Nachoka kuwaza. Sasa nimeanza kuona giza… giza nene. Sio la usiku. Hapana. Ni giza la maisha. Giza la matumaini yaliyooza kabla hayajachanua. Giza la haki iliyonyongwa hadharani huku waliopaswa kulia wakishangilia.
Moyo wangu huwaka moto wa huzuni kila ninapotazama mwenendo wa siasa zetu. Moto unaowaka kimya kimya, bila mwanga, lakini wenye joto la uchungu.
Utekaji. Uchawa. Uonevu. Usaliti. Na hii hali... hii hali ngumu ya maisha inayowakaba maskini koo hadi hawana sauti ya kulia tena.
Wanaharakati... wale wachache waliobaki na ujasiri wa kupaza sauti — wanatoweka. Wengine wanateswa, wengine hawarudi nyumbani.
Ni kosa kuwa na maoni tofauti? Ni dhambi kusema "hii si sawa?"
Nauliza tu. Labda niulize kama mwendawazimu anayezungumza na mti.
"Mpaka lini? Mpaka lini tutalazimika kuishi kwa hofu?"
Au pengine, jawabu ni rahisi sana kuliko tunavyodhani. Kuna wazo limenijia, huenda likawa jawabu mujarabu kwa madhila yote.
Kwanini tusijaribu wazo hili..?
Wote tuwe wanachama wa chama tawala.
Ndiyo, kila mmoja! Nchi nzima tuvae mashati ya kijani, tusifie bila kuchoka, tupongeze hata jua likiwa linachomoza, tushangilie hata wakati wa kilio.
Wote tuwe mashabiki wa kila tamko, kila amri, kila kauli ya mamlaka. Tuwe chawa wakubwa kuliko Steve Nyerere.
Tumeze kauli mbiu na ilani ya chama kikuu kuliko tulivyomeza misahafu.
Tuondoe fikra huru, tuzike maswali.
Tuwe kama maji yaliyogandishwa — maji baridi, kimya, bila mtikisiko.
Kama nchi nzima tukiwa wanachama wa chama kikuu, hakutakuwa na tatizo tena. Polisi hawatakuwa na haja ya kupiga, kwa sababu hatutakuwa na la kupingwa.
Magereza yatabaki tupu, kwa sababu wote tutakuwa huru. Watetezi wa haki hawatachukuliwa usiku, kwa sababu hakutakuwa tena na haki ya kutetewa.
Na labda... labda tukifanya hivyo, maisha yatakuwa rahisi. Bei ya unga haitashuka, lakini angalau hatutazungumza kuihusu. Ajira hazitaongezeka, lakini hatutakuwa na sababu ya kupiga kelele.
Huduma duni hospitalini hazitakuwa na ubavu wa kutufanya tulalamike. Kwa sababu sote tutakuwa kitu kimoja—watulivu, wenye furaha na kujiamini.
Tutakuwa wazalendo wa kweli; wenye kusahau haraka. Tutasamehe kila jeraha hata kama bado linavuja. Sote tutakuwa mashujaa wenye uwezo wa kuimba nyimbo za sifa mbele ya majeneza ya matumaini yetu.
Labda… labda Tanzania itageuka kuwa nchi ya maziwa na asali!
Hakutakuwa na wanyonge wanaoteseka tena, kwa sababu kila mmoja atakuwa amevaa barakoa yenye tabasamu la kijani.
Au unafikiri ni wazimu?
Ndiyo… ni wazimu. Lakini angalau ni wazo. Wazo ambalo bado halijazikwa.
Na kama hili nalo ni kosa… basi nishaurini, tufuate njia ipi?