Barua Ndefu kwa Prof. Shivji (Mrejesho)

Ado Shaibu

Verified Member
Jul 3, 2010
99
225
BARUA NDEFU KWA PROFESA SHIVJI (MREJESHO)

Na Ado Shaibu

Kwa Profesa Issa Shivji,
Ustaarabu wetu adhimu wa Kiafrika tuliourithi toka kwa wahenga unatutaka vijana kuwa na heshima na kufanya maamkizi kwa wakubwa. Shikamoo Komredi Issa Shivji!

Ninakuandikia barua hii nikifahamu pasi shaka yoyote kuwa kamwe hautaishangaa. Kama ujuavyo, uandishi wa barua za namna hii una historia ndefu yenye mizizi yake tangu zama za kale za Uyunani za Mwanafalsafa Plato na hata karne nyingi kabla yake.

Ninakuandikia barua yangu kuuendeleza utamaduni huu jalili.
Jambo pekee linaloutia mshawasha mkono wangu kuandika barua hizi ni kiu yangu ya kutoa maneno yenye kufaa; maneno ya kuwatia moyo na kuwahamasisha wanyonge kama zilivyofanya barua nyingi katika historia ya Ulimwengu.
Mifano ya barua za namna hii ipo chungu tele na bila shaka mwanazuoni galacha wa aina yako lazima aifahamu.

Ni imani yangu kuwa bado unakikumbuka kile ambacho Patrice Lumumba, kiongozi wa Kongo alikifanya akiwa chini ya udhibiti wa waasi kabla ya uhai wake kupokwa kinyama kwa msaada wa mabeberu wa ng’ambo ambao sasa ndiyo wahubiri wetu wa haki za binadamu!

Lumumba hakuandika barua kwa siri kwenda kwa mkewe Pauline? Hakutuahidi wana wa Afrika kunako barua ile kwamba siku yaja kwa bara la Afrika kuiandika historia yake badala ya ile feki iandikwayo kwa kalamu za Washington, Brussel na London?

Unadhani kauli hii ya Lumumba ilikuwa maneno matupu na ndoto ya mchana ambayo haitotimia kamwe?

Unadhani bara la Afrika, licha ya utitiri wa waitwao wasomi, litaendelea kuwa likizo kifikra na kusubiri mustakabali wake upikwe toka ng’ambo?

Barua ya Lumumba si mfano pekee. Sina shaka hata kidogo kwamba bado unakikumbuka kile alichokifanya Komredi V. I. Lenin, yule mwanafalsafa, kiongozi na mwanamapinduzi wa Urusi umauti ulipomnyemelea. Hakuandika waraka kuhusu mustakabali wa Urusi ambao uliwatetemesha kwa hofu na kuwaogopesha kina Joseph Stalin na alivyoaga dunia wakahaha huku na kule ili maudhui yake yaliyokuwa kikwazo kwa ndoto yao ya kutamalaki yasijulikane kwa umma?

kama waraka tu hutetemesha waroho wa madaraka kwa kiwango hiki unadhani ni njia gani nyingine thabiti niwezayo kuitumia kuwasilisha hisia zangu zaidi ya hii?

Mfano mwingine ni ule wa barua za Mahtma Gandhi, baba wa taifa la India. Hazikusafiri barua za Gandhi, enzi hizo akiwa mwanasheria machachari Afrika ya Kusini, zikachanja mbuga, milima na mabonde hadi Urusi kwa mwanafalsafa wa Kirusi Leo Tolstoy?

Wewe na mimi tunafahamu kwamba utaratibu huu wa kuandikiana barua baina ya Gandhi na Tolstoy ndio ulionoa makali ya fikra za Mahtma Gandhi hasa kwenye falsafa yake ya uasi wa jamii dhidi ya mfumo kandamizi (Civil Disobedience).
Kuna raha gani kwa kijana mwenye hamu ya kuleta mapinduzi kwenye jamii zaidi ya kuifuata njia kama hii aliyosafiri Gandhi? Nijuze Tolstoy wangu!

Hata hapa nyumbani Tanzania, si unazikumbuka zile barua za ndugu Ali Nabwa, yule mwandishi mkongwe kutoka Zanzibar aliyekumbwa na mikasa ya kila namna ikiwemo kupokonywa uraia?

Si unakumbuka jinsi huyu bwana alivyozipenyeza barua zake kutoka jela pale Ukonga na kuonyesha madhila na vitimbi walivyokuwa wakikumbana navyo kwenye lile sakata la kesi ya uhaini kufuatia mauaji ya Rais Abeid Amani Karume?
Hivi karibuni nimezipitia barua zake, moja baada ya nyingine na kwa kweli zimenisisimua zidifu ya kifani.

Kwa hiyo, upokeapo barua hii, fahamu huu ni mwendelezo wa jadi hii ya enzi. Orodha ya waliowahi kuitumia jadi hii ni ndefu na ndani yake yumo pia mwandishi wetu nguli wa Kiswahili Shaaban Robert ( Rejea barua kwa nduguye Yusuf Ulenge zilizochapishwa kwenye kitabu cha ‘Barua za Shaaban Robert 1931-1958’ ).

Prof. Joseph Mbele, mtanzania anayefundisha Chuo Kikuu cha St. Olaf huko Marekani anasema, kutokana na ujumbe wake murua wa kimaadili, hiki ni kitabu kinachofaa kuwemo katika nyumba ya kila Mtanzania ili kisomwe na wazazi na vijana. Baada ya kukisoma na kuufaidi uhondo wake, nami nimekubaliana moja kwa moja na rai ya Prof. Mbele.

Hata ile barua ya Jenerali Ulimwengu kwa Rais Kikwete baada ya kuukwaa ukuu wa nchi mwaka 2005 nadhani bado unaikumbuka. Huwa naipitia tena ile barua na kwa kweli, mengi ya yale yaliyonenwa na Jenerali yangalipo hata sasa. Kwa kimombo, ningeweza sema, that was Jenerali at his best! Kwa hakika, yule alikuwa Jenerali Ulimwengu katika kilele cha ubora wake!

Pengine hapo ulipo unajiuliza kuhusu shabaha hasa ya barua yangu. Ngoja nikukumbushe kidogo Profesa wangu. Unaikumbuka ile barua niliyokuandikia mwaka jana? Ninamaanisha ile barua niliyokuhoji kuhusu alipo jemedari shupavu unayemtarajia kuirudisha misingi ya utu, usawa na ujamaa ambayo umekuwa ukiihubiri miaka nenda rudi kwenye maandiko yako na mihadhara ambayo wewe ni hatibu.

Kwenye barua ile, kama unavyoweza kukumbuka, niliweka wazi mashaka yangu kuhusu kuwepo kwa viongozi ambao kwa dhati ya mioyo yao wako tayari kuisimamia misingi ya utu na usawa.

Basi baada ya kuiandika barua ile, ambayo ilichapishwa kwenye gazeti hili ili iwafikie watu wengi zaidi, nilipata mwitiko wa aina tofauti kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu.

Wapo wachache ‘walionihusia’ kuwa ni hatari kuandika maandishi yanayotishia maslahi ya watu na kwamba nikiendelea na utaratibu huo, yanaweza kunikuta ya Keni Saro-Wiwa, mwanaharakati wa Kinaijeria aliyeonja umauti kwa kutetea wanyonge wa Ogoni huko Nigeria.

Unadhani hawa ningewapa jibu gani zaidi ya ile kauli mliyoitoa zaidi ya miongo minne iliyopita pale Mzee Msekwa (Akiwa Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) alipowaamuru kulifunga jarida lenu la kimapinduzi la Chechen a kikundi chenu cha kiharakati cha USARF enzi hizo mkiwa vijana machachari hapa Mlimani?

Mlitamka bayana: ‘’Watu wanaweza kuuawa; vyama vyaweza kufutwa; lakini, fikra za kimapinduzi hazifi kamwe. Fikra za kimapinduzi huishi milele!’’

Kulikuwepo pia na watu, tena hawa walikuwa wengi mno ambao waliniandikia na kuwasiliana nami kwa njia mbalimbali ili kunipongeza, kunitia moyo na kunipa changamoto juu ya kile nilichokiandika.

Miongoni mwao alikuwepo Ndugu Karim Hirji, Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili ambaye amewahi pia kufundisha vyuo vingi ikiwemo UDSM na Chuo Kikuu cha Calfornia.

Kwa kweli siuoni umuhimu wowote wa kumtambulisha mtu huyu kwako kwa sababu itakuwa ni sawa na kinda la ndege lizaliwalo leo kisha likatamani kumfundisha mamaye kuruka!

Kwani wewe na kina Zakia Meghi, Yoweri Museveni, Henry Mapolu, George Hajivayanis na wenzenu wengine wengi hamkusoma pamoja pale Mlimani mwishoni mwa miaka ya sitini na mwanzoni mwa miaka ya sabini?

Sasa huyu ndugu Hirji alipoisoma barua yangu kwako, aliniandikia maoni yake na kunikaribisha nyumbani kwake kwa mjadala zaidi.

Kwa maoni ya Prof. Hirji, wakati uulizaji wa maswali kama nilivyofanya kwako kuwa si jambo baya, vijana lazima tuelewe mambo mawili kabla ya kuiporomosha mvua yetu ya maswali.

Mosi, Ndugu Hirji anasema, hakuna majibu ya moja kwa moja kwa maswali mengi niliyokuuliza. Hivyo basi, vijana hatupaswi kutafuta majibu ya maswali yetu kwa pupa. Sharti tufanye utafiti wa kina.

Pili, Hirji anatuasa kuwa ingawa wazee kama yeye wangali bado na mchango mkubwa kwenye kutafuta majibu ya maswali yanayotusumbua vijana wa leo, si lazima kwamba majibu waliyoyatoa kipindi chao, yatumike sasa kama yalivyo kwa vile mambo mengi yamebadilika sana. Anatupa rai kwamba kilicho cha muhimu ni kwetu sisi vijana kujifunza kutoka kwao; wapi walijikwaa na wapi walikuwa sahihi.

Jambo lililo la msingi ni kwa vijana wa sasa kuketi chini na kuchambua kwa mapana safari ya wazee wetu na kujifunza yalo mabaya na mazuri. Tena kujifunza huko hakupaswi kuwa kwa mwigo wa kimakanika mithili ya mitambo. Tofauti na mitambo, binadamu aliye na upeo sharti ajenge tabia ya kudadisi na kuhoji.

Lakini, kama wote tujuavyo, kuhoji, hasa kuhoji maslahi ya watu kuna gharama zake. Hivi karibuni nimefanya utafiti wa kina kuhusu changamoto ambazo vijana wa vyuo vikuu wamewahi kukutana nazo kwa kuthubutu kuhoji.

Si unakumbuka baada ya Walowezi wachache wa Zimbabwe (enzi hizo Rhodesia ya Kusini) kujitangazia uhuru Afrika ilivyochachamaa dhidi ya Uingereza? Tanzania tulikwenda mbele zaidi na kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Uingereza. Je wanafunzi wa Chuo Kikuu walikaa kimya? Hawakuandamana hadi ubalozi wa Uingereza mwaka 1965 wakiongozwa na Joseph Sinde Warioba?

Wewe na mimi tunafahamu kwamba licha ya Mwalimu kuwa mpinzani mkubwa wa Serikali ya kimabavu ya Ian Smith kule Zimbabwe, kina warioba walipoandamana waliambulia kuwekwa mahabusu kwa masaa kadhaa na baadaye kuitwa Ikulu kuzungumza na Mwalimu.

Kilimkuta nini kijana aliyethubutu kumpinga Mwalimu Nyerere pale alipowataka kuomba msamaha kwa serikali ya Uingereza. Hakuamuru mwalimu kwamba kijana yule achapwe viboko vitatu? Niliwahi kuongea na Mzee Warioba kwa simu akanieleza kuwa kijana huyo alikuwa Wilfred Mwabulambo ambaye baadaye alikuwa katibu mkuu kwenye wizara kadhaa nchini.

Wapo vijana wengine ambao baada ya kuthubutu kuhoji waliambulia kufukuzwa masomo na hata wengine kupoteza maisha. Usidhani najaribu kutia chumvi hapa Profesa! Prof. Luhanga kwenye kitabu chake Courage for Change: Re-Engineering the University of Dar es Salaam anatoa ushuhuda wa wanafunzi kadhaa waliofariki kwa kihoro cha kufukuzwa chuo kufuatia migomo ya miaka ya tisini.

Kwa maoni ya Prof. Hirji, ili vijana wasomi wafanikiwe katika mapambano yao ya kuleta mabadiliko katika jamii, ni lazima waishike misingi muhimu. Yeye anapendekeza misingi ifuatayo;

Mosi, kuwa na moyo halisi wa kupigania haki za wanyonge badala ya kufanya hivyo ili kujipatia vyeo au manufaa binafsi kama ilivyo kawaida kwenye vyama vingi vya kisiasa na Asasi za Kiraia.

Pili, Hirji anatuasa kushirikiana na watu wa kawaida kwenye shughuli zao. Mabadiliko hayawezi kuletwa na watu ambao wamejitenga na jamii.

Karibuni nimekisoma kitabu cha Kiongozi mashuhuri wa India Jawahral Nehru kiitwacho Glimpses of World History. Pamoja na mambo mengine, Nehru anasimulia kilichowapata vijana wasomi wa Kirusi waliochoshwa na utawala wa kifalme walipokwenda vijijini kuwahamasisha wakulima kuasi. Vijana wale ambao hawakujiweka karibu na jamii zao hapo kabla hawakupata mwitiko mzuri kwa wanavijiji. Wengi waliishia kwenye mikono ya Mfalme Tsar.

Tatu, Hirji anasisitiza kuwa ni lazima pawe na umoja miongoni mwa wanaharakati. Pengine, tatizo pekee katika hili ni ukweli kwamba jina “Wanaharakati” sasa linatumika vibaya. Hata wachumia tumbo nao wamejivisha kilemba cha harakati. Hivyo basi, wakati umoja ukiwa jambo zuri, ni muhimu kuwa na muongozo wa kimaadili na kiitikadi unaopambanua wanaharakati gani hasa wanaolengwa.

Mwisho, Profesa Hirji anatoa rai kuhusu umuhimu wa vijana kujielimisha kwa kina kuhusu masuala mbalimbali ya kihistoria, uchumi, sayansi na maendeleo kwa ujumla. Hili litawezekana iwapo vijana tutaukumbatia utamaduni wa kujisomea vitabu na kujadili. Chambilecho Betroit Bretch, mwandishi mashuhuri wa Kijerumani “Kitabu ni Silaha”.

Hayo ndiyo maoni ya Prof. Hirji aliyonipa yapata mwaka sasa baada ya kuisoma barua yangu kwako. Kwa kuhitimisha, ninaomba nikuhakikishie mambo mawili;

Kwanza, sitakuandikia tena barua kukuhoji alipo mwokozi wa kuirudisha misingi ya utu na usawa nchini mwetu na Afrika kwa ujumla. Hakuna mwingine zaidi yetu vijana ambaye anaweza kulinusuru bara la Afrika kutoka katika minyororo ya unyonywaji.

Kama alivyowahi kusema mwandishi wa kimapinduzi Frantz Fanon kwenye kitabu chake cha “The Wretched of the Earth” (Mafidhuli wa Dunia) kwamba kila kizazi, katika utata wa kipindi chake, lazima kiutambue wajibu wake halafu kiutekeleze au kiusaliti.

Pili, ninakuhakikishia kuwa siku yaja ambapo vijana wasomi wasio na ajira, wafanyakazi waliofukarishwa na wakulima wanyonywao kila uchwao watafumbua macho na kung’amua kuwa mfumo uliopo hauwezi kutoa majibu kwa madhila yao.

Wakati huo utapofika, wakulima na wafanyakazi watatambua jukumu lao la kimapinduzi la kuijenga historia.
Siku hiyo ikifika,
Wakulima kuzinduka,
Viwandani kadharika
Minyororo kukatika,
Madhila yote futika…

Kunako siku hiyo, hata rundo la maswali yangu kwako kwamba tuujenge ujamaa au la litakuwa halina maana tena kwa sababu wanyonge wenyewe watachukua kalamu yao na kuiandika historia yao wenyewe. Naitamani siku hiyo.
…………………………..
Mwandishi wa makala haya yaliandikwa mwaka 2014 na kuchapishwa kwenye gazeti la Raia Mwema mwandishi akiwa mwanafunzi wa kitivo cha Sheria, UDSM
 

cyrax

Member
Mar 12, 2017
93
125
Kweli kabisa hata mimi nasuniri siku ya wanyonge na vijana kuandika historia yao wenyewe katika nchi hiii.
Mimi pia nikiwa mmoja wao Mungu anipe uzima.


Sent using Jamii Forums mobile app
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom