Wizi huwa haulipi na majuto ni mjukuu

Ghaysh

Member
Feb 12, 2015
24
43
Mwenzetu damu zikawa zinamchuruzika kichwani tukajua anakufa….!

Nakumbuka tukio hili lilitokea mwaka 2005 wakati nilipokuwa nikifanya kazi katika hoteli moja ya kitalii iliyoko katika ufukwe ulioko kusini mwa jiji la Dar es salaam. Naomba nisiitaje hiyo Hoteli.

Hoteli hiyo ilikuwa ni mbali na mji ilikuwa imezungukwa na vijiji kadhaa ambavyo ni Gomvu, Kichangani, Ngobanya na Mbalajange ambavyo Kijiografia vilikuwa viko mbali na Hoteli hiyo. Hivi ndiyo vijiji ambavyo tulikuwa tunaenda kutafuta totoz kila weekend tukiwa mapumziko na kula starehe.

Ili kurahisisha huduma kwa wateja mwekezaji alikuwa amejenga nyumba za wafanyakazi umbali wa nusu kilomita ili wafanyakazi waishi Jirani na hoteli.

Kwa kawaida wafanyakazi walikuwa wanajinunulia vyakula vya kupika vijijini au mjini wakienda mapumziko kusalimia majumbani kwao au familia zao ambapo kwa waliokuwa wakiishi maeneo ya mjini kama Kinondoni, Ilala au Temeke walilazimika kusafiri umbali mrefu kabla ya kuvuka ferry kiasi cha kilomita 50 kutoka Hoteli ilipo.

Sasa kutokana na labda kubana matumizi au kuishiwa chakula cha kupika wapo baadhi ya wafanyakazi wasiyo waaminifu walikuwa anaiba chakula hotelini na kutoka nacho kwa kificho huku wakiwa wameficha katika sehemu za mwili ambazo siyo rahisi askari kugundua wakati tukisachiwa getini kabla ya kurudi kambini kwa sababu huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa Hoteli.

Siku moja mchana jua likiwaka tulipokuwa tunatoka tukiwa tumepanga foleni kusubiri kusachiwa na mlinzi wa getini tulimuona mwenzetu ambaye alikuwa amevaa baraghashia akivuja damu kichwani tukashtuka sana tukajua mwenzetu labda kaumia. Tukimsogelea ili kumvua kofia tumuangalie kapatwa na nini, akawa anatukwepa lakini alikuwa anatetemeka na jasho likimtoka.

Baada ya kuona mwenzetu yuko katika hali ile tukalazimika kwa kushirikiana na walinzi kumshika kwa nguvu na kumvua ile kofia.

Lahaulaaaa kumbe alikuwa na nyama kaificha kichwani kwa kufunika na kofia ili isionekane na walinzi wakati wa kusachiwa. Ukweli ni kwamba ile nyama ilikuwa imeganda na barafu kwa sababu alikuwa ameichukua kwenye jokofu na kitendo cha kupigwa na jua wakati wa kusubiri kusachiwa ikawa inayeyuka ile barafu na hivyo kuchuruzika maji yaliyochanganyika na damu kutokea kichwani.

Walinzi walimuweka chini ya Ulinzi na kumuita Meneja rasilimali watu na baada ya kesi yake kusikilizwa siku iliyofuata akapoteza kibarua.

Ni tukio ambalo lilitutisha kuona mwenzetu anatokwa na damu kichwani lakini baada ya kukuta ni nyama aliyokuwa ameificha kichwani tulicheka sana japo halikuwa jambo la kufurahisha kwa sababu tulijua mwenzetu anapoteza kibarua.

Kwa tukio hilo nikawa nimejifunza kwamba wizi huwa haulipi na majuto ni mjukuu.
 
Back
Top Bottom