Agano Jeusi

Sonko Bibo

JF-Expert Member
May 24, 2019
286
286
Nionyeshe tajiri ambae njia zake hazijaunga kwa shetani, Nikupe hii..... bure. Aliniambia huku kanikazia macho.
Muonekano wake haukuakisi uwezo wake hata kidogo. Shuka nayo...
 
Now we go,,,

A G A N O J E U S I .1

Miaka sasa imesonga, nimekua mtu mzima.

Lakini najuta maana naukumbuka utoto wangu ambapo hatma yangu ya siku ilikuwa kwenye mikono ya Wazazi.

Yaani nikihisi njaa basi nitalia weee! ili nitimiziwe hitaji langu. Tofauti na leo hii ambapo mimi ndiye mwenye jukumu hilo kwa wanangu wawili.

Naachaje kujuta sasa wakati kila kitu sina, kazi sina, elimu sina, biashara sina, mnyororo wa ukoo wangu wote mimi ndiye jicho la matumaini kwao maana niko mjini wao wako vijijini……. Imani yao?,,<<< Mjini tunachezea pesa>>>.

Wanaweza kuwa sawa, maana ukiwatazama sana hawa vitukuu vya Eva wanavyovaa ni kama wanakutahadharisha kuwa, kumiliki pesa yataka moyo wa bastola na pesa haikai kwa mjinga...

Namkumbuka mama yangu kipindi kile nikiwa mdogo ananiambia, “Mwanangu usiwekeze ujana wako kwenye starehe na zinaa. Maana huko kuna mitego ya kila namna. Najua tu watakupenda kutokana na kwamba una juhudi, hivyo juhudi zako zinashawishi kuwa mbeleni watapata mtelemko kwako, usikubali kuwa punda wa hao wanawake kwani watakuigizia kuwa wanakupenda kwenye nyakati za mkate na asali.

Lakini ukweli ni kinyume chake,we jitahidi tu kuwajali wanao na mkeo na wao pia usijitoe kwao kupitiliza maana hawatakulipa bali utafanya kama jukumu lako.”

“Sawa mama nimekuelewa na nitajitahidi sana nizingatie haya unayoniambia” Nilikuwa nikijibu.

“Nashukuru mwanangu kama umenielewa. Jitahidi sana kupambana ili ukae mbali na maisha ya dhiki si unamuona baba yako alivyo?

Kuna siku mlishawahi kulala njaa labda?”

Mimi: Hapana.

Mama: Basi na wewe nataka uwe kama baba yako ili uje kuiepuka laana ya kutelekeza watoto.

Mimi: Sawa mama nimekuelewa.

Ni kumbu kumbu tu maana leo hii wazazi wako kijijini huko nguvu zao zimepungua kifupi wanakula kile walichohifadhi wakati wa utafutaji wao. Si vyema kwangu kuanza kutaka sehemu ya fao lao hilo.

Maana hata wakinipa haliwezi kunifikisha sehemu mimi na familia yangu, hivyo kila mmoja abebe mzigo wake kwa nguvu zake mwenyewe.

Nikiwa nimekaa napokea simu kutoka kwa rafiki yangu Hamadi, huyu ni rafiki yangu wa tangu shuleni japo niliishia kidato cha pili. Kutokana na changamoto za kifedha.

Hamadi ananiambia kuwa kuna mchongo sehemu, anahisi unaweza ukanifaa kwa pesa za matumizi. Hivyo niwahi mpaka maeneo ya kawe Ukwamani ambapo nitamkuta hapo ili tuongozane pamoja.

Mimi naishi Temeke mitaa ya nyuma ya Giraffe Hotel, mtaa maarufu kwa jina la Ngeta.

Basi kwa kuwa ni mida ya saa sita na kama ulijuavyo jiji la Dar mida hii, kwa nyumba zetu za uswahilini ni kwamba panatokota haswa.

Hivyo nachota maji kidogo kwenye jaba na kuingia maliwatoni kujimwagia, baada ya dakika ishirini niko pale kituo cha basi cha Hospitali nadandia daladala la kwenda mwenge maana za kawe ni kama leo hazitaki kuja.

Nikiwa kwenye gari mara nasikia majamaa wawili wakisema “Yaani yule fara ana pesa mwanangu halafu bado mdogo sana ukimuona, daah watu wengine sijui hata walizaliwaje?”

Maneno haya yananivuruga sana akili maana ukizingatia mimi ndio kwanza naitafuta miaka thelasini na tano lakini sijajipata.

Ukaja ule msemo wa <<<<Ukitaka kufanya mambo yako usiyazingatie ya watu>>>.

Ni kweli maana hatukutoka huko kwetu mbwinde kuja kujua nani anatumia pesa zake vibaya, ama nani amepata pesa zake kwa njia haramu. Zaidi ni kwamba tumewaacha wazazi wetu wakiomba dua njema ili tufanikiwe.



Nikiwa kwenye lindi la mawazo nilishituliwa na mlio wa simu, kucheki alikuwa ni Hamadi, nikapokea.

“Oya mwanangu Mswati, mbona hufiki tu kwani umepanda baiskeli?

Mimi: Nisubiri kidogo Mswati nafika muda sio mrefu,

Hili ni jina maarufu baina yetu maana tunaitana hivyo kutokana na namna tulivyokuwa tukimkubali yule mwamba wa Swaziland kwa kuoa wanawake wazuri kila mwaka.

Simu ikakatwa, baada ya muda wa kama lisaa na dakika kumi tulifika mwenge kipindi hicho stendi haijahamishiwa makumbusho.

Fujo zilikuwa ni nyingi na hapa kila mwanamke unaemuona basi ni kama kajiumba mwenyewe, yaani ile kwamba alikuwa anaona tako la huku limepwaya anajiongezea tu.

Kifupi huchoki kuwaangalia vile wanavyojizungusha hapo stendi wakijifanya wanatafuta nguo huku wakiwa wapo mingo.

<<<Unaambiwa jichanganye uishe>>>.

Muhuni nikashuka kutoka kwenye gari ile, konda kazungukwa na watu kibao akiwa anadai nauli miksa kurudisha chenji. Nikazuga kama najisachi, nikazunguka nyuma ya gari fasta nikavuka barabara hadi upande wa pili nikadandia hiAce ya kwenda kawe.

Hii mia nane itanisaidia kununua dagaa-mchele pale mitaa ya Sudani Temeke nikirudi nyumbani baadae.

Kufika kawe, namkuta Hamadi yuko bize kwenye simu, tunapeana tano tu za mikono ama gwara kisha ananyanyuka tunaanza mwendo wa kuelekea Kawe, Maringo.

Tulivyofika Tanganyika pekaz tunachanizia humo uwanjani maana Hamadi ananiambia mchongo upo Kawe ya chini barabara ya Mwai Kibaki.

Naona safi maana kunyoosha na lami na jua hili sio poa .

Tumeyafikia magofu ya mle Tanganyika pekaz nawaona wahuni wanapiga mazoezi huku wengine wakipuliza, tunawapa salamu kiaina kisha wananitembezea kijiti kama pafu tatu hivi nakaa sawa mawazo yote na uoga vinaondoka kisha namkusanya Hamadi tunasebenza misele yetu.

Kufika Kaw echini kule tunasimama nje ya geti moja jeusi. Umaridadi tu wa geti hili unaonyesha ndani yake kuna bangaloe la kwenda,, nabaki tu kumwambia Hamadi “Oya Mswati kuna watu wanaishi aisee cheki huu mgeti yaani bajeti yake mi si nanunua kiwanja huko mkuranga na kuezeka kabisa?”

Hamadi anacheka tu kisha ananiambia, “Ndio tupambane sasa, nyeupe nyeusi ili tuishi mwanangu ujue sisi hapa duniani hatuishi bali tunadumu, hawa ndio wanaishi sasa”

“Laivu kabisa mwanangu hivi fikiria mtu una mtoto mchanga wewe na mkeo mnalalaje kitanda cha tano kwa sita si mnakuwa mmenyooka badala ya kulala? Maana mmoja akisema ajitanue tu atakakalalia kachanga hivyo inabidi mjinyooshe tu” Nilisema. Hamadi akacheka huku akibinya kitufe cha kengele.

Haukupita muda geti dogo likafunguliwa, Sura ni ya kijana makamo yetu. Akatukaribisha ndani akionekana kuegemeza stori zake zaidi kwa Hamadi maana ndie wanafahamiana nae.

Tuliingia na kukaa varandani ambapo kulikuwa kumesheheni hadi sio poa, yaani pa kibabe sana.

Hamadi: Oya Mswati huyu anaitwa Denis baba yake ni Injinia wa wizara ya ujenzi. Oya Denis huyu ni mwanangu sana anaitwa Boyo.

Denis: Ndio yule uliyekuwa unaniambiaga kuwa una mwanao mmoja mmeshibana sana kama Chanda na pete?

Hamadi: Yap Denis na usimuone kakaa kinyonge hapo ni mwamba sana hata zile mishe yaani anapasua anga tu bila tabu.

Denis: Mi mwenyewe namwona, haihitaji maelezo muonekano wake tu ni maelezo tosha.

Nikabaki najiuliza ni michongo gani hiyo ambayo inahitaji mtu uwe mwamba kiasi hicho? Nikabaki na tashwishwi tu.

Mara Denis akazama mfukoni na kutoa kimfuko kidogo cha nailoni nyeupe, ndani yake kulikuwa na unga mweupe utadhani ni glucose.

Akampatia Hamadi, kisha Hamadi akanisogezea karibu na macho. Akaniuliza mswati unafahamu hii kitu?

Mimi: Hapana, ni glucose ama?

Denisi na Hamadi wakacheka kidogo kisha Hamadi akaniuliza unaisikiaga Player au maradona?

Mimi: Hapana.

Hamadi: Mswati hii ni cocaine grade one, mashanta tunaita Player. Kilo moja ya hii kitu inaenda kama milioni mia sasa hivi huwezi amini yaani.

Kitendo cha kuambiwa vile nikahisi kupagawa hivi, yaani mimi na madawa ya kulevya wapi na wapi? Nikamshika mkono Hamadi na kumvuta pembeni kidogo.

“Oya Mswati michongo gani hii sasa tunaleteana, mbona sikusomi mwanangu?” Nilimwambia.

“Mswati, wewe si unataka good life lakini? Sasa wewe maisha mazuri unadhani yatakufuata pale Temeke umekaa tu getto mara mnapiga spana na watoto wadogo wenye umri wa darasa la tatu?” Hamadi alinikata kauli.

Uhakika ni kwamba yale maneno ya Hamadi sio tu kwamba yaniumiza, bali yalipenya ile kisawa sawa na kuingia kwenye mtima wangu.

Ni kweli pale Temeke wengi tunashinda chini ya uvungu wa magari, yaani ni full kupiga spana, muda wote tumetapakaa oil chafu tena ukija mitaa hiyo ya Sudani unakuta madogo kibao wako hapo wanapambana kujifunza spana.

Nahisi kwa Tanzania nzima hakuna sehemu watu wana mzuka na spana kama Temeke sijui kwa sababu tu ya waarabu wengi mitaa ile si unajua tena waarabu hawana ujuzi mwingine nje ya spana na wanaipenda utadhani wameianzia tumboni.

Nikayatafakari maneno ya Hamadi, nikaona mwamba mbona yuko sawa tu sasa kinachonifanya napaniki ni nini?

Kwanza mimi mwenyewe nimepiga ruti kutoka Temeke mpaka huku Kawe nikiwa ninatamani mchongo wa kuingiza pesa, kwani nilitegemea uwe mchongo gani? sikupata jibu.

Nikasikia sauti ndani yangu ikisema Boyo acha ukina, nyaka fasta mchongo huo, sababisha kisha pita hivi, usirembe sana.Wanaume hawajiulizagi mara mbili kwanza huna maajabu mfukoni halafu unachagua cha kufanya?

Nikajikuta namwambia Hamadi “Oya Mswati Fabilillah!! Twende kazi kikubwa unyama uwe wa kutosha isijekuwa tunaleteana mazegere ya kiwaki. Si unanijuaga toka skonga sipoagi nikiwaka?”

“Mswati baaab we amini hii ni kazi tena ya kwenda, Huyo Denis unavyomuona hapo hanaga mba-mba-mba” Aliniambia Hamadi.

Tukarudi tena kwa Denisi kujumuika nae baada ya kuyajenga na mwanangu Hamadi.

“Oya Denis toa fudo mwamba akazie si unajua kule anakotoka yuko kinyonge?” alitanguliza Hamadi.

Denisi akatoka na kuingia ndani kama dakika tano hivi kisha akaja na bonge la hot pot.

Kulifungua hivi namuona kuku mzima na nusu yake, duu!! yuko dry ile mbaya miksa masontojo kama yote, yaani full udambwi dambwi . Akaliweka juu ya meza lile dude.

Denis akaniambia nawa hapo nyuma tu kuna koki. Nikamuambia Hamadi oya twende tukanawe. Akasema yeye yuko njema wala hana mzuka na msosi.

Nikamwambia na Denis nikaona nae ni vile vile tu nikawaza sasa hawa wananiletea mimi peke yangu Kuku na nusu wananitakia nini hawa? kwanza siwezi kummaliza huyo mmoja tu mwenyewe sembuse na nusu yake?

Nikawaza kifaza sana…, nawezaje kula kuku kipande hiki kwa watu halafu kule familia yangu inasokota nguna na wakudunga(dagaa mchele)?

Baada ya kunawa nikamuomba Denis kama kuna kifungashio nimuweke yule kuku mzima kisha nile ile nusu.

Huyu mzima nitawapelekea familia nao wakainjoi, yap ndio maana tupo hai na wao wanaweka matumaini yao kwetu na pale wanaume tunapokuwa tumetoka kwenda kwenye utafutaji basi matarajio ya familia zetu huku nyuma huwa ni kwamba Mshua akirudi mambo yatakuwa gudi sana japo kuna time tunaambulia patupu, basi ni vile tu hatujui jinsi wanavyokuwa Dissappointed yaani.

Baada ya kusema vile Denis alisimama akatabasamu kidogo kisha akaninyooshea kidole cha shada huku akitikisa mkono wake akaniambia maneno yafuatayo, “Nigga, you are a man and a daddy at the same time.What a fucking loving Nigga?”

Kisha aliingia ndani na kutoka na aluminium foil pamoja na mfuko mkubwa wa kutosha kuweka na mazaga mengine ikiwa ningekuwa na pesa ya kuhemea vitu vingine.

Denis alimwambia hamadi kuwa “Una kila sababu ya kuwa bampa to bampa na huyu mwamba. He is such a loyal nigga.”

“Haha haha haaa!!! Denis mbona huo ni mwanzo tu ukimwelewa mbona utampenda tu bure, yaani muonekano wake ni tofauti na roho yake huwezi amini”

“Ujue ile first sight niliwaza kidogo nikahisi huyu jamaa anaweza kuja kutugeuka yaani. But I was wrong!” Alisema Denis.

Niliwasikiliza tu huku nikimfunga vyema yule kuku kwenye foil na kumuweka kwenye mfuko kisha nikaanza kula Ile nusu na chombeza(chipsi kidogo) zilizokuwepo mle kwenye hotpot.

Nikawaza ina maana hiki kitendo kidogo tu kimeweza kunijengea Imani kubwa kwa huyu Denis, kumbe watu hudifainiwa kwa vile vitu vidogo ambavyo wao pengine hawakuwa serious navyo kabisa.Duuh!!

Baada ya kumaliza kula maongezi ya kazi yalianza.

Denis alileta ramani ya kazi mezani, kiasi ilikuwa inatisha ila sio kwa mimi maana mazingira niliyokulia hata watoto wenzangu walikuwa wakinihanya na mbaya zaidi hata wazazi wao walikuwa wakiwazuia watoto wao wasinikaribie.

Laiti wangejua kuwa mimi mwenyewe ni introvat sitakagi junction kwenye maisha yangu wasingehangaika kutumia nguvu kubwa kiasi kile.

Nilianza kwa kufundishwa kwanza vituo ambavyo ningekuwa natembelea na kushinda muda mwingi. Na majina yake ya kishanta yaani code maalum ambazo tungetembea nazo vichwani mwetu.

Baada ya kuyacheki maeneo yote nikagundua kuwa hakuna eneo la kizembe hata moja, yaani mbona kote ni kwa mashefa?

Nikaona mbona kazi kama inaanza kunitoa hata kabla sijaanza kuifanya?

Baada ya hapo nilipewa jina sasa rasmi la kinyoka, Nikaitwa Noriega.

Si nikakumbuka ule wimbo wa Rick Ross BMF maana nasikia sana hili jina likitajwa mle kwenye huo wimbo.

Ndio nikajua kuwa kumbe wale jamaa huimba vitu halisi kutokana maisha yao.

Basi Noriega nishakuwa nyoka tayari kinachofuata, nikapewa unga kidogo kwenye mfuko Denis akaniambia kuwa mimi niko safe zone sitaweza kutest wala nini maana mashefa wote wanatumia so wanatest wenyewe mimi nijitahidi tu nisijetumia maana nitawalisha hasara na hapatakalika tena.

Nikamwambia kuhusu hilo asiwaze kikubwa tumalizane kuhusu malipo ili niwe huru kupiga kazi.

Denis akacheka kidogo kisha akaniambia unadhani naweza kukupa mzigo wa mamilioni halafu nikuletee mboyoyo kwenye malipo hapo una mzigo wa kama milioni ishirini na tano.

Malipo tunaanza nayo sasa kwanza chukua hii, akazama mfukoni akatoa noti saba za dola mia mia.

Kwa time zile chenji ilikuwa inasimamia kwenye elfu mbili mia mbili so nikazidisha fasta nikaona inakuja milioni moja na ushee yaani chenji ya juu yake inatosha kuweka banka(mahemezi ya mahitaji muhimu) ndani ya mwezi mzima

Si unajua tena sisi watu wa hali ya chini mahitaji yetu huwa sio mengi ukishaweka mchele kilo hamsini, unga dona kilo mia, sukari kilo ishirini na tano, mafuta kindoo lita kumi na mtungi mdogo wa gesi umejaa vyema na gunia la mkaa kwetu sisi hiyo inatosha hatuna mambo ya kuweka sijui nyama kwenye friji kwanza uswahilini kwetu unaweza hisi tumeazimwa transfoma,,, maana sio kwa kukatika umeme huku. Utawekaje vitu kwenye friji sasa hata ukiwa nalo ujue mgogoro wa umeme wewe ndiye victim muda wote.

Kama feni tu watu wanagombana itakuwa hilo friji si watasema unamiliki mtambo kabisa ujue asili ya uswahilini kwetu ni kwamba watu wanayajua mambo na mienendo yako kuliko hata wanavyoyajua maendeleo ya watoto na ndugu zao so ukiishi huku kwetu ujipange, yaani uwe unaamka saa kumi na moja alfajiri na kurudi saa tano za usiku.

Na ole wako wasijue unapojishughulishia!! Utabambikiwa kila jina baya linaloendana na wizi.Hasa ukiwa mkimya na kaksi kama nilivyo yaani wewe utapata tabu.

Ratiba ilitakiwa ikifika saa mbili za usiku ndipo nisogee kwenye kituo changu cha kwanza kwa siku hiyo.

Basi tuliagana pale lakini Denis aliniambia neno moja ambalo liliniingia na nikalizingatia sana “Nigga, I see you far!! Yaani ukiwa muaminifu, hili jiji utaliweka kiganjani mwako haijalishi una elimu ama huna elimu man.” Kisha alinipatia kiasi cha laki moja nje ya malipo yangu akaniambia This is for our hommies, you have that, we have this.

Akimaanisha kuwa ile pesa ni kwaajili ya familia yangu ambayo nayo anaizingatia kama familia yetu wote kwamba mimi nina yule kuku, ila wao wana kile kiasi cha pesa alichonipa.

Denis hupenda sana kuchanganya lugha nafikiri ni kutokana na kwamba pengine amekaa sana Ulaya huko akiwa anasoma ama kwasababu ya mishe mishe zake hizi maana mara nyingi huwa anasafiri sana kwenda nje.

Basi mimi na Hamadi tulimuaga pale Denis kisha tukashika njia tuliyokuja nayo.

Hamadi alishauri tufanye vile ili kuweza kuitawala pesa badala ya kuruhusu pesa itutawale yaani isiwe ile nimepata tu vipesa kidogo nianze matumizi yasiyokuwa ya msingi kama kuchukua bajaji kutoka kawe hadi Temeke ambapo ingenigharimu elfu ishirini na tano. Alinishauri niwe mtulivu sana maana issue nazozifanya natakiwa kuishi kama mtu ordinary ili nisivute attention za watu kuanza kujiuliza juu ya kazi zangu maana watu wanapenda waone mnafanana na haubadiliki.

Hivyo ikitokea mabadiliko kidogo wanaanza kusaka chanzo cha yale mabadiliko wakikijua tu oya!!! Umeisha man.

Kweli tulitembea mpaka Kawe ukwamani, ambapo tulikaa tukapiga stori moja mbili tatu huku nikiwa nasubiri gari la Temeke.

Nakumbuka katika zile stori Hamadi aliniambia kitu ambacho kiliniacha mdomo wazi kwanza aliniuliza, “Mswati unadhani mimi sina pesa? Pesa ninazo yaani kwenye akaunti imo zaidi ya milioni hamsini. Lakini ona bado naishi uswahilini, lakini huko nyumbani kwetu Geita nimewajengea wazazi nyumba ya zaidi ya milioni ishirini. We nione hivi tu”

Kwanza nilishangaa sana maana muda mwingi ambao tulikuwa tunakutana mimi na hamadi ni kweli bili za misosi kwenye migahawa ya kati hii isiyo mikubwa sana wala midogo sana alikuwa analipia yeye na muda mwingine ananipa hata elfu hamsini kwaajili ya kurekebisha mambo ya mezani pale nyumbani kwangu, lakini sikuwahi kuwaza kama huyu mshikaji ni milionea tena amekaa kimya tu.

Hapo ndio nikajisemea ama kweli usiseme una rafiki we sema una mshikaji ambae mnashea kile kinachowafanya muwe pamoja kwa muda huo maana urafiki ni gharama sana

Asikwambie mtu, yaani kuwa na mtu ambae utamshirikisha michongo ya namna unavyopata riziki wakati huo yeye hana mbele wala nyuma halafu akakuacha salama!! Basi ujue hapo unae rafiki na bado haitoshi maana anaweza kuja kukusaliti hata kwa mkeo sehemu ambayo hukuamini kama ataanguka, kumbe ikawa ndio udhaifu wake.

Baada ya kuniambia vile alizama mfukoni nae akatoa laki mbili na kunipa akidai kuwa zile ni Baraka ni kawaida kumbariki mtu anapokuwa anaanza kazi.

Basi nilipokea huku nikijiona kama nimekuwa mpokea michango kila mtu sasa ananichangia lakini hii ni baada ya kuungana na familia yao mpya.

Hatukukaa sana, gari la Temeke likaja DCM moja watu wakaanza kuingia kwa fujo mimi nikamuaga Hamadi na kujitoma ndani ya gari nikikaa siti ya dirishani na kumpungia mkono Hamadi. Nae akanipungia, haukupita muda gari ikaanza mwendo Nilifika mtaa wa Ngeta mida ya saa kumi na moja kasoro ambapo nilipofika kwanza nilanzia kwa mangi upande wa kulia kuna watu wa ukoo wa Mtei jina kwa Paschal, ana duka lake hapo nyumbani so mahemezi yangu nilipenda kuyafanyia hapo kutokana tuna muunganiko Fulani na hao watu kiaina.

Baada ya kununua unga na baadhi ya vitu nilipeleka nyumbani ambapo niliikuta familia imejikusanya kwenye kideo ni sauti ya Juma Khan Chikongwe imetawala sebule nzima.

Unashangaa nini sasa? Sisi huku uswahilini kwetu huyo ndiye mwamba anaefagiliwa mno. Yaani wanamhusudu kama vile Sharuh Khan huko India.

Pisi nyingi za huku kwetu hazijui mara burger mara pizza zenyewe ziambie mihogo ya kukaanga na chachandu pale kwa mama Faridu basi utazikonga nyoyo. Na ukitaka kuwang’oa wewe waambie mvua zimekaribia kuanza utakuwa unawabeba mgongoni unawavusha maji wakitaka kurudi ama kutoka nyumbani basi hapo ni wewe tu ila hakikisha mvua zikianza kunyesha uwe umehama huo mtaa maana utawabeba hadi wake za watu hapo ndio utajua kwanini wahuni hutembea na mafuta nyuma ya sikio.

Uswahilini kwetu mwenyekiti ana nguvu kuliko greda linalochimba mitaro na barabara, maana kesi nyingi za pale mtaani anakalisha, zinaisha bila kwenda mahakamani.

Halafu kila mwenyekiti ni aliwatani, maana madili mengi ya pale mtaani lazima ashirikishwe ili likitokea soo analizima. Yaani hiyo ndio torati ya sehemu kibao kuanzia pande majumba sita, kiwalani, vingunguti kwa pera pera, kushuka tabata liwiti mpaka kule mitaa ya Ghana buguruni shuka hadi marapa kwa mwamba Chidi benz hapo mwendo ni huo huo. ukizingua night watu wanakusaka na vitofa. Kifupi watu hawapendi mambo ya kupelekana polisi wanapenda sana street justice.

Uswahilini watu wanazijua sheria sana lakini ni zile za kuchonga mdomo tu wakisikia kuna mwenzao kaenda hata selo tu polisi hawaendi hata kumpelekea msosi wote wanaogopa, sasa unaanza kushangaa si ni hawa waliokuwa wanachonga mdomo kuwa hata polisi na mahakama hawaziogopi?

Ingia mkenge sasa, utiwe lupango uone, hautamuona mtu hata mmoja kutoka pale mtaani kwenu uswahilini akiileta sura yake pale kituoni ulipo zaidi ya ndugu zako. Ambao nao watakuja ile tu kuondoa lawama huku wakikusema ile vibaya maana umewaharibia hesabu zao za hela ile mbaya.

Na kama huna ndugu mjini Daslam, umekuja kama gunia la mkaa utaishia segerea baada ya miezi sita au mwaka ukitoka unawakuta wahuni wameshikilia pole nyingi hakuna cha maana.

Ukiwauliza mbona hamkuja kuniona? utasikia mara walikusanya michango wakampa sijui nani nani akatokomea nazo wanamwangushia jumba bovu msela ambae wanajua alishahama kitaa chenu.

Basi baada ya kuingia ndani ilikuwa ni full shangwe kwa familia maana nina makid wawili tu na mke wangu. Makid ni wa kike na wa kiume wana fujo hao na wote wanasoma shule iliyopo hapo jirani tu yaani pale uwanjani tunapopigia mazoezi jioni ni uwanja wa shule yao.

Basi kwakuwa tayari ni uelekeo wa jioni mke wangu huyu ambaye ni mzuri yaani sometimes nikitafakari alinipendea nini nakosa majibu maana pesa sina uhakika wa maisha ya kesho pia sina zaidi ya ahadi za kujiamini tu za mdomoni kuhusu fyucha yetu.

Ujue wanawake nao wana maamuzi yao ambayo yanabaki kuwa siri yao pengine huwa wanatuonea Imani tu ama huwa wanapenda kitu ambacho wewe mkulungwa hukijui kama ndicho kinamzuzua yaani yote heri tu.

Kikubwa tuendelee kuwa pamoja sisi wanaume na wanawake maana tunafaana sana achana na hizi swaga za kifala mara eti haki sawa mara vijana hawataki tena ndoa wanataka kuwa wanachapa na kusepa Jiulize je wewe baba yako angechapa kwa mazaako na kusepa ungeinjoi vipi mapenzi ya baba na mama ama ndio ungekuzwa na mama yako peke yake ili uwe na tabia za kike kike zile za wote mna mitondoo ndani ya kukojolea usiku hakuna wa kumsindikiza mwenzake nje kukojoa?.

Wakati mke wangu anapambana na vyombo na majiko mimi nilikuwa nikicheki time kwenye simu yangu muda wote nisije nikazingua siku ya kwanza.

Maana nakumbuka niliambiwa mida ya saa mbili na madakika yake niwe kituo namba tatu yaani ilikuwa ndio jina la siri la eneo husika.

Basi saa kumi na mbili na dakika kumi niliaga huku nikichukua koti langu kwaajili ya kujihami na baridi la usiku.

Mke wangu aliuliza tu kwa hamaki kuwa naenda wapi maana hajazoea mimi kutoka mida hiyo ya jioni labda kama kuna mechi za Ulaya ambapo napo mimi sio mpenzi sana kihivyo.

Nilimuaga kuwa natoka japo naweza kuchelewa kurudi maana kuna watu natakiwa kuonana nao niseti mipango ya kazi. Basi baada ya wife kusikia kuhusu mipango ya kazi akawa kichwa juu juu Enhee kazi gani baba?

Nikamwambia taratibu sasa mchele wenyewe hata haujaoshwa uanze kutengeneza kachumbari kweli?.

Wife ni muelewa ikabidi anyuti huku akinitakia mafanikio mema huko niendako.

Basi raundi hii sikwenda pale stendi ya hospitali bali nilipitia njia ya nyuma nikapandia stendi ya Girraffe hotel.

Huyo!!!! saa moja ikanikuta ndani ya Mwenge. Niliamua kukaa na kupoteza muda pale mwenge kutokana na kwamba kuna vile vitu vyetu yaani sisi ambao hatujajipata basi huwa tunapenda kukaa sehemu ambayo wanapita akina dada wengi hususani mitaa ile wanayopita masista duu wengi hii huwa ni kwaajili ya kuburudisha macho na kusuuza roho kwa kuangalia maumbo yao hawa wadada huku mara moja moja tukivaa mabomu na kuwatongoza kujaribu bahati yetu wanasema usipoamini ndipo linatokea jambo halafu pale ambapo unaamini sana ndio hakitokei kitu eeeeh!! Maana si hatuna Kamba za kuwavutia?

Sasa mwanaume nikijiangalia mfukoni sina maajabu, nyumba sina, gari sina kazi ya kunikutanisha nao muda wote wawe wanaililia saini yangu sina nitawashikia wapi wadada wanaoingia salooni na kuacha karibia laki mbili na nusu kwa mara moja?

Halafu unajifariji eti mapenzi hayaangalii? Sio kwa hawa wauza ngono. Na wengi wa wauza ngono ndio hutuvutia kingono maana wanajibrand kingono ngono ili wawaingize wanaume kwenye kumi na nane halafu natokea mimi mnuka jasho mwenye sugu mikononi nataka nipendwe na huyu muuza ngono daaah nitasubiri sana.

Basi nikiwa pale Mwenge mara nikamuona mwanamke mmoja namfahamu kindaki ndaki anaitwa Vero, huyu tulisoma wote shule ya Ally hassan Mwinyi pale Magomeni makuti, barabara ya Magomeni- Sinza,, yuko na Nadia.

Huyu Nadia ni mtoto shombe shombe nae pia tunafahamiana vizuri japo yeye alikuwa anasoma shule ya Benjamin mkapa nayo iko mazingira hayo hayo kiasi kwamba ukiwa hauko sawa unaweza usijue kama kuna shule tatu tofauti lakini Benjamini mkapa na Ally Hassan Mwinyi ndizo zinaonekana kama shule moja zaidi huku shule ya Turiani ikiwa pembeni kidogo tena hii ni ya sekondari.

Umaarufu wa Nadia ni kwasababu huyu mtoto wa kike ni mzuri kuanzia sura mpaka umbo sema ana mwili Fulani hivi wa kivivu sana lakini ni mtu ambae muda mwingi anapenda kucheka sana hususani akiwa amekuzoea na hakawii kumzoea mtu.

Sasa huyu Vero baada ya kumaliza shule ya msingi alienda jangwani pale ambapo tulikuwa tukikutana mtaani kipindi cha likizo tu ndio nikaja kurusha ndoano lakini niliulizwa swali moja tu kuwa kwetu tuna nini mpaka nimshawishi awe na mimi?

Kiukweli alinikata maini kipindi hicho niko form two ilikuwa ni mwezi wa sita ambapo miezi miwili baadae niliachana na masuala ya shule na kutokomea mtaani mazima.

Baada ya kumuona nilipata mshawasha tu wa kumsalimia ambapo nilimuita Vero akageuka lakini aliponiona ni mimi akanywea yaani dizaini ile ya mtu ambae hakutaka kabisa akute ni mimi naemuita.

Lakini Nadia alipogeuka na kuniona alijawa na furaha ya ghafla sijui tu ni kwanini akamvuta mkono Vero waje kunisalimia lakini Vero aligoma, ndipo akamuacha na kuja peke yake akanikumbatia huku akinishikilia mikono yangu miwili kwa muda mrefu.

Sasa kutokana na kwamba watu ni wengi, hata sehemu za kupita kuna muda inakuwa ni shida na sisi bila kutambua kuwa tumeingia njiani kidogo tu nilishituka nikisukumwa na jamaa mmoja aliekuwa anajifanya yuko kasi na haraka hata sielewi alichokuwa anakiwahi ni nini, huku akifoka “Mnakaa kaa njiani kama ni mahaba si mwende bongo muvi mkatuonyeshee kwenye tivii?

Sasa kile kitendo cha kusukumwa na ikumbukwe alinisukuma mgongoni kwenda mbele kwakuwa sikuwa nimetarajia,, nilikosa balansi na kujikuta namkomba Nadia tukaangukia kwenye meza ya dada mmoja alikuwa anauza nguo za ndani.

Fasta nikajizoa zoa toka kwenye mwili wa Nadia maana nilimwangukia kwa juu , kichwa changu kikajam sana.

Lakini Nadia yeye alinipa pole huku akitabasamu tu kama vile hakuna kilichotokea. Huku akijitahidi kunitengeneza shati pale lilipokaa vibaya.

Yule dada mwenye meza ni mtu na nusu maana baada ya kuinuka na kusimama alitabasamu tu na kutuambia haya jamani wapendanao mniungishe sasa kila mmoja amnunulie mwenzake maana hapa kuna boxer za kiume na chupi za kike aina zote na tight pia.

Nadia bila kupoteza muda alianza kukagua Boxer pale, nikabaki najiuma uma sijui hata nifanye nini.

Lakini mara alifika Vero na kumvuta mkono Nadia kwa nguvu huku akimwambia “We Nadia umechanganyikiwa? Unataka kumnunulia huyu nguo za ndani? We Nadia wewe haumuheshimu Hassan eti?” Basi alimvuta mkono ile wangu wangu lakini nadia aligeuka na kunipungia mkono, lakini Vero aliachia msonyo mrefu huo sijapata kuona.

Kifupi niliuona wivu ndani ya Vero tena ule wa wazi.

Basi saa moja na nusu nilichukua bajaji pale mpaka Masaki hapa ndio ilikuwa kituo namba tatu. Nilisogea mpaka kwenye Lounge moja upande wa kushoto ambapo bajaji ilifika na kupaki nje maana mule ndani hawakuruhusu piki piki na bajaji kuingia maana mlinzi kazi yake ni kuminya rimoti kisha geti kubwa linafunguka hapo ujue linaingia ndinga la kifahari.

Baada ya kumlipa dereva ujira wake nilishuka na kuingia kupitia geti dogo yaani hata mlinzi hakuamini kuwa kwa muonekano ule naweza kuwa nimedhamiria kuingia mle ndani.

Ambapo alinifuata upesi na kuniuliza “We jamaa unaenda wapi?”

Nikamwambia naenda mle ndani kwani kuna tatizo?

“Kuna mtu unamjua mle labda?”

Nikaona huyu mlinzi anataka kunizoea vibaya yeye kazi yake ni kulinda hapo getini huku akifanya kazi ya kufungua na kufunga sasa hivi anajikuta kanipata mnyonge wake anataka anioshee aisee haiwezi kuwa kweli.

Nikaweka koo la mamlaka kisha nikamuuliza “Ndio kazi iliyokuweka hapo si ndio? Acha upumbavu fanya kazi yako ilyokuweka hapo” Baada ya kutamka vile sikutaka kumpa nafasi ya kujiweka sawa maana nilimuona kaingiwa na kiwewe na mie kupitia upenyo huo huo nikautumia kusogea mpaka kwenye meza moja ambayo ilionekana amekaa mtu mmoja tu.

Baada ya kukaa tu, Mhudumu wa kiume alikuja na kunipa menu ambapo niliangalia haraka haraka sana nisijue niagize nini maana vingi vya vyakula pale sikuwa nikivijua hata vinafananaje japo niliona burger na pizza sikutaka kuagiza.

Baada ya kutuliza macho vizuri ndipo nikaona grilled meat kwenye mabano nikaona goat bei yake elfu sabini.

Nikamuonyeshea muhudumu ambapo aliondoka chap baada ya kuonekana kama nimemchelewesha kuchagua msosi kwa muda mrefu nikashangaa hajataka kusubiri nimwambie labda alete na ugali au ndizi ama wali. Yeye tayari keshaondoka.

Angejua angenisamehe tu bure kwa kuchukua muda mrefu kuagiza maana sisi tushazoea migahawa yetu ya huko uswazi ambapo kwanza ukiwa unanawa unakuwa unatoa maelekezo kwa muhudumu tena kwa sauti kubwa.

“Nipakulie wali nyama na maharage weka ya kutosha, jitahidi nyama iwe nzuri isiwe na mifupa sana” Hizo ndio oda zetu sehemu za chakula uswahilini kwetu.

Nikiwa nashangaa shangaa mazingira ya mle ndani mara muhudumu huyu hapa kafika na bonge la sinia juu yake kuna sahani na vibakuli kama vyote yaani nikawaza kwani kabeba oda double?

Mara akashusha vyote pale mezani kwangu, mi nipo macho kodo tu baada ya kumaliza kushusha akanikaribisha “Broo karibu sana” Akaninawisha mikono na kuondoka.

Ile fujo ya vyakula iliyokuwa pale mezani ndio niliamini kwanini bei ni elfu sabini. Kwanza kulikuwa na supu ya mboga mboga, supu ya utumbo wa mbuzi ikiwa imewekwa vikorombwezo kama vyote hiyo nyama ya mbuzi iliyochomwa ilikuwa nyingi sana na kulikuwa na pan-cakes mikavu Fulani iliookwa ndani yake kukiwa na mayai ya kuku wa kienyeji.

Mwanaume nikaanza kula pale huku nikitazama mazingira ya pale. Aisee ndio maana watu wanaopata pesa wakishazijua hizi starehe ni vigumu sana kuacha mpaka pale wanapohakikisha kuwa wamefilisika kabisa mpaka kukosa hata pesa ya kuagizia andazi humu.

Maana wanawake unaowaona kwenye masaloon makubwa makubwa yale wakiwa wanaonekana kama malaika wote huishia maeneo kama haya maana huku huuza miili kwa watu wenye pesa.

Niliona wanawake wazuri wa ajabu mpaka nikajiuliza hivi sisi watu wa kawaida tukifa tukaulizwa kama tumewafaidi hawa viumbe tutakuwa na uwezo wa kujibu ndio kweli?

Nilianza kuhisi kuwa hawa sio wanawake wa kawaida aisee ila nikiri tu kwamba Kuna wanawake wazuri yaani ukisikia mtu anasemwa kuwa alikuwa yuko vizuri kiuchumi halafu akafilisiwa na Malaya Usije ukampinga mtu huyo kwa niliyoyashuhudia ni kweli wanawake hawa wana uwezo wa kumfilisi Mwanaume yeyote yule ikiwa atawakenulia meno tu hata awe na ukwasi kiasi gani.

Maana kwanza bia zinazouzwa humu ni zile za kutoka nje ambapo Windhoek moja ambayo mtaani tunauziana elfu tano tena hapo unakuta muhuni nabana manzi asinywe zaidi ya nne huku moja tu inauzwa elfu ishirini. Na watu wanawaagizia hawa wanawake mpaka mwanamke analewa yaani.

Savanah nazo ni vivyo hivyo. Nikiwa ndio nimemaliza kupata msosi wa nguvu mara alinisogelea mdada mmoja na kuulizia kampani yangu, nikamwambia aniache kwanza kuna mambo nayatafakari then muda ukifika kama atakuwa available basi tutaungana wote.

Mara nikasikia sauti kwa nyuma yangu “Noriega” Nikashituka na kukaa sawa kumcheki ni namba moja ya kilatino imeweka nywele mtindo wa bambucha ina vipuli masikioni vinang’aa sana vya silva.

Likavuta tu kiti likakaa na kuongea Kiswahili cha kuunga unga ambapo lilinitajia namba tatu, nikalionyesha karatasi moja alinipa Denisi imechorwa vidoti vitatu tu.

Baada ya kumuonyesha ile karatasi, akanishika mkono na mimi nikanyanyuka akaniachia akinielekeza kuwa nimfuate tukaingia kwenye ukumbi baada ya kusukuma mlango upande wa kulia.

Humo nilikutana na mimoshi tu watu wapo bize kusmoke yaani ni fujo tu huyu ana shisha yule ana Ciga mara huyu kitu cha Jamaica basi Yule mwamba akaniuliza nasmoke nini?

Nikamwambia nasmoke marijuana zikaletwa puli mbili zikawashwa nikataka kusmoke mara simu ikaita kucheki namba ni ngeni nikapokea na kuweka sikioni sauti nasikia ni ya Denis huwa sisahau sauti hata kama mtu nimekutana nae mara moja.

Akaniambia “Noriega, no smoking bro. Even though I forgot to tell you”

Duuh ilikuwa kidogo tu nismoke, hata sijui ingetokea nini hebu Mungu nilinde. nikajikuta najisemea.

Ghafla nikajikuta naitupa ile puli chini huku nikimuangalia usoni yule jamaa wa kilatino.

Akaniambia njoo huku, tukafika kwenye meza moja kubwa hapa walikuwepo mashanta wakubwa wamekaa na vikaptura tu matumbo makubwa yakiwa yanachezewa na wadada wakali sana. Ile kufika tu hivi Jamaa mmoja akaniuliza Noriega?

Nikajibu yap yap sikutaka kukaa kizembe nikaamua kuanza kwenda sambamba na hizi code.

Namba tatu nikafungua kikaratasi pale chap nikamuonyesha akapiga vidole viwili cha shada na cha kati kama vile mtu anaomba ulinzi kwake. Baada ya ile ishara tu nikaona wale wanawake wote Malaya wakisambaa, na kuwaacha wale watu peke yao. Kisha akaja mtu mmoja ni baunsa ana kiboksi kidogo akanipatia huku akiniambia zikague uhesabu nikafungua kile kiboksi na kutoa zile noti nikazihesabu zilikuwa ni noti za dola mia zikiwa noti mia na ishirini.

Baada ya kuzihesabu, yule mlatino alitoa katochi kadogo na kunipatia akiniambia hako ni maalum kwaajili ya kukagulia pesa kama feki au zenyewe. Akanipa maelekezo na jinsi ya kukatumia kale katochi. Kisha mimi nikazama sehemu ya maliwatoni na kutoa mzigo wao nikawaletea hapo baada ya wao kuutesti mzigo wao na kujiridhisha kuwa ndiyo mali kusudiwa, chap nikatoka humo smoking room nikaenda zangu hadi nje kabisa ambapo simu yangu iliita,, sauti ni ya Denis, yaani sijui ni kwanini sikutaka kuendelea kubaki kwenye yale mazingira tena sijui ni kwasababu ya ile pesa au ni nini.

Denisi aliniuliza unaona upande wa kulia kwako kuna gari inapiga indicator ifuate haraka ingia humo.

Niilifuata fasta ambapo ile naikaribia tu hivi mlango wa nyuma ushafunguliwa nikaingia na ikapiga moto tukaondoka pale na kunyooka hadi eneo la Msasani club ambapo dereva alisimamisha gari kisha ikaja gari nyingine na kupaki pale pale tulipo sisi nikamuona Denis akishuka na kuingia kwenye hii gari yetu, Alikaa nyuma ambapo tulikuwa wawili mimi na yeye tu nikatoa kile kiboksi nikamkabidhi nae akakipitia kile kiasi cha pesa na kufurahi sana.

Basi dereva alipewa tu maelekezo ambapo aligeuza gari tukarudi tena uelekeo wa kisiwani ambapo tulivuka mataa ya morocco pale na kwenda mpaka pale Biafra wakanishusha pale, Denis akiniambia nichukue taxi inipeleke temeke maana kwenye gari alinipa kiasi cha dola mia nane na laki moja ya usafiri kwa usiku huo.

Kwanza nilianza kuhisi mbona Dunia inanifungukia kwa haraka sana kiasi hiki? Kulikoni au ndio baada ya hizi ruti zote nitaambiwa niende nje ya nchi nikamezeshwe madawa tumboni?

Pia Denis alinishauri kuwa kama nataka niwe accurate kwenye hizi kazi basi sina budi kuhamia mitaa ya karibu yaani kifupi niwe ndani ya wilaya ya Kinondoni.

Akaniambia itakuwa vyema kama nitatafuta chumba maeneo ya Mbezi beach ama Sinza. Nikajibu sawa.

Basi niliwasogelea madereva taxi wa pale Biafra ili tu kumridhisha Denisi lakini uhalisia sikuwa nazungumzia issue ya safari ya kwenda Temeke bali nilimlenga jamaa mmoja nilimuona kavaa jezi ya Simba nikamzuga mimi ni wa Yanga tukaanza kubishana masuala ya mpira pale mpaka ile gari aliyomo Denis ilipoondoka na mimi ndio nikaaga na kuondoka.

Mbele nilimpata boda boda mmoja tukaelewana bei ambapo alianzia elfu ishirini, Nikamwambia nina elfu kumi kwakuwa ilikuwa usiku kuelekea saa nne tukafunga hesabu kwenye elfu kumi na tano

Nikakwea chuma tukatambaa zetu hao nikiwa kwenye pikipiki mara nasikia simu inaita kucheki ni wife, nikapokea Ananiuliza vip mme wangu kwema huko lakini?

Nikamwambia niko kwenye piki piki nakuja kisha nikakata simu dereva akawasha tena tukaendelea na safari maana nilimwambia apaki pembeni kidogo niongee na simu.

Baada ya kufika mtaani kwangu nilishuka na kumpa dereva cha kwake akasepa na mimi nikaingia ndani nikatulizana.

Mwanamke akanivaa na maswali yake Enhee vip baba Fulani mipango yako iliendaje?

Nikamwambia kuwa Mungu anabariki naona kama nitafanikiwa ila nijipe muda tu, Uhhu!!! Afadhali sasa labda tutaweza kubadilisha hata maisha yetu maana yaani kiukweli nimepachoka hapa ni vile hujui tu natamani hata tuhame kesho kama ingekuwa inawezekana.

Nikamwambia hiyo jeuri ya kuhama hapa kwenye gharama ndogo unaitoa wapi wewe mama Fulani?

Kiukweli sio kwamba napapenda hapa kihivyo ni vile tu uwezo wa kipato na uungwana wa mwenye nyumba wetu kwanza haishi hapa yeye anaishi huko Kigogo hata kodi ikiisha anaweza kukaa hata mwezi ukapita ndio anakuja kukudai.

Hata ukimwambia umepungukiwa atakusikiliza tu na kukutia moyo ili kesho uzidi kupambana mambo yaende sawa, kifupi hii ndio sababu inayonifanya niendelee kuishi hapa japo maji ya bomba hamna zaidi ya maji chumvi ya visima tena kuna kisima maarufu tu ukiwa unaenda mashariki kuna nyumba moja ya mzee muarabu ndio hutuuzia maji ndoo shilingi hamsini anasema anauza bei ya chini ili ile nusu iwe kama zaka kwa Allah..

Wapi nitaenda nipate chumba na sebule kwa elfu thelasini niambieni mimi. Kama sio huko msasani lutamba ama tandale kwa mtogore , ukikoswa sana kigogo luanga au Kino shamba.

Unapajua huko kwanza? Huko wanaishi nusu duniani nusu kuzimu na hapo bado mvua hazijanyesha, unashangaa ulienda kwenye utafutaji unarudi jioni hata ile nyumba uliyopangapo chumba huioni ishaenda na maji.

Niacheni na Ngeta yangu mie, kwanza huku kuna watoto wa kike mashombe shombe wasio na idadi kutokana na wingi wa waarabu halafu wanakula spidi ile mbaya, hiyo ni miguu ya kuku na utumbo wa kuku poa usipime.

Ukiwanunulia chipsi au ndizi mzuzu umewamaliza wanatulia halafu wanazipenda ndoa kama nini yaani ni kama wanashindana kuolewa ila hao waoaji ndio wa kuhesabika hivyo wapo wapo tu majumbani kwao kutwa kupokezana vibao vya mbuzi na mama zao jikoni

. Sasa wataenda wapi unadhani?

Na wengi ni masingo maza mimba kapigwa na msela wa mtaa wa pili hapo msela mwenyewe bado anaishi kwao hana mitikasi yoyote basi mimba inalelewa na mtoto anazaliwa na kulelewa hapo hapo kwa akina binti.

Siwezi sema kuwa sababu ni uchumi hapana pia kutojitambua kwa vijana kunachangia maana sisi wengine tulivuta jiko ndani hatuna hata godoro.

Na mpaka leo hii life tunalisebenza kiaina.

Mida ya saa tano nilitoka bafuni maana lazima nioge kwanza kutokana na mizunguko niliyotoka pili kuupoza mwili ili uende kukabiliana na joto la ndani maana kuna muda ,hata feni inanyoosha mikono juu nayo inaanza kutema joto .

Baada ya kutoka bafuni sikuwa na uhitaji wowote ule wa chakula maana nilikuwa niko full sana kutokana na ile shoo ya kule Masaki.

Tulikaa muda mfupi na wife kitandani huku tukingojea watoto wazame usingizini, ili tuweze kula chakula cha uzima.

Hatimaye mida iliwadia nikaukwea mlima nikiwa na nguvu kama simba kutokana na mawazo juu ya pesa kuwa hayapo tena hata namna moyo wangu ulivyokuwa ukidunda nilihisi mabadiliko makubwa sana. Kifupi nilikuwa comfortable sana yaani.

Hii ni nguvu ya pesa,, kwa sasa halipingiki hilo yaani michongo ya pesa ikivurugika tu hata performance kitandani inapungua kwa mwanaume maana tendo lile hisia zinaanzia kwenye akili jinsi unavyoitafsiri picha ya utupu wa aliyepo mbele yako.

Ni muda gani nilipitiwa na usingizi? Hata sikumbuki, si unajua tena baada ya mshindo ni kiasi tu cha dakika kadhaa usingizi unakuvaa?

Niliamshwa na simu mida ya saa kumi na moja na madakika yake, Namba ni ile ya Denis. Akaniuliza kama bado niko home, nikamjibu yeye ndie kaniamsha maana sikuwa na ratiba ya kudamka.

Akanipa ramani ya kazi ya siku hiyo maana ilitakiwa mapema sana nifike namba saba kuna mtu ana mzigo natakiwa niupokee kisha nisambae nao mpaka napopajua kusubiri maelekezo ya baadae.

Basi nilijiwasha kimoja cha fasta ili kuiweka akili sawa.

Mida hii najiwasha alipita mwanangu mmoja wa hapo kitaa tu ambae huwa tunawasha wote mida ya jioni kwa jina la Hamza.

Akaniambia kuwa ana mzigo mmoja amenunua juzi tu yaani ni mkali ile mbaya hajui hata unalimwa wapi, Akasema kama sio kitu cha Tukuyu Mbeya kile, basi kitakuwa cha Kisimiri Arusha, au Kilibho Tarime.

Nikamwambia kama kitu kinawaka sana akilete chote maana nahitaji mzigo mzuri kwaajili ya matumizi yangu binafsi.

Alikubali ambapo aliondoka na kuchukua kama dakika kumi akawa amerudi tayari. Tukaanza kuvuta kitu chetu.

Ni kweli kitu ni kikali tena sana maana nilivuta puli moja hata sikuimaliza nikawa niko juu sana, nikamuacha Hamza akivuta baada ya kubeba mfuko mzima ambao ulikuwa kama kisado hivi nilimpa kama elfu ishirini hivi, ile kimemba tu. Nikarudi zangu ndani kujiandaa maana ilitakiwa nimuwahi mtu huyo ambae niliambiwa mida ya saa mbili na nusu atakuwa kituo namba saba.

Saa mbili kamili ilinikuta niko mtaa wa Uwazani kwenye mgahawa mmoja maarufu sana kwa mitaa ya magomeni unaitwa Mnaa hoteli.

Nilikaa zangu pale nikaagiza maziwa na maandazi Fulani hivi malaini sana ni mgahawa ambao unasimamiwa na watu kutoka Pemba kuanzia mapishi mpaka wahudumu wa hapo so nafikiri wapemba wengi hujaa sana hapo kutokana na vyakula vya jadi yao kupatikana hapo.

Saa mbili na dakika zake nilikuwa nasogea taratibu kutoka uwazani kwenda mtaa wa dosi ili nifike kituo namba saba.

Ile nimefika kwenye kona ya mkono wa kulia inayoingia New bondeni hotel au maarufu sana kwa jina la Kwa Macheni.

Kuna gari moja nyeusi, imekaa utamu ile mbaya ilikunja kutoka kwenye kona hiyo na kunipiga mkasi kwa mbele, kisha kioo kikashushwa kidogo nikakutanisha macho na Kaburu moja lenye macho ya paka janki Fulani tu hivi miaka kama thelasini hivi.

Likauliza tu “Who?”

Nikajibu “Noriega”

“Stop number?”

Nikajibu “Seven”

Likanirushia kibegi kidogo kama hivi ambavyo wanavipenda hawa watoto wa kiume uzao wa masingo maza.

Nikakidaka na kukivaa kisha gari ikapiga mwendo na kutoweka pale.

Kibegi kilikuwa kizito kwa makadirio ni kama mzigo uliomo unafika kilo tatu.

Basi nikageuka ili niondoke lakini nikahisi kama kuna gari nyuma yangu. Ni kweli nyuma yangu niliona gari ikija kwa kasi sana na hivi ni njia ya vumbi basi vumbi lilikuwa likitimka nyuma yake.

Na baada ya kunifikia dereva alifanya kuzungusha matairi ya nyuma na kutimua vumbi zaidi Akili yangu ilikuwa inawaza ni kitu gani kinataka kutokea hapa ?

Yaani mikago nishaiotea halafu kunataka kuibuka maseke tena? Mungu niepushie dhahma ya aina yoyote ile maana si unajua tena nishaupima mziki kupitia vibunda nikajua kuwa nacheza sebene la bei. Sasa nani yuko tayari kupishana na vile vitita vya dolari? Yaani ile wanji wanji mshindo mmoja unaiona milioni hii hapa, walete.
<<<<<<<<<<<<< ****** ********** >>>>>>>>>>>>>>>>>>>...

Ile gari ina heri ama shari kwa Boyo?

Tutaendelea tena panapo majaaliwa ya aliyetuumba.

Wako katika utunzi Sonko Bibo.

0653532222 Piga masaa 24 itapokelewa..
 
Mwendo
AGANO JEUSI .2.

Ile naendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu mlango wa mbele kushoto kwa dereva ukafunguliwa nikaambiwa ingia.

Kuangalia sura nikaikumbuka kumbe ni yule dereva alienipakia kutoka kule Masaki.

Nikajitoma ndani haraka na gari ikawashwa na kutembea.

Nikamuuliza dereva kuwa ni nani anampa taarifa kuwa mimi niko mazingira yale?

Jamaa kwanza akacheka kidogo kisha akaniita “Boyo”

Nikashituka, “Duuh kumbe hadi jina langu analimanya?”

Akaniambia kuwa natakiwa kushukuru kwa kuingizwa kwenye hii familia maana kwanza mshiko ni uhakika watu hawana longo longo. Na familia haina machawa tofauti na familia zingine ambazo unakuta wanaishi kisnitch.

Akaniongezea kuwa hapa tulipo tupo chini ya monitoring ya hali ya juu ikitokea tatizo backup inafika muda huo huo.

Nikashangaa kidogo nikamuuliza vipi kama ikitokea tukakamatwa na masskari njiani halafu wakatusachi na kukuta hii mizigo?

Jamaa akaniambia niachane na ndoto hizo maana hii familia ni kubwa sana tofauti na ambavyo naweza kuikadiria.

Ikabidi niwe kimya huku nikiyatafakari haya maneno ya jamaa nikijiuliza kwanini anaiita familia wakati huo mimi nikiangalia naona ni kikundi Fulani tu.

Jamaa akaniuliza nikupeleke wapi?

Nikawaza kwa nukta kadhaa nikamwambia anipeleke Buguruni aniache pale kituo cha Matumbi.

Kweli jamaa alinipeleka pale na kunishusha kisha nilitembea mdogo mdogo nikavuka na kwenda kwa mnyamani stendi pale nikajipakia kwenye gari ikanipeleka mpaka mitaa ya vingunguti.

Pale kuna mwamba wangu mmoja anaitwa Kipacha. Huyu ni mwamba ambae tulifahamiana kupitia ndugu yangu mwingine anaitwa Nyakato.

Huyu Kipacha anajihusisha na usafirishaji wa madumu ya gongo usiku kutoka Tabata Liwiti kwenda viunga vingine kama vile vingunguti na mabibo mpaka kigogo na Tandika yote hiyo.

Kipacha nilimkuta kwenye kibanda kimoja cha chipsi mtaa wa nyuma kutoka lilipo duka lake.

Ile kuniona tu hivi akaanza fujo “Oya Boyo mwanangu mbona ukanikalia kimya hivyo mwamba wangu kulikoni?”

Nikamwambia ni michakato tu ya hapa na pale ndio inatufanya tusionane, so asiwaze sana.

Naona ushaanza kuwa kama vijana wa Kino, unatembea na vibegi na wewe siku hizi, huku akikishika kile kibegi.

Nikamwambia kausha halafu mimi sio kijana wa Kino mtu wangu. Heshima zangu zote unazo na unajua kabisa mimi ni mtu wa kazi sijakaa kiree kabisa yaani.

Au umeamua kusukuma ndunga mwenyewe akimaanisha nimeamua kuuza bangi sasa.

Nikamwambia “ Kuuza msuba ni kazi moja ya kirembo sana wala haina ugumu wowote ule so time yoyote ile nikiamua nabeba begi”

Akaniambia huku akikishika kile kibegi kama anaedadisi ndani kuna nini. “Nigee kidogo basi na mimi nipaishe stimu.”

Nikamwambia, “Humu mimi sina hicho unachokiwaza nina mikago yangu tu private ambayo haihusiani na wana.”

Sikutaka aweke mazoea na kibegi kile nikamvuta mkono nikimuongoza tuelekee pale dukani kwake, nilitaka nikae pale mpaka ifike saa sita nikale ugali wa muhogo na nyama choma pale Mashujaa pub.

Mashujaa pub kwa mama Sakina, hao ndio watemi wa supu na nyama choma kwa time zile sijajua kwa sasa <<<Maana those sons of yesterday, today they’ve grown to men>>>.

Tuliondoka pale na kuelekea dukani kwake. Daah yaani kama isingekuwa hii michongo ambayo imeanza kuniingizia vitita yaani ningeyatamani sana maendeleo ya huyu jamaa maana nilikuta duka limejaa.

Yaani pale ni uswahilini lakini huyu Kipacha alikuwa ameliweka duka lake katika mfumo kama wa Supermarket.

Duka lilikuwa limeshona sana na pia kaweka na vijana wawili wanamuuzia pale dukani yaani mzigo ni mkubwa kwa makadirio ya haraka haraka jamaa mle kawekeza sio chini ya milioni Arubaini na ushee.

Nikamuuliza Kipacha mbona umepiga hatua sana mwanangu nini siri ya ushindi?

Akacheka sana kisha akaniambia “Wewe si nilikuambia uwe mtu wangu wa mkono ukakataa sasa napambana ile kisolo tu.”

Akaniambia kuwa kuhusu kujaza duka sio issue sana kuna mali kibao za magendo wana wakivunja maduka ya watu wanamletea ananunua kwa bei ya kutupa.

Akaniambia hata wewe ungekuwa na duka la mazaga kipande Fulani ungefaidi sana hii mizigo. Maana mimi huwa inanielemea mpaka naitema wanapeleka kwingine.

Sishangai maana Kipacha mara ya kwanza tunafahamiana ndio alikuwa ametoka jela.

Akaniambia pia walanguzi wa madumu ya gongo wanamlipa pesa zake japo muda mwingine inahitaji ubabe lakini ameshaimasta hiyo sekta na maaskari hawammudu tena tofauti na pale mwanzo maana sasa pesa ya kudili nao ipo.

Wakija tu hata awe na msala gani anausovu bila shida hivyo hii imempelekea kujiamini sana kila dili analimudu vyema maana kwa sasa watu wanamtambua kama <<fogo la mtaa>>.

Ukija kumuulizia vibaya hawakwambii hata kama umesimama mbele ya duka lake watakuambia yuko mtaa wa nane huko.

Nilikuja kwa Kipacha kuangalia kama kuna nafasi ya mimi kufanya mishe za kuzungusha madumu ikitokea hizi biashara zikaenda mrama.

Sikutaka kazi za kutafuta ugali ziwe za mchana niliamua kutafuta zile za usiku tu ili mchana niwe najifungia ndani nalala mpaka ikifika usiku. Maana nilihisi hawa watu tunaoitana famila kuna siku isiyo kuwa na Jina tutatibuana na kuwekeana street wanted ambayo inaweza kukulaza njaa wewe na familia yako kama huna pa kuegemea. Au unajikuta unatafuta genge jingine ili kuilisha familia na mimi sikutaka hayo yatokee ikiwa sina pa kushika.

Nilipomgusia Kipacha kuhusu utayari wa yeye kunishirikisha kwenye michongo yake ile, alidai kuwa Unakaribishwa any time ukiwa tayari maana si unajua kuwa kazi hii nilifundishwa na kaka yako Nyakato?

Nikamkumbuka broo Nyakato kama ambavyo sisi humuita huko kwetu kanda ya ziwa.

Huyu ni broo from another father. But ukoo Fulani wa Machui matupu, wachache wazembe, hatuishiwi kupambana ili kujiweka sawa kiuchumi.

Basi stori ziliendelea mpaka ilipotimu saa sita na madakika tukaelekea pale mashujaa ambapo tulikaa meza moja hivi.

Wakaja wahudumu kutusikiliza tukaagiza nyama nyingi na ugali wa kutosha tukawa tunakula huku stori za hapa na pale zikitawala baina yangu na Kipacha.

Wale wahudumu baadae waliondoa vyombo huku sisi tukiinuka bili yote akiibeba Kipacha, maana kwanza mimi ananichukulia kama mdogo wake, pili anahisi ni kama fadhila anazomlipa broo wangu Nyakato kwa kumbeba pindi hana mbele wala nyuma.

Basi tuliagana na kila mtu akaendelea na mambo yake.

Mimi nilipanda gari mpaka kwa mnyamani ambapo nilichukua zile za kwenda tandika nikashukia Temeke hospitali.

Baada ya kushuka nilitafuta bucha yenye nyama nzuri nikanunua kilo mbili na kuwapelekea familia nao wasikae kinyonge.

Mimi nikapanda kitandani kuuchapa usingizi nikimuacha wife akitayarisha chakula kwaajili ya familia lakini mimi nilimuambia asinihesabu maana niko njema.

Wife akaanza kuleta zake “Mume wangu unakula wapi huko unarudi ukiwa umeshiba hutaki hata kuonja chakula changu? Isijekuwa umepata sabu yangu tayari huko nje”

Nikamtoa wasi wasi miksa kumsifia na ukizingatia mtoto ni mzuri yaani yule asilia kabisa sio hawa wa kujitengeneza wa dukani maana ni kama masalia Fulani hivi ya kiarabu ya huko Tanga. <<Toto la kibondei hili>>.

Kwenye sifa zangu huwa hapati nafasi tena ya kununa na kulalamika huwa anakuwa mdogo kisha uso wake unachanua kwa tabasamu linaloacha vishimo kwenye mashavu yake yanayorembeshwa na vinywele laini vinavyoanzia pembeni ya masikio na kushuka chini kidogo mpaka kwenye mataya.

Mimi ni mtu wa wanawake waliojazia nyuma ile mbaya hata mama yangu anaijua hii hulka yangu tangu nikiwa mdogo, napenda sana hawa wanawake wenye tela la maana nyuma.

Haijalishi ni orijino ama la kuchonga mi kikubwa liwepo yani huo ndio ugonjwa wangu.

Nafurahi sana kuwa na mwanamke wa hivyo.

Nililala zangu mpaka ilpotimu mida ya jioni nikapokea simu ya Denis akiniambia ule mzigo kuna sehemu natakiwa niupeleke mida ya saa tatu usiku.

Akaniambia ni kituo namba moja.

Na mimi nikaandika kwenye kikaratasi.

Nikaanza kucheza na familia yangu huku tukitaniana na kufurahi maana watoto walishatoka shule wote.

Kifupi niliuona upande mzuri wa maisha ya kuwa na familia huku ukiwa na uhakika wa pesa, Kwanza hasira zinapungua unakuwa haukoromi muda mwingi zaidi ya kuwa humble kwa familia na kuwasikiliza ni zawadi gani wanataka.

Sasa wewe pata picha ni asubuhi hujui msosi wa mchana utatokea kwa muujiza gani na ndio unaaga uende kwenye mihangaiko yako then mtoto anakuambia Baba baadae niletee <<<chukuleti>>,,,,,, na ukipiga hesabu chocolate zinauzwa shillingi elfu tano. Ukiwaletea wote watatu na mama yao inakuwa elfu kumi na tano. Kwanini usifoke?

Nyie watoto msiwalaumu sana wazazi eti enzi mko wadogo hawakuonyesha mapenzi kwenu kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wenzenu hapo ni kwamba usawa ulikaba.

Aliona chakula chenu na mavazi ni muhimu kuliko hizo zawadi na mitoko ya kula bata. Muwaelewe tu.

Saa moja jioni ilinikuta pale Nguruko annex nikinywa juice moja taratibu huku nikisubiri muda uende ndipo nisogee taratibu kuelekea Mbezi Africana ambapo nilitakiwa kuonana na mtu pale nimkabidhi mfuko mmoja, maana mle kwenye kibegi kulikuwa na vimifuko sita vikiwa vimefungwa sawa yaani vinalingana ujazo sijui ilikuwa ni kiasi gani vile.

Basi nikiwa pale niliweza kuwaona watu wakiwa wanatembea barabarani upande wa kushoto kwetu huku, ukiwa unaelekea mjini.

Mara nikamuona Vero akitembea kidogo kidogo. Shobo zangu nikamuita, kiukweli ni mwanamke mmoja ambae namtamani sana hata siku moja nishiriki nae japo mara moja.

Maana kumuoa ni uongo siwezi kumuoa mke wa pili huyu kwanza atamletea tu taabu mke wangu yule mpole na msikivu huenda huyu akamfanya wife akabadilika pia maana Vero ni mkorofi halafu hajatulia hata kidogo.

Huyu anapendezea kuchapa tu maana amekaa kimkao haswa.

Akaja mpaka pale maana hakuwa akijua ni nani aliyemuita baada ya kufika tu na kugundua kuwa ni mimi kwanza akabetua midomo.

Kisha akasema masikini nae akitaka kujichanganya na wenye uwezo ataishia tu kuumbuka ona sasa umekaa eti unakunywa kajuice. Sasa umeniitia nini maana najua huwezi kulipa bili nitakayotumia hapa.

Hebu ongea haraka ulichoniitia mimi niondoke, nikamwambia kwanza kaa agiza unachotaka, Akaniuliza “Serious?”

Nikawaza hivi hawa wanawake huwa wanajikuta nani vile? any way acha niishi niwaache tu.

Nikamwambia agiza ili wakati tunazungumza uwe unaweka vitu kuhusu bili usijali nitalipa. Nikaona kama kamshangao Fulani usoni kwake ila hakutaka kukaweka wazi.

Basi akaagiza huku akijaribu kuweka pozi Fulani kuonyesha kuwa yuko na mimi, chakula alichoagiza kilikuja na vinywaji.

Ambapo nilimwambia anywe tu wala asijali na asione mtu kafika baa akaagiza kitu tofauti na pombe akahisi huyo mtu hana pesa, hapana ni kwasababu pengine hajisikii au si mtumiaji wa pombe.

Akaanza kupiga savanah baadae akadai hazipandi kamuita muhudumu akamwambia alete bapa moja kubwa, akaletewa akawa anapiga. Nilipoona amekolea nikamuingizia stori za Nadia, akaukunja, maana alijua nitamuongelea yeye lakini matarajio yakaenda tofauti.

Akauliza kwahiyo kichwani mwako amekukaa Nadia peke yake mbona siku nyingi tu ulikuwa unanifukuzia imekuwaje umehamia kwa Nadia?

Nikamjibu kuwa sikuwa nimepata wasaa wa kumdadisi Nadia vizuri mpaka ile siku niliyowaona nae yaani jana yake.

Akatishia kuwa kama nimeanza habari za Nadia basi yeye anaondoka. Nikamwambia kuwa akiondoka namuita muhudumu na kuikana ile bili ili alipe yeye.

Akawa mpole nikamuomba namba ya Nadia, akanipa nikapiga kabisa mbele yake ili kuhakikisha kuwa ni yenyewe.

Nadia akapokea nikajitambulisha, aise Nadia alifurahi sana hata sikujua ni kwanini. Basi nikamwambia niko na Vero na ndie aliyenipa namba. Kusikia hivyo, Nadia akakatisha mazungumzo na kuniambia subiri kidogo nitakutafuta baadae Boyo, bye”

Vero kusikia hivyo maana niliweka loud speaker akasonya huku akisema “Hakuna lolote umalaya tu unamsumbua huyo Nadia, au kisa shombe shombe ndio maana unampapatikia?”

Nikamuuliza “Yamekuwa hayo tena? Si ni wewe mwenyewe umekuwa ukinikwepa kama ukoma ukidai mimi sio type yako?”

Akaniambia “Tuachane na hayo kwahiyo sasa hivi unafanya kazi gani?”

Nikamwambia “Kwa sasa nimeajiriwa na shirika moja la nje linajihusisha na utafiti wa masuala ya kilimo na ufugaji.” Akashituka kidogo kisha akauliza “Kwahiyo wanakulipa vizuri eti?”

Nikamwambia “Sio kivile lakini ni kiasi kinachonifanya nimudu kuilisha na kuivisha familia yangu.” Akashituka kusikia hivyo kisha akauliza “Boyo ulishaoa kumbe?”

Nikamjibu “Siku nyingi tu na watoto wawili juu”

Akasema “Aisee hongera sana Boyo mimi mwenzako bado hata huyo mchumba sina, kila naempata hatufiki nae mahali tunaishia kugombana na kuachana mpaka nahisi labda nina gundu. Iwe huyo mtoto ambae sijui hata nitajaaliwa lini?”

Kalikuwa kanaongea ile kilevi lakini huzuni na wivu niliubaini ndani yake na ukizingatia tayari umri wake ulishagota miongo mitatu.

“Mi mwenyewe maisha yamenivuruga sana, ila haka kamevurugwa zaidi” Nikajisemea.

Nilicheki mida nikaona ni saa mbili , nikaona hilo lisaa linatosha kabisa kujisogeza taratibu mpaka Afrikana kutoka hapo Makonde. Maana ni kituo kimoja tu cha jogoo ndio kinayatenganisha hayo maeneo. Nililipa bili kisha nikamuaga Vero na kumwambia kuwa kuna sehemu nawahi kuna mtu naenda kumuona, ambapo alimaindi kimtindo huku akidai kuwa anajua tu kuwa namuwahi Nadia ila sitaki kumuweka wazi.

Sikuwa na muda wa kumuelewesha huyu mwanamke nilitemana nae na kusepa.

Nilifika pale Afrikana nikakuta gari moja imepaki upande wa kulia karibu na shamba la mitiki pale taa zikiwa zimewaka halafu kuna mtu kasimama kwa nje anachezea simu.

Mara simu yangu ikaita namba ngeni nikapewa maelekezo kuwa niifuate ile gari.

Nikaisogelea na kulakiwa na yule mtu, ni Muafrika lakini anaongea kiingereza cha Nigeria, Baada ya utambuzi na code maalumu nikampa mzigo kulingana na maelekezo niliyokuwa nimepewa nae akampasia aliyekuwa kwenye gari kwaajili ya kuuhakiki mzigo kisha nikapewa bahasha.

Nikachungulia ndani kuna dola kadhaa nikazihesabu kisha nikampigia Denis simu muda huo huo na kumuambia kuwa nimepewa kiasi kadhaa nae akanibariki na kuniambia niondoke hapo haraka sana.

Ile nimerudi barabarani na vuka kwenda upande wa pili nikaona kuna gari aina ya mark X ikiniwashia taa full nikahisi ni ishara ya kutaka nisimame maana nilikuwa kwenye kiambaza cha bara bara katikati nikisubiri zile za kwenda mjini zitoe gepu nivuke.

Ikanibidi nisimame pale pale nisivuke ambapo ile gari ilpofika usawa wangu ilisimama bila kujali kama kuna gari nyingine kwa nyuma zinaomba njia.

Dereva alishusha kioo nikamuona ni yule jamaa wa asubuhi akaniambia fungua mlango wa nyuma nikafungua na kuingia hapo tukaondoka fasta maana waliopo nyuma walishaanza kupiga honi ovyo huku wakilaumu kile kitendo.

Safari ilienda moja kwa moja mpaka pale Shamo towers tanki bovu, dereva akapaki pale, kisha Denis alitoka kwenye duka moja la nguo mle ndani akiwa na nguo kadhaa kwenye mifuko.

Akaja moja kwa moja mpaka kwenye gari yetu akafungua gari na kuingia akiomba pesa na mzigo uliobaki aliniambia niondoke nao atakuwa ananipa maelekezo wapi niupeleke.

Denis alifungua ile bahasha na kutoa noti ishirini na tano za dola mia na kunikabidhi huku akinipa na ile mifuko yenye nguo ambayo sikujua ndani yake kuna nguo za dizaini gani.

Baada ya hapo alinipa tena nauli kiasi cha laki huku akinitakia usiku mwema na wenye uangalifu mwingi nikatambua ni kwasababu ya kile kibegi ndio maana ananitahadharisha kuwa niwe makini sana.

Niliaga na kuondoka hiyo ikiwa ni mida ya nne kasoro hivi maana muda nao ulikuwa haujaenda sana kihivyo.

Baada ya kuachana nao nilichukua gari ya mwenge ambapo baada ya kufika nilidaka gari za mwishoni kabisa za Temeke maana zinawahi kukata yaani katika gari zilizokuwa zinakera kwa Dar ni zile zinazotoka Mwenge kwenda Gongo la mboto na hizi za kwenda Temeke na Tandika yaani zinawahi sana kuisha kwenye vituo vya daladala.

Saa tano na dakika ishirini ilinikuta nikiwa nyumbani maana siku hii hatukutumia muda mwingi njiani.

Niliikuta familia iko sawa, ina furaha kama zote na hotpot la msosi lilikuwa mezani kufunua nikakuta ni nyama imerostiwa vizuri ni harufu nzuri inatawala pale mezani na kaugali kangu ka muhogo maana ndio lishe ambayo naipenda sana kwaajili ya kulinda afya yangu ya mwili.

Maana hiki chakula hunifanya niwe na nguvu sana kuanzia zile za mwili mpaka zile za kitandani.

Nilikaa kula huku katoto kangu ka kike ambako ndio kadogo kakija pale kunipa kampani. Yaani ni mwendo wa maswali hadi niseme.

Baada ya kula tulijumuika wote pamoja kuangalia muvi hapo kwenye sofa.

Nikiwa naangalia muvi hiyo ni mida ya saa sita maana kesho yake ilikuwa ni weekend watoto hawaendi shule hivyo uhuru wa kukesha kwenye runinga ni juu yao ndipo simu yangu ikaita kuheki namba ni ya Denis.

Denis alinisisitiza sana kuhusu kuhama huku Temeke ili niwe karibu na viunga vya watasha.

Na mimi niliiona mantiki katika maelezo yake lakini nilikuwa nawaza kuwa sio sahihi kuisogeza famila yangu karibu na watu hawa ambao bado sijawajua vyema inaweza ikaja siku wakaidhuru familia yangu ambayo naipenda mno.

Na ndiyo inayonifanya niende resi ili kuitafutia ugali.

Nilimjibu tu kuwa nitaliangalia kwa upana wake, kisha akanitakia usiku mwema ilivyoonekana alikuwa kiwanja akiweka vitu maana nilweza kuzisikia sauti za wanawake pembeni yake na mziki uliokuwa ukirindima japo sikujua ni kiwanja gani haswa alikuwepo.

Baada ya kukata simu wife aliuliza kuwa ni nani huyo, nikamwambia kuwa nadhani ni vyema asijikite sana na simu zangu maana zinaweza kuvuruga hali ya hewa muda wowote maana sitapenda kuzitolea ufafanuzi kila simu itakapokuwa inapigwa.

Akasema kuwa yeye ni mke wangu na hiyo ni haki yake kujua. Nikamjibu hiyo haki nani alimpa?

Akabaki kimya nikamuambia kuwa najitambua siwezi kufikia hatua ya kuvuruga upande wake.

Akaridhia tukaendelea kuangalia muvi. Sasa ile nimekaa sina hili wala lile si simu ikaita tena nikaangalia jina nikaona ni Nadia, akili ikacheza fasta yaani nikaipokea fasta na kuiweka sikioni huku nikitanguliza neno “Mkuu nimefika salama nyumbani, lakini kuhusu ile issue nitakutafuta kesho ili nikupe maelekezo ya kutosha.”

Yaani sikumpa nafasi hata kidogo Nadia kuongea na nashukuru kuwa Nadia aliielewa ile code akakata simu mwenyewe akiniacha nikijiona mshindi kwa hili.

Wanaume tuna mambo yetu wote tunajua hilo.

Wife ndio kuanza “Kumbe ushaanza na kazi kabisa ?”

Nikamwambia bado niko kwenye majaribio ya awali ili waone kama nafaa wanipe mkataba maana si unajua kitengo nilichopo nimepewa majukumu ya kuwashawishi wabia waweze kuingia ubia na shirika letu ili Material mbali mbali wawe wanachukua kwetu.

Hivyo mimi nimepewa jukumu la kuyashawishi mashirika matano katika hayo matano ikitokea yamepatikana mashirika matatu tu basi napewa mkataba wa ajira katika kitengo cha Marketing and Branding.

Wife akaanza kupiga dua pale ili Mungu awe upande wangu hatimaye hayo mashirika yaweze kukubali ili mumewe nipate kazi.

Basi muda kidogo wife alisema yeye kachoka anahitaji kwenda kupumzika, nikamkubalia ili pia nipate nafasi ya kuchati na Nadia.

Basi wife aliingia chumbani akiniacha hapo sebuleni ambapo niliendelea kubaki na binti yangu wa kike mdogo wa miaka mitano akiwa ameniegemea mapajani akiwa ananesanesa.

Nilimchatisha Nadia akaibuka na mimi muda huo huo yaani ni kama alikuwa ananisubiri hivi.

Akaniuliza kuwa hivi ni kwanini wanaume huwa mnatuchiti hivyo? Maana nina uhakika umeoa na una watoto.”

Nikamuuliza hizo taarifa kazipata wapi? Akaniambia kuwa Vero alimpigia simu sio muda tu na akampa hizo info huku akimtahadharisha kuhusu kumwagiwa maji ya moto.

Nikawaza kuwa Vero kweli kaamua kunivurugia, yaani taratibu ni kama anageuka kuwa kidudu mtu kwangu.

Nikamuambia kuwa asiyaamini sana maneno ya Vero maana yule hapendi kutuona tuko pamoja.

Akaniuliza ina maana taarifa alizozisikia ni za uongo?

Nikamuuliza kuwa je yeye anaamini nini juu ya hizo taarifa akasema kuwa anaamini kuwa ni kweli nina mke.

Nikamuuliza sasa kama anaamini nina mke je malengo yake ya kupiga simu muda ule ilikuwa ni kuniharibia au ni nini?

Akasema samahani maana lengo haikuwa hivyo navyodhani bali ilikuwa ni kuhakikisha kuwa aliyoambiwa na Vero ni kweli?

Nikamuambia kuwa tayari sasa ameshaivuruga ndoa yangu na nilikuwa na matarajio ya kupewa mkate wa uzima lakini kutokana na simu yake nimeishia kunyimwa na kufokewa kisa yeye.

Alisikitika sana na kuniomba msamaha huku akidai nimsamehe tu wala haikuwa nia yake kuniingiza katika mgogoro na mke wangu.

Nikamuambia kuwa sawa nimemsamehe lakini vipi kuhusu hamu zangu natolea wapi?

Akacheka kisha akaniambia kuwa tutaongea vizuri nikiwa mbali na home. Tukaishia hapo.

Baada ya kumaliza kuchati na Nadia nilimbeba binti yangu ambae muda wote kumbe alikuwa amelala hapo hapo mapajani mwangu nikaenda kumlaza kisha mimi nikaingia chumbani.

Ile kuingia chumbani namkuta wife yuko macho wala hajalala kama alivyokuwa anadai, na kitandani kuna ile mifuko ya nguo na kile kibegi lakini kingine kikubwa zaidi ni zile pesa yaani dola kazimwaga zote hapo kitandani akiwa ametulia tuli akinisubiri nije ili aanze kuniswalika vyema.

“Mume wangu mbona una pesa nyingi hivi, zote hizi umezitoa wapi? Na vipi kuhusu huu unga ni wa nini?” Alianza mke wangu.

Nikamuambia, “Si umesikia kuwa nimeanza mchakato? hicho ni kiasi cha kuniwezesha katika majukumu yangu, maana hao watu ni wakubwa huwezi kwenda kwao ukiwa mnyonge na unaona mpaka mavazi hayo nimenunua ili niweze kuubeba vyema uhusika wangu nisije nikawa nazungumzia habari za mikataba ya mamilioni ya pesa ilihali wakinitazama muhusika mwenyewe nimechoka siendani na kile nachowaambia.”

Wife alionekana kunielewa maana sio kwamba hajui kuwa zile pesa ni kiwango kikubwa cha pesa kwa pesa za hapa kwetu anajua sana tu.

“Vipi na huu unga?” Aliuliza tena. Kwakuwa ule unga ulihitaji majibu yaliyoshiba ili asishitukie dili nikaona ngoja nimsogeze mjomba baiolojia akae mdomoni kwanza ili nimpige chenga huyu mwanamke.

Nikamuambia kuwa huo unga ndio kishawishi maana material zetu sisi ili wajue kuwa zina-function vyema ninawapa na huo unga kama sample ili wakati wa uchakataji wa zile material zetu basi end product inatakiwa iwe sawa bila kupishana na huo unga. Hapa wife akaonekana kuelewa nikamuongezea tena kuwa “usiuone hapo huo unga una gharama sana yani shirika linalipa pesa nyingi ili kuuandaa huo unga na ikitokea ukapotea basi kazi yangu itabaki kuwa ndoto na kwenda jela kabisa.

Hivyo ikitokea siku nyingine amesachi kwenye mifuko yangu hata akiukuta kidogo kiasi gani basi ajue kuwa ni kitu cha muhimu sana kwenye kazi za shirika na anatakiwa autunze kwa umakini mkubwa na asiruhusu watoto kuufikia.

Nilimwambia pia kuwa habari hizi zibaki kuwa siri kati yangu mimi na yeye, hata mama yake asimwambie akanikubalia tukalala.

Asubuhi niliamka muda wa kawaida saa mbili na vidakika vyake nikajisogeza sehemu kununua mahitaji Fulani kwajili ya siku hii maana nilienda sokoni kabisa ambapo nilipata kuku wa kienyeji kwaajili ya kutengenezwa supu.

Niliwaambia wamchinje na kumnyonyoa kabisa kuepusha shari za huko uswahilini, usije pigwa mazonge bure maana ukinunua kuku sawa unachinja na kumnyonyoa halafu namna ya kwenda kutupa manyoya yake inakuwazisha. Maana watu ni wapana wa kufuatilia maisha ya watu hawakawii kwenda kupekua mfuko wa taka ili kujua ndani mwako mlipikwa nini.

Basi baada ya kupata mahitaji nilirudi zangu nyumbani ili wife asababishe madiko diko,

Kweli kufika saa tano watu tulikuwa mezani kupata chapati laini na mchemsho wa kuku huku tukitelezeshea na juice ya kusaga ambayo tuliipoza kwa kuweka barafu ndani yake maana friji hatuna.

Kiujumla wanasema kuwa ukipata pesa na hulka yako inaanza kubadilika taratibu ndivyo ilivyokuwa inatokea kwangu yaani nilianza kuchoka hii staili ya kujibana maana nilitamani kununua friji na baadhi ya vitu ambavyo vingenifanya niishi maisha standard kabisa kulingana na matamanio yangu.

Hapo sasa ndio nikaona wazo la Denis ni wazo zuri lakini ni wapi haswa ambapo nitahamia?

Maana kama ningehamia sehemu tofauti na hii kwanza ingekuwa rahisi kwangu kulipandisha viwango life langu maana kule wasingejua background yangu nilivyokuwa naishi hivyo wasingeweza kubaini kuwa kuna mabadiliko yametokea tofauti na huku uswahilini ambapo kila hatua ndogo ingedhihirisha mabadiliko.

Basi nilimpigia Denis Simu mapema ili niijue ratiba ya Jumamosi hii nijue napangilia vipi mikakati yangu.

Akaniambia kazi itakuwa kwenye mida ya saa mbili kwenye kituo namba moja.

Basi aliniambia kuwa kama sitajali atanipa mtu ambae atanisaidia kutafuta nyumba ikiwa niko tayari kufanya vile alivyoniambia kuhusu kuhamia maeneo ya karibu.

Nikamuambia ahsante wala asijali hilo nitalishughulikia, bila shida yoyote.

Basi ilibidi niwasiliane na jamaa mmoja namfahamu huwa ni kontawa sana wa mambo ya nyumba na vyumba vizuri nikampa maelekezo akaniambia “Mkuu Boyo kama Boyo consider it done.” Kisha nikaendelea kuchill pale kihome.

Mida ya saa saba hivi yule dalali ambae anajulikana kama Konka alinipigia simu akiniambia kuwa niende anionyeshe nyumba moja kali sana mitaa ya Kawe Joseph.

Basi baadae nilifika na kumkuta Konka akiwa kijiweni ambapo alinikomba tukateleza zetu mdogomdogo mpaka mitaa ya Joeph tukakatiza pale msikitini mpaka mtaa mmoja wenye utulivu sana mtaa wa Bin Abard.

Hapo nilipata nyumba moja iko ndani ya fensi na kila kitu kimo ndani parking ni kubwa kwa maana ya uwanja hapa nikilenga mazingira ya watoto wangu kucheza.

Ndani tulikuta nyumba ile ina wapangaji wengine wawili hivyo jumla tutakuwa wapangaji watatu tu huku kila mmoja akijitegemea mita ya umeme lakini maji ndio tunashea.

Katika hawa wawili hakuna hata mmoja anaemiliki usafiri wa gari, hivyo uwanja ni mkubwa na unafaa kwa watoto wangu na wa hawa jirani zangu kama wanao kucheza.

Konka alimtafuta mwenye nyumba kwenye simu akampanga kuwa keshapata mpangaji wa pale hivyo azungumze na mimi ambapo tulizungumza.

Mwenye nyumba akasema kuwa anahitaji shilingi laki mbili kwa mwezi na angependa kodi ilipwe kwa mwaka ili aweze kupata kiasi cha kumsaidia kusolve jambo lake.

Nikamuambia kuwa nina kodi ya miaka miwili ambayo ni milioni tatu ambapo yeye baada ya kupiga hesabu akakuta kwa mwezi nimemdrag down mpaka laki na ishirini na tano.

Akasema ni bora hata ningefanya laki na hamsini kama alivyokuwa analipa alieondoka.

Nikamuambia kwamba mimi naangalia hali yangu ya uchumi maana nafanya hivyo ili kuondoa kufikiria masuala ya kodi kwa muda mrefu ili nipate muda mzuri pia wa kutafuta, lakini kama anaona inatoka nje ya mipango yake basi acha niendelee kutafuta mpaka pale nitakapopata tutakaeendana kwa bei hiyo.

Nilikuwa na uhakika kuwa hawezi kukataa maana hii ni mbinu moja aliwahi kunipa jamaa mmoja ambaye ni bingwa sana wa kufunga mikataba iwe ni ya kibiashara ama ya nyumba za kuishi.

Mara mwenye nyumba akaniambia nipo tayari kulipia lini?

Nikamuambia jioni ya leo. Maana kichwani mwangu nilipanga baadae nikachenji zile pesa kiasi ili niweze kutekeleza jambo hili.

Basi baada ya hapo tuliagana na Konka huku nikimuambia kuwa ahesabu kuwa ile biashara imeisha maana ni suala la muda mpaka kufika jioni.

Nilimuachia li-teni kwaajili ya kumlinda mpaka jioni maana maisha ya madalali nayajua yalivyo, baada ya kumpatia kile kiasi yeye anapitia sokoni ili ahemee.

Mimi niliachana nae nikaunga gari mpaka mjini posta nikakutana na duka moja tu ndio wanajiandaa kufunga wakale weekend, hili ni duka la kubadilishia fedha.

Nikazama ndani na kucheki viwango vya siku hiyo ambapo buy ilikuwa inasimamia kwenye 2000 na sell ilikuwa kwenye 2200.

Nikaona sina ujanja nilitarajia niikute buy kwenye 2200 lakini hapa nimekuta 2000.

Nilibadilisha dola 2000.

Ambapo niliondoka na risiti yangu, sikuona haja ya kwenda na zile pesa nyumbani maana kazi yake ilikuwa ni kulipa nyumba.

Nilimpigia simu Konka kumwambia amtayarishe mwenye nyumba tumalize baiashara niendelee na mambo mengine hivyo wakati napanda gari za Mwenge ndio na mwenye nyumba alikuwa anajiandaa kutoka Goba.

Maana ndiko anakoishi. Baada ya kufika Kawe Joseph nilishuka na kwenda moja kwa moja pale mtaani maana Konka aliniambia kuwa tayari wako pale na mwenye nyumba wananingojea.

Baada ya kufika nilimkuta ana nakala ya mkataba mkononi ambapo tulisogea hadi kwa mwenyekiti ambapo haikuwa mbali na hapo.

Maana shughuli za hawa watu mara nyingi humalizia majumbani mwao.

Bahati nzuri tulimkuta, tukaanguka maandishi na sahihi zetu huku shahidi upande wangu akiwa ni Konka.

Baada ya kumaliza ile biashara mwenye nyumba yeye aliondoka na kitita chake akiwa na furaha huku akinitakia maisha mema pia akinipa taratibu za pale ambapo kibinadamu ni za kawaida.

Mimi na Konka tulibaki kwa mwenyekiti tukipiga stori na kuzoeana huku mwenyekiti akiniambia mtaani kwake hakuna shida sana kama ya wizi hivyo niwe na amani na atanitambulisha kwa vijana wenyeji wa pale ambao wako kama sungu sungu. Hawa kazi yao ni kuimarisha ulinzi pale mtaani nyakati za mchana na usiku maana wengi ni wale ambao bado hawana mishe za kufanya.

Baada ya hayo tuliondoka mimi na Konka lakini hatukwenda mbali sana kila mtu akitawanyika kivyake.

Nikajaribu kupiga raundi za hapa na pale kujaribu kuangalia mazingira ya mitaa mingine ambapo nilizungukia mitaa ya kawe mzimuni mpaka pande za maringo nikijaribu kuwacheki wana katika vijiwe, pia kuangalia ni mazingira yapi nitakuwa nashitulia vijiti vyangu mbali na home kidogo.

Katika kuzunguka ndipo nikakutana na jamaa yangu mmoja tulisoma wote kidato cha kwanza shift one pale Makongo.

Huyu anaitwa Zuberi, Zuberi akanikumbuka haraka sana maana tulikuwa tunakaa kwenye vimbweta karibu na ukumbi wa mabati pale unaoitwa nyambizi(Hall ya kugongea paper) sina kumbu kumbu nzuri kuwa ukumbi ule unabeba watu wangapi but ni zaidi ya watu mia mbili kwa siku za mtihani.

Nakumbuka enzi za kidato Zuberi alikuwa ni mwanafunzi wa kutwa halafu mimi niko bweni la General Mboma. Tukiwa chini ya utawala wa Mr Africa ama Nanga.

Basi kwakuwa mimi nilikuwa nikijaribu sana miondoko ya wagumu kipindi niko skonga, mara nyingi mimi na Zuberi tulikuwa tunakutana kwenye ofisi za muziki chini ya Mjeshi Captain Mfaume.

Basi hivyo ndivyo uhusiano wetu na Zuberi ulikuwa, Zuberi alinichukua na kunipeleka kijiweni kwao ambapo ni mitaa hiyo hiyo ya Bin abard ambapo hapo nilikutana na watu wapya pia na mwanangu mwingine anaitwa Mulla Jr. musician moja mkali sana mpaka kesho yaani.

Huyu alikuwa mwanangu sana pia, maana alikuwa ni mtu wa kuimba hivyo tunafahamiana tangu makongo.

Huku nilikutana na Jamaa ambae tulipatana sana, Ndulli huyu ukimsearch hata youtube utampata ana track zake kadhaa. Japo mimi masuala ya muziki nilitokea kuyaacha na kuyachukia kabisa.

Nikabaki kama mpenzi tu na hii ni baada ya kufanya shoo moja pale Diamond Jubilee na kudhurumiwa pesa zote na promota wetu uchwara ambae haitapendeza kumtaja maana yalikwishakupita na nikasamehe.

Promota wetu alikuwa ni Captain kicheo, lakini waandaaji wa shoo ile walikuwa ni East Africa Entertainment, nawakumbuka akina Allan kipindi kile wakiwa wa moto sana.

Nakumbuka wakati imefika zamu yangu kuperform hapa ikiwa ni nyakati za kumaliza shoo watu waondoke, gundu lilianzia pale backstage ambapo machipukizi kibao walidai wanataka wapande na mimi stejini ili nikimaliza wimbo wangu ambao wote wangenipa kampani kwa kuufatisha na wao waimbe track zao tatu ili kuonyesha uwezo wao,wapate kuchomoka.

Promota akaweka ngumu kuwa inatakiwa niimbe nyimbo zangu zote, tena akadai kuwa ameshaongea na Allan ambae ndie MC wa shoo kuwa nipewe na dakika tano za kufreestyle pale jukwaani kuhusiana na event hiyo.

Sasa ile nimepanda stejini tu hivi yaani huwezi amini nimeshika mic naamsha mashabiki, ile wanaamka tu hivi mitambo yote ikazima hakuna cha sound mic wala nini.

Allan akanifuata chap akaniuliza babu vip mbona hivi? Hebu piga piga mic kwa mkono, wasanii wanaijua hii hali ikitokea mic imezima ghafla hasa zile za waya pengine labda msanii kauvuta waya nje ya kipimo chake.

Mimi Kichwani nilikuwa nishawaza kwamba hii ishabuma tayari. Maana nimeanza na gundu ni sawa na umeenda bush halafu siku ya kwanza tu unaenda shambani ile kujaribu kupalilia halafu unajikata mguuni kwa jembe, sio ishara njema hiyo.

Baada ya kuhangaika karibia lisaa lizima watu wa mitambo walihangaika sana yaani mpaka mitambo inakuja kukaa sawa hawa jamaa walikuwa wamelowa jasho.

Mashabiki wao walikuwa wapo kimya huku wakiutumia muda huo kununua na kuagiza vyakula kiukweli niwasifu tu maana sio kama kwenye matamasha baadhi ambapo tumewahi kushuhudia hadi wasanii mashuhuri wakitupiwa chupa za mikojo majukwaani.

Nadhani Imani ya mashabiki kwangu ilikuwa ni kubwa ni kubwa mno hakuna hata muhuni mmoja aliepiga kelele kuwa nishuke zaidi ni kwamba baadhi walikuwa wananyanyuka na kuja mpaka kule backstage wanachungulia upande wa mitambo kisha wanarudi kukaa.

Na heshima kwa East Africa kwa wakati huo nayo ilichangia sana. Wasanii walikuwa wengi sana tena wale wakali unaowajua kwa Tanzania waliokuwa wakihiti kuanzia 2009 kurudi nyuma.

Baadae mitambo ilikaa sawa nika-perform mpaka mwisho huku mapokezi yakiwa makubwa sana wengi wakishangazwa na uwezo niliouonyesha pale stejini.

Nilipata nafasi ya kuzungumza na mkubwa wa wakati ule Bwana Rashidi Makwiro (Chidi Benz) akanipa moyo na kunisisitizia sana kuwa nikaze na nitaweza kufika mbali.

Kikubwa nipambane nipate Lebo nzuri na studio zenye dawa za kutosha.(dawa hapa alimaanisha zile studio zenye mchujo mzuri na vyombo makini vya muziki na sio mazindiko)

Lakini baade baada ya kutathmini kile nachokifanya na uhalisia wa maisha nikagundua kuwa ni kama nakosea, maana hata mshua amekuwa akinipinga sana nisifanye muziki akiniambia yeye mwenyewe aliachana na masuala ya muziki miaka ya mapema sana mwa themanini hivi.

Basi sikuona haja ya kupambana kwenye muziki ilihali ndoto ya Mshua ilikuwa ni siku moja nivae gwanda na kupiga saluti.

Sijajua yeye aliona nini jeshini, hilo namuachia yeye maana enzi tayari imepita mimi siwezi kuwa yule niliyemtaka kwa wakati ule wala yule ambae mshua angependa kumuona ndani yangu. Sorry dad.

* ************ ****

Baada ya kuachana na wana pale kijiweni niliondoka zangu na kurudi Temeke haraka sana kujiweka sawa kwaajili ya kazi ya usiku huo ambapo ilitakiwa niwe Kituo namba moja.

Majira ya saa tatu kamili usiku yalinikuta pale kivulini nikiwa nasikiliza michezo kupitia mawingu fm.

Baadae niliona gari ikitoka Mlimani city na kusogea taratibu kama inaenda Ubungo mara ikapaki kituoni pale.

Kwakuwa mimi nilikuwa upande huu wa pili niliweza kuimark ile gari kutokana na ufahari wake maana nilijua tu hii ni ya kifisadi.

Baada ya kupaki pale simu yangu iliita na kupewa maelekezo kuwa niisogelee haraka sana.

Ambapo niliifuata jamaa kuwacheki sura ni kama wakenya hii nikawapa mifuko miwili. Wakaihakiki na kunipa bahasha na mimi niliipokea na kuihakiki baada ya kujiridhisha nilimpigia Denis kumwambia kiasi nilichopewa akaniambia sawa.

Nikashuka toka kwenye gari ile na kuwaacha waende zao, nikajaribu kuangaza huku na kule sikuona gari yoyote ile yenye attention na mimi nikadaka piki piki na kumpa maelekezo anipeleke mwenge njia ya nyuma hii inayoenda Sinza Afrika sana.

Tukiwa tumefika pale kwa wamakonde wachonga vinyago tunataka kukata kona tu simu ikaita nikamwambia dereva weka pembeni kwanza.

Kucheki ni Denis akanipa maelekezoa kuwa mwambie jamaa anyooshe na hii bara bara ya Coca mikocheni, akulete mtaa wa chato huku mtanikuta hapa.

Sikushangaa amenionaje maana nishaambiwa familia ni kubwa hii.

Nikamwambia dereva akanyoosha hadi pale, kweli nilimkuta Denis pale akiwa na baadhi ya watu ambao siwajui muda kidogo wale jamaa waliingia kwenye gari zao maana zilikuwepo gari tatu yaani mbili za wale jamaa na moja ya Denis.

Basi baada ya kubaki peke yetu tuliingia kwenye gari, Denis alihakiki mzigo wake na kuniambia kuwa niendelee na ratiba zingine mpaka hapo baadae atakaponipa ratiba ya jumapili ambayo ni kesho yake. Hakunipa malipo ya dola safari hii zaidi ya laki moja ya nauli.

Na mimi sikutaka kuonyesha mashaka yoyote maana kama ni mshahara nilikuwa sijui ni kiwango gani vipi kama mtu atakwambia kuwa kile kiasi cha pesa ambacho ni zaidi ya milioni sita ndio malipo yako ya mwezi mzima je nitakuwa na uhalali gani wa kukataa maana hakuna sehemu tuliyoandikiana kwamba kila baada ya kazi ya siku moja malipo yake ni yale yale?

Lakini tukiwa pale mara simu ya Denis iliita akasogea pembeni na kuzungumza akarudi akaniambia kuwa anajua kuwa sijazoea kufanya kazi usiku lakini ananiagiza nipeleke mzigo kituo namba sita.

Akanipa ramani yote kisha akaniambia niwahi fasta maana watu wako pale wananisubiri sio kazi ya kwenda kusubiri tena.

Basi nilichukua Boda usiku huo huo mpaka mitaa ya Hyatt Regency Hotel kufika pale niliikuta kuna gari tatu ziko pale mbali kidogo na hoteli ile, Nikapokea simu nikiulizwa Wewe ndie Noriega? Nikajibu ndio.

Nikaambiwa niende moja kwa moja mpaka pale kwenye gari.

Kufika pale nakuta watu ni vibosile vya kwenda viko na walinzi wametuna utadhani sifa yaani.

Nikawapa mifuko miwili na wakanikabidhi change utaratibu ni ule ule nikaondoka kwa piki piki niliyoichukulia mtaa wa mbali kidogo na pale.

Nikamuuliza Denis namkuta wapi akaniambia niende moja kwa moja hadi kwao pale.

Kufika pale nikaminya kitufe kengele ikaitika, Punde denis huyu hapa, kafungua geti nikazama ndichi.

Nikamkabidhi bahasha tena, lakini nilikuwa nawishi mwamba anikatie mpunga maana kumbuka mchana nimenyofoa akiba yangu kulipia chumba eti.

Baada ya Denis kuridhika nikamchomekea kuwa kesho ndio natarajia kutafuta chumba mitaa ya karibu. Akanijibu short tu Ok.

Sikujua amelipokeaje hilo, ila nikawa mvumilivu maana unaweza kuomba dola miambili za geto kumbe ungekaa kimya ungepata zaidi.

Wakati wa kuagana ndio niliyaona maajabu ya ukimya wangu. Denis alitoa kitita cha dola elfu nane yaani noti themanini za dola mia na kunikabidhi akiniambia humo kuna malipo yangu na pesa za nyumba.

Ni kweli maana kwa makadirio ya kawaida nilikuwa nimeuza mzigo wa pesa ndefu sana.

Hata Denis aliniambia kuwa nyota yangu ni kali maana kuna mafanikio na njia nzuri zimefunguka baada ya mimi kuingia katika familia huku watu wakiongeza uaminifu zaidi kwa familia hii kitu ambacho anadai kuwa wengine walikuwa wanarubuniwa na kupewa mzigo wa hovyo wanamix hivyo kupelekea chanel kuyumba.

Kuna kitu niligundua kuwa ukisikia polisi wamekamata mzigo wa madawa ya kulevya huwa sio kazi waliyoifanya wao, bali ni either manyoka ama Mashefa ya mzigo wameamua kuharibiana chaneli ndio huwatumia maaskari kuharibu chanel ya mtu ambae hawamuhitaji wao.

Denis aliniasa pia aliniambia baadhi ya miiko ya kazi hii kuwa kama sina dawa nazoziamini yaani nategemea tu nyota yangu basi nikae mbali na hawa wanawake wanaofanya biashara ya kuuza mwili tena niwaogope kama ukoma.

Akadai wengi wa wadada hao wana nuksi kali ambapo ukitembea nae tu basi mambo yanaanza kwenda mrama, utashangaa mara unapoteza mzigo au unaingia matatani.

Baada ya kunipa nasaha hizo ambazo kwangu ilikuwa ni vitu vya msingi sana niliondoka hapo kwa yeye kunitoa na gari yake mpaka aliponifikisha pale kisiwani mataa ya Morocco akanishusha na yeye akarudi mi nikatafuta usafiri wa kwenda nyumbani ambapo nilipata Boda ya haraka hiyo ikiwa ni saa sita kuelekea saa saba mara simu ikaanza kuita nikacheki ni wife wasi wasi wake ni ule ule kujua kama niko salama.

Nikamwambia niko salama na pia niko njiani kurudi.

Akasema sawa.

Tulifika salama nyumbani nikaachana na boda yeye akapiga misele yake mimi nikazama ndani.

Baada ya kuingia sebuleni nilimkuta wife lakini nilipoutazama uso wake sikuiona nuru niliyoizoea nikajua ana mashaka na mida yangu ya kurudi home nikajipanga kumkabili iwe kwa nyeusi ama nyeupe.

“Hivi kweli mume wangu kazi gani hiyo inakuweka nje mpaka siku inabadilika wewe uko nje tu?

Nilimtazama nikaona huyu kiumbe kwanza ni mzuri sana so sitakiwi kumlisha Imani ovu kwenye moyo wake maana kama atabadilika aisee huenda ikanitesa sana kuja kupata mwanamke wa kiwango chake atakaenipa sikio kama yeye.

Sawa naweza kujifariji kuwa kwaajili ya pesa naweza kumpata nimtakae lakini kumbuka inawezekana mwanamke mwingine mwenye kaliba hii anaweza kuwa ameolewa na mwenye pesa pengine kuliko mimi.

Je nitaivunja ndoa yake ili nimuoe je na yeye atakuwa mjinga kurubuniwa akubali? Nikaona kuwa pesa itaishia tu kuniletea machangudoa wa kila sampuli na sio mwanamke wa kunifaa.

Kama ni hawa wauza miili mtandaoni sawa nitawala mpaka athumani mdogo ataota sugu lakini sio kumpata mke kama huyu.

Maana sijui baada ya kuachana nae hatma itaamua nini juu yangu hapo baadae, hivyo natakiwa nimtunze na kumficha kutoka kwa hawa walimwengu waharibifu ambao wengi ni wanawake waleta ushosti kumbe wamekula posho za vibopa ili wamsogeze mke wangu kitandani achafuliwe na kupandikizwa pepo la ukahaba maana mwanamke akishauza mwili mara moja haachi ataendelea kuuza tu maana ataizoea hii dhambi.

Nilizama kwenye mfuko wa koti langu la leather nikatoa karatasi ya ule mkataba niliofunga mchana na kumuonyesha huku nikimwambia kuwa nisingeweza kuondoka bila kukabidhiwa mkataba huu maana shirika limenilipia nyumba hiyo na kunitaka nisiondoke bila kuhakikisha nimepewa mkataba huo.

Akaniuliza hiyo nyumba ni ya nini sasa ndipo ofisi yako itakapokuwa?

Nikamwambia kuwa sisi kama familia tunatakiwa kuhamishia makazi yetu pale.

Wife alisahau hasira zake zote akaruka juu na kunikumbatia kwa furaha mno.

Akasema walau sasa tutaondoka hapa, palikuwa pamenichosha ni vile hujui tu.

Nikamwambia kuwa asijali kila jambo huja kwa wakati wake.

Basi aliniandalia chakula nikaanza kula, wakati nakula ujumbe wa maandishi uliingia kwenye simu yangu, kucheki ni Nadia akiuliza vipi hali yangu pia akiniomba msamaha maana kutwa nzima hakuweza kunitafuta kutokana na mtingo wa majukumu ya weekend.

Nikamjibu nipo home nitamcheki kesho yake asijali.

Maana na mimi nilikumbuka sikupata hata wazo la kumfikiria kutokana na kashi kashi za siku hiyo.

Baada ya chakula tulipanda kitandani kulala huku mawazo yakiwa ni lini nifanye utaratibu wa kuhamia kule kawe maana nilihitaji uhuru zaidi maana hapa mtaani kutokana na mfululizo wa kurudi night kali naweza kujikuta nashinda kwenye kura za wizi hapa mtaani. Na hii sura yangu ya mkataa pema.

Asubuhi saa moja wife ananiuliza “Baba Fulani si leo uende hata kanisani ukamuombe na kumshukuru Mungu akufungulie milango ya Neema?”

Nikamuuliza “Nani kamfungia Mungu huko kanisani kiasi kwamba hatuwezi kumuomba hata tukiwa majumbani mwetu?

Akaniambia kuwa unawezaje kupokea sakramenti ukiwa hapa nyumbani?

Nikamwambia kuwa kanisa ni faida ya watu wachache na mimi si miongoni mwao hivyo aende yeye kama anaona matunda yake.

Ile tunaongea pale mara simu ikaita kucheki nikaona ni Mama yangu mzazi, tukasalimiana na baada ya kujuliana hali akasema kuwa baada ya wiki moja anatarajia kuja kunitembelea awaone na wajukuu wake.

Sikujibu nikamuuliza Baba yuko wapi?

Akajibu yuko nae hapo nikamwambia ampasie simu.

Nikaongea na mzee ambae niligundua hayuko sawa kupitia sauti yake, lakini hakutaka kuniweka wazi juu ya hilo hata nilipomuuliza alikataa akidai yeye yuko sawa ni kwa sababu ya tumbaku alilovuta sana limepelekea koo lake kukauka.

Nikamwambia kuwa kuna kiasi cha fedha nitamtumia kwenye simu yake kwaajili ya kumsogeza kwa mahitaji ya hapa na pale.

Akasema sawa atashukuru sana.Nikamwambia amrudishie mama simu, tukaendelea kuongea na mama nikamkaribisha sana na kumwambia kuwa aniletee mrenda mkavu maana nimeumisi sana, ambapo aliniambia kuwa atanifungashia na michembe pamoja na karanga. Tukaagana baada ya kuwa amemaliza kuongea na kila mmoja hapa home.

Basi siku ilienda kama ilivyo ada na kufika mida ya kazi niliweza kufika mazingira ya Mayfair Plaza ambapo nilifanya biashara pale na kumaliza mzigo kabisa maana hawa waarabu wa hapa walinunua mzigo wote niliokuwa nao wakidai kuwa wamekuwa hawapati mali grade kama hii.

Baada ya kukutana na Denis tulifanya yale yaliyo desturi, nae akanipa kiasi cha Dola elfu sita. Yaani huu mzigo niliochukua kwa yule mdachi ni kwamba ulinipa pesa sana maana kwa makadirio ya chini haipungui milioni ishirini na tano halafu ndani ya wiki moja tu.

Ni sawa maana kama mzigo wenyewe una gharama zaidi ya milioni miatatu si vibaya mimi nikipata hicho kiasi.

Hapa baada ya kurudi home Denis aliniambia kuwa naweza kuwa free ndani ya siku tatu hizi huku tukisubiri mzigo mwingine uingie nchini.

Nikaona huu ndio muda wa kutumia kuhamia Kawe. Pia nimtafute Nadia tuyajenge vizuri maana pesa na muda vyote vipo.

Hapo mimi mwenyewe hata nikijiangalia kwenye kioo naona kabisa kuna mabadiliko.Yaani kuna siha Fulani hivi inajitengeneza ya kuwaambia watu kuwa sasa niko njema zile dhiki ndogo ndogo natengana nazo.

Tulipanda kitandani kulala lakini simu ikaita kucheki namba ni ngeni nikaipokea, Sasa kama ningejua kuwa siku yangu itaharibiwa na hii simu ni bora ningezima hata simu, haijalishi ningepishana na taarifa gani muhimu maishani mwangu lakini sio kuruhusu hii simu iingie wakati huu.

Je simu hii imebeba nini kwa Boyo?

Tukutane panapo majaaliwa,

Wenu katika utunzi Sonko Bibo. +255,653-532222.
tena
 
Back
Top Bottom