SI KWELI MYTH Binadamu Anatumia Asilimia 10 Tu Ya Ubongo?

SI KWELI MYTH Binadamu Anatumia Asilimia 10 Tu Ya Ubongo?

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
The claim is rooted in traditional beliefs or stories but lacks scientific evidence or factual verification.
Dhana potofu: Binadamu hutumia asilimia 10 tu ya ubongo wao.

Ukweli: Uchunguzi wa picha za ubongo unaonyesha kuwa karibu kila sehemu ya ubongo ina kazi na inafanya kazi hata wakati wa kufanya shughuli rahisi.
1787118062726.jpeg
 
Tunachokijua
Binadamu tunatumia asilimia 10 tu za ubongo wetu?

Kwa mujibu wa Idara ya Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu (Neurology) katika Chuo cha Tiba cha UAMS, watu wasiokuwa na matatizo ya mfumo wa fahamu hutumia karibu ubongo wao wote. Ubongo huwa na shughuli muda wote, ukidhibiti kazi za mwili zinazofanyika kwa hiari na zile zinazotokea bila hiari. Huku kwa wastani, ubongo hutumia takribani asilimia 20 ya nishati yote ya mwili.

Kituo cha elimu ya sayansi, chuo kikuu cha Uingereza kinabainisha kuwa;

Ukweli ni kwamba binadamu hutumia karibu ubongo wake wote wakati wote, ingawa si neuroni zote hufanya kazi kwa wakati mmoja. Tafiti zinazotumia teknolojia za kisasa za upigaji picha za ubongo, kama Functional Magnetic Resonance Imaging (fMRI), zimeonyesha kuwa maeneo mbalimbali ya ubongo huwa na shughuli kulingana na kazi inayofanyika. Hata wakati wa usingizi, hakuna eneo la ubongo linalozimika kabisa.

Aidha, hoja nyingine inayopinga dhana ya asilimia 10 ni matumizi makubwa ya nishati ya ubongo. Ingawa ubongo unaunda takribani asilimia 2 tu ya uzito wa mwili, hutumia karibu asilimia 20 ya nishati ya mwili kwa watu wazima, na hadi asilimia 60 kwa watoto wachanga.

Kama tungetumia asilimia 10 tu ya ubongo, isingekuwa na mantiki kwa mwili kutumia nishati nyingi kiasi hicho kuendesha kiungo ambacho hakitumiki kikamilifu. Hii inaonyesha wazi kuwa dhana hiyo haina msingi wa kisayansi.

Namna watu wengi walivyoamini dhana hii.

Dhana kwamba binadamu hutumia asilimia 10 tu ya ubongo wake imeenea na kuaminiwa na watu wengi. Katika utafiti mmoja ulibainisha, kati ya asilimia 43 na 59 ya walimu kutoka sehemu mbalimbali duniani walisema wanaamini madai hayo ni ya kweli.

Utafiti wa mwaka 2013 nchini Marekani ulibaini kuwa 65% ya Wamarekani walikuwa wakiamini kuwa binadamu anatumia 10% ya ubongo wake.

Ni wapi ilipotokea nadharia hii?

Haijulikani kwa uhakika chanzo cha dhana kwamba binadamu hutumia asilimia 10 tu ya ubongo wake. Hata hivyo,makala iliyochapishwa na Medical News Today inazitaja zifuatazo kama sababu zilizopelekea dhana hiyo kushika kasi miongoni mwa jamii.

Moja ya maelezo yanayotajwa ni makala ya mwaka 1907 ya mwanasaikolojia William James, ambaye alisema binadamu hutumia sehemu tu ya uwezo wao wa kiakili, lakini hakuwahi kudai kuwa ni asilimia 10.

Dhana hiyo iliendelea kusambaa mwaka 1936 baada ya kutajwa katika kitabu How to Win Friends and Influence People cha Dale Carnegie. Pia, huenda ilichangiwa na ukweli wa kisayansi kwamba takribani asilimia 10 ya seli za ubongo ni neuroni, huku seli nyingine nyingi zikiwa za glia zinazosaidia kazi za ubongo.

Kadiri miaka ilivyopita, madai hayo yameendelea kurudiwa katika vitabu, vipindi vya televisheni na filamu, jambo lililoifanya iaminike na watu wengi licha ya kukosa ushahidi wa kisayansi unaounga mkono kuwa binadamu hutumia asilimia 10 tu ya ubongo wake.

Hitimisho

Madai ya kuwa mwili wa binadamu unatumia asilimia 10 tu ya ubongo si ya kweli ni dhana tu iliyojengeka miongoni mwa jamii kwa muda mrefu na kupewa nafasi mara kadhaa katika vituo vya habari na filamu.
Back
Top Bottom