Zanzibar kuna mafuta machafu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,320
33,125
Kumeibuka wimbi kubwa la vyombo vya moto kuharibika yakiwemo magari na pikipiki kutokana na wamiliki kuuziwa mafuta machafu katika Manspaa ya mji wa Zanzibar.

Tatizo hilo limeanza kujitokeza siku moja tangu kumalizika kwa uhaba wa mafuta ya petroli na dizeli uliyokuwa umeikumba kwa muda wa wiki mbili na kuathiri harakati za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Zanzibar.

Uchunguzi wa NIPASHE umebaini baadhi ya vituo vya mafuta vimekuwa vikiuza mafuta machafu yakiwemo yaliyochaganywa na maji na mafuta ya taa.

Wakizungunza kwa nyakati tofauti mafundi katika gereji ya Mkunazini na Mombasa Vikokotoni walisema kwamba kumekuwepo na wimbi kubwa la magari kuharibika kutokana na matumizi ya mafuta machafu.

Fundi Mohammed Iddi wa gereji ya Mkunazini alisema gari nyingi na pikipiki wanazopokea zimeharibika sehemu ya injini kutokana na matumizi ya mafuta machafu na kusababisha hasara kwa wahusika.

Alisema serikali lazima iwe na utaratibu wa kuchunguza viwango vya ubora wa mafuta kabla ya kuingizwa katika soko la ndani ili kuhepusha athari za kiuchumi kwa wananchi wake.

"Wafanyabiashra wao wanajali zaidi biashara hawaangali maslahi ya wananchi wanaoumia na tatizo la mafuta machafu," alisema Fundi Iddi.

Naye Fundi Juma Ali wa Mombasa alisema kwamba Serikali ifanye uchunguzi kuhusu tatizo hilo na wamiliki wa vituo vya mafuta wachukuliwe hatua za kisheria.

Dereva teksi katika kituo cha Mkunazini Abdulsamad Omar Salum, alisema kwamba kilio kikubwa katika kituo hicho ni gari nyingi kuharibika kutokana na tatizo la kuuziwa mafuta machafu.

"Mafuta tunayouziwa katika vituo ni machafu tunaomba serikali kufanya uchunguzi na kuchukuwa hatua za kisheria kwa wahusika," alisema Abdulsamad.

Alisema kwamba yeye binafsi ameuziwa mafuta machafu katika kituo cha mafuta kimoja huko Kiembesamaki na kusababisha chombo chake kuharibika.

Dereva teksi Mzee Abdalla mkazi wa Vikokotoni Zanzibar alisema hajafanyakazi siku sita baada ya kuuziwa mafuta machafu ambayo yamesababisha gari yake kuharibika na kulazimika kutumia Shilingi 300,000.

"Mpaka sasa gari yangu ipo katika gereji ya Vikokotoni kwa kweli nimepata hasara kubwa ni tatizo la mafuta."alisema Abdalla.

Hata hivyo, Kamishina wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Mohamed Hashim Ismail alisema kazi yake kubwa kukusanya kodi ya mafuta na siyo kusimamia viwango vya ubora wa mafuta.

Alisema kwamba jukumu la kusimamia viwango vya ubora wa mafuta kabla ya kuingizwa katika soko la Zanzibar ni la Wizara ya Nishati.

"Kazi yetu ZRB kukusanya Mapato suala la kupima viwango vya ubora wa mafuta jukumu la Wizara dhamana ya nishati waulizeni wao," alisema Kamishina Hashim.

Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi Maji na Nishati, Zanzibar Mwalim Ali Mwalim alisema kwamba Wizara yake haihusiki suala la kupima viwango vya ubora wa mafuta.

Alisema kwamba jukumu hilo ni la ZRB kwa vile wao ndiyo wanaotoa lesseni za biashara ya mafuta na kukusanya mapato kupitia sekta hiyo.

"Kwa mujibu wa Sheria Bodi ya Mapato ndiyo wanaotoa lesseni za biashara ya mafuta jukumu lao pamoja na kusimamia viwango vya ubora wa mafuta," alisema Katibu Mkuu huyo.

Zanzibar kwa mwezi imekuwa ikitumia lita Milioni sita za mafuta ya aina mbalimbali lakini upatikanaji wake umekuwa wa mashaka kwa muda wa miaka 10 tangu SMZ ilipoifukuza kampuni ya Kimataifa ya Mafuta ya ECOTEC kutoka Nchini Uingereza.



CHANZO: NIPASHE
 
Kumeibuka wimbi kubwa la vyombo vya moto kuharibika yakiwemo magari na pikipiki kutokana na wamiliki kuuziwa mafuta machafu katika Manspaa ya mji wa Zanzibar.

CHANZO: NIPASHE

Hivi kumbe ile ni manispaa tu na wala sio nchi kama wengine tunavyofahamu!
 
Kweli mwenzangu, mafuta sijui wana yachanganya na nini na hiyo foleni ya kusubiri mafuta ndio usiseme, tunanunua mafuta kwenye dumu yani adha moja kwa zote .....
 
Back
Top Bottom