‘Aika mbe’ Kamanda Fabian Masawe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

‘Aika mbe’ Kamanda Fabian Masawe

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzito Kabwela, Jan 30, 2012.

 1. Mzito Kabwela

  Mzito Kabwela JF-Expert Member

  #1
  Jan 30, 2012
  Joined: Nov 28, 2009
  Messages: 17,520
  Likes Received: 1,691
  Trophy Points: 280
  NIANZE makala hii kwa usemi wa lugha maarufu mkoani Kagera, Kihaya, usemao kwamba "ebitagira mahyo tibyera". Usemi huo hauna tafsiri ya moja kwa moja katika Kiswahili isipokuwa kwa maelezo yaliyozunguka ili kupata maana yake.

  Ni kwamba Wahaya wanaamini kwamba mtu akiwa analima shambani asipopata mtu wa kumpa pole ya kazi mazao anayoyalima hayawezi kusitawi vizuri. Lakini hata hivyo mantiki ya usemi huo ni kwamba juhudi zozote zisizothaminiwa inakuwa ni kazi bure.

  "Ebitagira mahyo tibyera".
  Nimeanza na maelezo hayo kusudi nipate kueleweka katika kusudio langu la makala hii ya kumpongeza mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Masawe, kwa juhudi zake anazozionyesha za kuuinua tena mkoa huo ambao kwa miaka ya karibuni uliporomoka sana kimaendeleo.Itakumbukwa kwamba tangu enzi za wakoloni kulikuwepo na jamii za makabila mawili katika iliyokuwa Tanganyika zilizokuwa juu kimaendeleo ambazo ni Wahaya na Wachaga.

  Kuwepo juu kimaendeleo kwa jamii hizo mbili kulileta aina ya ushindani kati ya Wachaga na Wahaya, ushindani wa kimaendeleo wa kutaka kuonyesha nani zaidi kati yao.
  Ni katika hali hiyo kulipojitokeza imani kwamba Mhaya asingeweza kuongea Kichaga wala Mchaga kuongea Kihaya.

  Lakini kwa sasa hayo yamekwisha na kubaki kwenye historia.
  Hiyo inatokana na ukweli kwamba hakuna tena ushindani wa kimaendeleo kati ya jamii hizo mbili ambapo hali halisi kwa sasa inaonyesha kwamba Wachaga wamewaacha mbali Wahaya kimaendeleo. Huo ni ukweli usio na ubishi.Hilo linajidhihirisha kwa njia mbalimbali.

  Nakumbuka siku moja nilimshukuru kiutani rafiki yangu Mchaga kwa lugha yake kwa kumwambia ‘aika mbe' jamaa mmoja aliyekuwa karibu akabaki mdomo wazi akisema kwamba kweli dunia sasa imebadilika!
  Akaongeza kuwa zamani Mhaya kuongea Kichaga au Mchaga kuongea Kihaya ilikuwa sawa na Mwislamu kula nyama ya nguruwe! Lakini kwa sasa Wachaga wanaongea Kihaya na Wahaya wanaongea Kichaga. Hiyo ni kwa sababu upinzani uliokuwepo wa kimaendeleo kati yao haupo tena. Tumekubali yaishe.Lakini hata hivyo nimegundua kwamba ukosefu wa ushindani wa kimaendeleo si jambo jema.

  Unadumaza maendeleo kwa ujumla. Kunapokuwa hakuna changamoto kutoka upande wowote ni vigumu jamii kupaona mahali ilipozembea ili ipafanyie kazi.
  Kutoweka kwa ushindani wa kimaendeleo uliokuwepo kati ya jamii ya Wachaga na jamii ya Wahaya ni jambo ambalo haliwafurahishi Wachaga, pamoja na kuonekana kwa sasa wako mbele ya Wahaya kimaendeleo.Kumbe Wachaga wangependa ule ushindani wa karibu kati yao na Wahaya uendelee ili uzidi kuchochea kasi ya maendeleo.

  Ukweli wa jambo hilo umedhihirishwa na uteuzi wa Kanali Fabian Masawe, Mchaga, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Katika maneno yake, Kanali Masawe, anaonyesha kutoka rohoni mwake jinsi anavyosononeshwa kuuona mkoa ambao ulikuwa ukitamba kwa maendeleo ukiwa ni mfano kwa ajili ya mikoa mingine kuiga, ulivyorudi nyuma kwa kasi ya kutisha.
  Ni kwa sababu hiyo Kanali Masawe ameamua kuupeleka mchakamchaka mkoa huo ili kujaribu kuurudisha katika kiwango ulichokuwa nacho huko nyuma.

  Moyo huo alio nao Masawe wa kuuinua Mkoa wa Kagera siwezi kusema kwamba unatokana na bidii tu ya uchapa kazi ni lazima kuna kitu cha ziada, kuna msukumo wa ziada. Na msukumo huo ni historia niliyoiongelea kidogo hapo juu.
  Si kwamba mkoa huo mpaka unadorora kiasi hicho haukuwa nao wakuu wa mkoa, maana kwa kipindi cha karibu miaka 30 na zaidi mkoa huo umekuwa nao wakuu wa mkoa kadhaa wakichapa kazi ila kwa namna tofauti na namna anavyofanya Masawe kwa wakati huu.

  Waliomtangulia walichapa kazi lakini hatahivyo mkoa ukawa unarudi nyuma badala ya kusonga mbele.
  Pia wapo waliokuwa wakienda Bukoba kwa vitisho wakisema kwamba mkoa huo muda wote umekuwa juu kimaendeleo kwahiyo ingebidi ufunge breki na kuisubiri mikoa mingine.Vilevile yupo aliyewahi kutamka kwamba mie nimekuja kiboko yenu mtanitambua!

  Katika hali kama hiyo ni kitu gani kingeuzuia mkoa huo usidorore?
  Kwa kuyakumbuka hayo ndiyo maana nasema utendaji wa Masawe una kitu cha ziada zaidi ya uchapa kazi. Masawe ni lazima anasukumwa na historia ya jamii ya mkoa wake na ile ya jamii ya mkoa anaoutumikia kwa sasa.

  Bila shaka anashangazwa na kusikitishwa na tofauti inayojionyesha kwa sasa kati ya jamii hizo mbili, jamii zilizokuwa zimekabana kimaendeleo miaka ya nyuma.
  Kwa kuzitumia sifa alizo nazo Masawe ameanza kuonyesha matumaini ya kuuinua Mkoa wa Kagera na kutaka kuurudisha tena kwenye chati. Na kwa vile anaonyesha dhamira inayotoka rohoni mwake, dhamira yenye msukumo wa kihistoria, sina shaka atafanikiwa kutimiza lengo.

  Lengo la kuuona Mkoa wa Kagera ukirudi katika ushindani wa kutambiana kimaendeleo na Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa mingine ambayo nayo kwa sasa imechomoza kimaendeleo.Kama ninavyoonyesha, Masawe ni kamanda mstaafu wa jeshi. Hiyo ni sifa ya kwanza inayoonyesha kuwa mkuu huyo wa mkoa yuko tayari kuongoza katika hali yoyote ngumu.

  Kama alikuwa tayari kuongoza katika hali ya vita, au katika vita, sioni ni ugumu gani utakaomfanya ajione mnyonge katika hali ya amani na kushindwa kuwaongoza raia dhidi ya ufukara usio na silaha wakati alizoea kuwaongoza wanajeshi katika mapambano ya silaha.
  Sifa nyingine ni kwamba yeye ni mwalimu kitaaluma.

  Mwalimu anazo mbinu na maarifa ya kumwezesha mtu kukielewa kilichokusudiwa.
  Kwa sifa hiyo Masawe anayo nafasi ya kuwafanya wana Kagera wauone ukweli wa kwamba wamerudi nyuma sana kutoka pale walipokuwa miaka ya nyuma, na si kuuona ukweli huo tu bali kuuchukia na hivyo kutamani kurudi kwenye nafasi yao waliyokuwepo na hata zaidi.

  Fikiria Wahaya, kabila moja maarufu mkoani Kagera, lililokuwa linajivunia elimu kiasi cha kujulikana kiutani nchi nzima kama "nshomile" kwa maana ya nimeelimika, sasa hivi shule zilizo katika maeneo yao ndizo zinazofanya vibaya zaidi katika mitihani ya taifa!
  Neno "nshomile" limebaki kutumika tu katika utani uliojaa kebehi.

  Haiwezekani watu wa jamii hiyo wafanye madudu kielimu halafu neno hilo liendelee kuwa na maana.
  Lakini kulingana na mikakati aliyonayo Kanali Masawe kwa upande wa elimu, na ikizingatiwa kuwa yeye ni mwalimu kitaaluma, nina imani kwamba atawarudisha kina "nshomile" kwenye majivuno yao hayo yakiwa ya kweli na siyo majivuno ya kubaki wameegemea kwenye historia ya kwamba iliwahi kutokea eneo lao likatoa wasomi.

  Yeye anataka Bukoba na Kagera kwa ujumla paendelee kutoa wasomi wa kweli kweli kama ilivyo mkoani Kilimanjaro, kusudi wengine watakapokuwa wanasema wale ni kina "nshomile" wawe ni nshomile kweli na siyo kebehi.
  Kudorora kwa Mkoa wa Kagera kulikuwa kumeingilia tabia mpaka tamaduni za watu wa mkoa huo!

  Mfano kabila la Wahaya ni moja ya makabila yenye utamaduni wa usafi hapa nchini.
  Ni utamaduni huo uliowaepusha na milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu ambayo imeyasakama makabila karibu yote nchini isipokuwa Wahaya tu.Lakini kwa miaka ya karibuni utamaduni huo ulianza kuingiliwa na kuonekana kama unabadilika.

  Hali halisi ya mabadiliko hayo ilikuwa inajionyesha mara tu mtu alipokuwa anaingia katika mji wa Bukoba, mji ambao umo katika eneo la Buhaya.
  Uchafu ndio uliokuwa ukitangulia kumkaribisha mgeni aliyekuwa akiingia kwenye mji huo na kuyaonyesha mabadiliko yaliyokuwa yanaukabili utamaduni wa Wahaya.Kwa sasa jambo hilo nalo linaonekana kushughulikiwa kiukamilifu na Kamanda Masawe.

  Kwa mujibu wa mwandishi Joyce Lobozi aliyezungumza na mkuu huyo wa mkoa hivi karibuni, Kanali Masawe anasema mwitikio wa wananchi katika kuyaweka mazingira kwenye hali ya usafi ni mzuri.
  Masawe amejipangia kila siku ya Alhamisi kuwa siku ya kukagua usafi katika maeneo mbalimbali mkoani humo. Kwa maana hiyo Bukoba bila uchafu inawezekana, kama ilivyowezekana huko nyuma.Pamoja na hayo yote ningependa nimkumbushe Kamanda Masawe kitu kimoja.

  Ni kwamba mganga yeyote hawezi kuutibu ugonjwa asiouelewa. Mtu anayeumwa tumbo lakini akienda kwa mganga anadai anaumwa kichwa ni vigumu kupata msaada wa mganga.
  Ni kwamba tofauti na ilivyozoeleka kwamba Wahaya ni watu wanaojipendelea, ukweli ni kwamba Wahaya ni watu wa ajabu sana. Tunaweza kujiuliza, iweje watu wanaojipendelea maendeleo yao yarudi nyuma kwa kasi ya kutisha kiasi hiki?Hilo ni tatizo la kuumwa tumbo lakini kwa mganga ukadai unaumwa kichwa, mganga atatibu kichwa huku tumbo likiendelea kukusumbua.

  Tatizo la kweli linaloisumbua jamii ya Wahaya, jamii kubwa kuliko zote mkoani Kagera, liko hivi. Wahaya hawana umoja wala mshikamano. Anapotokea mmoja akapatwa na tatizo inakuwa shangwe kwa wengine, wataanza kusema, muache aipate…..kakoma kuringa…..kaisha yule na kadhalika.
  Likimpata mwingine naye itakuwa hivyohivyo. Hawana wazo la kuunganisha nguvu ili kulikabili tatizo linaloanzia kwa mmoja kusudi lisisambae kwa wengine.

  Matokeo yake ndiyo haya, mkoa uliokuwa kinara sasa unaburuza mkia!
  Akitokea mtu kwenye jamii ya Wahaya akatoa wazo lenye manufaa kwa jamii nzima ni nadra sana wazo hilo kuungwa mkono wala kukubalika. Imani iliyozoeleka ni ya kwamba mtoa wazo ataringa iwapo wazo lake litaleta mafanikio.Kwahiyo ili kumkomoa, bila kuelewa kuwa wanajikomoa wenyewe, watalipinga wazo hilo kwa nguvu zao zote.

  Mambo yatalala doro, watabaki kwenye shida ileile ilimradi wasionekane wamemnufaisha aliyetoa wazo la kuimaliza shida inayoleta usumbufu.
  Jambo lililotokea kuwa maarufu sana kwa kina "nshomile" ni kwamba pakitokea mtu akapata nafasi ya juu atahakikisha chini yake anapajaza watu wa jamii yake, lengo si kuwainua, atahakikisha wanabaki hapo muda wote wa uhai wake, ili aweze kuwapata watu wa kumsujudia kwa gharama rahisi.

  Wasiolielewa tatizo hilo wanawachukulia watu hao kuwa wanajipendelea na wana ukabila!
  Kwa ufupi ni kwamba kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Mkoa wa Kagera yamerudishwa nyuma na hulka hizo za ajabu za wakazi wa mkoa huo. Kwahiyo mtu wa kuusaidia mkoa huo ni lazima kwanza atafute namna ya kuwashawishi wakazi wa mkoa huo wajaribu kubadili tabia na mitazamo yao, hasa tabia ya "kantamuhira" neno lenye maana ya sitaki niungue kwa ajili yake, neno linaloleta maana ya kuwa na roho ya korosho.

  Nimeyasema haya kwa nia njema kabisa ili Kamanda Masawe aweze kulijua tatizo lililojificha na kutafuta namna ya kulipatia tiba, kama kweli amedhamiria kuuona Mkoa wa Kagera unainuka tena na kurudi kwenye ushindani wa kimaendeleo na Mkoa wa Kilimanjaro kama ilivyokuwa tangu zamani. Maana Waswahili walisema kwamba mficha maradhi…..msomaji utamalizia mwenyewe.


  Tahadhari yangu kwa Kamanda Masawe ni kwamba katika uchapaji kazi wake aiache demokrasia ichukue mkondo wake.
  Historia inatuonyesha kwamba wote waliojaribu kutumia uchapaji kazi wao kama kishawishi cha kuichokonoa demokrasia waliishia kuangamia bila kupewa shukurani yoyote kwa mambo mazuri waliyokuwa wameyatenda.Nimalizie kwa kueleza kiini cha matumaini niliyonayo kwa Kamanda Masawe.

  Nimemfahamu Kanali Fabian Masawe tangu akiwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee iliyo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa, Mgulani, Dar es Salaam. Mafanikio aliyoyaonesha katika shule hiyo, kutoka shule changa hadi kufikia kuwa shule ya kuchuana na shule kongwe za jijini Dar es Salaam na katika taifa kwa ujumla, ni mafanikio yasiyo ya kubeza.

  Ni mafanikio hayo yanayonipa imani kuwa hata kule Kagera ataweza.
  Wahaya wanasema: "ebitagira mahyo tibyera", ndiyo maana hata mimi nataka nimshukuru Kamanda Masawe kwa lugha yake, "Eka Masawe saa". Najua kule Bukoba watakuwa wanamuita Mangi kama tulivyozoea kuwaita wanaume wa Kichaga kote tunapowaona.

   
 2. TODO

  TODO JF-Expert Member

  #2
  Jan 30, 2012
  Joined: Jul 14, 2011
  Messages: 219
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Kazi yako sio rafiki wa wasomaji.tafadhali weka paragraphs.nilianza kuisoma lakini nimekuta napata tabu bila sababu.
   
 3. TECHMAN

  TECHMAN JF-Expert Member

  #3
  Jan 30, 2012
  Joined: May 20, 2011
  Messages: 2,677
  Likes Received: 162
  Trophy Points: 160
  sasa si uirekebishe ikae vizuri ili wote tusome, imekaa kama vile imechapwa na mtoto wa darasa la kwanza,
   
 4. l

  luckman JF-Expert Member

  #4
  Jan 30, 2012
  Joined: Oct 11, 2010
  Messages: 1,202
  Likes Received: 174
  Trophy Points: 160
  anaweza kuwa na mantiki sema uandishi wake sio, namshauri abonyeze edit then aitenge kwenye paragraph!kasinge waitu kumpuliliza!
   
 5. PakaJimmy

  PakaJimmy JF-Expert Member

  #5
  Jan 30, 2012
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 16,236
  Likes Received: 308
  Trophy Points: 180
  TTOZI BWEKA= ZITTO KABWE..............By MTM!
   
 6. MNYISANZU

  MNYISANZU JF-Expert Member

  #6
  Jan 30, 2012
  Joined: Oct 21, 2011
  Messages: 7,056
  Likes Received: 41
  Trophy Points: 145
  Ipange upya kazi yako watu tuisome! Unakuwa kama mtoto wa chekechea bwana.
   
 7. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #7
  Jan 30, 2012
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
  Hii naona kama vile imetulia!
   
Loading...