Niruhusuni nitundike haya machache kwa haraka kuhusu Kwanini watanzania wanamlaumu mwalimu nyerere kwa kukosa elimu?
Hakujatokea Rais wa Tanzania ambaye alikazania elimu, kama Mwalimu Nyerere; tusisahau Nyerere alikuwa Mwalimu!
Mtihani wa Territorial Standard Eight uliondolewa nilipokuwa Darasa la 7 (1958), wale waliokuwa Darasa la 8 wakawa wa kwanza kuandika mtihani wa National Primary School Leaving Examination.
Territorial Standard Eight ulikuwa kikwazo kikubwa kuwapata wanafunzi wa sekondari, ambazo wakati huo zilikuwa nichache sana! Manake ilikuwa mwanafunzi ashinde Daraja la Kwanza au la Pili!
Kuna uwezekano mkubwa hata kwa hao waliokuwa wakishinda Daraja la Tatu kuweza kujifunza zaidi na kushinda hata Daraja la Kwanza wafikapo sekondari!
Wakati huo huo, sekondari za serikali karibu zote zilianza na mifumo miwili. Badala ya wanafunzi 45, zilichukua wanafunzi 90 Darasa la 9!
Darasa letu la 8 lilikuwa la mwisho kabla elimu ya Shule ya Msingi kuwa miaka saba. Hii ilisaidia kuwapata wanafunzi wengi waliokuwa wamemaliza elimu ya msingi ili waweze kuendelea na sekondari mapema.
Wanafunzi wa Darasa la 7, pia, walikubaliwa kuandika mtihani wa Darasa la 8 ili washindapo waingie sekondari bila kizuizi.
Serikali iliondoa ubaguzi wa rangi ( za Wahindi na Wazungu) na dini zote (Waismailia, Wakatoliki, Wasabato, Waprotestanti, na kadhalika) katika mfumo wa elimu zote.
Nilimaliza Darasa la 9 wakati wa uhuru. Nikiwa Darasa la 9, serikali ilitoa Mtihani wa Territorial Standard Ten. Hiki kilikuwa ni kikwazo kikubwa kuwapata wanafunzi wa kuendelea na Darasa la 11! Manake ilikuwa mwanafunzi ashinde Daraja la Kwanza au la Pili!
Mwaka uliofuata karo ikaondolewa katika mashule yote nchini. Wanafunzi wa Darasa la 11 waliruhusiwa kuandika mtihani wa Darasa la 12 wa Cambridge School Certificate, Ordinary Level ili washindapo waingie Darasa la 13 bila kizuizi.
Wakati huo huo, Mwalimu Nyerere alikuwa amefanya safari nchini Amerika na Ulaya Magharibi kuomba serikali na wafadhili wengine kuisaidia Tanganyika katika mambo ya elimu: kuanzisha Chuo Kikuu hapo Lumumba Street.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu (kampasi ya kwanza) walikuwa wakila na kulala hapo Dar es Salaa Technical College, kabla ya kuanza kujenga na kuhamia kampasi ya Mlimani!
Akiwa Amerika, Nyerere alipata pia msaada wa walimu wa Peace Corps, baada ya walimu Waingereza kufunga mizigo yao kufuatia uhuru. Peace Corps walifundisha shule za msingi hadi sekondari. Wengine watakumbuka uji wa oatmeal katika shule za msingi!
Ikumbukwe kwamba tulikuwa na koleji moja tu ya Makerere, kampala, Uganda, kwa nchi zote za Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na kupokea wanafunzi kutoka Selisheli na Nyasaland (Malawi).
Lakini hiyo koleji yetu ilikuwa chini ya mbawa za London University wanafunzi walikuwa wanapata digrii za London University.
Kila nchi (Tanganyika, Uganda na Kenya) zikaamua kuanzisha University of East Afrika (Uganga na Kilimo, Makerere; Uhandisi na Biashara, Nairobi; na Sheria na Elimu, Mlimani).
Nikiwa Darasa la 12, mwaka huo tukawa wa kwanza kuwa pre-selected kwenda Darasa la 13 kabla ya majibu kutoka Uingereza.
1964 nilijiunga na Tabora Sekondari (Wavulana). Mwaka 1965 tukawa wa kwanza kuingia Chuo Kikuu kwa Principal moja na Subsidiary moja ili kuongeza idadi ya wanafunzi wenye digrii ya kwanza.
Kwa kuwa Tanzania ilikuwa na walimu wachache, wengi wetu iliwabidi waombwe kuchukua kozi ya Ualimu (Education Option). Kwa kila mwanafunzi wa Tanzania aliyechukua masomo yasayansi alilazimishwa kuchukua hiyo Education Option!
Kudhibiti ujinga kwa elimu ya watu wazima (kisomo, elimu ya watu wazima na maendeleo vijijini) kuliiwezesha Tanzania kuinua kisomo karibu 95% (kushinda nchi zote za sub-Saharan Africa)!
Tusisahau Azimio la Musoma: waliomaliza Darasa la 12 na kufanyakazi miaka miwili waliruhusiwa kuomba kujiunga na Chuo Kikuu. Wengine walikuwa wakijiunga kupitia mtihani wa Mature Age Entry ukidhibitiwa na Elimu ya Watu Wazima ya Mlimani.
Alileta mapinduzi katika elimu: Elimu ya Kujitegemea ili taifa lijitegemee. Tukashindwa utekelezaji wake, shauri ya kasumba nyingi za kikoloni, hadi leo hii!!!!!