Sheria mpya ya madini kuanza kutumika ramsi Aprili mwakani
Na Kizitto Noya
WAZIRI wa Nishati na Madini William Ngeleja amesema sheria mpya ya madini itakamilika na kuanza rasmi kutumika Aprili mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri Ngeleja alisema kwa sasa izara yake inakamilisha sera ya sheria hiyo kabla ya kutengeneza muswada na kuufikisha bungeni kwa ajili ya kutungwa sheria.
"Bado tuko katika mchakato wa kukamilisha sera, lakini ni mategemeo yetu kwamba zoezi hili tutalikamilisha mwishoni mwa mwaka huu na sheria nyenyewe iwe tayari ifikapo Aprili mwakani,"alisema.
Waziri Ngeleja alisema hayo alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari aliowaita ofisini kwake kuzungumzia hatma ya mgodi wa almasi wa Williamson Limited (Mwadui).
Alisema katika sheria hiyo mpya, serikali inapitia vipengele mbalimbali kuhakikisha haiwabani kukindi cha watu na kuwapa unafuu wengine bali iwe ni sheria inayojali maslahi ya taifa kwa kuhakikisha matumizi ya rasilimali zake yanakuwa kwa faida ya wananchi.
Maandalizi ya sheria hiyo mpya ya madini yametokana na kazi ya kamati aliyoiunda Rais Jakaya Kikwete Novemba 12 mwaka jana kupitia mikataba yote ya madini na kupendekeza maboresho ili rasilimali hiyo ya taifa ivunwe kwa manufaa ya nchi.
Rais Kikwete aliiagiza kamati hiyo iliyoongozwa na Jaji Mark Bomani kuchambua mfumo wa kodi unaotumika katika sekta ya madini na kupitia mfumo wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji mkubwa unaofanywa na serikali.
Kamati hiyo ambayo awali ilitakiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi mitatu, ilikuwa na jukumu la kukutana na taasisi zinazosimamia madini na wadau wengine, kupitia mikataba ya madini na nyaraka nyingine zitakazohusu migodi mikubwa nchini.
Mbali na Jaji Bomani, wajumbe wengine walioteuliwa katika kamati hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo.
Wajumbe wengine ni Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange, Kamishina wa Sera Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi Wizara ya Ardhi, Edward Kihundwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe.
Rais pia alimteua Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, Peter Machunde kutoka Soko la Hisa, Dar es Salaam (DSE), Mkaguzi wa Mahesabu kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Mahesabu, PriceWater Coopers, David Tarimo ambaye ni mtaalam wa masuala ya kodi na Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa, Wizara ya Katiba na Sheria, Maria Kejo kushirikiana na wenzao hao katika kazi hiyo.
Kuundwa kwa Kamati hiyo kunafuatia hoja binafsi ya Zitto Kabwe aliyoitoa bungeni kutaka kuundwa kwa Kamati Teule yakuchunguza mazingira ya kusainiwa kwa mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi huko Uingereza na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi Februari mwaka huu.
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Kabwe alifungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge hadi hapo Januari mwakani. Hatua hiyo ya Bunge iliibua mjadala mkubwa miongoni mwa makundi mbalimbali wakihoji sababu za kumfungia mbunge huyo kijana. Hivi karibuni wakati Rais Kikwete akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi katika Ukumbi wa Kizota , mjini Dodoma aliahidi kuunda kamati hiyo itakayojumuisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kuangalia mikataba mipya ya madini.
Tuma maoni kwa Mhariri
Facebook