Ya kina Chenge na dhana ya ‘EJUL’

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
Ya kina Chenge na dhana ya ‘EJUL’

Johnson Mbwambo Aprili 1, 2009

Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

NILIPOKUWA nasoma sekondari, kuna kazi mbili tu ambazo nilizitamani kuzifanya maishani – uhakimu au upelelezi wa polisi.

Nikiri kwamba uchaguzi wangu huo wa kazi ulitokana na kusisimshwa na utendaji wa hali ya juu wa mahakimu na wapelelezi wa polisi niliokuwa nawasoma katika vitabu maarufu vya riwaya vya wakati ule; kama vile Perry Masson, Nick Carter, Agatha Christie, Henry Denker, James Hadley Chase na hata waandishi wa sasa kama vile Simon Kernick katika Relentless.

Nilikuwa navutiwa na jinsi wapelelezi na makachero katika vitabu hivyo walivyokuwa wakihaha kupeleleza na kukusanya ushahidi juu ya kosa la jinai lililotendeka; iwe ni mauaji au wizi.

Lakini zaidi ya yote nilikuwa navutiwa na busara na hekima za mahakimu au majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hizo. Wote hao walikuwa wakiongozwa na kiu ya kutaka kuona haki inatendeka.

Ni kupitia vitabu hivyo vya riwaya nilikuja kuvutiwa maishani na wapelelezi mahiri wa polisi wa aina ya Tom Lepski au wa masuala ya bima; kina Maddux katika James Hadley Chase n.k.

Kwa hakika, mpaka leo (miaka 30 baadaye) bado nakikumbuka vyema kitabu cha Henry Denker cha A Place for the Mighty. Katika kitabu hicho nakumbuka busara na hekima ya Jaji Robertson aliyesikiliza kesi ya mauaji ya jaji mwenzake mzungu, Harvey Miller yaliyofanywa nje ya Mahakama Kuu na Midge Grove - Mwafrika Mmarekani asiye na ajira ambaye alikuwa hapendi misimamo ya jaji huyo.

Licha ya kwamba jaji aliyeuawa alikuwa rafiki yake, Jaji Robertson katika A Place for the Mighty aliiendesha kesi hiyo kwa hekima na busara kubwa; huku akiupa nafasi ya kutosha upande wa utetezi (chini ya Lincoln Winkler) ambao katika kuhalalisha mauaji hayo ulikuja na utetezi wa aina yake waliouita Doctrine of Social Inevitability.

Utetezi wa mauaji hayo uliojengwa katika msingi wa hiyo Doctrine of Social Inevitability uliingia vichwani mwa wazee wa baraza (jury); kiasi kwamba haikushangaza, mwisho wa yote, kijana yule kupatikana na hatia ya mauaji ya kutokukusudia (manslaughter) na si mauaji ya kukusudia ambayo adhabu yake ingekuwa ni kifo.

Japo A Place for the Mighty ni riwaya tu, lakini yaliyomo ndani ya kitabu hicho yanaonyesha ukweli ulivyo katika Marekani kuhusu nchi hiyo inavyoheshimu dhana ya haki sawa kwa wote mbele ya sheria.

Maneno Equal Justice Under the Law -EJUL (haki sawa kwa wote mbele ya sheria) si tu utayakuta yameandikwa nje ya majengo mengi ya mahakama katika Marekani, lakini pia ndiyo mwongozo wa uendeshaji kesi zao zote.

Tangu nikisome kitabu hicho nimekuwa muumini kweli kweli wa dhana hiyo ya EJUL, na hata sasa bado navutiwa kuangalia chaneli ya televisheni inayoitwa Law and Order katika DSTV na kusisimshwa na jinsi wanasheria katika nchi za wenzetu wanavyohaha kuhakikisha si tu haki inatendeka; bali ionekane imetendeka.

Lakini hapa kwetu Tanzania, dhana ya Equal Justice Under the Law (EJUL) bado ni kitendawili. Ilikuwa inaheshimika sana enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, lakini si katika awamu za uongozi zilizofuatia.

Na kiasi nchi yetu inavyozidi kujikita katika ufisadi; ndivyo pia dhana hiyo inavyozidi kupoteza maana katika asasi zetu za kusimamia sheria. Ni kama vile sasa tuna sheria mbili zisizo rasmi – moja ni kwa ajili ya walalahoi na masikini, na ya pili ni kwa ajili ya vigogo, matajiri na mafisadi!

Labda nifafanue kwa kutoa mfano mmoja ulionijia haraka kichwani mwangu. Wako Watanzania ambao wamo gerezani wakitumikia vifungo kwa kukutwa na madini kinyume cha sheria, lakini enzi za utawala wa Rais Mwinyi tulishuhudia akiagiza Rubani Aziz atolewe jela eti kwa sababu mama yake ( Rubani Aziz) alikwenda kumwombea msamaha.

Wasiolifahamu tukio hilo la mwanzoni mwa miaka ya tisini ni kwamba Rubani Aziz alikuwa amekamatwa na madini Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam.


Mifano ipo mingi, na sitaki nikuchoshe nayo; lakini mlio wengi mnakumbuka pia jinsi kesi za watoto wa vigogo (nyingine zikihusu mauaji) zilivyopata kuvungwavungwa, na hatimaye wahusika kuachiwa huru. Nazungumzia kesi zilizopata kuwakumba watoto wa vigogo kama vile Paul Rupia, Kingunge Ngombale Mwiru, Frederick Sumaye, kwa kutaja wachache tu.

Lakini pia mnakumbuka jinsi Rais Jakaya Kikwete alivyotumia mamlaka aliyonayo kumtoa rumande aliyekuwa mtuhumiwa wa mauaji, Ditopile Ukiwaona Mzuzuri (sasa marehemu); ilihali watoto wa walalahoi wenye tuhuma kama hizo wanaozea rumande! Yeye Ditopile alikuwa na tofauti gani na watoto wa walalahoi wanaoendelea kusota rumande kwa tuhuma kama hizo?

Hilo pembeni, tafakari mfano mwingine: Wakati maelfu ya watoto wa walalahoi wamerundikwa pamoja katika vyumba vidogo vya mahabusu mbalimbali hapa nchini, mtakumbuka pia jinsi serikali ilivyoharakisha kutengeneza vyumba maalumu katika rumande ya Keko kwa ajili ya baadhi ya watuhumiwa wa EPA na kwa ajili ya kina Daniel Yona na Basil Mramba.

Mtakumbuka pia jinsi Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha alivyofanya ziara ya haraka ya kukagua rumande ya Keko ikiwa ni saa chache tu baada ya Yona na Mramba kupelekwa huko!

Na sasa kuna suala hili jipya linalomhusu aliyekuwa mwanasheria mkuu wa zamani wa Serikali na Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge. Huyu, usiku wa manane, kagonga bajaj na kuua abiria wake wawili.


Katika hali ya kawaida, hii ni kesi ya trafiki ya ajali ya gari iliyosababisha vifo. Ni sawa na kesi nyingi tu za aina hiyo zinazotokea kila siku kote nchini, lakini kwa kuwa mhusika ni Chenge (kigogo wa CCM na tajiri), inaundwa tume maalumu kuchunguza ajali hiyo; tena ikishirikisha hata Usalama wa Taifa!

Kwa uamuzi huo, mtu unajikuta ukijiuliza maswali kibao yasiyo na majibu: Inaundwa tume maalumu kwa sababu mtuhumiwa ni Chenge ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na tajiri mkubwa au ni kuweka mazingira ya kukwepa lawama baadaye?

Je, kuundwa kwa tume hiyo maalumu kunalenga katika kuhakikisha haki inatendeka au ni mbinu na ujanja tu wa hatimaye kumlinda Chenge bila serikali kutupiwa lawama?


Vyovyote vile; kwa nini tuwe na taratibu tofauti kwa kosa hilo hilo moja? Kwa nini sheria na kanuni zinazohusu namna ya kushughulikia makosa ya usalama barabarani zibadilike inapotokea watuhumiwa ni vigogo?

Hata kama Chenge atakuja kupatikana na hatia ya kuendesha gari kizembe na kusababisha vifo vya wanawake hao wawili, sitashangaa baadaye akitolewa lupango kwa msamaha wa Rais; kama Mwinyi alivyofanya kwa Rubani Aziz au hata Rais Kikwete mwenyewe alivyofanya kwa Ditopile alipomtoa rumande wakati akikabiliwa na kesi ya mauaji.

Mpenzi msomaji; ukitafakari hoja yangu na mifano niliyoitoa mwanzoni kabisa, utakubaliana nami kwamba tuna sheria mbili hapa nchini – sheria kwa ajili ya walalahoi na makabwela na sheria kwa ajili ya vigogo, matajiri na mafisadi!

Na kama hivyo ndivyo, basi tunapanda mbegu za kuvuruga amani kwa kasi ya kutisha; maana huwezi kuitosa dhana ya Equal Justice Under the Law (EJUL), na bado ukatarajia nchi kuendelea kuwa ya amani.

Tafakari!
 
Back
Top Bottom