Waziri wa Maji, Lwenge ataka wahujumu wa miundombinu ya maji washtakiwe kwa kosa la uhujumu uchumi

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,557
21,512
index110.jpg

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge ametaka watendaji wa Halmashauri nchini kuwashtaki watu wanaohujumu miundombinu ya maji kama wahujumu uchumi.

Hayo aliyasema leo alipofanya ziara katika kijiji cha Bumila kata ya Lupeta Halmashauri ya Mpwapwa baada ya kupokea taarifa ya hali ya huduma ya maji katika kijiji hicho.

“Naagiza Halmashauri muwatafute watu wote waliohujumu miundombinu ya maji na washitakiwe kama wahujumu uchumi, hatuwezi kuwaachia watu wanaosababisha wananchi wasio na hatia kukosa huduma muhimu ya maji”

Miundombinu ya maji katika kijiji cha Bumila imehujumiwa kwa mabomba zaidi ya 40 ya nchi 2 yenye urefu wa mita 6 kwa kila kipande cha bomba kung’olewa na hatimaye maji kutokuwafikia wananchi.

Katika hali ya kulikabili tatizo la maji katika kijiji hicho Mhandisi Lwenge ameiagiza Halmashauri ya Mpwapwa kuchimba kisima katika kijiji cha Bumila haraka ili kuwaondolea adha wananchi wa kijiji hicho.

Katika hatua nyingine Waziri Lwenge amewataka viongozi na watendaji wote nchini kushughulikia maswala ya maji badala ya kuachiwa yeye Waziri wa Maji peke yake.

“Kila mmoja wetu kwa nafasi yake ana jukumu la kufatilia maswala haya sio ya waziri wa maji peke yake, Wilayani mkishindwa mpeleke Mkoani nao wakishindwa wataleta Wizarani nasi tukishindwa tutapeleka kwa Magufuli kitu ambacho sitegemei” Alisema Waziri Lwenge.

Akiwa Wilayani Chemba, Waziri Lwenge amekataza tabia ya baadhi ya vijiji, kata na jamii za watu wanao wabagua jamii nyingine katika miradi ya maji. Akiwa wilayani humo Lwenge aliagiza kuwa miradi yote ya maji ni mali ya serikali hivyo jamii zote bila kujali mipaka ya kijiografia kupata huduma hiyo.

“Maji yote ni mali ya serikali, hamna mtu wala kikundi cha mtu chenye kumiliki maji, hivyo hairuhusiwi kwa mtu au kikundi cha watu kujimilikisha maji na kubagua baadhi ya jamii ya watu wengine wasipate maj, sisi sote ni watanzania”. Alisema Waziri Lwenge.

Ziara ya Waziri Lwenge ilianza katika Halmashauri za Chemba na Kondoa na kuishia katika halmashauri ya Mpwapwa ikiwa ni ahadi aliyoitoa bungeni kwa mbunge wa Chemba Juma Nkamia na Mpwapwa George Lubeleje.
 
Back
Top Bottom