(Contd...)
Kuhusu ajira yake serikalini, Zombe alisema tayari amewasilisha notisi ya kuacha kazi Agosti 18, mwaka huu ikiwa ni siku moja tangu ashinde kesi, kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ambayo gazeti hili lina nakala yake.
"Nilipokuwa nikiishi gerezani, nilikuwa nikiwaza mambo mengi, likiwemo hilo la kuacha kufanya kazi serikalini, nimeamua kuchukua hatua hiyo nikihofia kuwa kama nikiendelea kufanya kazi serikalini nitaweza kubambikiziwa kesi nyingine," alisema Zombe.
Notisi hiyo ambayo ina kichwa cha habari kisemacho; 'Ombi la kustaafu kwa hiari baada ya kutimiza miaka 55 katika utumishi Jeshi la Polisi jalada Na. PF 12599 Check Na. 48812558' inaonyesha kuwa ilipokelewa na ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI).
"Ifikapo Septemba 21, mwaka huu, nitakuwa natimiza umri wa miaka 55 ambapo kwa hiari yangu mwenyewe pasipo kushawishiwa na mtu yeyote, nimeamua nistaafu kwa hiari, hasa nikizingatia matatizo ambayo nimeyapata kwa kubambikiziwa kesi ya mauaji na huku taratibu za kisheria zikikiukwa wazi wazi kwa hila na kunikomoa. "Napenda kufahamisha ofisi yako kuwa, ifikapo Septemba 21, mwaka huu, mimi naomba nistaafu kwa hiari na nilipwe mafao yangu yote kama sheria inavyoelekeza katika kifungu Na.58(4) cha "Police Force and Auxilliary Service Act, R.E 2002', baada ya kuonekana sina hatia ya kosa hilo la mauaji na nilipoachiliwa na Mahakama Kuu Agosti 17 mwaka huu, na vifaa vya serikali ikiwemo sare za jeshi nitazirudisha pasipo shaka," inasema sehemu ya notisi hiyo.