Zanzibar Heroes, Rwanda leo
Na Sophia Ashery
TIMU ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes', leo inavaana na Rwanda 'Amavubi' katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Zanzibar Heroes imetinga hatua ya robo fainali hiyo baada ya kuibuka vinara katika kundi lake la C, ikiwa na pointi nne ikiwa imetoka sare ya mabao 2-2 na Sudani kabla ya kuichapa mabao Ethiopia 3-1.
Kwa upande wake Rwanda ilishika nafasi ya pili katika Kundi B ikiwa na pointi sita sawa na Uganda, ina mabao 11 ya kufunga, imefungwa matatu, imepoteza mchezo mmoja, imetoka sare mmoja na imeshinda michezo miwili kati ya mitatu iliyocheza.
Rwanda ilivuna pointi hizo baada ya kuanza vizuri michuano hiyo kwa kuichapa Eritrea mabao 3-0 kabla ya kuifanyia mauaji timu dhaifu ya Jibuti kwa kuibanjua mabao 9-0.
Zanzibar inayoongozwa na Kocha Abdulghani Msoma inatarajiwa kuteremka kwenye uwanja huo kwa nguvu na bila shaka itacheza kufa au kupona kuhakikisha inatinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa kishindo.
Katika mchezo huo Zanzibar Heroes itaongozwa na mpachika mabao wake hodari, Abdallah Juma anayecheza timu ya Mtibwa Sugar inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ambaye atashirikiana na kiungo wa pembeni, Abdi Kassim na beki mwenye nguvu, Nadir Haroub 'Cannavaro' wanaocheza Yanga.
Kipa mzoefu katika michuano ya kimataifa, Farouk Ramadhani anatarajiwa kuwepo katika lango kuhakikisha wapinzani wao hawaleti madhara. Mchezo mwingine unaotarajiwa kufanyika leo ni kati ya Kenya 'Harambee Starsa' na Uganda 'The Cranes'.
majira
l e o hapendwi mtu tunataka wazenji wale eid kwa kujinafasi