Bariadi: Mama aliyetarajia pacha akabidhiwa mtoto mmoja

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,814
4,547
Hali ya sintofahamu imeikumba familia ya Mayenga Nigonzala, mkazi wa kijiji cha Kidinda Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu baada ya mkewe, Zawadi Sayi kuelezwa kujifungua mtoto mmoja, licha ya vipimo na maelezo ya awali ya madaktari kuonyesha alikuwa na ujauzito wa pacha.

Sintofahamu hiyo imeongezeka baada ya maelezo ya wataalamu na wahudumu wa afya waliomhudumia na taarifa rasmi zilizopo kwenye jalada la mama huyo kutofautiana na yale aliyopewa kabla na wakati wa kujifungua.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu nyumbani kwake wiki iliyopita, Zawadi aliyejifungua kwa upasuaji katika Hospitali ya Halmashauri ya Bariadi ya Somanda Mei 23, mwaka huu, alisema kwa vipindi viwili tofauti wakati wa mahudhurio ya kliniki, madaktari na wauguzi walimweleza kuwa ujauzito wake ni wa pacha wawili.

“Hata Mei 23, nilipofikishwa hospitali kwa ajili ya kujifungua, daktari aliyenipima alinieleza kwa umri wangu wa miaka 16 nisingeweza kujifungua kwa njia ya kawaida; niliambiwa lazima nifanyiwe upasuaji kwa sababu watoto walikuwa wamechoka na wote wawili walikuwa wanataka kutoka kwa wakati mmoja,” alisema Zawadi.

Alisema mama yake mzazi, Joyce Lujiga aliyemsindikiza hospitalini siku hiyo alitakiwa kusaini fomu za kukubali afanyiwe upasuaji baada ya kuwasiliana na kupata idhini kutoka kwa mume wake.

“Baada ya mama kusaini alipewa orodha vinavyohitaji, alikwenda kununua kwenye duka la dawa lililoko nje ya hospitali kwa Sh130,000.

“Vifaa hivyo ambavyo ni dawa, maji ya kuongezwa mwilini (dripu) pamoja na mipira ya kuvaa mikononi vilinunuliwa kwa stakabadhi mbili tofauti zenye namba 11049 na namba 11050,” alisema.

Kukabidhiwa mtoto mmoja
Joyce, mama mzazi wa Zawadi alisema baada ya upasuaji alishangaa kukabidhiwa mtoto mmoja wa kiume badala ya pacha kama vipimo na maelezo ya madaktari yalivyoeleza awali.

“Nilikabidhiwa mtoto mmoja baada ya upasuaji kwa sababu mtoto wangu Zawadi alikuwa hana fahamu kutokana na dawa za usingizi,” alisema Joyce.

Alisema alipohoji daktari aliyehusika kwenye vipimo ambaye pia ndiye alimkabidhi mtoto (jina linahifadhiwa) alimjibu kuwa amezaliwa mtoto mmoja pekee.

“Daktari huyo alieleza mtoto aliyezaliwa alikuwa na uzito mkubwa wa kilo nne ndiyo maana kuzaliwa kwake kulikuwa na ukinzani; nilibaki na maswali mengi kichwani japo sikuwa na la kusema zaidi,” alisema Joyce.

Alisema hata Zawadi naye alipopata fahamu na kukabidhiwa mtoto mmoja badala ya pacha kama alivyoelezwa na kutarajia awali aliamini maelezo hayo ya daktari.

“Hata tuliporuhusiwa na kurejea nyumbani, familia nzima iliamini maelezo ya daktari kuwa Zawadi alijifungua mtoto mmoja,” alisema.

Utata ulivyoibuka
Wiki mbili baada ya kujifungua na kuruhusiwa kurudi nyumbani, Zawadi alirejea hospitali kwa huduma za kiafya ndipo mmoja wa wauguzi wakunga waliomhudumia wakati wa kujifungua alipohoji alipo mtoto wa pili baada ya kumwona akiwa na mtoto mmoja wakati alijifungua mapacha.

“Kwa sababu sikuwa natarajia swali hilo, nilimwangalia muuguzi yule na kugundua alielekeza swali lake kwangu; ilibidi nimuulize anamuuliza nani naye akanijibu nakuuliza wewe….kwani wewe si ni Zawadi,” alisimulia Zawadi

Aliongeza; “Baada ya kumwitikia, muuguzi yule akaniambia alikuwepo wakati najifungua kwa upasuaji na nilijifungua watoto wawili. Nilipigwa butwaa nikabaki nimeduwaa. Baada ya kugundua mshangao wangu, yule muuguzi aliondokea kimya kimya.”

Muuguzi apasua jipu

Alisema muda mfupi baadaye, muuguzi yule ambaye hamfahamu kwa jina, japo akimwona anaweza kukumbuka sura yake alimfuata tena na kumweleza kuwa alijifungua watoto pacha wa kiume.

“Baada ya kunieleza hivyo, muuguzi yule aliondoka akiniacha nimeduwaa nisijue la kufanya,” alisema Zawadi.

Familia kutafuta ukweli
Baada ya kupokea taarifa iliyomchanganya kuhusu idadi ya watoto aliojifungua, Zawadi alimweleza mama yake mzazi, Joyce Lujiga aliyeamua kwenda hospitali kutafuta ukweli wa alipo mtoto mwingine.

Akisimulia ufuatiliaji wake, Joyce alisema “Nilienda kuonana na uongozi wa hospitali kuhoji kwa nini tulikabidhiwa mtoto mmoja badala ya wawili kwa sababu walizaliwapacha. Majibu niliyopewa yalinikatisha tamaa.

“Tofauti na matarajio yangu, wauguzi waliohusika kwenye upasuaji walipoitwa kupata ukweli walianza kunishambulia kwa maneno makali na kejeli wakisema hakuna mtoto mwingine huku wakitamba niende popote sitafanikiwa,” alieleza.

Alisema alirudi nyumbani na kujadiliana na familia na kuamua kumwachia Mungu kwa sababu hali yao ya kiuchumi ni duni na wanaamini waliohusika kumpoteza mtoto wao mmoja huenda ni watu wenye madaraka na uwezo wa kifedha.

‘Gwaride’ la utambulisho
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na uongozi wa hospitali, Zawadi alisema siku chache baadaye yeye na mama yake waliitwa hospitali na kukutanishwa na madaktari na wauguzi walihusika kwenye upasuaji wake, ili amtambue aliyenipa taarifa hizo, lakini hakuweza kufanya hivyo kwa kuwa aliyenipa taarifa hakuwa miongoni mwao.

Alisema licha ya juhudi za uongozi wa hospitali za kutafuta ukweli wa suala hilo, familia yake imeanza kukata tamaa kutokana baadhi ya madaktari na wauguzi waliomhudumia kuanzia kwenye vipimo na kujifungua kutoonyesha ushirikiano zaidi ya kumkejeli.

“Kuna daktari mmoja aliniambia niende nyumbani nipumzike nimlee mtoto wangu; na kama ninataka mapacha nitazaa wengine, kwani ninayemtafuta sitampata,” alisema Zawadi huku akijifuta machozi.

Alisema katika hali ya kuikatisha tamaa familia yake kumtafuta mtoto wake wa pili, mmoja wa madaktari aliwaeleza wanaowasukuma kuendeleza juhudi hizo wana nia ya kuwafanya wauze mifugo yao yote kushughulikia suala ambalo hawatafanikiwa.

“Daktari yule alinionya kuwa nisishirikiane na watu wanaofuatilia taarifa hizi kwa sababu ni matapeli wanataka kumaliza mifugo yangu. Alinisihi nisiiseme vibaya Hospitali ya Somanda kwa sababu kuna siku nyingine nitahitaji huduma yao. Nachukulia kauli hizi kama njia ya kuniziba mdomo,” alisema Zawadi.
 
Hii ni kawaida kama sikosei kwa kusababishwa ná makosa ya wachukua vipimo. Pia kuna wajawazito wengi waliambiwa kutokana na vipimo watapata mtoto mmoja na siku ya kujifungua akapata twins au hata triplets. Pia inawezekana pacha mmoja aliharibikia tumboni mimba ikiwa changa.

Best Sky Eclat hebu pita mtaa huu umwage maujanja yako.
Hali ya sintofahamu imeikumba familia ya Mayenga Nigonzala, mkazi wa kijiji cha Kidinda Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu baada ya mkewe, Zawadi Sayi kuelezwa kujifungua mtoto mmoja, licha ya vipimo na maelezo ya awali ya madaktari kuonyesha alikuwa na ujauzito wa pacha.
 
Hii ni kawaida kama sikosei kwa kusababishwa ná makosa ya wachukua vipimo. Pia kuna wajawazito wengi waliambiwa kutokana na vipimo watapata mtoto mmoja na siku ya kujifungua akapata twins au hata triplets. Pia inawezekana pacha mmoja aliharibikia tumboni mimba ikiwa changa.
Best Sky Eclat hebu pita mtaa huu umwage maujanja yako.
Hata wao waliamini, shida ni huyo muuguzi aliyepasua jipu
 
Back
Top Bottom