1.
Nimepata wa thamani, ni hakika si majungu,
Mwingine sitatamani, nimefunga moyo wangu,
Sikupotea ramani, nimezikubali pingu,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
2.
Kila nionapo wingu, mbingu nayo ni dhahiri,
Huwezi ingia mbingu, bila liingia wingu,
Wingu liko na mbingu, mbingu zina mawingu,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
3.
Hayawi hayawi yawa, thelathini siku zawa
Sio nyingi kama chawa, zi nyepesi kama buwa,
Kwa sala na zote duwa, maombi yamejibiwa,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
4.
Tangu tulipozianza, ndoto za baba na mama,
Ni mengi tumejifunza, tukabakiza kuhama,
Na sasa twende kufyonza, tamu iliyofichama
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
5.
Mwaka ule si karibu, subira ndio mtaji,
Tele hayo majaribu, yasiyopozwa na maji,
Imara kama bawabu, makini kama hujaji,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
6.
Nyakati nayo majira, na zama zimetimia,
Mapenzi haya imara, silaha kuu ya ndoa,
hazijalishi ngawira, mapendo tumekamia,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
7.
mpira ulipoupiga, niliepa nisidake,
kwa mengi ulinikoga, japo hunayo makeke,
na sasa nimejibwaga, hirimu wangu nishike,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
8.
za mwizi hazikawii, zetu walizikamia,
pamoja nayo bidii, ya maombi kuazimia,
agizo sasa kutii, la ndoa na familia,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
9.
asante mpenzi wangu, kimasomaso menitoa,
mapendo kama uchungu, kwa machozi nimeloa,
lishike vizuri rungu, kwako nimeshajitoa,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
10.
tuijenge hiyo nyumba, yenye kujaa vicheko,
watoto nao kuumba, mbinguni tupate heko,
wala tusije kuyumba, kwani tunao upako,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
11.
udumu cha nyumba kichwa, mimi ni wako ubavu,
bidii ipite mchwa, ushinde wote uchovu,
nyuma tusije kuachwa, kwa Yesu uko wokovu
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!
12.
Asante wote wapendwa, kwa maombi nazo dua,
Ni kweli hamkushindwa, shetani kumkemea,
Upendo uliopandwa, hitaji kuu la ndoa,
Mimi nawe Naimani, ni kama wingu na mbingu!