduzi ni dhambi. Au kwa maneno mengine ya kizushi: kutokuwa mwanachama wa CCM ni dhambi! Mtu anaweza kufanya mema mengi kwa Taifa, lakini akihama Chama cha Mapinduzi kujiunga na Vyama vya Upinzani anapoteza sifa zote na heshima anayokuwa amejijengea kwa miaka yote kama ilivyojitokeza kwa Balozi Ngaiza.
  Sifa za Balozi Ngaiza, ndizo sifa tulizozizoea katika Taifa kwa wale waliopata mazishi ya heshima na kutunukiwa heshima ya utumishi wa nchi uliotukuka. Heshima hii haifuati chama cha siasa, haifuati dini ya mtu, haifuati jinsia ya mtu, haifuati rangi wala kabila la mtu. Ni heshima ya uzalendo, heshima ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu! Awe mwanamichezo, awe mwalimu, awe daktari, awe askari, awe mwanasia, anayetoa mchango wa kutukuka katika Taifa atukuzwe awe hai au marehemu!
  Je, tuamini kwamba wanaobaki CCM hadi mwisho ndio wazalendo wa kweli? Tuamini kwamba utumishi uliotukuka uko ndani ya CCM peke yake? Tufumbe macho tusione maovu yanayotendwa na baadhi ya wana CCM? Tuamini kwamba kukihama CCM ni dhambi? Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40, wanachama wa CCM ni karibia milioni tano hivi, hawa ndio watakatifu wa Mungu? Hawa ndio wazalendo peke yao? Hawa ndio wenye nchi? Ina maana gani kuwa na vyama vingi vya siasa? Ina maana gani kama chama kinachotambulika kwa uzalendo ni CCM peke yake? Tuna Watanzania wangapi ambao si wanachama wa CCM, na wanalipenda Taifa kiasi cha kujitoa muhanga?
  Utamaduni huu wa kutanguliza chama cha siasa mbele ya kila kitu, utamaduni huu wa kukifanya chama cha siasa ni kigezo cha kuwaenzi mashujaa wa Taifa, utamaduni huu wa kufikiri kwamba chama cha siasa ni uzalendo, ni utaifa, ni utamaduni wa kishenzi.
  Ni lazima ajitokeza mtu au kikundi cha watu kulisema hili. Vinginevyo Taifa linaelekea pabaya. Ni lazima tujenge Taifa ambalo kila mtu ana haki sawa. Taifa ambalo vyama vyote vya kisiasa vina haki sawa, taifa ambalo dini zote zina haki sawa. Taifa ambalo linaheshimu mchango wa kila mwananchi bila kuangalia anatoka nyumba gani. Tukishindwa kufanya hivyo tutalazimika kujililia sisi na vizazi vyetu badala ya kuwalilia wale waliotangulia mbele ya haki kama Balozi Christopher Ngaiza.
  Pamoja na ukweli kwamba Balozi Ngaiza, hakupata mazishi ya kitaifa; familia yake, Watanzania wenye mapenzi mema na watu wote walioonja utumishi wake ndani na nje ya nchi hawawezi kumsahau; watamkumbuka na kuendelea kumpenda ndani ya mioyo yao na kufuata kadiri wanavyoweza mema yote ambayo Balozi Ngaiza alitenda wakati wa uhai wake. Mungu, ailaze mahali pema peponi roho ya Balozi Christopher Pastory Ngaiza. Amina!
   
 2. N

  Nasolwa JF-Expert Member

  #2
  Apr 30, 2010
  Joined: Jun 12, 2008
  Messages: 1,830
  Likes Received: 43
  Trophy Points: 145
  Rip balozi ngaiza
   
Loading...