Bora Kikwete amalize aondoke

Elly B

JF-Expert Member
Jan 11, 2011
1,194
906


UKISIKILIZA vizuri hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya mwisho wa mwezi uliopita kuhusu kukwama kwa Bunge la Katiba, lazima utamwombea kila aina ya dua kwa Mwenyezi Mungu, kwamba afadhali amalize kipindi chake apishe rais mwingine mwenye umakini na maisha ya wananchi.

Niliwahi kusema kwamba iko mizaha ya kufanywa na viongozi kwa wananchi wanaowatawala, lakini inapaswa kuwa na kiasi. Wakati mwingine huwa najiuliza maswali ni wapi hasa mipaka ya taasisi ya urais inaishia.

Nimemsikiliza Rais Kikwete vizuri lakini nitakuwa wa mwisho kuamini kile alichokisema kwamba hausiki kwa namna yoyote na kukwama kwa Bunge Maalum la Katiba.

Huu ni utani uliopita kiasi usiopaswa kufanywa na kiongozi mkubwa kama yeye. Hapa hakuna neno jingine zaidi ya kusema anaidhalilisha taasisi ya urais.

Laiti Rais Kikwete angekuwa jasiri na mkweli mwenye dhamira ya dhati ya kuwapatia Watanzaia katiba mpya, ni dhahiri asingekubaliana na wahafidhina ndani ya CCM waliomwingiza mkenge wa kumshinikiza Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta kukanyaga kanuni ili kumtanguliza Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha rasimu yake.Kanuni ya 47 (g) na (h) ya Bunge Maalum inaeleza wazi kwamba alipaswa kutangulia Rais Kikwete, kulihutubia Bunge hilo na kisha Jaji Warioba awasilishe rasimu (kitendea kazi) ili wajumbe waanze kuijadili.

Lakini kwa uoga wa wahafidhina wa CCM, walitumia wingi wa wajumbe wao bungeni kumzunguka Sitta ili kumlazimisha Jaji Warioba, atangulie kuwasilisha rasimu yake kwenye Bunge ambalo kimsingi halikuwa limezinduliwa rasmi ili baadaye Rais aje kujibu mapigo.

Huu ni utoto wa kisiasa, ni ujinga uliopitiliza na unathibitisha ukomo wa fikra kwa chama tawala kongwe kama CCM. Hata kichaa katika hili lazima atabakia na swali kwamba Jaji Warioba aliwasilisha rasimu kwa watu gani ikiwa rais alikuwa bado hajalizindua rasmi Bunge la Katiba?

Haya sasa na katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete azidi kuchekesha wananchi kwamba haikuvuruga mchakato kama inavyodaiwa na wapinzani kwani siku ile alikuwa anatoa maoni yake kama Mtanzania.

Eti hiyo ndiyo ilikuwa sehemu muafaka kwake kutoa maoni yake kama walivyopaka fursa watu wengine kutoa maoni yao baada ya rasimu ya pili kutoka. Na kwamba kama kiongozi mkuu wa nchi alipaswa kutoa angalizo. Hapa ndipo hofu yangu iliongezeka zaidi na kuendelea kujiuliza tangu lini rais akaenda kulihutibia Bunge na kulieleza maoni yake binafsi? Rasimu baada ya kukamilika tume ya Warioba ilimpelekea akaipitia kwanza na kujiridhisha haina tatizo kwa mustakabali wa muungano wetu na hivyo akaisaini na kuagiza ikabidhiwe kwa Bunge la Katiba.

Sasa huu ukigeu geu wa hofu ya muundo wa serikali tatu zinazopendekezwa kuwa na shaka ulitoka wapi kwa rais ambaye si mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na kutoa kauli ya kuwatisha wananchi halafu anasema yalikuwa mawazo yake binafsi?

Nijuavyo rais akienda kwenye msiba wa mtu binafsi, kumtembelea mgonjwa hospitali, kuhudhuria sherehe kama harusi, kitchen party ya ndugu zake au akaenda disko, hayo yanaweza kuwa masuala yake binafsi kama sehemu ya jamii. Lakini popote anapokuwa kwa kofia ya taasisi ya urais, amebeba dhamana yetu hana mambo binafsi. Vinginevyo tunahitaji tafsiri ya mipaka ya urais.

Kama Rais Kikwete anasema pale bungeni ndipo palikuwa sehemu sahihi ya yeye kutoa maoni yake, lazima atueleze sasa kwamba kumbe hata Jaji Warioba aliwasilisha maoni yake wala si mapendekezo ya tume yake.

Tume ilikusanya maoni kwenye maeneo ya wazi ambapo wananchi walikusanyika na kueleza kile wanachotaka kiwemo katika katiba mpya, hata rasimu ya kwanza na pili ilipotolewa bado watu binafsi na makundi walipata nafasi ya kutoa maoni ama kila mmoja kivyake au kimakundi kupitia jumuiaya na taasisi zao. Lakini Rais Kikwete na wakubwa wenzake walipata fursa ya pekee ya kufuatwa na kusikilizwa tena kwa kwa faragha kila hatua iliyokuwa imefikiwa na pale tume walipoambiwa sawa ndipo walisonga mbele. Sasa rais wetu alikuwa wapi kutoona kasoro hizo na kushauri zirekebishwe kabla ya rasimu kukabidhiwa kwa ngazi ya Bunge la Katiba?

Kwa fikra mpya na pana naweza kukubaliana na Rais Kikwete kwamba anaweza asiwe na tatizo na muundo wa serikali tatu unaopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu anaona hali tete ya muungano uliopo baada ya yeye na viongozi wenzake kushindwa kulinda na kuitetea katiba ya nchi.

Lakini shinikizo kubwa lililoko ndani ya chama chake vile vile hana ubavu wa kulishinda. Maana viongozi wengi wa CCM na serikali wamejawa na hofu kubwa ya kutojua hatima yao baada ya katiba mpya kupatikana.

Wako wanaohofia kukosa vyeo ikiwa serikali tatu itapita, wako wengi wanatishika na miiko ya uadilifu na uwazi kwamba hawataweza kufanya ufisadi tena. Wale waliozoea kutumia madaraka yao kupeana ajira kindugu wanajua utakuwa mwisho wao huku wale waliofisidi rasilimali za umma wakati wa utawala wao wanahisi safari ya maisha yao itahitimishwa gerezani.

Hawa ndio wanakesha wakimzonga Rais Kikwete asikubali kabisa muundo wa serikali tatu kwa kisingizio cha hofu ya muungano kuvunjika. Lakini wanasahau kuwa kuendelea kujificha kwenye muundo dhaifu wa serikali mbili bila kutafuta ufumbuzi wake sasa, madhara yake yatakuwa mabaya baadaye.

Nalazimika kumwombea Rais Kikwete kuwa bora naye amalize aondoke, pengine Mungu anaweza kutupatika kiongozi mwenye maono kama Nyerere. Tafakari!


Source: Tanzania Daima
 
Back
Top Bottom