Zitto alipua ufisadi wa bil. 20/- za madini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Zitto alipua ufisadi wa bil. 20/- za madini

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Jul 1, 2011.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jul 1, 2011
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,759
  Likes Received: 82,733
  Trophy Points: 280
  Zitto alipua ufisadi wa bil. 20/- za madini

  Na Grace Michael, Dodoma
  Majira

  MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, jana aliibua kashfa nyingine dhidi ya serikali ya upotevu wa sh. bilioni 20 zinazolipwa na kampuni za
  madini.

  Kutokana na kashfa hiyo, mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alipendekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi.

  Mbali na hilo, mbunge huyo pia alielekeza lawama zake kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na Waziri wa Fedha, Bw. Mustafa Mukulo kwa kutoa misamaha wa kodi kwa kampuni zinazokuja nchini kwa utafiti wa mafuta na gesi.

  Alisema kuwa misamaha hiyo haina tija kwa taifa kwa kuwa inasababisha upotevu wa mabilioni ya fedha za Watanzania.

  "Nimekuhusisha Waziri Mkuu kwa kuwa ulikwenda kufungua mkutano wa wawekezaji ambao kupitia wewe walipata fursa ya kutoa ombi lao kwako, na hii ndio maana ya kurubuniwa...ifike mahali tutunge sheria itakayozuia kurubuni lakini halikuwa jambo jema kumchukua Waziri Mkuu kwenda kufungua mkutano huo," alisema Bw. Kabwe.

  Bw. Kabwe aliyasema jana bungeni wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu, ambapo alisema kuwa ni hatari kuona upotevu wa sh. bilioni 20 kwa mwaka mmoja tu.

  "Kuna sheria ya madini ambayo tuliipitisha hapa bungeni na serikali iliingia katika mpango wa uwazi katika sekta ya madini (EITI) na baada ya wakaguzi wa mpango huo kupita katika makampuni ya madini kuchunguza fedha wanazotoa serikalini kwa kuonesha risiti na upande wa serikali kwa maana ya kilichopokewa, ilibainika upungufu wa sh. bilioni 20," alisema Bw. Kabwe ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji wa CHADEMA.

  Alisema kuwa ukaguzi huo ulifanyika katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 ambapo upotevu wa fedha hizo ulipobainika na akasema kuwa wizara husika ilipobanwa kuhusiana na suala hilo ilieleza kuwa nyaraka zinazohusiana na fedha hizo zimeshateketezwa.

  "Inashangaza kuona nyaraka za serikali tena zenye umuhimu kama huo zinachomwa moto kwa muda wa mwaka mmoja...tunaomba CAG achunguze suala hilo tena kwa muda wa miaka 10 iliyopita kwa kuwa inaonesha kuna kundi fulani linanufaika na fedha hizi," alisema Bw. Kabwe.

  Akizungumzia suala la misamaha ya kodi kwa kampuni za utafiti wa mafuta, alisema kuwa haikuwa na sababu yoyote kutolewa kwa kuwa baada ya kipindi kifupi Tanzania itakuwa ni nchi pekee ambayo haina mshindani katika mafuta na gesi.

  "Hatuna sababu yoyote ya kuendelea kutoa vivutio kwa wawekezaji katika sekta hizi, na ninashangaa kuona Wizara ya Fedha kushikilia msimamo wa kutoa misamaha hiyo tena kwa muda mrefu huku suala hili likiwa limekataliwa na Kamati ya Fedha na Uchumi...hivi kwa mazingira haya tukisema mmehongwa mtakataa?" alisema Bw. Kabwe.

  Akizungumzia suala la kupandishwa kwa kodi ya mafuta ya taa, alipendekeza fedha hizo zielekezwe katika mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA) ili wananchi wapate umeme na hatimaye kupunguza gharama za maisha.

  "Ili wananchi wetu waone tunawapa unafuu ni lazima sasa fedha hizi zielekezwe kwenye umeme ili matumizi ya mafuta ya taa yapungue na hapo watapunguza gharama kwani suala hili limefanyika kwa nia njema ya kupambana na tatizo la uchakachuaji wa mafuta," alisema Bw. Zitto.

  Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Suzan Kiwanga (CHADEMA), alisema kuwa ili nchi hii iendelee ni lazima serikali iachane na starehe inazoendekeza kama za kutenga sh. milioni 1,900 kwa ajili ya chai ya ikulu.

  Alisema kuwa inashangaza kuona mwaka jana fungu hilo lilitengewa sh. milioni 300 ambayo kwa mwaka huu imepanda na kufikia sh. milioni 1,900.

  "Wakati uchumi ukikua taratibu matumizi yanakuwa mengi, serikali iache haya mambo ya chai ili fedha hizi ziende kwenye maendeleo, hatuwezi kuendelea kwa starehe hizi," alisema Bi. Kiwanga.

  Alishauri kuwa ili mambo yaweze kutekelezeka ni lazima serikali ijielekeze katika jambo moja ambalo litazaa matunda na sio kuwa na vitu vingi ambavyo havitekelezeki.
   
 2. Ikumbilo

  Ikumbilo JF-Expert Member

  #2
  Jul 1, 2011
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 455
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Zitto afichua ufisadi madini


  Na Muhibu Said
  1st July 2011

  [​IMG]
  Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe


  Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ameshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua mapato katika sekta ya madini ya miaka 10 iliyopita, kutokana na jumla ya mapato yaliyolipwa na makampuni ya madini kwa serikali kubainika yalikuwa na tofauti ya Sh. bilioni 20.

  Zitto alisema kuwa kiasi ambacho wawekezaji walidai kuwa walilipa kama kodi kilikuwa pungufu ya Sh. bilioni 20 kulinganisha na kiasi kilichoelezwa na serikali.

  Alitoa ushauri huo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, bungeni, mjini hapa jana.
  Alisema tofauti hiyo ilitokana na ripoti iliyotolewa na Taasisi iitwayo Extractive Industries Transparency Initiative (EITI) baada ya kukagua malipo yaliyofanywa na makampuni ya madini kwa serikali mwaka huo.

  Zitto alisema ushauri huo ni muhimu kutekelezwa kwani utasaidia kuepuka ugonjwa unaoikumba nchi ya Nigeria, ambako fedha zinalipwa kama mapato ya serikali, lakini zinaishia kuingia mifukoni mwa watu binafsi.

  Alisema mamlaka husika ya serikali ilipoulizwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC, ambayo yeye (Zitto) ni mwenyekiti wake, ilidai kuwa nyaraka zinazohusiana na suala hilo zimechomwa moto.

  Alisema baada ya ushuru wa mafuta ya taa kuongezwa kutoka Sh. 52 hadi 400.30, serikali inapaswa sasa kutoa agizo ushuru huo upelekwe kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili ukasaidia umeme vijijini.

  Alisema wakati wa bajeti kulikuwa na malalamiko mengi yaliyotolewa na baadhi ya wabunge kuhusu misamaha ya kodi, lakini serikali ilishikilia msimamo wake kwamba, lazima misamaha hiyo iendelee.

  Hata hivyo, alisema kuna msamaha wa kodi uliotolewa na serikali, ambao anadhani serikali haikufikiria vizuri katika kuutoa.

  Alisema jambo hilo alilijadili vizuri kwenye Kamati ya Fedha na Uchumi na kwamba, alitarajia kuwa lingebadilishwa kwenye Bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi, lakini haikufanyika.

  Alisema Waziri Mkuu alikutana na makampuni ya kutafuta mafuta nchini wakamuomba kwamba, waondolewe kodi katika mafuta wanayotumia katika kutafuta mafuta kwa madai kwamba, jambo hilo litasaidia uwekezaji zaidi.

  Hata hivyo, alisema kwa sasa hivi kwenye eneo la utafutaji mafuta na gesi hakuna wa kushindana na Tanzania na pia serikali haiwezi kutoa vivutio kama ambavyo Kenya wanatoa, kwani wana makampuni manne yanayotafuta mafuta wakati Tanzania ina makampuni zaidi ya 22.

  Alisema pia Tanzania haiwezi kutoa vivutio kama Msumbiji wanavyotoa, kwani faida pekee waliyonayo (Msumbiji) ni gesi waliyoigundua, ambayo iko kusini mwa Mkoa wa Mtwara. Zitto alisema kitu, ambacho serikali inatakiwa kukifanya ni kuhakikisha kiwanda cha gesi (LNG plant) kinajengwa haraka iwezekanavyo kabla Msumbiji hawajafanya hivyo.

  Alisema Tanzania haitakuwa na faida ya kutoa vivutio kwa mafuta ya makampuni, ambayo yanatafuta madini, kwani itapoteza fedha bila sababu ya msingi.

  "Na jambo hili ni la kuangalia kwa sababu kwenye mikataba yetu ya mafuta tuna vitu viwili; kuna kitu kinaitwa profit oil na coast oil. Coast oil maana yake ni kwamba kampuni ya mafuta ikishapata mafuta inatoa gharama zake zote, wanajilipa. Wakishajilipa zile gharama za mafuta yaliyoabaki ya ziada ndio tunayogawana," alisema.

  Mbunge wa Viti Maalum (Chadema-Morogoro), Suzan Kiwanga, aliitaka serikali kubadili utaratibu wa chai ofisi zake ili fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo zipelekwe kugharamia miradi ya maendeleo.

  Mbunge wa Viti Maalum (Chadema-Mbeya), Naomi Kaihula, aliitaka serikali kutumia rasilimali zilizopo kuanzisha mfuko wa kuwatunza watoto nchini.
  Mbunge wa Viti Maalum (Chadema-Pemba), Raya Ibrahim Khamis, alisema anasikitishwa kuona Wazanzibari wakisahaulika kwenye kitabu cha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...