Anaandika Mwafrika Merinyo

Alex Fredrick

JF-Expert Member
Jun 21, 2016
680
1,338
KWANINI MWANAMKE?
Mwafrika Merinyo

Kwanini abebe mimba
Abebe na jembe begani?
Kwanini abebe ndoo
Abebe na kuni kichwani?
Kwanini abebe mawazo
Sambamba na zigo la shida
Za kwendea maji mbali
Na matibabu ya mashaka na tabu?
Kwanini umbebeshe shida
Za vipigo na mengi matusi
Kwanini hasa wambebesha
Mzigo wa tabia zako dhalili
Na mirathi ya mila potofu?
Kwanini abebe malezi
Sambamba na mzigo wa lawama?
Kwanini abebe mapishi
Na adha za utafutaji juuye?
Kwanini afue nguozo
Na matapishi ya kero zako?

Umeshindwa nini
Kumtwanga ngumi za huba?
Kwanini ikushinde
Kumkaba kwa kumbatio la penzi?
Washindwaje kumkaba pumzi
Kwa mfululizo wa mabusu motomoto?
Washindwani kumtukana mwanamke
Kwa maneno “mpenzi” au “muhibu”?
Mkemee kwa neno la mahaba
Mrambe moyowe laini
Kwa tabasamu la meno yako meupe
Mpapase kifua chake chororo
Kwa mawaridi yasisimuayo
Ya ndevu zako za shaba

Mwondoshee mzigo mzito
Wa ndoo na kuni kichwani
Mletee mzigo wa maji safi
Ya bomba jirani mlangoni

Yakushindaje hayo machache
We mwanaume wa shoka?
Mbebee mwanamke mbeleko ya liwazo
Mwondoshee adha ya mengi mateso
Mfunge kamba ya wako ushirikiano
Mlevye kilevi cha maelewano
Mbebeshe zigo zito la haki
Kwa kuwajibika kwako kiume
Mtie mwanamke wazimu wa furaha
Mkogeshe moyowe kwa maji ya faraja
Washindwani kumbebesha hayo
Kiumbe umwitaye dhaifu?
Kwa umwamba na akili yako
Umeshindwaje mwanaume wa shoka?
 
Back
Top Bottom