Mimi haya mambo ya ukware niliyaanza kitambo kidogo,na ndio maana siishi kusimulia masaibu niliyokutana nayo ujanani.
Nakumbuka siku hiyo nilikuwa natokea zangu Kariakoo narudi nyumbani Tegeta jioni ya saa 11 hivi. Kama mjuavyo kwa hapa jijini Dar usafiri mida ya jioni unakuwa na kasheshe zake, na kama huna ubavu unaweza kujikuta unakosa siti na ikakulazimu usimame, kitu ambacho nilikuwa sikipendi.
Baada ya kupimana msuli na abiria wenzangu nilibahatika kupata siti na kwa bahati nzuri nilibahatika kukaa na mtoto mmoja mbaye naweza kusema Mungu alimjaalia hasa kwa uzuri. Kwa sababu ndio zangu kuunganisha hesabu kwenye daladala nilishukuru sana. Niliomba foleni ianzie Faya ili safari ya Tegeta iwe ndefu, iwe ya saa 3 badala ya dakika 50 au saa nzima.
Ile kukaa tu, nikatupa salaam ya kiungwana, ‘habari yako sista.' Yule dada alijibu kwamba hajambo. Nikasema nashukuru sana, ‘za kazi?' Alijibu kwamba, kwa uwezo wa Bwana ni nzuri. Hilo neno ‘Bwana' sikulizingatia. Najuta ni kwa nini sikulipigia mstari. Naomba niwaambie vijana wa Dar wajue kwamba, msichana akijibu salaam na kuingiza mambo ya ‘Bwana,' ni lazima mtu ajiulize maswali.Basi tulipofika Jangwani nilishukuru kuona kuna foleni ya aina yake.
Nilisafisha koo na kuanza kufanya mazoezi ya namna ambavyo ningemwaga sera zangu za kumkaribisha ibilisi. Hatimaye nilipata njia. ‘Samahani, kama ninakufahamu, sijui tumewahi kuonana wapi, Tegeta, labda, au pale maeneo ya njia panda ya Wazo.'Yule binti alitulia kidogo na kujibu kwa kifupi, 'bahati mbaya, ninaishi Makongo.' Niliona nimepungukiwa na vituo, hivyo kama ni kumwaga sera ingebidi nianze haraka. ‘Ahaa. Oke, naona tumekuwa tukikutana huku huku mjini, sijui unafanyia wapi mwenzangu?' Niliuliza. Yule binti akajibu, 'sifanyi kazi, nasoma chuo cha biashara.' Niliona mitego yangu inapachuka kila nikitega.
Nilitulia kidogo na kutafuta pointi nyingine. 'Sijui mwenzangu unaitwa nani, mimi naitwa…..' Nilitaja jina langu na kabla sijaendelea, nilisikia: 'Kwa jina la Yesu ushindwe, ni nguvu za giza zimekuzunguka. Huwezi kunitia majaribuni….' Alikuwa akipaza sauti, halafu alikuwa akiongea kwa sauti kama ile itumiwayo na wahubiri wa kilokole wakemeapo mapepo. Kama kwamba hiyo haitoshi, alisimama na kutoa kitabu chake kitakatifu. Halafu aliendelea kunishutumu kwamba mimi ni ibilisi ambaye namjaribu mtu wa Mungu. ‘Huwezi kupambana na mwamba, huwezi kabisa, kwa nguvu zake baba ushindwe na uuone mwanga.'Kama mjuavyo watu wa Dar wasivyo na dogo, Basi zima lilivunja shingo.
Kuna waliokuwa wakishabikia kwamba, nimezoea kutongoza hovyo, kama vile walikuwa wananijua. Konda alikuwa akishabikia kweli, na alimtaka yule binti wa Kilokole anitoe katika Giza la upotevu, ili mradi kulikuwa na kila aina ya shutuma na kushangilia. Nililazimika kusimama na kusogea mbele kiaina, maana dhihaka na kejeli vilizidi.
Basi lilipofika Magomeni, nilisogea mlangoni na kushuka fasta. Yule binti alicharuka zaidi wakati nashuka kwenye basi kwa kudai kwamba, nilikuwa nimeshindwa. 'Ameshindwa Ibilisi, ameshindwa kwa nguvu za Bwana, anaona aibu.' Washabiki au wapambe walikuwa wakishangilia kwa nguvu ili kumchagiza yule binti wa kilokole aendelee kunikemea. Nilijilaumu kimoyomoyo kuhusu kosa lile.
Mpaka leo nikiwaona mabinti waliokaa kilokolelokole, nawapitia mbali.