Ameandika Pd. Titus Amigu, Serikali iingilie kati

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,011
9,876
SERIKALI ZETU ZIINGILIE KATI

Imeandikwa na Pd. Titus Amigu.

Kila taifa lapaswa kutazama mbele. Vivyo mabara yetu. Lakini katika uhalisia, mustakabali wa mataifa ya Kiafrika unatisha. Vivyo mustabali wa bara letu. Kwa kisa hicho ninaziomba serikali za nchi zetu ziingilie katika na hali kadhalika Umoja wa Afrika uingilie kati, vinginevyo tunajimaliza wenyewe.

Wazungu walitukuta dhoofu hali, sasa kwa mwenendo huu, tunajitia wenyewe “udhoofu hali” mbele ya hao wanaotutawala kwa ukoloni mambo leo. Najiuliza: katika kujifanyia hivyo tunatafuta nini? Tunatafuta nafuu au umahututi? Nitajieleza.

Mustakabali wa Mataifa Yetu Upo Hatarini

Mataifa ya Kiafrika yanaangamia kwa kukosa maarifa (Hos 4:6). Hata kama mataifa mengi ya Kiafrika yametangaza kutokuwa na dini maalumu, watu wake wanaolofazwa ni mzigo kwayo yenyewe. Raia waliolofazwa ni mzigo kwa nani kama si kwa serikali yenyewe? Raia wenye njaa ni mzigo kwa nani? Raia wajinga ni mzigo kwa nani? Raia wagonjwa ni mzigo kwa nani? Raia wanaodanganyika na chochote kile ni mzigo kwa nani?

Fikiria, raia wako wanaamini kwamba wamelaaniwa, watajiamini saa ngapi hata kuyachukua maisha yao mikononi mwao? Wao ni mzigo kuliko mifugo!

Fikiria, raia wako wanaamini ardhi za nchi zao zimelaaniwa, watajifunza saa ngapi namna ya kutumia rasilimali zao? Watajifunza lini kilimo cha kisasa?

Fikiria, raia wako wanaamini wanakumbwa na maradhi kwa sababu ardhi walipojenga nyumba zao ina mapooza, watajifunza saa ngapi kanuni za afya na lishe bora?

Fikiria, raia wako wanaamini watapata mazao mengi wakinyunyizia mashamba yao maji ya upako, watajifunza saa ngapi kilimo cha umwagiliaji?

Fikiria, raia wako wanaamini watapata mali wakinywa maji aliyooga mchungaji, watajifunza saa ngapi kutumia nguvu zao katika kilimo na ujasiriamali?

Fikiria, raia wako wanaamini watapata pesa wakivaa chupi za upako au wakila keki za upako, watajifunza saa ngapi kutumia nguvu zao katika kilimo na ujasiriamali? Watajifunza lini stadi za mikono?

Fikiria, mabinti zako wanaamini wataolewa na mabwana watakaoletwa na upepo wa kisulisuli, watajifunza lini tabia njema za kuwafaa kuwa wake za watu na mama watoto wa watoto wao?

Fikiria, vijana wako wenye nguvu wanaamini watapata nyumba kwa kukesha kwenye makongamano, watajifunza lini kufyatua matofali ya kuchoma na kujijengea nyumba zao?
Fikiria, raia wako wanaamini wakijambiwa “ushuzi” na mchungaji watapata ajira, watajifunza lini kujiajiri wenyewe?

Fikiria, raia wako wanaamini kwamba watapata nguvu za kiume wakipunguziwa nguvu za kiume na mchungaji, watajua saa ngapi kujilea wawe na nguvu za kiume?

Fikiria, raia wako wanaamini kwamba watapata magari wakifanyiwa maombi, watajifunza lini sayansi na teknolojia wajiundie vyombo vyao wenyewe?

Fikiria, raia wako wanaamini kwamba wataenda Marekani na Ulaya wakifanyiwa maombi, watajifunza wapi uzalendo wa kuzijenga nchi zao wenyewe? Si hao watakaokubali kuwa mbwa Ulaya au Marekani kuliko kuwa watu nchini na barani mwao?

Ukijumlisha Haya Yote, Hakuna la Kushangaza

Ukijumlisha yote niliyodokeza hapo juu, tunashangaa nini? Ukijumlisha haya yote, tunashangaaje nchi za Kiafrika zikiendelea kujiburuza katika umaskini wa kunuka, njaa na maradhi?

Tunashangaa nini sisi Waafrika tukiwa watembeza bakuli tu? Tunashangaa nini tunapodharauliwa na watu wa mabara mengine?

Ukijumlisha haya yote, tunashangaa nini sisi Waafrika tukipewa misaada ya aibu, ya fedha, ya mitumba hata ya chupi na sidiria? Sisi hatuna ujanja mwingine isipokuwa kutumia mitumba ya kila sampuli: vyombo vya usafiri, nguo, vyombo vya majumbani n.k. Sisi ni watumiaji wa vitu vilivyowahi kutumiwa. Sisi ni wauzaji wa vilivyowahi kuuuzwa. Sisi ni wanunuzi wa vilivyowahi kununuliwa. Aibu sana! Sisi tumezoea vya kunyonga, vya kuchinja hatuwezi!

Sasa, ukijumlisha haya yote, tunashangaa nini sisi Waafrika tukipewa misaada ya hata ya kuchimbiwa vyoo? Shule ya msingi yenye watoto 700, baba na mama zao wanashindwa kuwachimbia vyoo watoto wao hadi wanakuja Umoja wa Ulaya kufadhili vyoo. Ha! Aibu sana! Yaani Waafrika tunajua kula tu, “kujisaidia” tunashindwa! Ha! Siku hizi tunafadhiliwa hata taulo za kike. Ha! Kweli jamani!

Ukijumlisha haya yote, tunashangaa nini sisi Waafrika tukilishwa vyakula vya msaada, hata vingine vilivyotiwa sumu kusudi kuua nguvu zetu za uzazi? Watu wanalalama juu ya kupungua nguvu za uzazi siku hizi. Jiulize, kwa nini vijana wengi siku hizi wanakunywa sana vinywaji vya “energy” au kutafuta sana “vumbi la Kongo?” Je, hatujatiliwa vitu vibaya kwenye vitu vya misaada?
Vyakula na vinywaji tunavyoletewa pamoja na mitumba tunayovaa sote vina usalama gani kwetu? Hivi, mpango wa kupunguza idadi ya Waafrika kwa sumu mbalimbali, aliotangaza P. W. Botha, tarehe 15.8.1985, uliishia wapi? Tunakumbuka?
Ukijumlisha haya yote, tunashangaa nini sisi Waafrika tukipewa vyakula vibaya kama vile vya GMO? Hivi tutakula sote hata wale wanaohubiri Injili ya Mafanikio maana hata wao hawafanyi miujiza ya kuongeza mikate wala ya kugeuza maji kuwa divai.

Ukijumlisha haya yote, tunashangaa nini sisi Waafrika tukipewa dawa zenye sumu za kutudhuru? Hizo tutajitibia sote hata wale wanaojinasibu ubingwa wa kufanya miujiza maana, kiukweli, hawana uwezo wa kumponya yeyote na wala hawana uwezo wa kumfufua yeyote seuze mwanadamu.

Ukijumlisha haya yote, tunashangaa nini sisi Waafrika tukipewa mitaala ya ovyo wanayopenda wanaotulisha? Ni ukweli usiopingika kwamba wanaokamata tumbo, ndio wanaokamata vichwa!
Ukijumlisha haya yote, tunashangaa nini sisi Waafrika tukipewa misaada iliyofungamanishwa na masharti kama ya kukubali matumizi ya kondomu, utoaji mimba, ushoga na ndoa za jinsia moja?

Afrika Tushukuru na Tusali “Asante China”

Bahati yetu kidogo kuna mataifa ya kigeni wasionuia sana kutumaliza Waafrika. Hao ni Wahindi, Wachina na Warusi. Hawa tuwashukuru na kuwaombea heri mbele ya Mungu. Wanatuauni pakubwa sana.

Tunajua sote, madai ya kiungwana. Fukara wanapobahatika kupewa senti, nguo au chakula na matajiri waliowaonea huruma, huwa wanawaombea mema wahisani wao. Maneno wanayosema ni kama haya: “Mungu akubariki, akujazie mahali ulipopunguza!” au “Mungu akubariki sana!”

Sasa kutokana na jinsi Wachina walivyotuwezesha kupata usafiri mzuri (rejea mabasi ya Yutong na malori aina aina), pikipiki za bei rahisi (SANLG n.k.), nguo za bei nafuu, viatu vya bei nafuu, vyombo vya ndani vya bei nafuu, “sola” za bei nafuu, tochi za bei nafuu, radio za bei nafuu, TV za bei nafuu, daftari, peni na kalamu za bei nafuu na kadhalika, Waafrika tuwaombee Wachina heri kwa Mungu.

Tunapoingia makanisani, misikitini na kadhalika na hata tunapokusanyika kwenye makongamano tusali, “Mungu wabariki Wachina wako, wajazie pale wanapopunguza kwa ajili yetu Waafrika!” au tusali kifupi lakini mara kwa mara, “Mungu wabariki Wachina maana wanatufaa sana Waafrika!”

Nasema hivi kwa moyo wangu wote, maana tungelibwetekea maneno ya wazee wetu tu, ya eti tuna uwezo wa kuruka usiku wakati hatuwezi lolote, au ya kwamba tuna uwezo wa kuhamisha chakula kutoka mashamba ya watu wengine, wakati hatuwezi lolote badala yake tunakandwa na njaa kila mwaka, ya kwamba eti tunaweza kuleta pesa kwa vyuma ulete, wakati nchi zetu ndizo zinazotembeza mabakuli duniani, ya kwamba tunaweza kuroga, wakati Al Shabab, Boko Haramu na kadhalika wanatukosesha amani na kutuua, ya kwamba tunaweza kupata ajira kwa maombezi, wakati hatuna ajira zozote, ya kwamba Mungu anaweza kutujalia kupona kwa maombezi wakati tunaugua na kufa, ya kwamba tunaweza kupata vyeo kwa maombezi wakati hatuna vyeo vyovyote, ya kwamba tunaweza kufaulu mitihani pasipo kusoma isipokuwa kwa maombi tu wakati tunakopea mitihani au tunapata divisheni O, tungelikuwa hoi kabisa. Basi, tuseme wote kwa Wachina, “Asant!” na “Asante Mungu kwa kutuinulia waja wako Wachina!”

Usiamini Ulaghai, Wenzako Wanajenga Mahoteli

Watu wanaochukua pesa mifukoni mwetu kwa kutuuzia neno la Mungu wanatajirika binafsi. Ushahidi upo tele kabisa. Wengine wanajenga maghorofa. Wengine wananunua ndege. Wengine wanatembelea magari ya gharama. Wengine wanajenga mahoteli. Wengine wanasomesha watoto wao kwenye shule bora. Wengine wanakula vinono kweli kweli. Wengine wanavaa mavazi ya gharama sana. Wengine wanapougua wanakwenda kwenye hospitali bora. Wengine wanatembea duniani kwa ndege na kadhalika. Nakuamsha. Jitafiti sana wewe “uliyechangia huduma” hizi au zile umebakia wapi? Si hoehae bado? Huna maradhi bado? Huna ufukara bado? Ukiwete umekutoka? Upofu umekutoka? Uziwi umekutoka? Ada za watoto wako unazimudu sasa? Nyumba yako si ile ile? Mavazi yako si masurupwenye yale yale? Chakula chako si cha kuunga unga bado? Chakula chako si cha unga robo bado?
Mwafrika mwenzangu zidi kujiuliza na fanya utafiti japo mdogo.

Wangapi wamekuwa mabilionea baada ya makongamano mengi ya Arusha, Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Makambako, Mbeya, Moshi, Musoma, Mtwara, Mwanza, Njombe, Sumbawanga, Songea au Tabora? Bila shaka, hapana.
Sasa, basi, funguka macho ujue umeliwa pamoja na wenzako. Ukome basi! Makongamono ya Jangwani au Uwanja wa Benjamini Mkapa yametengeneza mabilionea wangapi au yamewaponya wangapi? Je, makongamano ya Unga Limited, Arusha? Je, makongamano ya Furahisha, Mwanza? Kwa hakika, hakuna. Maana yake? Maana yake watu wamedanganywa. Ndipo serikali ingalipofaa kuingia kati. Serilali itaachilia watu wake wanalofazwa na kuibiwa hivi hadi lini? Ushahidi wa kwamba hali ni mbaya na kwamba watu wamegota kufikiri hadi kutumaini maombi tu, upo tele. Ni jinsi viwanja na viwanja vya makongamano vinavyojaa watu pomoni. Hii maana yake hao wote wameshindwa kuwekeza katika akili na rasilimali za nchi zetu na hata kisomo hakifui dafu tena.

Nakuamsha Mwafrika mwenzangu! Asikudanganye mtu, Ulaya, Marekani, Asia (Japani, China, Korea ya Kusini n.k.) hawakuendelea kwa sala na mikesha. Wametumia akili, nguvu, jasho na rasilimali. Nguvu zingine na rasilmali zingine ni zetu sisi Waafrika. Kumbuka biashara ya utumwa, unyonyaji, ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo. Dini zisiendelee kutulofaza! Tangu zamani malengo ya dini hayakuwa haya.

Mwafrika mwenzangu usikubali kuwa ngazi ya kilofa ya mwenzako kujipatia utajiri wa bure. Ulofa huo mwisho wake Chalinze. Akili ya kuambiwa, changanya na yako. Usiwe mjinga aliwaye. Nakusihi, usiyaamini maneno ya wachungaji. Hawana kitu hao. Wenyewe wanavaa mitumba! Wenyewe wana magari ya sekendihendi! Wenyewe wana “boxer” za China! Sasa, unawaaminije?

Usiamini maneno ya waganga wa kienyeji. Hawana kitu hao. Wenyewe wananunua baiskeli na boda boda za China! Wenyewe wanakwenda hospitali na kulazwa! Wenyewe wamevaa mitumba!

Naendelea kidogo. Usiamini maneno ya wachungaji na waganga wa kienyeji eti utapata utajiri, vyeo au utafaulu mitihani pasipo jitihada au kwamba utapata mali kwa dawa fulani. Fumbuka macho! Hao wenyewe wanatafuta mali kwa usanii huo wa uchungaji au uganga wa kienyeji.

Wenyewe na watoto wao hawapati utajiri kwa maombi wala kwa dawa.
Wenyewe na watoto wao hawana vyeo vikubwa. Wenyewe na watoto wao wako hoi, kama wewe ulivyo, sasa unawaaminije?

Hapendwi Mtu bali Pochi

Mwafrika mwenzangu uwe unajiuliza. Umewahi kusikia makongamano yakifanyika vijijini: Njalamatata, Nanguruwe, Nanjirinjiri, Kingoruwila, Uyui, Kagondo au Mbigili? Bila shaka hapana. Kwa nini? Kwa sababu moja tu: Hapendwi mtu, bali pochi. Ni “ujasiriadini” haramu. Ni utafutaji wa kipato cha aibu (1Pet 5:2). Ni “kubiasharisha” Injili. Ni kuuzwa kule kule kwa Yesu na Yuda. Ni mtego ule ule wa Injili ya Mafanikio.

Makongamano yanarudiwa tena na tena katika miji minono, maana huko kuna pesa, hasa za akina mama waliokaa mkao wa kuliwa! Ashakum si matusi! Basi, amka! Ajabu, akina mama katika dhiki zao ukiwadanganya na kuvuruga nguvu zao za maamuzi, unaweza kuwapiga pesa maisha yao yote.

Wakishadanganyika, wanaweza kugombana na waume zao au na watoto wao ilimradi wachukue pesa wapeleke kwa wachungaji au waganga wa kienyeji wanaowaamini kwa mioyo yao yote. Maskini! Basi, tuwasaidie! Tusaidiane kuwaamsha akina dada na akina mama wetu. Wanaliwa mno. Ashakum si matusi tena!

Raia Maskini Wanaitesa Serikali

Hivi, raia wanapokuwa fukara kwa sababu wanabwetekea sala na mikesha “siku sita katika saba” badala ya “siku moja katika saba” alivyoamuru Mungu (Kut 20:9), na kwa kufanya hivyo wakajiumiza kwa GDP ndogo, anayehangaika na raia fukara ni nani, si serikali?

Hivi, raia wanapoteseka kwa njaa na ufukara kwa sababu ya kukodolea mno macho matunzo ya Mungu wakilialia kwenye mikutano yao ya sala, anayedhalilika kwa kuomba misaada kutoka nchi zanje ni nani, si serikali?

Anayedhalilika kwa kukopakopa kwa ajili ya raia wake ni nani, si serikali?

Hivi anayekwenda kwenye mikutano ya viongozi wenye mipango makini huko nje ya nchi, akaaibika kwa vile anavyowaongoza watu wajinga na fukara ni nani, si wakubwa wa serikali?

Ndipo hapa ninapoziomba serikali za Afrika ziingilie kati, raia wanazidi kubwetekea maneno ya kijinga. Ni ushahidi kamili wa jinsi raia wao walivyofukarika kimwili na kiroho. Afrika hatuwezi kuendelea katika ulofa huu. Serikali zetu zitusaidie kutofautisha kati ya IMANI na UPUMBAVU (Mk 7:22-23) baada ya kutusaidia kutofautisha kati ya UTAMADUNI na UFUKARA.

Kuamini kwamba kuna Mungu aliyetuumba na kutupatia akili, utashi na rasilimali ni imani. Kuamini kwamba tutapata mali kwa maji ya upako au kwa kula keki ya upako ni upumbavu. Ongeza mwenyewe mifano ya namna hii. Kulala katika nyumba mbovu ya miti ni ufukara.

Kuwaheshimu watu na kuwa wakarimu ni utamaduni. Kuvaa ngozi kiunoni tu ni ufukara, kuvaa heleni ni utamaduni n.k. Ongeza mwenyewe mifano ya namna hii, mimi nimeshachoka!

Paulo Kagame Kaonesha Mfano wa Kimwamba

Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paulo Kagame ameshayapiga mafuruku makanisa 700 na kuwafanya Wanyarwanda waanze kufikiri vizuri kama wanadamu. Wanyarwanda wameshaanza kufikiri kama watu wazima sasa. Heko! Kongole zake! Marais wengine mwigine mwenzenu.

Kumwiga mwenzenu mwenye maono si aibu hata kidogo! Ninyi ni wachungaji wa raia wenu pia. Au serikali zetu mnapata furaha gani raia wenu tunapozidi madaraja ya ujinga? Hivi kweli hampati maumivu na aibu yoyote?

Mzee wenu Pd. Titus Amigu.
 
Best ever post of 2023, i copied and kept it in my library..

Mimi siongezi kitu hapa, i agree 100%, umaskini wa akili ni umaskini wa kila kitu, elimu bora ndio ukombozi wa Taifa lolote lile na serikali ipige marufuku makanisa ya uyoga niyaite na waganga wa kienyeji, na watu wafunzwe vema kabisa kuwa kupata maendeleo njia pekee ni kufanya kazi kwa akili na bidii na akili inajengwa kwa elimu bora na mazingira bora yasiyo na uchawi au waganga au makanisa ya uyoga au makanisa tapeli tuite.. Makanisa ya utapeli ni chanzo kikubwa cha umaskini kwa wananchi, kwanza sbb huwadanganya na kuwadhoofisha kufikiri na pili huwaibia hela nyingi kwa njia ya sadaka feki.

Muda mwingi mtu kawa brain washed anasali tu, yeye ni kusali hafanyi kazi yoyote ya maendeleo kujipatia kipato, yaani anaaminishwa Mungu atashusha neema tu yaani lazima uwe maskini fukara kabisa. Watu wanaangamia sbb ya kukosa maarifa.
 
Na hili la LGBTQ linashika Kasi sans. Hali ni mbaya sana
 
Best ever post of 2023, i copied and kept it in my library..

Mimi siongezi kitu hapa, i agree 100%, umaskini wa akili ni umaskini wa kila kitu, elimu bora ndio ukombozi wa Taifa lolote lile na serikali ipige marufuku makanisa ya uyoga niyaite na waganga wa kienyeji, na watu wafunzwe vema kabisa kuwa kupata maendeleo njia pekee ni kufanya kazi kwa akili na bidii na akili inajengwa kwa elimu bora na mazingira bora yasiyo na uchawi au waganga au makanisa ya uyoga au makanisa tapeli tuite..

Ukifika mbezi luis unakutana na wachungsji kila mmoja ametega upande wake uku bakuri lipo katikati anahimiza watu kutoa sadaka na utaona watu wanaenda toa pale binfsi sifarigii hayo mambo wachungaji wengi makamisa mengi kama ugomvi hapana nahili liangaliwe
 
Maelezo mazuri mno, kwamaana hiyo tusisali,kuabudu na kuomba bali tujikite kutatua matatizo na kutafuta maendeleo kwa kufanya kazi na kuwa wabunifu. Ahsante sana hili fungu langu la kumi wacha nikajumue kuku wa kuuza nikuze kipato changu nijikwamue na umaskini wa kifedha. Ahsante Fr kutusanua.
 
Kinachowauma ni hawa viongozi wa makanisa kongwe ni kuona waumini wengi wanawakimbia na sadaka zina isha. Hamna tofauti nao hao wachungaji wa makanisa binafsi mana kama sadaka kote mnahitaji.
 
Tunahitaji mapinduzi ya ukombozi wa kifikira. Katika hizi zama za mapinduzi ya teknolojia. Haya ndiyo maandiko tunayoyahitaji hata wakielimika wachache inatosha maana yanaleta afya kwenye akili. Hakuna wa kutuambia ukweli, ingawa Tanzania tunaupenda ukweli ila siyo tuambiwe ukweli unaotuhusu. Tunapaswa kuwa na KIASI kwenye kila jambo si tu kwenye masuala ya IMANI.
 
Back
Top Bottom