Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe ataka TBS, Vipimo kutoa vipaumbele kwa wafanyabiashara

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amewataka watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Vipimo (WMA), kuwapa kipaumbele wafanyabiashara ili waweze kutengeneza bidhaa za Tanzania zinazokidhi matakwa ya soko la ndani na nje.

Waziri Mwambe aliyasema hayo alipokuwa akizungungumza na menejimenti na wafanyakazi wa TBS na WMA, alipofanya ziara katika taasisi hizo akifuatana na Naibu Waziri wa Viwanda, Exaud Kigahe na baadhi ya wakurugenzi wa wizara.

Akiwa TBS, Waziri Mwambe aliliagiza shirika hilo lifanye ukaguzi wa bidhaa kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika na ukaguzi wa mizigo bandarini na mipakani ili kupunguza muda unaotumika kukagua bidhaa hizo, kupunguza mianya ya rushwa na kurahisisha utoaji wa mizigo hiyo kwa haraka.

Aidha, aliitaka TBS ipunguze muda wa kuandaa viwango kutoka miezi 9 hadi miezi 3 na muda wa usajili wa bidhaa na kutoa alama ya ubora kutoka miezi 3 hadi mwezi mmoja, ili kuwarahisishia wajasiriamali kuweza kufanya na kukuza biashara zao kwa urahisi.

Vilevile Waziri Mwambe aliiagiza TBS kufanya kazi kwa pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwand Vidogo (SIDO) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuandaa viwango na miongozo yenye vigezo rahisi, vitakavyowawezesha wajasiriamali kuanzisha viwanda vidogo majumbani ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa, kukuza biashara , kuongeza ajira na kuongeza pato la taifa.

Mwambe pia alihimiza TBS kufanya kazi kwa karibu na maofisa biashara wa halmashauri ili kurahisisha utoaji wa elimu na usimamizi wa viwango kwa wajasiriamali ili kupanua uwigo wa utoaji huduma na kuwafikia wajasiriamali wengi walioko katika halmashauri hizo.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Kigahe alizitaka TBS na WMA kuhakikisha zinasimamia viwango na ubora pamoja na vipimo sahihi vya bidhaa za Tanzania ili kuziwezesha kuingia katika soko la ushindani ndani na nje ya nchi kwa ufanisi.
 
Back
Top Bottom