Bajeti 2010/11 ni ya kujumlisha na kutoa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bajeti 2010/11 ni ya kujumlisha na kutoa

Discussion in 'Biashara, Uchumi na Ujasiriamali' started by MziziMkavu, Jun 11, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 11, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  [​IMG] Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo akiwasili katika viwanja vya Bunge tayari kwa kusoma bajeti ya 2010/11

  Andrew Msechu

  SERIKALI jana ilitangaza bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2010/11 ambayo inaonekana kupunguza makali kwenye baadhi ya sekta huku ikiongeza makali kwenye maeneo mengine.Bajeti hiyo ya Sh1.1 trilioni inaendelea kuweka kipaumbele katika uboreshaji miundombinu, elimu, afya, kilimo, na maji huku ikielekeza nguvu katika kubana matumizi ya serikali, ukusanyaji zaidi wa kodi, kitu kilichopigiwa kelele na washirika wa maendeleo ambao wamezuia Sh297 bilioni wanazotarajiwa kuchangia kwenye bajeti hiyo.

  Bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo imeanisha maeneo mengi ambayo yatasaidia kufanikisha mpango wa Kilimo Kwanza, ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi na ushuru katika pembejeo za kilimo na zana za ufugaji na kupunguza kwa asilimia moja kodi ya mapato ya wafanyakazi kutoka asilimia 15 na kuwa 14 kwa kima cha chini cha mishahara.

  Hata hivyo, bajeti hiyo haijaonyesha kama imepanua wigo wake wa kodi ili kuhakikisha inatimiza malengo yake ya kukusanya angalau asilimia 70 ya fedha za bajeti hiyo, ambayo inaonekana itaendelea kutegemea wahisani ili kufanikisha miradi ya maendeleo.

  Mbali na kupunguza kodi ya mapato kwa asilimia moja kwenye mshahara wa kima cha chinim serikali pia imeitikia shinikizo la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) kwa kutangaza kuwepo kwa ongezeko la mshahara kwa kima cha chini, lakini kiwango kamili kitatangazwa na waziri husika.

  Tucta imetishia kuitisha mgomo wa wafanyakazi wote kutokana na serikali kuchelewa kutangaza ongezeko la kima cha chini cha mishahara baada ya pande hizo kufikia makubaliano katika mkutano uliofanyika Mei 8. Waziri husika alitakiwa atoe tangazo hilo ndani ya siku 21 tangu tarehe ya maafikiano, lakini hadi leo bado halijatolewa.

  Mkullo alilieleza Bunge kuwa bajeti ya mwaka huu wa fedha ni muendelezo wa mkakati wa miaka mitano, ambapo baada ya mwaka wa fedha 2009/2010 unaomalizika mwezi huu, inakamilisha kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya Awamu ya Nne iliyoingia madarakani Desemba 2005.

  Mkulo alisema serikali imezingatia umuhimu wa kupunguza kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi kutoka asilimia 15 hadi asilimia 14 na nyongeza ya kima cha chini cha mshahara, ikiwa na lengo la kuwaongezea kipato na kuwapunguzia mzigo wa kodi watumishi wa umma wenye kipato cha chini.

  Hadi sasa, serikali ilikuwa ikikata kodi ya asilimia 15 kwenye mshahara unaoanzia Sh100,001 hadi Sh360,000, kiwango ambacho wafanyakazi wamekuwa wakikilalamikia kuwa kinatafuna mshahara wao. Hata hivyo, kwa tangazo hilo, viwango vinavyokatwa kwenye mishahara ya kuanzia Sh360,001 vitabakia kama vilivyo.

  Bajeti hiyo pia imeweka unafuu mkubwa kwenye kilimo ambacho kimetengewa Sh903.8 bilioni kutokana na kuweka misamaha mingi katika vifaa vya kilimo, pembejeo na usafirishaji wa mazao. Hata hivyo, bajeti hiyo haijagusia kabisa sekta ya uvuvi, ambayo katika siku za karibuni imeonekana kuwa inaweza kuliingizia taifa mapato makubwa.

  Katika kuhamasiaha maendeleo ya kilimo, serikali imefanya mabadiliko kadhaa katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka shambani hadi kwenye viwanda vya usindikaji kwa wakulima wenye kilimo cha mkataba wa miwa, mkonge na chai.

  Pia imesamehe kodi hiyo kwenye mashine na vifaa vya kukusanya, kusafirisha na kusindika maziwa, kutoa unafuu wa kodi ya ongezeko la thamani vifaa vinavyouzwa kwa wataalamu wa mifugo waliosajiliwa, zana za kilimo, usafirishaji wa maua kwa ndege kwenda nje ya nchi, huduma za kuzalisha mifugo kwa njia ya kupandisha mifugo na kutumia mashine maalum za kuzalishia/kutotolea vifaranga.

  Pia imeweka nafuu maalum kwa kodi kwenye mabanda yanayotumika katika kilimo cha maua, uuzaji wa bidhaa na huduma zitolewazo kwa wakulima waliosajiliwa au mashamba ya vyama vya ushirika kwa ajili ya kujenga miundombinu ya mashamba kama vile mitaro ya umwagiliaji, barabara za mashambani, ujenzi wa maghala au huduma nyinginezo za namna hiyo.

  Hatua nyingine za kutoa ahueni ni kurekebisha kifungu cha 11 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuweka wigo wa ukomo wa maeneo ya uchimbaji wa madini kwa nia ya kudhibiti gharama zinazotakiwa kutolewa katika kukokotoa faida itakayotozwa kodi ya mapato kuwa ni zile za eneo husika tu, ikihusisha kampuni zote za madini.

  "Kwa kuwa bado kuna biashara nyingi zinazofanywa na watu wasiokuwa na namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN), napendekeza kodi ya zuio inayozuiwa na serikali kwa wauzaji wa bidhaa na watoa huduma waliokuwa na TIN, izuiwe pia na wafanyabiashara wote waliosajiliwa ili kuwahamasisha wasiokuwa na namba za utambulisho kwenda kusajiliwa.

  Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa pamoja zitapunguza mapato ya serikali kwa kiasi cha Sh 4.468 bilioni," alisema.

  Alisema marekebisho ya ada ya usajili na uhamisho wa umiliki wa magari na pikipiki yatafanyika kwa kuongeza viwango vya ada, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha Sh3.19 bilioni.

  Katika mapendekezo hayo, Mkullo alitaka kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa ili kupunguza ushuru kutoka Sh97 hadi Sh80 mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ili kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hapa nchini, ikiwa na lengo la kukuza viwanda, ajira na mapato ya ndani.

  Wakati serikali ikiondoa makali kwenye maeneo hayo, wananchi watalazimika kujikuna zaidi watakapotaka bidhaa za matumizi ya ziada baada ya serikali kuongeza ada kwenye magari, kuongeza kodi kwenye vinywaji vya kileo.

  Katika bajeti hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na Watanzania, Mkullo alisema viwango maalum vinavyopendekezwa ni katika vinywaji baridi, akieleza kuwa viwango hivyo vitaongezeka katika bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa.

  Alisema marekebisho hayo yanazingatia kiasi cha wastani wa mfumuko wa bei na kwamba sasa vinywaji baridi kodi itaongezeka kutoka Sh58 kwa lita hadi Sh63 kwa lita na bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini, na ambayo haijaoteshwa itapanda kutoka Sh209 kwa lita hadi Sh226 kwa lita.

  Marekebisho mengine ni kuongeza kodi katika bia nyingine zote, kutoka Sh354 kwa lita hadi Sh382 kwa lita, wakati mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 itapanda kutoka Sh1,132 kwa lita hadi Sh1,223 kwa lita, vinywaji vikali kutoka Sh1,678 kwa lita hadi Sh1,812 kwa lita, kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara.

  Alieleza kwamba bia nyingine zote zizizotengenezwa nchini pia zitapanda na mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 utapanda pia, hali kadhalika vinywaji vikali.

  Serikali pia imependekeza marekebisho ya viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara, ikitaka sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75 kwa kila sigara 1,000.

  Pia kwa sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, wakati sigara nyingine zenye sifa tofauti na hizo za awali kutoka sh34, 633 hadi sh26,604 kwa sigara 1000.

  "Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara pia kutoka shilingi 12,441 hadi Sh13,436 kwa kilo, na ushuru wa (cigar) unabaki kuwa asilimia 30. Hatua hizi katika ushuru wa bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 20.042 bilioni," alisema.

  Mkulo aliweka bayana kwamba bajeti hiyo aliyoiwasilisha katika mkutano huo wa mwisho wa Bajeti kwa Bunge baada ya miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne, ina nia njema ya kuwapa fursa ya kurudi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, kwa ajili ya kuomba ridhaa yao ya kurudi tena bungeni.

  "Bajeti ya mwaka huu, sera za matumizi zililenga kutoa upendeleo wa mgao wa matumizi kwenye sekta za kipaumbele ikiwa ni pamoja na Elimu, Miundombinu na Kilimo.

  Aidha sera za matumizi pia zilihusisha kuimarisha mfumo wa usimamizi wa fedha na ufuatiliaji wa matumizi pamoja na tathimini ya mpango wa bajeti ili kuhakikisha rasilimali fedha inatumika kwa ufanisi," alisema.

  Mkulo alisema kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele aliyoyaainisha, maeneo yaliyopata upendeleo wa ongezeko kubwa katika bajeti ni Miundombinu iliyopata ongezeko kwa asilimia 37.3, Kilimo iliyopata ongezeko la asilimia 35 na Elimu iliyopata ongezeko la asilimia 17.2.

  Afya imepata ongezeko la asilimia 25.2, Maji ongezeko la asilimia 14.5, Nishati na madini ongezeko la asilimia 14.6.

  Waziri Mkulo alisema Sh30 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utafiti na ufuatiliaji, kwa ajili ya maeneo yatakayopata upendeleo katika awamu ya kwanza ambayo ni ukarabati wa Miundombinu katika taasisi zinazohusika na tafiti mbalimbali.

  "Kwa hiyo, bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 inalenga kuendelea na utekelezaji wa sera na malengo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi hiki, yamekuwepo mafanikio ya kuridhisha katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha uchumi kukua na kupunguza umaskini," alisema.

  Bajeti hiyo pia imerekebisha kwa asilimia nane viwango maalum vya ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zinazotozwa ushuru huu isipokuwa zile za mafuta ya petroli, kwa kuzingatia kiasi cha wastani wa mfumuko wa bei.

  Katika kukabiliana na makali ya bajeti hiyo, Mkulo alisema serikali imeamua kudhibiti na kusimamia vyema matumizi yake, hasa katika mawasiliano, nishati na matumizi ya ununuzi na matengenezo ya magari.

  Katika bajeti hiyo, Mkullo alisema katika mikakati ya mwaka huu wa fedha, serikali itaendelea kutekeleza sera za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuweza kugharamia sehemu kubwa ya matumizi ya kawaida, ikiwemo kuendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha kuwa pale inapowezekana malipo yanafanyika kwenye mabenki.

  Mikakati mingine aliyoieleza ni pamoja na kuweka mkakati wa kuboresha huduma za utalii kwa kutathimini hoteli ili ziwe katika viwango vinavyokubalika kimataifa kwa lengo la kuongeza mapato yatokanayo na ada, kuhimiza utekelezaji wa Sheria ya Fedha inayoelekeza mashirika na taasisi kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali na kuendelea kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya na kuimarisha uchumi tulivu pamoja na kuweka mazingira bora ya biashara ili kuwezesha sekta binafsi kukua.

  Alisema serikali pia itaendelea kusimamia kwa karibu mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato (TRA) chini ya mpango wake wa tatu wa maboresho ya miaka mitano ambayo yamekuwa msingi wa kukua kwa mapato ya ndani mwaka hadi mwaka na kuchukua hatua za kuboresha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kutoka Wizara na Idara za Serikali.

  Pia kupitia upya utaratibu wa kutoa misamaha ya kodi kwa lengo la kuongeza udhibiti na kuendelea kuhakikisha kwamba watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa wanajengewa uwezo kwa kuwapatia utaalamu wa kutosha ili kuongeza ufanisi katika ukadiriaji na ukusanyaji wa mapato katika serikali za mitaa.

  Bajeti 2010/11 ni ya kujumlisha na kutoa
   
 2. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #2
  Jun 11, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  Bajeti: Wananchi wakata tamaa  Wengi watarajia machungu zaidi  [​IMG]
  Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo  Wakati Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa mkulo, anatarajia kuwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha 2010/11, makundi mbalimbali ya jamii yametoa maoni kuhusiana na matarajio yao.
  Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema ingawa Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (Mkukuta) awamu ya kwanza umefikia mwisho wake, umaskini wa Watanzania bado uko pale pale na maandalizi ya Mkukuta awamu ya pili hayajafanyika.
  Alisema malengo ya serikali ya kupunguza umaskini hadi kufikia mwaka huu kupitia mpango huo umeonyesha kushindwa kabisa na maisha yanazidi kuwa magumu.
  Alisema ingawa takwimu zinaonyesha kuwa uchumi umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia saba miaka ya karibuni, lakini hakuna unafuu wowote kwa wananchi.
  Alisema hata Malengo ya Mpango wa Milenia (MDGs) kupunguza umaskini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015 hayatafikiwa kwa kuwa uchumi bado ni tegemezi kwa kiwango kikubwa.
  “Bajeti inapaswa kujibu swali hili kwamba tufanye nini kupunguza umaskini, maana licha ya takwimu kuonyesha kuwa uchumi unakuwa maisha ya watu bado magumu sana,” alisema.
  Alisema serikali inaweza kujitegemea kwa kuimarisha makusanyo ya ndani na kuondoa misamaha ya kodi na pia kuanza kuyatoza kodi makampuni ya madini na kuachana na utaratibu wa mirabaha.
  Profesa Lipumba pia alikosoa hatua ya kufupisha muda wa Mkutano wa 20 wa Bunge la Bajeti kuwa wiki tano badala ya miezi mitatu.
  Alisema Bunge la bajeti lilipaswa kutoa mwelekeo halisi wa uchumi katika miaka mitano ijayo kwa wabunge kujadili kwa kina na kwa umakini mipango ya maendeleo ya nchi.
  Mvungi: Utegemezi miaka 50 aibu
  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, alisema ni aibu kwa miaka 50 ya uhuru kuona bado nchi inashindwa kujitegemea kwenye bajeti yake.
  Alisema bajeti inayosomwa leo haina jipya kwa kuwa haijabainisha njia za kutengeneza utajiri mpya kama vile kuongeza viwanda vya uzalishaji mali na kuwekeza nguvu kubwa kwenye kilimo ili kiwe na tija.
  “Ingawa mimi sio mchumi, lakini kama walivyoonyesha vipaumbele vyao inaonekana ni bajeti dhaifu na ya kivivu na mtu yeyote anaweza kuiandika hata akiwa amelala kitandani…ukishaona bajeti inajielekeza kuongeza kodi kwenye bidhaa za ndani ujue hakuna kitu kipya hapo maana unazidisha maumivu kwa wananchi badala ya kutafuta vyanzo vya mapato,” alisema Dk. Mvungi.
  Alisema Tanzania ni nchi ambayo sasa inapaswa kuongeza uwezo wake wa kuzalisha mali na kuuza nje ili hatimaye iweze kugharimia uendeshaji wa serikali badala ya kuombaomba.
  Alionya kuwa Tanzania ikiendelea na kawaida ya kuombaomba misaada kwa nchi wahisani kuna hatari ya kuwa maskini milele na nchi haitakuwa huru.
  Mrema: Mkukuta haujaleta nafuu
  Naye Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), John Mrema, alisema alisema awamu ya kwanza ya Mkukuta imekwisha, lakini hakuna unafuu wowote wa maisha kwa Watanzania.
  Alisema inashangaza kuona serikali imeshindwa kabisa hata kuweka kipaumbele sekta ya elimu ambayo ndiyo inaweza kuwa njia kuu ya kukuza uchumi na imeishia kujenga shule za kata.
  Alisema shule hizo za kata nyingi hazina walimu na zimeishia kuwa vijiwe vya wasichana kupata mimba kwa kuwa wanafika shuleni na kukaa bila kufundishwa.
  Mrema alisema serikali inapaswa pia kuweka kipaumbele katika kilimo kama kweli inataka kukuza uchumi na kujitegemea.
  Alisema Benki ya Rasilimali (TIB), inapaswa kufungua matawi katika mikoa inayozalisha kwa wingi kama Iringa, Mbeya na Rukwa ili kuwawezesha wakulima badala ya kukaa Dar es salaam na Arusha ambako hakuna wakulima.
  Alisema bila nishati hakuna kitu kinachoweza kufanyika kwani hata wakulima wanaozalisha wanahitaji viwanda vya kusindika bidhaa zao kwenye maeneo yao.
  Semboja: Tusitegemee faraja
  Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, alisema Watanzania leo wasitarajie faraja yoyote kutoka katika bajeti ya serikali.
  Dk. Semboja alisema hali hiyo inatokana na sekta binafsi ambayo imeajiri wananchi wengi kushindwa kuwezeshwa kikamilifu ili iweze kuchangia pato la taifa.
  Alisema sababu nyingine itakayoifanya bajeti ishindwe kuwa nzuri ni matatizo ya mtikisiko wa uchumi ulioikumba dunia hivi karibuni ambapo Tanzania nayo iliathirika.
  Alisema mapato mengi ya serikali yanatoka kwa wananchi, lakini kwa bahati mbaya kwa kipindi kirefu wananchi wamekuwa wakikabiliwa na ugumu wa maisha na hivyo kushindwa kuchangia.
  Alisema kutokana na sababu hizo wananchi wa kawaida wasitarajie neema yoyote kutoka katika bajeti hiyo.
  Alitaja sababu zingine zitakazoifanya bajeti ya mwaka huu 2010/2011 isilete matumaini ni kupungua kwa raslimali ukiwemo uwekezaji wa nje na misaada ya wahisani ambavyo vimepungua katika miaka ya hivi karibuni.
  Hata hivyo, licha ya kutabiri bajeti kuwa haitakidhi matarajio ya wengi, lakini alisema huenda serikali isipandishe bei ya bidhaa mbalimbali kutokana na kuwa ni mwaka wa uchaguzi.
  Matibabu bure kwa kila mzee
  Shirika lisilo la kiserikali la HelpAge limesema kuwa serikali itoe kipaumbele kwa kundi la wazee katika masuala mbalimbali ikiwemo matibabu na kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo.
  Mkurugenzi Mipango wa shirika hilo, Nicodimus Chipfupa, alisema serikali inatakiwa kutamka wazi kuwa kundi la wazee lipate matibabu bure kwa sababu ni haki yao ya misingi.
  Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, walisema kuporomoka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani kunaashiria bajeti ya mwaka ujao itakuwa ngumu zaidi kwa wananchi wenye kipato cha chini.
  Dereva teksi, Yahya Nyanzugu, alisema uwezekano wa bajeti ya sasa kuwanufaisha wananchi ni mdogo kwa kuzingatia kwamba makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hayatoshelezi mahitaji ya Serikali.
  “Inawezekana pia kwamba tunavyosikia bajeti imeongezeka kutoka Sh. trilioni tisa hadi 11 ni nadharia tu maana inawezekana ongezeko la fedha ni dogo sana kutokana na kwamba shilingi inaporomoka kila siku,” alisema.
  Dereva mwingine wa daladala, Yusuf Ali, alisema kupanda kwa bei ya petroli na dizeli kunaashiria kwamba wananchi watakaoumia zaidi ni wakulima kwa kuwa watashindwa kusafirisha mazao yao kutoka shambani au ghalani hadi sokoni.
  Serikali kukopa benki aibu
  Jennifer Mazengo, mkazi wa Sinza alisema kitendo cha TRA kushindwa kukusanya kodi ipasavyo na kupelekea Serikali kukopa benki, kinaashiria kwamba wananchi watakamuliwa zaidi ili wazibe pengo.
  “Kukopa benki ni kitendo cha aibu ambacho naamini kabisa serikali isingependa kitokee, lakini ili kuhakikisha jambo hilo halijirudii lazima wananchi wabanwe ipasavyo...na kama unavyojua thamani ya pesa yetu inazidi kuporomoka kila wakati, jambo hili linatuumiza sisi wananchi wa chini,” alisema.
  Deogratius James, mjasiriamali, alitahadharisha kuwa kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta kutasababisha nauli kupanda wakati mishahara kwa wafanyakazi wengi haitapanda jambo ambalo litawaathiri zaidi.
  Tamwa: Fedha zaidi Afya
  Nacho Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimeishauri serikali kuongeza bajeti yake katika Wizara ya Afya kwani sekta hiyo ni ya umuhimu na hatua hiyo itasaidia kwa asilimia kubwa watumishi kufanya kazi kwa kujitolea.
  Mkurugenzi wa Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya, alisema kuwa sekta hiyo inahitaji kuboreshwa bajeti yake ili huduma ziwe na ubora.
  Nkya alisema kuwa ukiachilia mbali katika sekta hiyo, serikali pia inatakiwa kuongeza bajeti yake katika Wizara ya Elimu ili ubora wa elimu upande.
  Alitolea mfano kuwa katika shule za kata hazina uboreshaji wa kutosha hasa katika suala la walimu, vitabu na mabweni.
  TGNP: Pengo la matabaka lipungue
  Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ussu Mallya, alisema wanatarajia serikali kuyapa kipaumbele mambo mengi yalioorodheshwa katika mwongozo wao, hususan kupunguza pengo la umaskini kati ya maskini na tajiri.
  Pia alisema wanatarajia serikali kuboresha miundombinu vijinini na mijini hususan kupunguza msongamano katika barabara za Dar es Salaam. Mengine ni kudhibiti uporaji wa ardhi
  Wakati wananchi wakisema hayo, serikali imesema wafanyabiashara wa Tanzania wana nafasi kubwa katika kusaidia kuimarisha Shilingi, kuliko ambavyo serikali inaweza kufanya.
  Wafanyabiashara wanaiua Shilingi
  Akizungumza na Nipashe mjini Dodoma jana, Naibu Waziri wa Fedha, Omar Yusufu Mzee, alisema ni kosa kuinyooshea serikali kidole kwa tatizo hilo badala ya wafanyabiashara.
  Alisema wafanyabiashara wa Tanzania wamebobea na wanaendelea kubobea katika shughuli za kuleta bidhaa nchini (imports) ambazo zinawafanya wagombanie dola chache zilizopo, badala ya kujikita katika biashara za kupeleka bidhaa nje (exports).
  Mzee alisema katika nchi ambayo imejikuta ikitumia takriban mara arobaini ya dola inazozihitaji kwa kuagiza biadhaa nje kuliko inazoingiza, ni vigumu kuimarika kwa sarafu yake.
  Naibu Waziri huyo alisema kitu kingine kinachochangia kuanguka kwa Shilingi na kinachosababishwa na wafanyabiashara ni ‘ugonjwa’ wa kuthamini Dola na hivyo kuitumia hata katika mahitaji ya ndani.
  Vitambulisho vya taifa vitavunja utegemezi
  Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa Tanzania ingekuwa imeshaondokana na tabia ya kutegemea wafadhili kwa ajili ya bajeti yake, kama ingeharakisha kutekeleza mpango wa kuanzisha vitambulisho vya taifa, baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge mwaka 1986.
  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Utambuzi ya Taifa (Nida), Dickson Maimu, alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana wakati akitoa semina kwa wabunge kuhusu umuhimu wa ‘Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa watu’.
  Katika mwaka wa fedha uliopita, bajeti ya serikali ilikuwa Sh. trilioni 9.5 ambay ilikuwa tegemezi kwa wahisani kwa asilimia 34 (sawa na Sh. trilioni 3.2).
  Maimu alisema Tanzania kutokana na kutokuwa na mfumo wa utambuzi wa wananchi wake, imeshindwa kuwajua walipa kodi wote na hivyo mzigo huo kubebwa na wachache kiasi kwamba lazima nchi kama hiyo itembeze bakuli katika kutekeleza bajeti yake.
  Alisema wakati takwimu zinaonyesha kwamba Watanzania milioni 14 (kati ya takriban milioni 43) wanatakiwa kulipa kodi, wanaolipa mpaka sasa, kwa mujibu wa takwimu za TRA) ni takriban watu milioni 1.5 tu.
  Alisema hiyo ni tofauti na Kenya ambayo kwa miaka mingi imekuwa na mfumo wa vitambulisho vya taifa, maarufu kama kipande, na kuwawezesha kukusanya kodi kwa watu takriban milioni 10. Kwa hali hiyo, alisema Kenya ina uwezo wa kuchangia bajeti yake kwa asilimia 95.
  Naye Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, amesema mtikisiko wa uchumi unaifanya bajeti hiyo kuwa ngumu.
  “Imebaki saa 72 niwasilishe bajeti bungeni…bajeti ya mwaka huu, ni ngumu kutokana na mambo matatu, kwanza ni mtikisiko ambao umetukabili,” alisema juzi.
  Imeandaliwa na Joseph Mwendapole, Richard makore, Restuta James, Romana Mallya, Beatrice Shayo na Theo Muchunguzi (Dar es Salaam) na Hamis Kibari na Sharon Sauwa (Dodoma).  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...