Wezi EPA waanikwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wezi EPA waanikwa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Aug 27, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 27, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,548
  Likes Received: 81,990
  Trophy Points: 280
  Wezi EPA waanikwa

  Mwandishi Wetu Agosti 27, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  Ni baada ya jk kuhutubia bunge

  SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuongeza muda wa kikosi kazi (task force) kinachochunguza sakata la wizi wa mamilioni ya fedha ndani ya Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), siri zaidi kuhusiana na wahusika wakuu zimedizi kuanikwa.

  Nyaraka kadhaa zilizoifikia Raia Mwema wiki hii zinaonyesha kwamba mbali ya makachero na asasi za kimataifa kujulishwa kuhusiana na wizi huo, wahusika wakuu wa wizi huo wameelezwa kuwekeza katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Uingereza, Falme za Kiarabu, Mauritius, Marekani na India na baadhi wamewekeza ndani ya nchi kwa kutumia majina tofauti.

  Kwa mujibu wa nyaraka hizo, mfanyabiashara maarufu Jayantulal Chandubhai Patel anayejulikana zaidi kwa jina la Jeetu Patel, ndiye anayeongoza kwa kuwa na vitega uchumi vingi ndani na nje ya nchi ikiwamo majumba na makampuni yenye rasilimali kubwa.

  Jeetu Patel ambaye anatajwa kuwa karibu na uongozi wa juu wa serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, anaelezwa kuwa alifanikiwa kufanya kazi kwa karibu na aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali (sasa marehemu), na kuwa na mtandao mkubwa wenye kuhusisha wafanyabiashara na wanasiasa na watumishi wa Serikali ambao walishirikiana katika kufanikisha wizi huo.

  Uchunguzi umebainisha kwamba Jeetu Patel na wafanyabiashara wakubwa wawili walioko nyuma ya kampuni ya Kagoda Agricultural Limited, ndio waliochukua zaidi ya asilimia themanini ya fedha za EPA kwa kutumia nyaraka za kughushi.

  Jeetu Patel pekee anahusika katika makampuni manane kati ya makampuni 13 yaliyothibitika na wakaguzi pamoja na wachunguzi kwamba yamechota shilingi bilioni 90 kati ya shilingi bilioni 133 zilizopotea katika akaunti ya EPA katika kipindi kifupi cha kati ya mwisho wa mwaka 2005 na mwanzo wa mwaka 2006 kipindi ambacho nchi ilikuwa katika Uchaguzi Mkuu.

  Ripoti ya Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young waliofanya kazi kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilionyesha kwamba kiasi cha Shilingi 90,359,078,804.00 zililipwa kwa makampuni hayo 13 ambayo yalitumia kumbukumbu, nyaraka na hati zilizo batili na za kugushi na kwamba makampuni hayo hayakustahili kulipwa chochote.

  Wakaguzi hao na Ikulu kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, Januari 9, 2008, walipendekeza moja kwa moja bila kuuma maneno kwamba wahusika wa kampuni hizo 13 wachukuliwe hatua za kisheria mara moja, kauli ambayo Rais Kikwete aliirejea katika hotuba yake ya wiki iliyopita, japo safari hii alionekana kutumia kauli ya kidiplomasia zaidi badala ya ukali alioonyesha wakati wa kupokea ripoti ya wakaguzi.

  Makampuni ambayo Jeetu Patel anahusika nayo na ambayo yamethibitika kughushi nyaraka na kuchota fedha BoT ni Navycut Tobacco (T) Limited, Ndovu Soaps Limited, Bina Resorts Limited, Bencon International Limited, Maltan Mining Company Limited, Bora Hotels & Apartments Limited, Venus Hotels Limited, and B.V. Holdings Limited.

  Pamoja na kampuni hizo za Jeetu Patel, kampuni nyingine zilizohusika na jinai ya kughushi nyaraka ni pamoja na Kagoda Agriculture Limited ambayo wanaoonekana katika nyaraka ni John Kyomuhendo mwenye hisa 40 na Francis William anayemiliki hisa 60 katika kampuni hiyo.

  Kampuni nyingine ni V.B & Associates Company zinazomilikiwa na Devendra Patel na Jantkumar Chandubhai Patel na Changanyikeni Residential Complex Limited inayomilikiwa na Jose Van de Merwe, Samson Mapunda na Charles Mabina ikiwa na makao yake, Sinza, Kumekucha, Dar es Salaam.

  Katika orodha hiyo pia kuna kampuni 13 zilizoghushi nyaraka ambazo wahusika wake wamependekezwa kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja ni Money Planners & Consultants inayomilikiwa na Paul Nyingo na Fundi Kitungi na kampuni ya Njake Hotel & Tours Limited inayomilikiwa Japhet Lema, Anna Lema, Abel Lema, Derick Lema na Benard Lema wa Arusha.

  Kampuni ya G&T International Limited, ambayo nyaraka zake zilishindwa kupatikana wakati wa ukaguzi zimebainika kumilikiwa na na Octavio Timoth na Beredy Malegesi, mwanasheria ambaye anadaiwa kufanyiwa njama za makusudi za kutumia ushahidi dhidi yake “kumziba mdomo” asiwataje wahusika wakuu wa wizi huo anaodaiwa kuwajua kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiwaongoza kufungua kampuni.

  Jeetu Patel katika baadhi ya kampuni anashirikiana na wafanyabiashara wengine wa Dar es Salaam ambao wanatajwa kushiriana naye katika kuhamisha fedha hizo kwenda nje kwa kuzibadili kutoka shilingi za Kitanzania kwenda Dola za Merakani ama Euro bila kufuata mkondo halali wa fedha kinyume cha Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu.

  Miongoni mwa wanaotajwa kushirikiana na Jeetu Patel ni Sidik Yacoubu kupitia kampuni yao ya Ndovu Soap Limited ambayo kwa mujibu wa nyaraka za Wakala wa Leseni na Usajili wa Kampuni (BRELA), kampuni hiyo yenye namba ya usajili 20536 ya Februari 3, 1992, wamiliki wake ni Jayantulal Chandubhai Patel na Sidik Yacoubu.

  Kampuni ya Bora Hotels and Apartments iliyosajiliwa Septemba 8, 2005 inaonyeshwa katika orodha ya BRELA kwamba wamiliki wake wamo Jayantkumar Chandubhai Patel na Devandra Patel wakati Bina Resort Limited iliyosajiliwa Machi 31, 2005, wamo Jayantikumar Chandubhai Patel na Devendra Patel.

  Kampuni ya Maltan Mining Company iliyosajiliwa Machi 8, 1993 inamilikiwa na Jantkumar Chandubhai Patel na Hariharier Radhakrishna wakati Navy Cut Tobacco iliyosajiliwa Oktoba 12, mwaka 1995 inamilikiwa na Jantkumar Chandubhai Patel na Radakrishna.

  Kampuni nyingine ni Bencon Limited, B.V Holdings, Venus Hotels na V.B & Associeties Company zinazomilikiwa na Devendra Patel na Jantkumar Chandubhai Patel, ambazo zote zilisajiliwa Aprili 4, 2005.

  Katika orodha ya BRELA imo pia kampuni ya Excellent Service Limited inayomilikiwa na Emil Samanya, Peter Sabas na Elisifa Ngowi ambaye anatajwa kuwa ni Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kampuni hiyo ilisajiliwa Mei 13, 1992 na kupewa namba 26959.

  Ngowi ambaye anaelezwa kushiriki kwa kiasi kikubwa katika kikosi kazi kilichochunguza sakata hilo, anahusishwa pia katika kampuni nyingine ya Clyton Marketing iliyosajiliwa Juni 6, 2005 akiwa na Edwin Mtoi, ambaye haikuweza kufahamika mara moja anafanya shughuli gani zaidi ya kuwa katika kampuni hiyo.

  Wamiliki wengine waliofahamika ni Rajabu Maranda na Thabit Katunda ambao wanatajwa kumiliki kampuni ya Liqiud Service Limited ambayo usajili wake ulifanyika Desemba 12, 2004 na kupewa namba 15007. Maranda anatajwa kuwa mmoja wa wana CCM mashuhuri mkoani Kigoma na alidaiwa kutaka kuiingiza familia ya viongozi wa juu serikalini katika biashara zake bila mafanikio hususan baada ya Rais Kikwete kuwa makini zaidi.

  Wamiliki wengine waliofahamika ni Johnson Lukaza na Mwesigwa Rutakyamilwa Lukaza ambao wao wanamiliki kampuni ya Karnel Meals Holdings Ltd ambayo usajili wake ulipatikana Agosti 4, 1998, Mibale Farm iliyosajiliwa Septemba 2, 2005 na kupewa namba 154039 ambayo inamilikiwa na Kizza Selemani na Farijala Hussein na Malegesi Law Chambers inayomilikiwa na Beredy Malegesi ambayo ilisajiliwa Septemba 24, 2001.

  Wamiliki wengine ni Paul Nyingo na Fundi Kitungi, wanaomiliki Kampuni ya Money Planners & Consultants iliyosajiliwa Machi 22, 2005 na Kiloloma & Bros Enterprises inayomilikiwa na Charles Kissa, ambayo ilisajiliwa Aprili 8, 2005.

  Wakaguzi na wapelelezi walithibitisha kwamba nyaraka na majina ya makampuni ya kigeni kama vile Marubeni Corporation, Matsushita Electiric Trading, Tomen Corporation zilighushiwa na watuhumiwa mbalimbali, ambao baadhi yao wanafahamika na wapo nchini lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao mbali ya kuelezwa kwamba wanalipa fedha walizoiba.

  Mifano iliyotajwa ni pamoja na majina kama Kito Morita wa Matshushita na Nakaoki Fujita wa Marubeni ni majina yanayodaiwa kuwa ya kughushi ambayo yalitumika kuchotea fedha hizo, bila ya maofisa wa BoT na serikali kufanya uhakiki na wahusika nchini Japan.

  Imethibitika kwamba majina hayo hayamo katika orodha ya wakurugenzi wa makampuni hayo na wala hawahusiki katika kuidhinisha malipo na kuna habari kwamba raia kadhaa wa Japan sasa wanaulizia imekuwaje majina ya makampuni wanayoyaheshimu kutajwa katika wizi mkubwa kama wa EPA. Wizi wa aina hiyo ni kashfa kubwa kwa wahusika nchini humo.

  Katika hotuba yake bungeni wiki iliyopita, Rais Kikwete aliitaja kampuni ya Marubeni akisema kwamba, ni lazima wachunguzi wajiridhishe kwa kufanya mawasiliano na wenzao katika nchi husika ili kuweza kutenda haki katika hatua watakazochukua dhidi ya wahusika wote, wakati mali za wahusika hao na hati za kusafiria zikiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

  Nyaraka ambazo Raia Mwema imeziona zinaonyesha kwamba, hati ya kughushi ya kampuni nya Marubeni ya Japan iliidhinishwa na BoT Oktoba 19, 2005 na kutolewa maelekezo ya kuidhinishwa kwa malipo kwa maelekezo ya maofisa wa kitengo cha fedha za nje ambao wanaelezwa sasa kuchukuliwa hatua siku moja kabla ya Rais Kikwete kuhutubia Bunge.

  Maofisa wanaotajwa kushiriki katika kuidhinisha malipo ya EPA ni pamoja na Imani Mwakosya, Esther Komu, Kimela, A.A.Chaula na M. Nderimo ambao wanadaiwa walifanya kazi kwa shinikizo kutoka kwa wakubwa zao akiwamo Dk Ballali ambaye naye alishinikizwa na viongozi wa juu na wanasiasa.

  Katika hotiba yake Rais Kikwete alisema uchunguzi kuhusu kampuni 13 yaliyochota Sh bilioni 90 umekamilika, wakati makampuni tisa yaliyochota shilingi bilioni 42, unalazimika kuhusisha washirika wa mataifa mengine ya nje na hivyo ametoa muda hadi Oktoba 31 kwa kamati aliyoiunda chini ya Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika kukamilisha kazi hiyo.

  Rais alisema wamekamata mali za watuhumiwa wote na kwamba “wale watu ambao kwa kweli walikuwa wanaonekana ni matajiri sana wapo katika hali ngumu sana. Wenyewe wanajijua hali zao zilivyokuwa ngumu sana.” Lakini Raia Mwema ina taarifa kwamba baadhi ya watuhumiwa hao wapo na wala hawaelekei kama wametiwa msukosuko.

  Alisema kwa sasa zimekusanywa shilingi 53,738,835,392/= na akaagiza fedha hizo kuingizwa katika mfuko maalumu kwa ajili ya kusaidia sekta ya kilimo zikichanganywa na nyingine zinazotarajiwa kufikia shilingi 64,844,770,688/= .

  “Kamati imeomba idhini kuwa madeni hayo yanayoendelea kulipwa yaendelee kulipwa mpaka tarehe hiyo, maombi yao hayo nimeyakubali. Lakini tumekubaliana kwamba itakapofika tarehe 31 Oktoba, 2008 mwisho ambaye hakulipa mpaka tarehe 1 Novemba, 2008 awe amefikishwa mahakamani ili Mahakama itusaidie kupata fedha za watu, hatuko tayari kulipa deni la Marubeni India, Japan na mtu amekula hela yupo pale Dar es Salaam, hapana,” alisema Kikwete.
   
Loading...