Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,802
- 31,814
Jaws Corner Mji Mkongwe ngome kuu ya CUF
Picha ilipigwa na mwandishi siku ya uchaguzi 22 Oktoba 1995
Sheikh Amar nilikuwa Zanzibar siku ile ya kupiga kura tarehe 22 siku ya Jumapili Oktoba mwaka wa 1995. Mvua kubwa sana ilinyesha. Katika shajara yangu nimeandika mengi hadi majumuisho ya kura zote pamoja nä butwaa iliyogubika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kumtangaza mshindi.
Nikiangalia nyuma leo naiona picha halisi ya viongozi wetu. Viongozi wetu bado hawajabadilika wanaendelea kuishi katika ndoto na hofu za uchaguzi. Kwa viongozi wetu uchaguzi ni jinamizi anaekuja na ndoto mbaya ya kutisha.
Election Calander Count Down iliyowekwa Jaws Corner wakati wa uchaguzi
Wananchi wa Zanzibar ndiyo waliosimama kwenye mstari toka 1995 hadi 2015 hawajatetereka katika upigaji wao wa kura. Wamekuwa wakipiga kura ya ushindi kila uchaguzi na matokeo ya kura zao wanayajua kwa hiyo uchaguzi hauwatii hofu. Waingereza wangesema, "It is like a walk in the park." Yaani ni kama mtu ana barizi kwenye bustani.
Zigo la gunia la misumari yenye ncha kali wamejitwisha viongozi wetu vichwani mwao na ukiwaangalia tu zile, "body language," zao zinafichua kila kitu. Sambamba na hali hii wananchi wa Zanzibar wanazo namna zao za ajabu kabisa za kujifariji na kujiburudisha kutokana na matatizo wayaonayo kwa viongozi wao.
Mara wanaweka kwenye mitandao ya jamii picha ya kinu cha umeme kilichokuwa Zanzibar nk. nk. Lakini kubwa Ijumaa kama ya leo wanaulizana Maalim Seif leo anaswali wapi? Allahu Akbar. Ikijulikana msikiti gani ataswali tayari ishakuwa adha. Hauna kuwahi jitahidi utakavyojitahidi jua utaswali nje juani. Wazanzibari wanawapenda sana viongozi wao...
Natamani nikuwekeeni yale niliyoandika katika shajara yangu ukurasa wa Jumapili 22 Oktoba 1995 siku ya kupiga kura lakini natia natoa maana sheria ya mtandaoni imekuwa kali kidogo. Unapoandika katika shajara uko faragha unajitanua upendavyo maana unazungumza na nafsi yako...niliwaonesha wachapaji vitabu shajara zangu wananitia hima niwaandikie kitabu kuhusu Zanzibar na matatizo ya uchaguzi.
Nawaambia haya siwezi kuyasema hadharani maana ithibati yake ni mie nipate upande wa pili na kwao huu ni muhali mkubwa. Wachapaji wao wanaangalia mauzo ya kitabu...si rahisi leo viongozi wetu kukubali baadhi ya nema zilizopotea Zanzibar...Wazanzibari wenyewe huzikumbuka neema hizi na kuziadhimisha kwa kuweka picha mitandaoni kisha wakaomba dua.
Viongozi wa Tanganyika wajitahidi sana wawajue Wazanzibari vinginevyo watakuwa siku zote wanajikwaa na kungo'a kucha ya dole gumba.
Ingia kuangalia picha: Mohamed Said: KUTOKA FB: WAZANZIBARI WATU WA SUBRA SANA WAKUMBUKAO NEMA KULIKO SHIDA ZAO