Yametimia ya Magufuli baki: Juma Nkamia awasilisha muswada Rais kukaa madarakani miaka 7 kama Kagame

Al-shabaab

JF-Expert Member
Aug 24, 2013
1,791
617
Nkamia.PNG

Akifanya mahojiano kwa njia ya simu na mtangazaji wa EATV, Mh. Nkamia amesema kuwa yeye ameamua kupeleka muswada huo binafsi kwa spika wa bunge kutokana na serikali kutumia gharama kubwa za kufanya uchaguzi kwa wakati mmoja yaani ule wa serikali za mitaa pamoja na ule mkuu.

"Napeleka hoja au muswada binafsi kwa Spika wa bunge tulijadili hili kama linaweza kufanywa sheria lifanyike. Ndani ya bunge kuna viongozi wetu wa chama kwa hiyo lazima nipeleke kwao ili kujadili na wao waweze kupitisha kama watakubaliana na mimi na kama ikifanikiwa kufika kwa rais basi iwe sheria ambayo itatuoongoza," amesema Nkamia.

"Nikipeleka hoja yangu kwa Spika nitachanganua gharama zinazotumika kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja uchaguzi mkuu. Tunaweza kufanya uchaguzi wote kwa pamoja kama wenzetu mfano Kenya wanakuwa na maboksi mengi sana wakati wa kura, hata sisi tunaweza kufanya kama wenzetu badala ya kutumia gharama mbili kwa kipindi kimoja" aliongeza Nkamia.

Aidha, Mh. Nkamia amefafanua kuwa aeleweke kuwa hajamlenga rais aliyoko madarakani ndiye aanze kwenda miaka saba bali ni kwa viongozi wote na kama wazo lake likitimia wakati Rais Magufuli akiwa madarakani nayo si vibaya.

"Muswada una 'process' zake kwani lazima upitie sehemu nyingi na kama ukishafika kwa wabunge ukajadiliwa na ikakubalika sheria ifanyiwe mabadiliko ndani ya sheria na rais akatia saini ndiyo itakuwa sheria kamili. Na ukifanikiwa kupita wakati Rais Magufuli akiwa madarakani ni vema tu kwani kuna matatizo gani?:", amehoji Nkamia.

Pamoja na hayo Mh. Nkamia amesema kuwa watu wengi na waoga wa kutoa hoja zao kwa kufikiria wananchi watamfikiriaje hivyo kwa upande wake huwa hana woga wowote linapokuja suala la kusimamia hoja.

========

Mapema wiki hii mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia aliingia kwenye vichwa vya habari kutokana na madai ya kuwa na mpango uliokosolewa na watu wengi.

Kupitia mitandao ya kijamii, mbunge huyo alikaririwa kuwa anakusudia kuwasilisha bungeni mswada wa marekebisho ya Katiba utakaowezesha muhula wa urais madarakani kuwa wa miaka saba badala ya mitano ya sasa.

Kwa mujibu wa Katiba, Rais wa Tanzania anapochaguliwa huongoza kwa muhula wa miaka mitano na baada ya hapo anaweza kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine wa muda kama huo.

Kwa kauli hiyo, mbunge huyo ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, anaungana na mbunge mwenzake wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani (Profesa Majimarefu) ambaye hivi karibuni alikaririwa akipendekeza Rais John Magufuli aongezewe muda wa kukaa madarakani hadi miaka 20.

Wazo kama hilo limewahi kutolewa mara kadhaa, akiwamo ofisa wa Rahco aliyependekeza Rais Magufuli aendelee kuwa mahakamani hadi Reli ya Kati inayojengwa ikamilike. Pia, wananchi wa Geita nao waliwahi kujitokeza na mabango kutaka Rais aendelee.

Majimarefu alisema Rais Magufuli ni jembe na ameletwa na Mungu na kwamba atahakikisha anasema katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ili aongezewe muda, kwa kuwa miaka 10 haimtoshi.

Hata hivyo, baada ya kauli ya Majimarefu, Rais Magufuli aliweka bayana kuwa hayuko tayari kukaa miaka 20 bali ataheshimu ukomo unaotajwa na Katiba.

“Ndugu yangu Majimarefu, uliposema niongezewe miaka 20 nilikuelewa kuwa unaniombea niishi miaka 20 ijayo. Ndivyo nilivyokuelewa,” alisisitiza Rais Magufuli.

“Unakamua majipu mengine ni makubwa na yanatoa harufu na kunisababishia hata nikirudi nyumbani nashindwa kula chakula,” alisema Magufuli.

Lakini katika ujumbe wa sasa wa Nkamia, anasema, kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ni gharama kwa nchi maskini kama Tanzania, kwani katika kipindi hicho nchi inakuwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu na hivyo kufanya gharama ya uchaguzi kuwa kubwa.

“Badala ya Serikali kushughulikia kero za wananchi imekuwa ikishughulika kutafuta fedha za maandalizi ya uchaguzi kwa muda mrefu,” inasema sehemu ya ujumbe wa Nkamia aliotuma kwenye kundi la WhatsApp la viongozi.

Mwananchi ilipomuuliza kuhusu ujumbe huo kama ni wa kwake na ni lini atawasilisha mswada huo, mbali na kukiri kuwa ni wake, Nkamia alisema tayari ameshapeleka hoja yake ambayo wakati wowote itawasilishwa bungeni.

Wazo hilo la Nkamia linaibua maswali kemkem kama, Je, katika hoja hii mbunge huyo yuko peke yake? Anashirikiana na watu gani? Kina nani walio nyuma ya ajenda yake?

Wachambuzi wa masuala la siasa wanasema huenda mbunge huyo ametangulizwa na watu wengine kama chambo, ili kumsafishia njia Rais Magufuli iwapo atataka kuongeza muda madarakani tofauti na Katiba inavyotaka.

Awali Nkamia alilieleza Mwananchi kuwa ataipeleka hoja hiyo katika Mkutano wa Bunge wa Novemba na kwamba anategemewa kuanza maandalizi ya hatua hiyo katika vikao vya kamati za Bunge vilivyofanyika mjini Dodoma.

Alipinga kuwapo watu nyuma yake kutoka katika chama chake, akisema ukweli ni kuwa hilo ni wazo lake binafsi ambalo limetokana na mahitaji ya muda na siasa za mfumo wa vyama vingi.

Alisema wakati wanaweka vipindi hivyo nchi ilikuwa kuna mfumo wa chama kimoja, lakini sasa kuna vyama vingi na chama kikimwamini mchezaji kuwa ni mfungaji bora kinamweka, pia wakati rais anaingia madarakani hadi anamaliza muda haumtoshi kutekeleza yale aliyoahidi.

Kauli ya Mwinyi

Kauli kama hiyo ya kutaka Rais Magufuli aendelee kuongoza kama si matakwa ya kikatiba, iligusiwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

“Amelipeleka Taifa mahali kuzuri, amerudisha nidhamu, sasa hivi ukienda hospitali unapata huduma vizuri, ukienda kwenye ofisi unapata huduma nzuri. Yako mengi mazuri, tumuunge mkono Rais wetu, kama isingekuwa Katiba, basi ningesema aendelee.”

Pia, Julai mwaka huu kuliibuka kampeni ya ‘Magufuli Baki’ iliyoanzishwa na Laurence Mabawa, ambaye amewahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Sengerema kwa tiketi ya CCM mwaka 2015.

“... Nitazunguka nchi nzima kwa gharama zangu kupata fursa ya kuwasikiliza wananchi kupitia kampeni yangu. Na sitavunjwa moyo na propaganda za baadhi ya vikundi vinavyonikejeli mitandaoni pasipo kuthamini maendeleo anayoyafanya (Magufuli),” alisema Mabawa.

Hali ilivyo Afrika

Nchini Rwanda Rais Paul Kagame ambaye sasa anaongoza kwa kipindi cha tatu, alibadilisha Katiba ya nchi iliyokuwa ikitoa fursa kuongoza kwa miaka saba na sasa imekuwa miaka mitano kuanzia 2024.

Mbali na mabadiliko hayo, Bunge la nchi hiyo pia lilibadili ukomo wa rais kuongoza vipindi viwili na kumruhusu kugombea kipindi cha tatu na kumwezesha Rais Kagame kuchaguliwa kipindi cha tatu.

Nchini Senegal pia Bunge limepunguza kipindi cha utawala hadi miaka mitano badala ya saba ya awali.

Rais wa nchi hiyo, Macky Sall ambaye alifanikisha mabadiliko hayo yaliyotokana na kupiga kura na kupata ushindi wa asilimia 63 hivyo kuwezesha nchi hiyo kuingia katika muhula wa miaka mitano ifikapo mwaka 2019.

Nchi nyingine zilizobadili mihula yao na kufikia miaka mitano kutoka miaka saba ni pamoja na Burkina Faso na Burundi.

Wakati nchi hizo zinafikiri kupunguza muda, wachambuzi wa siasa wanashangazwa na Nkamia anayefikiria kuongeza muda huo.

Hatua ya mbunge hiyo iliiibua mitazamo tofauti katika mitandao ya kijamii baadhi wakipongeza na wengine walioponda hatua hiyo.

Kupitia akaunti yake ya Facebook, mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la Mwanaspoti, Edo Kumwembe; “Rafiki yangu Juma Nkamia na suti yake maridadi, anasimama mbele ya Bunge, anadai anataka kupeleka muswada uchaguzi uwe baada ya miaka saba...anatolea mfano wa Rwanda eti kwamba uchaguzi wao ni kila baada ya miaka saba na mambo yao ni safi. Hivi Rwanda mambo yao ni safi kuliko Marekani ambayo uchaguzi wao ni kila baada ya miaka minne?”

Charles Mdendemi yeye aliandika; “Ingewezekana uchaguzi mkuu ungefanyika hata baada ya miaka 10 maana unatumia gharama zisizo na maana na zingine zinarudiwa wakati fedha hizo tungeziweka na kufanyia maendeleo. Nkamia anaweza kuwa hajatoa sababu nzuri zaidi ila hoja yake inaweza kutafutiwa sababu njema zaidi.”

Wasomi washangazwa

Akizungumzia hatua hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha, Profesa Gaudens Mpangala anaeleza kushangazwa na mbunge huyo na kwamba hiyo ni mbinu ya kumuongezea madaraka rais aliye madarakani.

Profesa Mpangala alisema miaka mitano kwa sasa ni sawa kwa kuwa ndiyo inayotumika na nchi nyingi na iwapo kiongozi akipewa muda mwingi, wakati mwingine inaweza kusababisha madhara makubwa.

“Nchi zetu nyingi za Afrika kiongozi aliye madarakani anafanya anavyotaka, sasa hapa kuna hatari kubwa iwapo utamuongezea mtu muda na katika utawala wake akawa anafanya mambo ya ajabu mtajuta na hamtakuwa na namna ya kumfanya.

“Miaka mitano inatosha kabisa na katika chaguzi zetu inakubalika kabisa ili kuepuka utawala wa aina hiyo,” anasisitiza Profesa Mpangala.

Alipouliza iwapo anafikiri kuna mtu au kikundi cha watu kipo nyuma ya ajenda ya mbunge huyo, Profesa Mpangala anasema ni kweli inawezekana kuwa ajenda ya mtu au kikundi cha watu kwa kuwa wapo waliokwishaanza kutamka tamka kwamba rais aongezewe muda.

“Sishangai kuona haya yanajitokeza sasa, lakini ukweli ni kwamba katika misingi ya demokrasia ya kiliberali, kumuongezea mtu aongoze miaka saba kwa vipindi viwili yaani miaka 14 ni mingi sana isije tukafika hatua tukajuta na maamuzi tuliyoyafanya.”

Si Profesa Mpangala pekee aliyemshangaa Nkamia, pia Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ally anasema mbunge huyo anang’ang’ania hoja hiyo wakati mwenyekiti wake wa chama, Rais Magufuli ameshafunga mjadala kuwa hana mpango wa kuongeza muda.

Dk Bashiru anahoji kuwa kwa mbunge huyo kupeleka hoja hiyo anamlenga rais gani hasa na kwamba kama lengo ni rais ajaye, sawa lakini Rais Magufuli hilo alishalihitimisha.

“Tatizo tumeshajenga utamaduni, tumeshafanya majaribio kwa zaidi ya miaka 30 sasa na tumeona mfumo tunaoenda nao wa kuwa na mihula miwili ya kipindi cha miaka mitano una manufaa tangu enzi za Mwalimu Nyerere, akaja mzee Mwinyi, mzee Mkapa na baadaye akaja mzee ndogo kuliko wote Kikwete, wote hawa wameonyesha mfumo uliopo hauna shida yoyote.”

Alisema hata mjadala wa Katiba ambao hata hivyo mchakato wake haukufika mwisho, suala la kuongeza muda halikuwa na mashiko, iweje liibuke leo.

“Unajua watu hawakummelewa mzee Mwinyi aliposema kama Katiba ingeruhusu basi Rais Magufuli angetawala milele, hakuwa na maana kwamba sasa tubadili Katiba yetu.”

Alisema hata Rais Magufuli mwenyewe ameshawajibu wanaopitapita na kusema aongezewe muda kuwa hana mpango huo na kwamba urais ni mzigo.

“Hakuna haja ya kurefusha au kupunguza muda, hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa Ikulu si pahali pa kukukimbilia. Naamini Nkamia hana hoja na hawezi kuipata, hivyo ni bora akaacha kufanya hivyo.”

“Hoja ziko nyingi sasa Tanzania inakabiliwa mfano unyaufu na tatizo kubwa la utapiamlo kwa asilimia 36 mpaka watu wanashindwa kufikiri, ni bora akaibeba hoja hiyo ili kuhakikisha tunajikwamua katika janga hilo,” aliongeza

Chanzo: Mwananchi
 
Hilo tangazo la kiwanda kwa tathimini ya kawaida ni Watanzania wangapi watanufaika wakuu?
 
Mimi nachojua mheshimiwa mkulu alisema *kwenye kampeni skuongelea katiba, kwa hyo sio kipaumbele, haya mambo naona kuna nia ya kuwekea mheshimiwa image mbaya kimataifa , naamini katiba yetu itaheshimiwa
 
Back
Top Bottom