Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Marando ambaye ni mwanaharakati wa siasa za vyama vingi na gwiji wa sheria nchini, aliugua ghafla mwaka jana akiwa nyumbani kwake na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili usiku wa kuamkia Septemba 4.
Baada ya kupatiwa matibabu katika wodi maalum aliyokuwa amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, hali yake ilionekana kuzidi kuwa mbaya na hivyo familia yake kulazimika kumpeleka India kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, uongozi wa Muhimbili katika kipindi hicho haukuweka wazi ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Marando. Taarifa za kuaminika ni kwamba, Marando alitibiwa nchini India na kurejea kwa ajili ya kuendelea na mazoezi madogomadogo ya kumsaidia kuimarisha afya yake.
Kwa mujibu wa watu wa karibu yake hali ya Marando imeimarika na ingawa hajaanza kazi rasmi, amekuwa akitoa misaada ya kitaaluma kila anapohitajika, hasa kwa baadhi ya wanasiasa kutoka Chadema.
Mmoja wa viongozi wakuu wa Chadema ambaye hakupenda kutajwa jina lake kwa sababu si msemaji wa familia ya Marando, alisema hali ya kiongozi huyo kwa sasa ni nzuri tofauti na ilivyokuwa mwaka jana.
"Kwa kweli Marando mwaka jana aliumwa sana (lakini) tunashukuru Mungu kwamba madaktari wamejitahidi kwa hali na mali wakampatia matibabu mazuri na hatimaye afya yake kwa sasa ni nzuri," alisema kiongozi huyo.
"Viongozi (wa Chadema) wamekuwa wakienda kumtembelea mara kwa mara."
Mwanasheria mkongwe huyo amekuwa akitegemewa katika kusimamia masuala mbalimbali ya kisheria ya Chadema, na kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana aliahidi kutangaza matokeo kadri ambavyo angekuwa akiyakusanya kutoka kwa mawakala wa chama hicho.
Matangazo hayo yangekuwa kinyume na Sheria ya Uchaguzi na huenda Jeshi la Polisi lingelazimika kumtia nguvuni, lakini aligumua muda mfupi kabla ya tarehe ya tukio hilo kubwa la kidemokrasia la kila baada ya miaka mitano nchini, hata hivyo.
Alipotakiwa kueleza ni lini hasa pengine Chadema inataraji Marando atakuwa amerudi kwenye shughuli zake za kila siku, kiongozi huyo alisema, "Nakushauri uonane na familia yake (maana) ndo wanaweza kukueleza vizuri zaidi."
Nipashe iliwasiliana na mke wa Marando ambaye alisema hawezi kuzungumza kwa niaba ya mume wake na kushauri kuvuta subira mpaka pale Marando mwenyewe atakapoamua kuonana na mwandishi yeyote wa habari.
"Mimi siwezi kuzungumza kwa niaba ya mume wangu, na naomba usininukuu," alisema mkewe huyo nyumbani kwa Marando.
"Subirini atatoka mwenyewe kuzungumza na nyie mpaka mtaridhika."
Marando ni miongoni mwa wanasiasa wa kwanza wa upinzani nchini baada ya kuwa mmoja wa waanzilishi wa jukwaa la NCCR na kisha chama cha NCCR-Mageuzi muda mfupi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Chanzo: Nipashe