ANGALIZO Kwa CHADEMA: Kukaribiana na CCM Kisera ni hatari!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
Kama chama kikuu cha upinzani nchini CHADEMA kitaendelea kujisogeza karibu na kubariki sera za chama tawala ndivyo hivyo hivyo CHADEMA itazidi kujiwekea mazingira ya kujiangamiza huko mbeleni. Na ndivyo hivyo hivyo tofauti kati yake na CCM itazidi kupotea na kwa upande wa sera kitaonekana hakina tofauti kubwa na matokeo yake badala ya kutofautishwa kisera watu wataanza kuangalia tofauti za watu tu.

Uhusiano kati ya Fikra, Sera, Itikadi na mfumo wa utawala


Watu wenye fikra zinazofanana huweza kukutana pamoja na kujadiliana na kujikuta kuwa wanakubaliana sana kuhusu mambo mbalimbali. Kwa mfano katika mazungumzo mtu anayeamini kuwa serikali inapaswa kutoa ruzuku kwenye shule za binafsi na mwingine naye anaamini kuwa shule na hata vyuo binafsi vinahitaji ruzuku ya kuviendesha hawa watakuwa wanafanana kifikra. Hawa basi wana fikra sawasawa.

Wakikaa pamoja na kukubaliana hata namna ya kutoa ruzuku hiyo au kujikuta wanakubaliana kwenye masuala ya maji, nishati, usalama, inteligensia n.k basi watu hawa wanaweza wakaamua kuanzisha chombo chao ili waweze kutekeleza fikra zao. Hivyo, itikadi huzaliwa. Itikadi basi ni mkusanyo wa fikra, mawazo na maono yanayotokana na kukubaliana fikra hizo ambayo huweka lengo la namna ya kutimiza fikra hizo kwa namna mbalimbali. Hivyo, kabla ya watu hawajakumbatia itikadi fulani ni lazima kwanza kabisa wajue kama itikadi hiyo inakubaliana na fikra zao.

Katika siasa na filosofia kuna itikadi mbalimbali ambazo zimesababisha makundi mbalimbali. Itikadi ya Kibepari kama vile ya Kijamaa ni mazao ya fikra za watu mbalimbali. Kwa upande wa Ubepari ni mazao ya watu kama kina Adam Smith na wenzake wa zama zake na miaka ya karibuni umekosolewa na kutengnezwa upya na wasomi wengine ambao wameondoka kidogo (au sana) kutoka katika fikra za kina Adam Smith. Ujamaa kwa upande wake ni mazao ya kina Lenin na Marx lakini vile vile umekuwa ukichukuliwa kwa namna tofauti na mawazo ya watu wengine.

Utaona basi watu wanaoamini kuwa uchumi ni lazima uendeshwe na watu binafsi (sekta binafsi) na kuwa soko liachwe kuamua mwelekeo wa uchumi hawa hugongana kifikra na wale ambao wanaamini serikali (state) ina nafasi katika kusimamia uchumi na hata mgawanyo wa mazao ya uchumi huo (iwe ni kugawa umaskini au kugawa utajiri). Tofauti hizi za kiitikadi kimsingi ni tofauti za fikra. Nyerere kwa upande wake alikuja na fikra zake – baada ya kusoma ujamaa wa Marx/Lenin na Ubepari wa Adam Smith na kujaribu kutengeneza (synthesize) aina ya ujamaa mpya. HIvyo, itikadi yake ya Ujamaa na Kujitegemea kinyume na watu wengi walivyoaminishwa ni mazao ya fikra za kuuelewa Uafrika na jamii yetu. HIvyo, Fikra huzaa itikadi.

Itikadi huzaa sera


Vyama vya siasa hufuata itikadi mbalimbali za kisiasa. Kutegemea na mazingira na nchi na hata historia za vyama hivyo itikadi hizo hutofautiana kwa namna mbalimbali. Kuna wale ambao wanaitwa wana msimamo kihafidhina wakati wengine ni wale wenye msimamo wa kiliberali na wengine wakiwa katikati ya pande hizo mbili na hata wenye msimamo wa pembezoni mwa pande hizo (extremes right or left). Sasa, hizo itikadi ndio huwa ndio msingi wa sera za vyama hivyo. Kwa mfano, chama cha kibepari kinachoamini katika soko na sekta binafsi sera zake za kisiasa zitaakisi ukweli huo.

Unapofika wakati wa kampeni vyama hupigia kampeni sera zao zinazotokana na itikadi zao. Sera hizo zinapokubaliwa na wananchi basi chama huingia madarakani ili kuanza kuzitekeleza. Kwa mfano, chama cha kibepari kinatunga sera ya ubinafsishaji wa mali za umma na serikali kujitoa kwenye shughuli za kiuchumi. Sera hizo zinavutia wananchi na kinashinda uchaguzi. Basi kinaanza kuzitekeleza sera hizo.

Sera huzaa sheria


Sasa chama kile ambacho sera zake zimekubaliwa na wananchi na wakakichagua kukipa madaraka basi kina haki ya kuanza kuzitekeleza sera hizo. Kama kilisema kina sera ya ubinafsishaji basi tunatarajia chama hicho kianza kubinafsisha mali za umma. Hivyo ili mpango huo ufanikiwe serikali hiyo italeta mabadiliko ya sheria na kutunga sheria zote muhimu za kusimamia zoezi hilo. Kama chama kiliahidi kitatoa elimu ya bure na kinaingia madarakani basi mara moja kinatarajiwa kuanza kuleta mabadiliko ya sheria ili kufanya ahadi zake zitimie.

Sheria huzaa miundombinu ya utendaji


Sasa ni kutokana na sheria hizo basi miundo mbinu mbalimbali huanza kutengenezwa. Hii ni pamoja na kuanza kuunda vyombo mbalimbali vya utekelezaji na usimamizi wa sera hizo. Taasisi ya kusimamia ubinafsishaji itaundwa, watendaji watatafutwa n.k Na kutoka hapo mfumo mzima wa utawala unaakisi mwelekeo wa sera za chama tawala.

Hivyo basi katika siasa tofauti ya sera ni muhimu sana kwani inaonesha tofauti ya itikadi. Kama vyama vya siasa havina tofauti kubwa ya kiitikadi ni wazi haviwezi kuwa na tofauti kubwa ya kisera na kama tofauti ya kisera ni ndogo sana baina yao basi ni vizuri zaidi kwa vyama hivyo kuungana na kushirikiana kwa sababu havina tofauti kubwa! Nalirudia wazo hili tena – kama vyama havina tofauti kubwa ya kiitikadi na kisera basi ni rahisi zaidi kwa vyama hivyo kuamua kushirikiana kuliko kushindana!

CCM na CHADEMA vimebadilishana sera na sasa vinakaribiana!

Kihistoria, vyama hivi viwili vilikuwa vinaangalia nchi na siasa za Tanzania kwa mitazamo miwili tofauti. CCM kwa asili yake ni chama cha kijamaa; kiliamini katika umiliki wa raslimali za nchi mikononi mwa wananchi na kuwa serikali ilikuwa na nafasi katika uendeshaji wa uchumi wa wa nchi. Kama chama cha Kijamaa CCM iliamini katika kugawa nafasi na utajiri wa watu wengi zaidi na hivyo kilikuwa ni chama cha “wakulima na wafanyakazi” kwani hao ndio waliokuwa wengi zaidi.

Kwa upande wake CHADEMA kilianza kama chama mbadala chenye mrengo wa wazi wa kibepari. Kilianzishwa na wafanyabiashara maarufu na watu ambao kihistoria walibeza itikadi ya kijamaa. Hawa waliamini kabisa kuwa ili Tanzania iinuke kiuchumi ilihitaji soko huru, uwekezaji mkubwa toka nje na ubinafsishaji. Sera zake kimsingi zilikuwa zimelenga zaidi katika uwezeshaji wa kiuchumi. Mwanzoni chama hiki kilionekana zaidi kuwa ni cha wafanyabiashara na kilionekana kuwa tayari kuja kukosoa sera za kijamaa za CCM.

Lakini kuna kitu kimetokea hapa katikati; CCM ikaamua kuukumbatia ubepari kwa kila namna na kwa kila kipimo wakati CDM ikitafuta mahali pa kusimamia. CCM ilipoamua kukumbatia sera za kibepari ilinyang’anya hoja ya CDM. Leo hii CCM ndio chama kinachopigia debe zaidi soko “huru”, ubinafsishaji (na ubinafsi wa ubepari bila ya shaka), uwekezaji mkubwa, kuboresha mazingira ya biashara n.k Leo hii pasipo shaka yoyote CCM ndio chama kikuu cha kibepari nchini kikikumbatiwa na wafanyabiashara wakubwa na kikinufaika na miradi ya kila namna.

Itikadi hii ya kibepari ya CCM ndio imezaa sera za kibepari ambazo ndio zimekuwa msingi mkubwa wa sheria mbalimbali nchini. Ikumbukwe kuwa ubepari haujali maskini, haujawahi kujali maskini na hauwezi kujionesha unajali maskini ukabakia kuwa ubepari. Matokeo ya ubepari mahali pote ni ongezeko la maskini. Lakini ongezeko hili linaendana na ongezeko la biashara, fedha na hata kile kinachoitwa “kukua kwa uchumi”.

Niliandika hivi majuzi juu ya jinsi Tanzania inavyofanana na Nigeria na kuwa kwa kadiri CCM itaendelea kuwa madarakani ndivyo tutakavyozidi kuwa kama Nigeria. Siku ya Jumatatu nilichokionesha kidogo hapa kimeoneshwa kwa kina na Shirika la Utangazaji la BBC la Uingereza. BBC wameonesha kuwa Umaskini Nigeria umeongezeka kwa asilimia 61 licha ya “kukua kwa uchumi”. Wapo wanaofikiria kuwa “kukua kwa uchumi” kunasababisha mara moja “kupungua kwa umaskini”! Si kweli.

Tanzania imekuwa ikikua kiuchumi lakini maskini nao wanazidi kuwepo na miaka ya karibuni hali inaonekana kuwa mbaya zaidi kwa maskini wetu. Hawa walihitaji mtetezi kwani ubepari ambao Watanzania waliambiwa na kuimbiwa kuwa ndio mwokozi wao umewageuka na kuwauma kama yule nyoka aliyemuuma chura!

Ulipofika uchaguzi wa 2010 CCM iliendelea kuuza sera zake za ubepari na CHADEMA ikajikuta inakumbatia sera za kutetea maskini, kutetea raslimali na kupigia debe nafasi ya serikali katika kuinua maisha ya wananchi. CHADEMA kikaanza kuonekana kuwa ni chama chenye mrego wa kijamaa zaidi au angalau niseme kikiwa kinakaribiana zaidi na itikadi ya Ujamaa wa Kiafrika wa Mwalimu Nyerere. Matokeo yake CDM ikajikuta inavutia maskini zaidi na watu wa chini na kuanza kuonekana ni mtetezi wa maisha ya watu wakulima na wafanyakazi.

CHADEMA wakikumbatia sera za CCM wanajiumiza wenyewe

Binafsi ninaamini ipo nafasi nchini ya sera zenye mrengo wa kijamaa – hata kama siyo ujamaa wa Lenin na Marx au hata wa Nyerere moja kwa moja. Tayari tumeona siasa hizo zina nafasi bado Afrika – Rais Michael Satta wa Zambia ameshinda na kuingia Ikulu kwa kukosoa sera za kibepari za waliomtangulia. Na siyo tu kukosoa lakini kutafuta uwiano wa sera mbalimbali ili kuweza kuinua maisha ya maskini na wale ambao hawana mtetezi.

Kwa Tanzania mtetezi huyo amepatikana ndani ya CHADEMA na hili naamini bado halijazama vizuri ndain ya baadhi ya viongozi. Upande mmoja kuna kujitambua kuwa CDM ni chama kilichoanzishwa kwa misingi na itikadi ya kibepari; hata hivyo upande wa pili hali halisi inaonesha kuwa sera za kibepari tayari zinatekelezwa na CCM na hivyo haja ya kuwepo kwa mbadala wa sera hizo. Huu ni mgongano wa kifikra (ideological conflict) ambao una matokeo mabaya sana kwa CDM kuliko kwa CCM.

Mojawapo ya matokeo yake ni kuwa baadhi ya viongozi wa CDM wanaweza kujikuta wanavutiwa na kukumbatia sera za CCM! Hawa wanaweza kujikuta wanasikiliza sera za CCM na wakajikuta wanakubaliana nazo kifikra na hivyo wakaaanza kutoa mawazo ya kuziboresha sera hizo za CCM. Ukiona viongozi wa CDM wanasifia sera za CCM na wanajaribu kuziboresha maana yake ni kuwa wanakubaliana nazo zaidi!

Maswali ya ugomvi!


Sasa kama viongozi wa CDM wanaona sera za CCM zina uzuri fulani na kuwa zinakubaliana na fikra zao ni kwanini viongozi hao au wanachama hao wasiamue kwenda kuungana na CCM na kuiboresha? Kama kwa mfano, wapo wanaofikiria kuwa sera ya maji ya CCM ni nzuri na kuwa labda ina mapungufu mawili matatu na hivyo wanasimama na kutoa maoni au “ushauri” kwa serikali ni kwanini watu hao wasiamue kwenda kule moja kwa moja ili mawazo yao yakubalike zaidi?

Kama viongozi hao wa CDM hawaoni kuwa sera za CCM ndio zimeshindwa na ndizo zimelifikisha taifa letu hapa sasa watu walio nje wataamini kuwa CDM ni tofauti na CCM? Hivi, ni kweli kuna watu bado wanaamini kuwa kuna sera yoyote mpya ya CCM ambayo inaweza kuliinua taifa? Hivi ni sera gani ya CCM ambayo tunaweza kusema imefanikiwa kiasi cha kutaka kuiiga? Sera ya nishati na madini? Sera yao ya elimu? Sera yao ya afya? Au sera ya ulinzi na usalama? Au sera yao ya kodi ni nzuri sana? Au ni sera ipi ambayo tunaweza kusema imefanikiwa kiasi cha kuitaka iendelee kuwepo? Maana kama kweli kuna sera “nzuri” za CCM ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho kidogo tu basi CDM ikae chini na CCM – wamefanya hivi kwenye suala la Katiba Mpya – na wajadiliane ili hatimaye CCM ifanyie marekebisho sera zake.

CCM ishawishiwe – kwa kumtumia rais – ili ikubali mawazo ya CDM na hatimaye CCM ianze kutekeleza sera za CDM vile vile (japo zitakuwa ni zake). Kwa kufanya hivyo, CDM haitakuwa na sababu ya kuwepo tena kama chama cha siasa. Kwa sababu kama sera zake zimechukuliwa na kutekelezwa na CCM chenyewe kinahitaji kuwa chama cha siasa kwanini? Au kinaamini kuwa jukumu lake ni “kuikosoa na kuishauri serikali”? Well, kama hili ni jukumu lake CDM ijibadilishe kutoka chama cha siasa na kuwa Kituo cha Fikra (Think Tank) ili kitoe mawazo chanya kwa CCM!

Vinginevyo


Vinginevyo, CDM iachae kukumbatia au kujaribu kuzisahihisha sera za CCM ili ziwe nzuri zaidi! Jamani wapo wana CCM wa kutosha na wenye akili ya kutosha ambao wanaweza kukishauri chama chao! Tumewaona Bungeni nan je ya Bunge. Wapo wanaoweza kusahihisha sera za chama chao na hilo ni jukumu lao! Kiongozi wa CCM au mwanachama wa CCM anaposimama jukwaani kutetea au kukosoa sera za chama chake hafanyi uasi. Anafanya lililo jukumu lake na kwa kweli binafsi namuunga mkono!

Hata hivyo inapotokea mwanaCDM au mpinzani anaanza kusifia sera za CCM au anajaribu kuziboresha kwa kuwashauri halafu anajivuna kuwa CCM inatekeleza sera “zetu” basi tuna matatizo makubwa zaidi. Siyo jukumu la CDM kufanya sera za CCM zipendeze! NI sawasawa – najua ni mfano mbaya – kwamba mwanamme anataka kuchumbia kwa mwanamke maarufu mjini na hivyo amejiandaa na sera zake kwenda ukweni. Halafu anakutana na mtu mwingine ambaye tayari anasema alishapeleka posa na kulikuwa na kama kukubaliwa anahitaji kuweka sera zake vizuri zaidi.

Sasa huyo mwingine anapokaa na kujitahidi kumshauri yule mwingine katika sera zake za posa ni kwamba anajisaidia yeye mwenyewe au anamsaidia yule mwingine? Hivi ni kweli umfundishe mtu mwingine kutongoza wakati unajua anaenda kumtongoza yule ambaye na wewe ulikuwa unamtaka? Au ni mfanyabiashara gani anayetafuta dili nzuri akakutana na mwingine ambaye naye anatafuta dili nzuri huko huko halafu akaenda kumpa mawazo yule wa pili jinsi ya kupata dili bora zaidi? Halafu yule akienda na kupata hiyo dili yule wa kwanza akienda na kukosa ataweza kweli kumlalamikia yule mwingine kwa kutumia “ujuzi” aliopewa kujinufaisha?

CDM ishambulie sera zilizoshindwa za CCM


Siri ya CDM kufanikiwa na kuendelea kukubalika zaidi ni kuonesha tofauti kati yake na CCM katika sera na mtazamo. Lakini siyo kuonesha kama kwa kuogopa bali kuonesha kwa kushambulia wazi na hadharani sera zilizoshindwa za CCM. Kuanzia sera za nishati na madini, elimu, maji, afya, barabara, maliasili na utalii, ulinzi hadi zile za Inteligensia. CDM isiogope kushambulia sera hizo kwa kuogopa kuonekana “inapandikiza chuki”. Naam, lengo hasa ni kupandikiza chuki dhidi ya sera hizo na kuwafanya watu waone tofauti iliyopo kati ya CDM na CCM. Ni muhimu kuona tofauti ya sera na siyo watu tu.

CDM isione huruma au kujisikia vibaya kushambulia sera za CCM. Kwa wale wanaofuatilia mwelekeo wa uchaguzi wa Rais wa Marekani na wabunge wa huko wanaweza kugundua kitu kimoja – wagombea wa Chama cha Republican hawana huruma na Barack Obama! Hawajali kama ni Rais na hawajali kama alikuwa maarufu sana miaka minne iliyopita. Wanachojali kwao ni kuonesha kuwa sera za Rais huyo zinaonekana kushindwa au wanajaribu kuzionesha kuwa ni sera zilizoshindwa. Hawajali sura yake, hawajali ving’ora, hawajali ana familia nzuri au vitu vingine vyovyote vile! Hawamjali hata yeye mwenyewe; wanajali kuwa sera zake zimeshindwa na kwa hilo hawana urafiki, ujamaa au undugu.

Kuelekea Arumeru CDM isiwe na urafiki wala udugu wa kisera na CCM vinginevyo wakae chini wanywe chai na waunganishe vyama ili tuwe na Chama cha Demokrasia na Mapinduzi ya Tanzania! Kama viongozi wote wa Chadema hawawezi kuwa mahali pamoja kifikra katika kushambulia sera mbovu za CCM ambazo zimeharibu sekta ya elimu, afya, nishati, madini, usalama, ulinzi, inteligensia, viwanda, kilimo, utalii n.k basi watangaze ushirikiano wa pamoja kwa kile ambacho tunauziwa kila kukicha ati kuwa ni “maslahi ya taifa”! Hakuna dubwasha nisilolipenda kama kusikia sera mbovu zinazoundwa na watu wale wale walioshindwa kuwa zinaungwa mkono kwa kisingizio cha “maslahi ya taifa!” It is absolutely offensive to the minds of those who want radical change in the country!


Kama CCM na Chadema havina tofauti kubwa ya kiitikadi na kisera, na kama wao wenyewe hawataki kuonesha tofauti hiyo kubwa (labda kwa sababu haipo au kwa sababu wanaona itawagawa wananchi) hawa wananchi wetu wanaounga mkono vyama hivi wataweza vipi kujua ni vyama tofauti?

Kama tofauti iko kwenye watu tu – kama tunavyoona siku hizi - basi vyama hivi viunganike maana vyote vinataka katiba mpya, vyote vinataka elimu bora, vyote vinataka nishati ya uhakika, vyote vinataka maisha bora kwa kila Mtanzania na vyote vinataka Watanzani wote tukae viwanja vya jangwani na kuimba tukiwa tumeshikana mikono huku machozi yanatutiririka “kumbaiya kumbaiya my Lord” tukikumbatiana, kubusiana na kupepeana huku tukikonyezana na kupongezana kwa amani, umoja, na utulivu wa wenye njaa!



Halafu turudi kwenye chama kimoja!


CHAMA CHA MAPINDUZI YA WALIOSHINDWA! Nitafute: Facebook: “Mimi Mwanakijiji”
 
Mkuu hivi watanzania wanajua sera za vyama kweli au huangalia ahadi tu wakati wa kampeni? Nina hakika hata wasomi wetu wengi hawajui sera wa itikadi wala itikisadi za vyama vya siasa vilivyopo hapa nchini hasa CDM na CCM.
 
mkuu hivi watanzania wanajua sera za vyama kweli au huangalia ahadi tu wakati wa kampeni? Nina hakika hata wasomi wetu wengi hawajui sera wa itikadi wala itikisadi za vyama vya siasa vilivyopo hapa nchini hasa cdm na ccm.

hali ndiyo hiyo, ni weli
 
Asante kwa angalizo mkuu, asante kwa kutuweka chonjo..... CCM ni wajanja sana na bila kuwa makini wanaweza kuimeza CDM, Kisera kiitikadi n.k
 
Mkuu hivi watanzania wanajua sera za vyama kweli au huangalia ahadi tu wakati wa kampeni? Nina hakika hata wasomi wetu wengi hawajui sera wa itikadi wala itikisadi za vyama vya siasa vilivyopo hapa nchini hasa CDM na CCM.

Ndio sababu ya kuandika. Siyo watu wote wanaojua jinsi miundo ya maji ya mvua na maji taka katika mji inatakiwe iwe. Lakini mafuriko yakitokea na kuharibu nyumba zao na barabara zao hawatahijita mtu kuwaambiwa ni kwa sababu ya ukosefu wa miundo mbinu hiyo. Siyo kila mtu ni lazima ajue kina na undani wa kila sera kuweza kuona matokeo yake mabaya. Anayenyeshewa na mvua haitaji kujua mvua inaundwaje!
 
Umesahau chadema haina sera mkuu..

Isipokuwa ufisadi...ufisadi...ufisadi..(sijasikia zaid ya hilo tangu nianze kuwasikiliza 2005)

Wakati huo huo wakishindwa kuthibiti ufisadi ndani ya chama chenyewe, ukabila udini na upendeleo wa wazi, na ubadirifu wa mali za chama unaofanywa na wenye chama..lol
 
Mkuu nashukuru umeliona hili kwa jicho la mbali nafikiri wenye macho na masikio watalichukuwa hili na kukifanyia kazi haraka nimejaruibu kulitazama hili muda naona moto au hari na kazi waliyokuwa nayo awali imepungua sana hajo zimekuwa hazina mshiko tna mbinu za upambanaji zibadilke kwani ccm wanatumia nguvu kubwa sana kujipanga
 
Hizo zilizoko kwenye tovuti nazifahamu nazipitia mara kwa mara za vyama vyote;

Lakini ulishawahi kuhudhuria mkutano wa hadhara wa chadema?

Mimi ni mhudhuriaji sijawahi kusikia wakiwaambia wananchi hizo sera zao ni ufisadi, ufisadi..no more..


Ndio lengo la kuwakumbusha na kukumbushana. Najua wanafanya hvyo mara nyingi tu wanazizungumzia sera zao lakini bahati mbaya wakati mwingine wanaonekana kama kujisikia vibaya kukosoa sera za CCM. Wapo ambao wanaamini sera za CCM zina uzuri fulani na hivyo zinahitaji kuboreshwa ili serikali itawale vizuri. Niliwahi kuandika huko nyuma siyo jukumu la upinzani kuishauri CCM ili itawale vizuri! Jukumu la upinzani ni kudhoofisha chama tawala ili kishindwa uchaguzi ili huo upinzani uingie madarakani kuja kutekeleza sera zake.
 
Ndio lengo la kuwakumbusha na kukumbushana. Najua wanafanya hvyo mara nyingi tu wanazizungumzia sera zao lakini bahati mbaya wakati mwingine wanaonekana kama kujisikia vibaya kukosoa sera za CCM. Wapo ambao wanaamini sera za CCM zina uzuri fulani na hivyo zinahitaji kuboreshwa ili serikali itawale vizuri. Niliwahi kuandika huko nyuma siyo jukumu la upinzani kuishauri CCM ili itawale vizuri! Jukumu la upinzani ni kudhoofisha chama tawala ili kishindwa uchaguzi ili huo upinzani uingie madarakani kuja kutekeleza sera zake.

Kwanini umechagua Chadema na siyo CUF? katika kukumbusha kwako??
 
Kwanini umechagua Chadema na siyo CUF? katika kukumbusha kwako??

Kwa sababu CDM wamekuwa tayari kupokea maoni yangu ( na ya wengine) na hawajasita kuomba ushauri au kuuliza kitu. Na ninaamini ndio chama ambacho kikijipanga vizuri zaidi kinaweza na kustahili kushika hatamu ya uongozi wa nchi! CUF siioni kihivyo.
 
Umesahau chadema haina sera mkuu..

Isipokuwa ufisadi...ufisadi...ufisadi..(sijasikia zaid ya hilo tangu nianze kuwasikiliza 2005)

Wakati huo huo wakishindwa kuthibiti ufisadi ndani ya chama chenyewe, ukabila udini na upendeleo wa wazi, na ubadirifu wa mali za chama unaofanywa na wenye chama..lol

Mkuu Topical naomba nitoke nje ya mada kidogo.

Hapo juu unasema CHADEMA haina sera, signature yako inasomeka hivi "Mbowe for Presidency 2015" ! very confusing!
 
Kwa sababu CDM wamekuwa tayari kupokea maoni yangu ( na ya wengine) na hawajasita kuomba ushauri au kuuliza kitu. Na ninaamini ndio chama ambacho kikijipanga vizuri zaidi kinaweza na kustahili kushika hatamu ya uongozi wa nchi! CUF siioni kihivyo.

Mimi kama mwana CUF nakuomba utushauri kwasababu na sisi tumejipanga kuchukua na kushika hatamu, safari yetu imeanzia visiwani tunataka kukomboa bara kwa kasi ya ajabu..

Karibu kwa ushauri wako, unahitaji malipo au ni bure???
 
Thanks a Million MMM.... its a genuine concern especially knowing that sera za CCM kwa sasa ni hasi na hazina tena future kwenye taifa hili

hakuna hata sera moja ya CCM unayoweza kuisimamia, kwani waliomo ndani wameshapoteza network and they dont know T-Mobile haishiki tanzania
 
Mkuu Topical naomba nitoke nje ya mada kidogo.

Hapo juu unasema CHADEMA haina sera, signature yako inasomeka hivi "Mbowe for Presidency 2015" ! very confusing!
hujui wengine ni wagagagigikoko?
 
Back
Top Bottom