Ndugu zangu,
HAKUNA chenye mwanzo kisicho na mwisho. Na utawala wa Gaddafi umefikia ukomo. Libya haiwezi tena kurudi kama ilivyokuwa enzi za Gaddafi.
Gaddafi aliitawala Libya kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miaka 40. Aliitawala Libya kidikteta. Pamoja na utajiri mkubwa wa mafuta wa nchi hiyo, utawala wa Gaddafi uliminya uhuru wa fikra kwa watu wake. Kamwe Gaddafi hakuvumilia fikra za kipinzani.
Mwanzoni kabisa mwa harakati za kumwondoa Gaddafi madarakani , kuna kijana aliyepata kutamka haya; Tunachotaka ni kuishi maisha ya kawaida. Kuwa na uhuru wa mawazo kama vijana wengine duniani. Alitamka kijana yule wa KiLibya kwa mwanahabari wa Kimagharibi.
Na hakika hicho ndicho kikubwa kilichokosekana chini ya utawala wa Gaddafi. Na siku zote, mwanadamu hata umpe nini, lakini ukimnyima uhuru wa kufikiri na kuchagua, basi, atajisikia mtumwa. Hatofurahi.
Na kwa Gaddafi, si tu aliitawala Libya kwa muda mrefu, lakini bado alikuwa na ndoto, kuwa akitoka madarakani , basi, familia yake iendelee kutawala. Na umma ukimchoka mtawala au chama cha siasa, basi, utaishi kwa matumaini, kuwa siku moja itafika, kuwa umma utaondokana nae, au kuondokana nacho, kama ni chama cha siasa. Ndio maana ya furaha kubwa ya wenye kutimiza ndoto zao za kujikomboa.
Ndio, kiongozi wa nchi haui watu wake, Moummar Gaddafi wa Libya alifanya hivyo. Aliwaua watu wake, tena mchana wa jua kali, na bado alisimama hadharani, akidai kuwa ni kiongozi wa WaLibya. Gaddafi hakuwa na aibu.
Hatukatai, kuwa Gaddafi alifanya mazuri kwa WaLibya, LAKINI, kosa kubwa kabisa alilofanya Gaddafi kwa WaLibya ni KUWAKANDAMIZA watu wake. Ndio, kuwanyima UHURU. Gaddafi aliwageuza WaLibya kama ngombe kwenye zizi. Waliotoa sauti kumpinga aliwakamata na kuwachinja, kimyakimya. Gadaffi aliifanya Libya kuwa ni mali ya Gaddafi na familia yake.
Ndugu zangu,
Gaddafi alipata kusimama hadharani na kuwaambia WaLibya waendelee kuimba na kucheza! Akatamka; WaLibya wote wananipenda! Hakika, Gaddafi alikuwa amepoteza mwelekeo na mguso wa hali halisi. Alipitisha viwango vyote vya ulevi wa madaraka. Wakati mwingine Gaddafi alionekana kama mwehu fulani aliyeshika bunduki na kupita mitaani. Na kwa kuhofia maisha yao, kuna vijana wengi wasomi wa Libya walilazimika kuikimbia nchi yao wanayoipenda. Walikwenda kuishi uhamishoni.
Tunajifunza nini?
Kwamba Afrika bado ina viongozi wengi, ambao, hata hii leo, wameingiwa hofu kwa kile kilichomtokea mwenzao Gaddafi. Hofu hiyo ina tafsiri nyingi; moja kuu ni ukweli, kuwa kuna viongozi Afrika wanaofanana fanana na Gaddafi. Kwamba nao hawapendi na hawaamini katika demokrasia na uhuru wa watu kutoa mawazo yao, hata yenye kushutumu Serikali.
Hawapendi uwepo wa vyama vingi na dhana ya kugawana madaraka. Hawapendi uwepo wa chaguzi huru na za haki. Hawapendi Katiba ambazo, mbali ya mambo mengine, zinampunguzia madaraka Rais. Kwao, kumpunguzia Rais madaraka ni sawa na kumpunguzia nguvu mtawala. Kwao ni jambo lisilowezekana.
Na Afrika bado ina watawala ambao watafanya kila hila kuhakikisha chaguzi za kisiasa haziendeshwi na tume huru za uchaguzi, bali, zitaendeshwa kutoka Ikulu zao. Na watawala hawa wa Afrika, kama kuna wenye kuandamana mitaani kuwapinga, basi, nao kama alivyofanya Gaddafi, hawatasita kutumia nguvu za kijeshi kuzima maandamano ya wananchi, ikibidi kuwaua wananchi wao. Ndio, Watatafuta visingizio vya kuwatwanga risasi watu wao ili kuwatishia wengine.
Na hakika, kinachotokea Afrika ni hiki; kwanza, mtawala atawaita waandamanaji kuku na majina mengineyo. Kisha ataamrisha vikosi vyake vitumie risasi za moto kuwadhibiti kuku waandamanaji. Si tunajua, kuwa Afrika kuku hachimbiwi kaburi.
Viongozi Afrika watambue sasa, kuwa Afrika kuna kimbunga kimelipuka. Ni kimbunga kinachosambaa. Kimeanzia Tunisia, kikaenda Misri na kimetua Libya. Kinasambaa. Ni kimbunga cha mabadiliko. Waafrika wengi wanaokandamizwa na watawala au vyama tawala katika nchi zao, leo wana kiu kubwa ya kujikomboa.
Na kiongozi mzuri hujitambua na kutambua wakati unaomzunguka. Huwa na uwezo wa kusoma alama za nyakati. Kiongozi makini, mwenye busara na mapenzi ya dhati kwa nchi yake hatosubirii watu wake wafikie ukomo wa uvumilivu ili afanye mabadiliko hitajika na yenye kukidhi matakwa ya wakati husika.
Nimepata kuandika, kuwa katika nchi, mabadiliko ya amani yanawezekana, lakini, kwa anayejaribu kuyazuia, atambue, kuwa mabadiliko yenye vurugu hayaepukiki.
Waafrika wameamka usingizini. Wameshatambua, kuwa hakuna risasi au kombora la mtawala litakaloweza kushinda nguvu ya umma uliodhamiria kuleta mabadiliko. Yametokea Tunisia, Misri, Libya. Yanaweza kutokea popote pale Afrika.
Busara ni kuenenda na wakati uliobadilika. Nahitimisha.
Maggid,
Dar es Salaam.
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
( Makala haya yamechapwa kwenye gazeti la Mwananci, leo Jumapili)