Barua ya wazi kwa Waziri Mkuu: Tukiongeza haya tutazuia maambukizi zaidi

EJL

Member
Jan 14, 2012
83
54
Mh. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mh. K.Majaliwa (MB)

Binafsi ninatambua jitihada kubwa sana ambazo Serikali imekuwa ikifanya tangu kutokea kwa mlipuko wa COVID-19 duniani na hata baada ya kuanza kupata kesi hapa nchini. Serikali chini ya uratibu wako ukishirikiana na Mh. Ummy Mwalimu umeendelea kuchukua hatua kadhaa zinazofaa ikiwemo kutoa taarifa kwa umma, kuongeza vituo vya kutolea huduma, kuhimiza ushiriki wa wadau wengine, nk. Mh. Hongera sana na Mungu wa mbinguni awabariki maana mnatenda kwa sehemu yenu.

Mh. Waziri Mkuu, pamoja na jitihada kubwa mnazofanya za kuuhabarisha umma juu ya maambukizi ya Corona (namna unavyoambukizwa, dalili na mbinu za kudhibiti maambukizi) bado jamii kubwa ya waTanzania, hasa waishio pembezoni hawana taarifa za KUTOSHA na SAHIHI. Hivi karibuni kituo cha television ya Taifa (TBC) ilionesha habari ya wananchi wa kijiji kimoja kata ya Mkutupa wilaya ya Chamwino wakiwa hawajui kabisa kuhusu Corona wala uwepo wake hapa nchini.

Taarifa ya mwandishi wa TBC inashabihiana na ile ya msanii Emanuel Mgaya (almaarufu Masanja Mkandamizaji) katika kipindi chake (ingawa ilionekana anahoji kwa utani lakini waliohojiwa walionesha wazi kutofahamu kwa usahihi juu ya Covid-19). Taarifa hizi na nyingine zinatoa picha ya nini kinachoendelea huku mtaani na vijijini kwetu hivyo lazima tuchukue hatua zaidi.

Mh. Waziri Mkuu, kwa wananchi kuendelea kutopata taarifa za kina na sahihi tutarajie maafa zaidi. Ushauri kwangu kwako ni kufanya uamuzi wa makusudi kutenga fedha kidogo na kuendesha semina kwa wanahabari wote (mkazo zaidi uwe kwa walio katika Radio za kijamii ambazo kwa sasa ni nyingi chini kote) ili wawe na uelewa wa kutosha.

Pia wito wako wa wadau kuchangia mfuko wa kukabiliana na Corona uende kwa wamiliki wa vyombo vya habari (hasa wa radio za kijamii) hawa watoe muda kila siku katika radio, television (hata za mtandaoni) kuelimisha umma juu ya janga hili.

Kwa nini tuelekeze nguvu kwa vyombo vya habari na wanahabari?
Vyombo vya habari, hususani radio za kijamii ndizo kwa sasa zinazowafikia wananchi kwa urahisi zaidi. Wakati huu ambao hatuwezi kukusanyika kufanya mikutano ya uhamasishaji, jukwaa salama linalobaki ni vyombo vya habari. Aidha kwa sasa wako wanahabari ambao wanajitahidi kutoa taarifa ingawa ni dhahiri sio wote wenye uelewa wa kutosha kuhusu tatizo hili.

Binafsi nimejaribu kufuatilia mijadala ya baadhi ya radio na kukuta mtangazaji anajadili zaidi taarifa potofu za mtandaoni. Ikibidi ifike mahali radio na television zote za kijamii zilazimishwe kualika mtaalam wa afya mwenye ujuzi na maarifa kuhusu Corona/ Covid-19. Mh. Waziri Mkuu, wanasema "taarifa ni nguvu", tukiongeza wigo wa kuwafikia wananchi na taarifa sahihi, tutawafanya kuchukua tahadhali hivyo kupunguza kasi ya maambukizo.

Tupia Macho athari za Covid-19 katika maeneo mengine
Mh. Waziri Mkuu, tayari sisi wananchi tumeshaanza kuonja athari za uwepo wa Corona-19 katika uchumi. Pamoja na kuendelea kupungua kwa kipato cha mtu mmojamoja (hasa wale tunaotarajia kipato cha siku) lakini inaonekana kipato hiki kushindwa kumudu mahitaji.

Tayari kuna ongezeko la bei za bidhaa sokoni (si kwa vitakasa mikono tu) bali hata mahitaji mengine hususani bidhaa za chakula. Mh. Waziri Mkuu, tayari bei ya sukari imepanda sana hapa jijini Dar es Salaam. Kwa siku chache tu sukari imepanda bei kutoka Tsh. 2500 na 2600 hadi Tsh.3000 hadi 3500/ kwa kilo moja.

Wakati hii ikitokea hakuna taarifa zozote kwa umma kuhusu nini kimesababisha kwani uzalishaji unaendelea. Ombi langu kwa Serikali na kwako Mh Waziri Mkuu ni kuagiza mamlaka zinazohusika (kama Wizara ya Fedha) kuhakikisha hakuna mwanya kwa wafanyabiashara kupandisha bei za bidhaa holela. Pamoja na kuwa, nchi yetu inafuata mfumo wa soko huria, lakini bado Serikali inalo jukumu na mamlaka ya kudhibiti mfumuko wa bei.

Ikiwa leo tunazo kesi chache tayari sukari inapanda kwa asilimia 34.6, je tutakapokuwa na kesi mia kadhaa? Ni vema sasa Serikali ikachukua hatua za makusudi kudhibiti mfumuko wa bei. Na endapo ni lazima bei ipande kwa baadhi ya bidhaa basi, Serikali ione namna ya kuweka ruzuku au kufidia ongezeko hilo ili kutuwezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu.

PAMOJA KWA MSAADA WA MUNGU -TUTASHINDA CORONA!

Edna, JL
 
Back
Top Bottom