Ali Kiba na studio AY na muziki Diamond muziki studio na biashara

NgugiAchebe

JF-Expert Member
Jul 11, 2016
1,025
688
ALI KIBA STUDIO, AY MUZIKI, DIAMOND BIASHARA STUDIO MUZIKI
FB_IMG_1487513188950.jpg


Wimbo Marry You ambao Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameimba na fundi wa sauti na kucheza kutoka Marekani, Shaffer Chimere Smith ‘Ne-Yo’ ni biashara yenye thamani kubwa kwa soko la Afrika.

Marry You, siyo wimbo wa kuushindanisha na soko la Tanzania, bali unamfanya sasa Diamond azidi kuvimba Afrika na unabisha hodi kwenye milango ya biashara ya muziki duniani.

Ukijaribu kuushindanisha Marry You na soko la Tanzania, siyo tu utakuwa unauvunjia heshima wimbo wenyewe, bali pia ni kukosa heshima kwa uwekezaji ambao umefanyika kufanikisha kazi yenyewe.

Marry You ni wimbo ambao unazidi kumpambanua Diamond kama msanii mwenye kasi kubwa ya kutafuta, habweteki, kila siku baada ya kufungua mlango mmoja, hakai kwenye sofa na kujisahau bali anatafuta mlango mwingine wa kumwezesha kwenda chumba kinachofuata.

Diamond angekuwa anawahi kuridhika, muziki wake ungeishia miaka mitano au sita iliyopita wakati alipokuwa anatawala soko la Bongo Fleva. Akiwa mwanamuziki aliyetumbuiza katika maonesho mengi na kuingiza fedha nyingi kuliko mwingine yeyote Tanzania.

Mwaka 2013 alianza kutafuta njia ya kung’ara Afrika kwa kufanya remix ya wimbo wake Number One, alipomshirikisha staa mtoto wa kitajiri Nigeria, David Adedeji Adeleke ‘Davido’.

Mpaka mwaka 2014, Diamond alikuwa nyota inayotambulika na kung’ara maeneo mengi Afrika. Tukashuhudia Diamond akishirikishwa na mastaa wa Nigeria kama Tiwatope Savage-Balogun ‘Tiwa Savage’, Iyanya Onoyom Mbuk, Kingsley Chinweike Okonkwo ‘Kcee’.

Afrika Kusini aliwavutia Mafikizolo na Kiernan Jarryd Forbes ‘AKA’ ambao walijisalimisha kwa mwana-Tandale Diamond na kufanya naye nyimbo. Tuendelee, Diamond alimvutia hata mkongwe Papa Wemba na walifanya kazi pamoja.

Kama Diamond angekuwa anatosheka na kuitwa mmoja wa ma-kingpin wa biashara ya muziki Afrika, angeweza kubweteka mwaka jana baada ya kutoa ngoma aliyowashirikisha ‘mafaza’ wa shoo za kibabe Afrika, P-Square.

Baada ya milango ya Tanzania na Afrika, Diamond anabisha hodi mlango wa soko la dunia. Kazi na Ne-Yo ni babkubwa, maana ukiachana na uzuri wa wimbo, muunganiko wao kikazi (chemistry) upo safi kabisa.

Ongezea pia kuwa Ne-Yo siyo mwanamuziki poa-poa, ni top class duniani na ni mshindi wa Grammy Awards. Kijana wa Kitanzania kumfikia Ne-Yo, kumleta Tanzania kufanya naye wimbo kisha kumfuata Marekani na kurekodi naye video, hiyo siyo kazi ya kuchukulia poa.

THAMANI YA DIAMOND

Diamond anaongozwa na tamaa. Anatamani kufika mahali pakubwa zaidi duniani. Na hiyo ndiyo tofauti kubwa iliyopo kati yake na wanamuziki wengine wa daraja lake Tanzania.

Tamaa ya Diamond inamwelekeza kutumia fedha nyingi kuwekeza. Na uwekezaji huo umekuwa ukimpa matokeo makubwa. Huwezi kummudu Ne-Yo, kumweka Tanzania na kurekodi naye wimbo kisha kufanya naye video Marekani bila uwekezaji.

Kuhusu tamaa bila shaka kila mwanamuziki anayo. Hata hivyo tofauti iliyopo kati ya Diamond na wanamuziki wengine ni jinsi ambavyo anashughulikia tamaa zake kuwa kweli. Anafanya uwekezaji mzuri kupata matokeo anayohitaji.

Kufanya ngoma na P-Square kisha kwenda kuwagharamia kukaa nao Afrika Kusini kurekodi video ya Kidogo, inahitaji uwekezaji.

Tofauti ya Diamond na wanamuziki wengine inaonekana pale kila mmoja anaposhika fedha na kutumia. Diamond hutumia fedha anazopata kuwekeza zaidi kwenye muziki, wakati wengine huzitumbua kwa starehe au kufanya uwekezaji mwingine nje ya muziki.

Wahenga walishatwambia kuwa mtu huvuna anachopanda. Diamond anaonekana ni mwanamuziki mwenye thamani kubwa Tanzania na Afrika yote kwa sasa, sababu ni uwekezaji ambao anaufanya kwenye muziki wake.

Hili ni somo ambalo wanamuziki wengine wanatakiwa kulichukua. Wengi ni wazuri na ubora wao studio ni mkubwa kuliko Diamond. Hata hivyo, Diamond anawashinda kwa ubora nje ya studio.

Narudia kwa msisitizo; Wanamuziki wengi Tanzania ni wazuri na wenye thamani kubwa studio kuliko Diamond. Wanaimba vizuri kuliko Diamond. Hata hivyo, Diamond ana thamani kubwa nje ya studio.

Thamani ya Diamond nje ya studio ni jinsi ambavyo hutafsiri tamaa zake za kufanikiwa kwa kuwekeza ili kupata matokeo anayohitaji. Kupata matokeo kama ya Diamond lazima uwekeze.

Ifahamike kuwa kuwekeza ni kujinyima. Kuna vitu utatamani zaidi lakini utalazimika kuviacha ili kuwekeza katika matokeo makubwa ambayo mtu unakuwa unayaota. Diamond alijinyima kwa ajili kuwekeza ndiyo maana anapata tunayoyaona.

NIMEANGUSHWA NA ALI KIBA

Mwaka jana, Ali Kiba alitoa wimbo mmoja ambao ulikuwa na thamani kubwa sana. Wimbo huo ni Aje. Kuanzia alipoutoa mpaka mwaka ulipomalizika, Aje ulikuwa kwenye chati ya juu kabisa Tanzania.

Baada ya kukaa muda bila kuachia wimbo mpya, ameamua kuachia Aje remix. Pamoja na kuwa ni utaratibu wake lakini kosa alilofanya ni kubwa.

Katika remix ya Aje, Kiba amemshirikisha rapa wa Nigeria, Jude Abaga ‘M.I’ ambaye haonekani kwenye video ya wimbo huo.

Video ya kwanza ya Aje, sehemu ambayo M.I anarapa kwenye audio, Kiba aliimba Kifaransa, hivyo kuufanya wimbo huo kuwa uliandaliwa maalum kwa ajili ya video. Kwa maana hiyo, video ya kwanza ya Aje ilikamilika vizuri.

Tatizo lipo kwenye video ya Aje remix. Kipande cha rap za M.I kipo lakini rapa huyo haonekani. Wakati M.I anarap, anaonekana Kiba na model wake wakidansi.

Hapo ndipo unaweza kuona tofauti ya Kiba na Diamond kwenye eneo la uwekezaji. Wakati Diamond anaweza kuwamudu P-Square na kufanya nao video, Kiba anashindwa kummudu M.I.

Zingatia kuwa thamani ya P-Square ipo juu mbali kabisa ya M.I, kisha ongezea kubwa kwamba Diamond kwa sasa anatamba na video mpya ambayo amefanya na Ne-Yo ambaye ni mwanamuziki mwenye thamani ya soko la dunia.

Kiba ana kasi ndogo ya kutoa nyimbo, kwani kutoka Aje mpaka Aje remix, Diamond alishatoa Je Utanipenda, Kidogo, Salome na sasa Marry You.

Hapo katikati Kiba ametamba kwa kazi za kushirikishwa na miradi ya pamoja kama Kajiandae aliofanya na Ommy Dimpoz, Nagharamia aliofunikana na Christian Bella pamoja na Unconditional Bae alioimba na Sauti Sol.

Kiba ni mwanamuziki mkubwa sana Tanzania, ana mashabiki wengi, anatakiwa kuitetea hadhi yake kwa kufanya kazi nzuri kwa kasi. Vilevile kutimiza matarajio ya soko. Kiba hatarajiwi kushindwa kummudu M.I na kufanya naye video.

UWEKEZAJI WA DIAMOND

Suala la Diamond kuwekeza siyo tu kwenye kufanya kazi na akina nani na kupata matokeo ya asilimia 100 kuanzia kwenye audio na video, bali pia katika promosheni. Diamond anawekeza sana kwenye promo na anavuna anachopanda.

Ambwene Yessayah ‘AY’ ameshafanya uwekezaji mzuri kwenye nyimbo zake na wasanii daraja la kwanza Afrika na duniani lakini uwekezaji wake kwenye promosheni ni mdogo.

Nguvu ambayo Diamond anaitumia kuwekeza kwenye promosheni ya nyimbo zake, kama AY angeitumia japo nusu yake, angekuwa anatikisa duniani kwa sasa.

Maana yake ni kuwa AY amekuwa mwekezaji mzuri kwenye muziki kuliko biashara. Thamani ya muziki wa AY ni kubwa lakini thamani ya biashara ya muziki wa AY siyo kubwa.

Nitakupa stori ya miaka sita iliyopita; wakati juzikati vyombo vya habari viliripoti kwa shangwe story ya blog inayomilikiwa na rapa 50 Cent Marekani kuandika habari ya kolabo ya Diamond na Ne-Yo, AY alitisha miaka sita iliyopita.

Mwaka 2011, AY aliandikwa na mitandao mingi Marekani, ukiwemo wa bilionea Russell Simons, alipotoa ngoma inayoitwa Speak With Ya Body, aliyomshirikisha Romeo na mrembo La’Myia Good.

Romeo ni rapa world class. Jina lake ni Percy Romeo Miller. Kwa sasa hupenda aitwe Maserati Rome au kwa kifupi Rome, zamani aling’ara na jina Lil Romeo. La’Myia ni mwanamuziki mzuri, japo hajawahi kukwea matawi ya kumng’arisha duniani lakini anafahamika na ana heshima kubwa Marekani.

AY aliwezaje kuingia studio na wakali hao na kupakua ngoma? Hiyo ni stori nyingine ya kuvutia. Ilikuwa hivi, mwaka 2010, mkali wa Reggae Fusion, Kisean Anderson ‘Sean Kingston’ alikuja Bongo kutumbuiza katika sherehe za baada ya tuzo za Kili (Kilimanjaro Tanzania Music Awards).

Kasi nzuri ya AY ilifanikisha kumpata Sean Kingston na kurekodi naye ngoma. Wakati wimbo huo ukiwa haujatoka, prodyuza tajiri Marekani, Percy Robert Miller ‘Master P’ alimtembelea Sean Kingston studio.

Master P alipomtembelea Sean Kingston, alipata pia fursa ya kusikiliza nyimbo mbalimbali za Mmarekani huyo mwenye asili ya Jamaica, na katika madude yaliyopenya kwenye masikio yake, ilikuwa ngoma ya AY aliyomshirikisha Kingston.

Master P akaomba kusikiliza sauti ya AY tena na tena, akamwambia Sean Kingston kuwa amevutiwa na AY hasa aina yake ya kurap Kiswahili. Master P akasema yupo tayari kugharamia wimbo kati ya AY na mwanaye, yaani Romeo.

Sean Kingston hakuwa na hiyana, akamuunganisha AY na Master P. AY alirekodi sauti kwenye studio za B Hitz kisha akaituma Marekani. Master P akaukalia kitako wimbo huo kwenye studio yake ya No Limit Records na kutoa kitu Speak With Ya Body kama kinavyosikika.

Master P akagharamia video. AY akakwea pipa mpaka Hollywood, akawa staa wa kwanza Bongo kufanya video Hollwood. AY aligharamia model na watu wa ziada kwenye video (extras) pamoja na nauli zake na malazi. Gharama zote nyingine zililipwa na Master P.

Siyo hapo tu, Master P mwenyewe aliuza nyago kwenye video hiyo. Kimsingi Speak With Ya Body ulipaswa kuwa wimbo ambao ungemtangaza AY kimataifa na kumfanya atambe Afrika lakini haikuwa hivyo. Maana yake hakuufanyia promosheni ya kutosha.

Matokeo yake Speak With Ya Body ni wimbo wenye hadhi kubwa lakini hauna umaarufu kwa watu. Wimbo huo haukupaswa kupoa bila kuwa na matokeo yenye heshima kulingana na hadhi yake. Sababu ni AY kushindwa kuupa promo ya kutosha.

AY alirejea tena Hollywood kufanya video na Sean Kingston, wimbo unaitwa Touch Me, ndani yake mrembo chotara wa Trinidad na Marekani, Jeanette-Triniti Marilyn Bhaguandas ‘Ms Triniti’ ameweka sauti na ni bonge la wimbo kusikiliza na kutazama kichupa chake.

Hata hivyo, Touch Me haujasumbua mawimbi ya Tanzania kutokana na hadhi yake wala haujamfanya atambe Afrika. AY anabaki kuwa mkali wa kurekodi nyimbo zenye hadhi kubwa kimuziki lakini siyo kibiashara.

Unawazungumzia P-Square? AY aliimba nao kitambo. Sauti Sol wakiwa hawajawa na umaarufu wa sasa, AY aliwaona na kufanya nao ngoma I Don’t Want to be Alone ambao ni mkubwa na hautakufa.

AY ni msanii mkubwa sana ambaye hufanya uwekezaji mkubwa kwenye muziki wake. Uwekezaji huo kwenye muziki AY angekuwa anaufanya kwenye biashara, kwa kufanya promosheni ya kutosha, hakuna ambaye angekuwa anasimama mbele yake Afrika.

Diamond anachokifanya ni mbele kidogo ya AY, kwamba baada ya uwekezaji kwenye muziki mzuri, anawekeza zaidi katika biashara. Na biashara ni matangazo. Diamond anajitangaza kuliko msanii yeyote Tanzania.

Kujitangaza maana yake ndiyo kujiweka sokoni, bidhaa inayojulikana zaidi ndiyo hununuliwa. Unaweza kufanya muziki mzuri na wenye hadhi kubwa lakini watu wakawa hawaujui. Lazima kujitangaza.

NAOMBA NIHITIMISHE

Ali Kiba ni mbabe sana ndani ya studio. Sauti yake ni silaha hatari. Ni kama Barnaba, Ben Pol, Jux na wengine kibao, ni wababe hasa wanapokuwa studio. Sauti zao huwapa umahiri ndani ya booth (chumba cha kuingizia sauti).

AY na Diamond ni wababe kwenye soko la Tanzania na Afrika kwa kuupa hadhi muziki wao kuanzia audio mpaka video. Wanapoamua kurekodi wimbo na staa wa kimataifa basi watampata kwa audio na video. Hawashindanishwi na yeyote Afrika Mashariki.

Diamond mtemi wa biashara. Studio utamuona wa kawaida lakini ubabe wake utauona kuanzia kwenye kuutafutia hadhi muziki wake, mwisho anawafunga wenzake magoli mengi kwenye biashara. Anajitangaza sana.

Ndimi Luqman MALOTO

Tovuti: www.luqmanmaloto.com
 
Sawa ila kashfa za ngada zinawaharibia sana. Ukishaanza kukimbizana na polisi sio dalili nzuri na inaharibu sana image - binafsi na biashara pia.
 
Ni makala nzuri yenye upembuz WA kina unaozingatia ukweli na research ya kina,lakini washabiki WA baadhi ya wanamziki uliowataja hapo ambao huwa hawataki ukweli watasema wewe ni team diamond Mara umelipwa na diamond na vitu vingine vingi vya hovyo.lakini ni ukweli mtupu uliouandika wakubali wasikubali Kiba na wenzake wanajibakiza zaidi Tanzania wakati mwenzao diamond anavuka zaidi ya afrika.makala yako ni 5 star
 
Master P akagharamia video. AY akakwea pipa mpaka Hollywood, akawa staa wa kwanza Bongo kufanya video Hollwood. AY aligharamia model na watu wa ziada kwenye video (extras) pamoja na nauli zake na malazi. Gharama zote nyingine zililipwa na Master P.

Siyo hapo tu, Master P mwenyewe aliuza nyago kwenye video hiyo. Kimsingi Speak With Ya Body ulipaswa kuwa wimbo ambao ungemtangaza AY kimataifa na kumfanya atambe Afrika lakini haikuwa hivyo. Maana yake hakuufanyia promosheni ya kutosha.

Matokeo yake Speak With Ya Body ni wimbo wenye hadhi kubwa lakini hauna umaarufu kwa watu. Wimbo huo haukupaswa kupoa bila kuwa na matokeo yenye heshima kulingana na hadhi yake. Sababu ni AY kushindwa kuupa promo ya kutosha.
 
Makosa mengi ya kimantiki katika makala hii. Mfano, unaposema utanipenda ya Diamond, na Nagharamia ya Kiba nq Bela zimetoka baada ya Aje unakuwa unapotosha. Na kingine haya mambo ya kuwashindanisha wasanii yataisha lini?Wote ni vijana wa Kitz wanaojitafutia riziki yao halali kupitia mziki. Tuwape support!
 
Kudos aisee hapa hakuna ukiba wala umondi ukwel tumeusikia full stop anaesika na asikie
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom