Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 1,900
- 944
Waziri, Mhe. Dkt. Ndumbaro Awataka Wahitimu Kutumia Elimu Zao Kusaidia Jamii
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amewataka wahitimu wa mahafali ya 42 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuitumia elimu waliyoipata kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto za jamii zinazowazunguka kupitia maeneo yao ya kazi ama makazi.
Dk Ndumbaro, ametoa rai hiyo Disemba 14, 2023 katika Uwanja wa Majimaji uliopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, alipohudhuria mahafali hayo kama mgeni rasmi.
“Mlichopata hapa siyo cheti, bali ni elimu ambayo ili iwe na manufaa inabidi mkaitumie kutatua changamoto zilizopo katika jamii kwa kuisaidia na kufanya tafiti zenye tija. Wakati tunaelekea kupata dira mpya ya taifa ya mwaka 2025, katumieni elimu mliyopata kutoa maoni, uzoefu na maono yenu kupitia mijadala itakayowezesha kupata dira makini kwa taifa letu.
Pia, mnapaswa kutumia ujuzi na maarifa mliyopata kuwa wabunifu wa kuziona fursa na kuzichangamkia ili kuzalisha ajira kwa vijana na jamii kwa jumla,” amesema Dk Ndumbaro.
Aidha, amekitaka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuutumia upekee wake kueneza na kukuza Kiswahili ulimwenguni, vilevile, ametoa rai kwa chuo kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa kuhakikisha ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni ndani na nje ya nchi unafanikiwa ili kuendana na ajenda mahsusi ya taifa ya kukuza, kueneza na kubidhaisha lugha hiyo katika Bara la Afrika na duniani kwa jumla.